Alhamisi, 18 Juni 2015

TANZU ZA USHAIRI WA KISWAHILI

TANZU ZA USHAIRI WA KISWAHILI
Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au kumbo mbalimbali. Mulokozi (1996), ameuainisha ushairi wa kimapokeao katika kumbo kuu tatu za kimtindo. Kumbo hizo ni: ushairi wa kijadi au kimapokeo; ushairi wa mlegezo; na ushairi wa maigizo.
1.      Ushairi wa Kimapokeo
Haya ni mashairi ya kijadi yenye kufuata kanuni za urari wa mizani na mpangilio wa vina vya mwisho na/au vya kati. Mfano wa shairi la kimapokeo ni huu hapa:
Namshukuru
Namshukuru Illahi, Mwenyezi mkamilifu,
Kwa kuishi nikawahi, kazini kustaafu,
Bado ningali sahihi, imara na mkunjufu,
Alihamdulilahi, namshukuru Latifu.
Ulimwengu wa rakadha, umejaa hitilafu,
Sikuweza mambo kadha: karibu mambo elfu;
Kanipa hii karadha, Bwana Mungu namsifu,
Alihamdulilahi, namshukuru Latifu.
Hii sikutazamia, kwamba litanisadifu,
Bahati imenijia, kwa kupenda Mtukufu,
Mfano kama ruia, Mungu hana upungufu,
Alihamdulilahi, namshukuru Latifu.
(Shaaban Robert, 2003: 102 – 104)

2.      Ushairi wa Mlegezo
Haya ni mashairi yenye kufuata baadhi ya kanuni za arudhi za kimapokeo ambayo wengine huyaita sukui au “guni” nay ale yasiyofuata kabisa kanuni hizo (mauve au mashairi huru).
(a)   Mfano wa shairi guni ni:
Muombwa
Muombwa ni wewe Mungu
Na jamii ya umati,
Miili itie nguvu
Na heri katika nchi,
Astawi kila mtu
Zitakae na nafsi.
(Shaaban Robert, 1968: 18)

(b)   Mashairi ya Mavue (tungo – mtiririko, mashairi – huru)
Wao Pia Walicheza
Na hao wafuasi wa Mzee
Askari wa Mapinduzi
Waliicheza ile ngoma.
Kama asingekuwa Nagona
Kutokeza hadharani
Wangevunja mifupa yao.
Anayeleta sasa ubishi
Amemsahau kiongozi wake.
(E. Kezilahabi, 1988: 18)
3.      Ushairi wa maigizo
Ushairi wa maigizo ni fani ngeni kidogo katika ushairi wa Kiswahili. Tunaposema fani ngeni tuna maana kwamba si fani ya siku nyingi kama zilivyo fani nyingine za ushairi wa Kiswahili. Ushairi huu unaweza kuwekwa katika makundi mawili ambayo ni: ngonjera na ushairi wa kidrama.

(a)   Ngojera
Ngonjera ni neno la kigogo lenye maa ya twende pamoja au kuambatana. Huu ni ushairi wa majibizano ambao uliasisiwa na Mathias Mnyampala katika kipindi cha miaka ya sitini ili kueneza siasa ya Ujamaa. Kabala ya Mnyampala, ushairi wa aina hii ulikuwepo lakini haukuwa na mtindo huu wa kingonjera, ulikuwa unatambwa tu. Kwa mfano shairi la majibizano ni kama lifuatalo:

Usawa wa Binadamu
I
Wasema watu ni sawa, nambie usawa wao,
Kina hohehahe hawa, ambao hawana vyao,
Na watu wenye vipawa, wenye vyeo, wenye vyao,
Nambie usawa wao, watu mbalimbali hawa.
Mwone mbilikimo huyu, na Mtusi wa Ruanda,
Huyu kimo cha kibuyu, na kanzu yake ni gwanda,
Yule ni kama mbuyu, pandikizi mtu panda,
Kibuyu na kingaranda, ni kibuyu si mbuyu.
II
Watu ni sawa nasema, zingatia neno watu,
Siwapimi kwa vilema, ambavyo ni udhia tu,
Siwafanidi kwa wema, ambao ni tabia tu,
Lakini watu ni watu, mawalii na wagema.

Niseme maji ni maji, pengine utaelewa,
Ya kunywa, ya mfereji, na yanayoogelewa,
Ya umande na theluji, ya mvua, mito, maziwa,
Asili yake ni hewa, hayapitani umaji.

Katika shairi hili kuna sehemu mbili au tuseme wazungumzaji wawili (pande mbili) lakini hawajibizani kama ilivyo katika ngonjera. Wazungumzaji hawa wanapeana nafasi, mmoja anazungumza hadi mwisho, na mwingine naye anaanza kujibu hoja za upande mwingine ili kutetea hoja hiyo. Tofauti na ngonjera, mwishoni hatuoni watu hawa kukubaliana na maelezo au majibu ya upande pili.

Katika ngonjera huwa kuna pande mbili zinazojibizana kuhusu jambo Fulani. Upande mmoja ndio ulio sahihi  kwa mujibu wa mtunzi na upande pili umepotoka. Lengo la mabishano huwa ni kuushawishi upande uliopotoka ukubaliane na upande wenye msimamo sahihi baada ya kuelimishwa. Hili ilinapotokea ngonjera huwa imefikia kilele chake, na ujumbe hudhihirika kwa hadhira bila matatizo. Kwa maneno hayo twaweza kusema kuwa ngonjera ni aina ya propaganda inayoigizwa jukwaani. Mfano wa ngonjera ni shairi lifuatalo:
Chama Chetu cha TANU
     MWANANCHI (Anamuuliza Mwanasiasa)
            Si chama cha Mabepari, cha watuta ndarahima?
Cha Makabaila thori, na Wanyonyaji wa Umma?
Ama bwanyenye viburi, na wapendao kutuma?
Siasa ya TANU sema, ni chama cha watu gani?
     MWANASIASA (Anamjibu Mwananchi)
Ndicho chama chenye heri, kisaidiaco Umma
Si chama cha matajiri, wachumao kwa dhuluma
Na ni chombo chenye ari, si chombo cha uhasama
Ni chama cha wakulima na wafanyakazi.
(Mnyampala, 1970)

Mifano zaidi ya ngonjera inapatikana katika Ngonjera za UKUTA kitabu cha kwanza na kitabu cha pili.

(b)   Ushairi wa Kidrama
Huu ni ushairi unaotumiwa katika baadhi ya tamthiliya. Mifano mizuri ya ushairi wa kidrama ni tafsiri za michezo ya Shakespeare. Ushairi huo ni sehemu tu ya mchezo wa kuigiza, ni mtindo mmojawapo wa kuandika mazungumzo ya wahusika katika tamthiliya, hivyo hauwezi kutenganishwa na fani hiyo ya tamthiliya. Kwa mfano:

METELLUS. Caius Ligarius hampendi kamwe Caezar
Ambaye alimkaripia kwa kumsifu Pompey:
Nashangaa hapana kati yeni al’yemtaja.

BRUTUS. Bas, Metellus mwema, nenda kamf’ate kwake:
Yeye anipenda sana na nimempa sababu;
Kamwambie aje hapa, mimi nitamshawishi.

CASSIUS. Asubuhi imetukuta: tutak’wacha, Brutus: -
Nanyi, rafiki, sambaeni; ila kumbukeni
Mliyoyasema, na kuweni Warumi wa kweli.

BRUTUS. Waungwana wema, changamkeni na furahini,
Nyuso zenu zisidhihirishe azma yetu;
Lakini tusitiri, kama vile wafanyavyo
Warumi wetu wachezaji, kwa mioyo baridi,
Na hali ya kawaida. Basi, nyote kwa herini.
W. Shakespeare, Julius Caezar (Mf. J.K. Nyerere, OUP 1963:34)

Katika dondoo hili ni ushairi wa mizani lakini hakuna vina. Pia kanuni ya kujitosheleza haijafuatwa au imekiukwa. Wazo la mshororo mmoja linaendelezwa katika mshororo unaofuata. Hili limefanyika ili kuufanya ushairi huu ukaribiane na lugha ya mazungumzo.

BAHARI ZA USHAIRI
Bahari za ushairi ni aina mahususi ya ushairi yenye yenye sifa Fulani kiumbo (nap engine hata kimaudhui na kimatumizi) zinazoipambanua na aina nyingine ya ushairi. Wataalamu wa jadi wa ushairi wameainisha bahari tofauti ambapo wengine wanasema zipo tatu tu yaani wimbo, shairi na utenzi. Wengine wanasema zipo tano, saba au hata zaidi.  ushairi kama utungo wa fasihi umeainishwa kwa kuzingatia idadi maalumu ya mishororo katika beti (Noor 1988, Kandoro 1983 na Abedi 1954). Zaidi ya kuzingatia idadi mahususi ya mishororo, mizani na urari wa vina katika ubeti, ushairi wa Kiswahili uliainishwa katika tanzu mbalimbali kutokana na:

♣Urari wa vina katika mistari au mishororo katika beti.
♣Mpangilio wa maneno katika mistari au mishoro katika beti.
♣Idadi ya vipande katika mistari au mishororo katika beti
♣Idadi maalumu ya mizani katika mistari au mishororo katika beti.

Katika muktadha wa vipengele hivyo vinne, muundo na maumbo ya ushairi huweza pia kuainishwa zaidi kama ifuatavyo:
♦Tathnitha - shairi ambalo lina mishororo miwili katika kila beti.
♦Tathlitha - shairi ambalo lina mishororo mitatu katika kila beti.
♦Tarbia - shairi ambalo lina mishororo minne katika kila beti.
♦Takhmisa - shairi ambalo lina mishororo minne katika kila beti.
♦Tashlita - shairi ambalo lina mishororo sita katika kila beti.
♦Ushairi ambao una zaidi ya mishororo sita.
Masivina - shairi ambalo lina mlingano wa mizani katika mishororo lakini si urari wa vina.
♦Ukawafi - shairi ambalo lina vipande vitatu katika kila mshororo.
♦Msuko - shairi ambalo lina kibwagizo kifupi.
♦Sakarani - shairi ambalo linashirikisha bahari mbalimbali.
♦Kikwamba - shairi ambalo linarudia neno moja katika kila mwanzo wa beti.

Kulingana na Wafula na Njogu (2007) na Mohamed (1990), ni katika kipindi cha urasimi-mpya katika fasihi ya Kiswahili ambapo palizuka istilahi maalumu za kuelezea dhana mbalimbali za ushairi wa Kiswahili. Istilahi hizo zilizotumika zaidi ni kama:
♠Mshororo - ambao ni mstari katika shairi
♠Mwanzo - mstari au mshororo wa kwanza katika ubeti
♠Mloto - mstari au mshororo wa pili katika ueti
♠Mleo - Mstari au mshororo wa tatu katika ubeti
♠Kipokeo - Mstari au mshororo wa mwisho katika ubeti
♠Ukwapi - Sehemu ya kwanza katika mshororo
♠Utao - Sehemu ya pili kaitka mshororo
♠Mwandamizi - Sehemu ya tatu katika mshororo
♠Tabdila - Kifupisho cha sauti kaitka neno linalotumika katika mshororo bila ya kubadilisha maana ya msingi.
♠Inkisari - Kunga ya kufupisha maneno katika mshororo
♠Mazida - Kunga ya kurefusha neno bila ya kupotosha maana ya asili.

       Kimsingi, istilahi hizi zilitumika kimakusudi kwa malengo ya kuutambulisha ushairi wa Kiswahili. Katika          muktadha wa nadharia ya Fomula ya kisimulizi ni kwamba, uwepo wa bahari na istilahi maalumu                   zinazotumika katika ushairi ni njia mojawapo ya kubainisha tanzu za ushairi na fasihi kwa ujumla.                   Uainishaji huo unazingatia zaidi ushairi wa Kiswahili unaotungwa katika muktadha wa arudhi za                      kimapokeo (King‟ei na Kemoli 2001). Hata hivyo, inabainika kuwa ushairi wa Kiswahili usiozingatia            arudhi hizo katika utunzi na uwasilishaji haushirikishwi katika uainishaji.

          Wataalamu wengine wakiongozwa na Ahmed Sheikh Nabhany wameainisha bahari kumi na tatu kama           ifuatavyo:
      1.       Shairi: Ni utungo wenye mishororo minne kila beti na vipande  viwili vya mizani 8+8 kila kipande.                      Maudhui yake yanatokana na jambo lolote lile analoliona mtunzi.
              Mfano wa shairi ni
              Mtovu ndumila kuwili, kwa haya hana mwafaka,
              Kwake haki na batili, kwa pamoja hujivika,
              Huku akakujamili, na kule akaitika,
              Ndumila kuwili si mwema, hujidhuru nafsiye.

         2.      Wimbo: Ni utungo wenye mishororo mitatu kila ubeti na kila mshororo una vipande viwili.                              Nyimbo nyingi huongelea mapenzi. Ipo mikondo mingi sana ya nyimbo ambayo imebainishwa na                   wataalamu mbalimbali. Mwalimu Ridhiwani amebainisha mikondo kumi.

        3.       Tenzi: Ni shairi la masimulizi, mawaidha au maelezo marefu. Tenzi nyingi zina mizani nane kila                          mstari. Vina vyake hubadilika kila mstari, ila kina cha mwisho kiitwacho bahari, hakibadiliki.                         Tenzi hazifanani kikanuni maana kila mtunzi huwa na maamuzi na namna yake ya kuandika utenzi                  wake. Kwa mfano



          Leo nataka binti
          Ukae juu ya kiti
          Ili uandike hati
         Ndogo ya wasia.

          Mimi kwako ni baba
          Hati hii ya huba
          Andika iwe akiba
           Asaa itakufaa
           (Shaaban Robert, 2003)

           Mfano mwingine wa utenzi ni


            Niliuliza mwanzoni,
            Sera hii ni ya nani?
            Serikali kuwa tatu,
Hapa Tanzania kwetu?

Ni ya serikali yetu,
Au ya Wabunge wetu,
Au ni ya SISIEMU?
Tungependa tufahamu.
          

(Julius K. Nyerere, 1993:1)


      4.      Inkshafi/Duramandhuma: Imepata jina lake kutokana na Utenzi wa Al-Inkshafi. Tenzi hizi zina                 maadili ya kidini japokuwa maudhui yake yanaweza kutumika katika maadili ya kidunia. Kila ubeti                 una      mishororo minne na kila mshororo una mizani 11 ya 6+5.  Kwa mfano:
           Makusudi yangu ya kudhamiri
           Nda kutunga koja kilidawiri
           Mivazi ya duri ikinawiri
           Mikinda ya lulu nyuma nitiye.
           Inkishafi, ubeti wa saba (Mulokozi, 1996:127)
      5.      Ukawafi: Hili ni shairi lenye mishororo mitatu au zaidi katika kila ubeti na vipande vitatu katika kila               mshororo. Mizani inaweza ikatofautiana au ikawa sawa.
       Mfano:  
              Sifa uta wangu       wa kitanzu      cha mti roo
              Upakwe mafuta      unawiri            kama kioo
             Zipo pia kawafi za mkondo wa 6+5+6. Maudhui ya kawafi nyingi huhusu dini, japo zipo chache                    zenye kuzungumzia masuala ya kidunia.

       6.      Wajiwaji/Takhimisa: Bahari hii huwa na mishororo mitano kila ubeti na mizanai 15 kila mshororo                 na vipande vitatu katika kila mshororo vina muundo wa mizani 6+ 4+ 5. Inaelezwa kwamba hapo               zamani wajiwaji ilitungwa na watu wawili tofauti. Maudhui yake yalihusu mambo mazito; huweza                   kuwa ya kidini au ya kimaisha tu. Mfano wa wajiwaji ni ule uliotungwa na Sayyid Abdalla bin Ali bin            Nasir uliohusu shujaa Liyongo:

              Anami shujaa samba ndole mwondoa ari
             Mvunda kilaa na husuni kizidabiri
             Nayipija kifa kayitia katika shari
             Sichi mata yao na mafumo yanganawiri
             Mandi mafuamati na magao mauya nyuma …

        7.      Hamziya: Bahari hii ilipata jina lake kutokana na Utenzi wa  Hamziya ambao ni utenzi wa kiarabu.
              Kilubeti una mishororo miwili yenye kina kimoja a Mishororo ya Hamziya ina vipande 3 vya mizani              5+ 4+ 6
        8.      Tiyani-Fatiha:   Bahari hii ni ya ushairi wa kidini wa kuomba toba. Huwa una mishororo 9 kila
              ubeti ambayo huweza kutofautiana kwa urefu/mizani kama inavyoonekana hapa chini.
            i.                    Mishororo ya 1-2: mizani 6+6
            ii.                  Mishororo ya 3-4: mizani 3+8
            iii.                Mishororo ya 5-7: mizani 4+4
            iv.                Mishororo ya 8-9: mizani 6+6
    Mfano:
Tiyani Fatiha           tuombe Rabana
Huinadi twaha          na Mursalina
Kwa nyute                jamiina
Ya Ilaha                    Sayidina
Mshabaha                 Wewe huna
Kwa swahiha             huniona
Moyo raha                 wangu sina
Taka mswamaha        tubu alayna
Rabi inaLlaha             maa  swabirina
            Bi. Rukiya binti Fadhil (1892 – 1968) katika Sharif, 1988:57 (katika Mulokozi, 1996:129).

      9.       Utumbuizo: Bahari hii haina idadi kamili ya mishororo na mizani, urefu wa mstari au mshororo                    hutegemea pumzi aliyonayo mwimbaji na lengo lake. Utumbuizo huwa na vina vya mwisho, mara                    chache huwa na vina vya kati, lakini bila mpangilio maalum. Wimbo ufuatao ni mfano mzuri wa                      utumbuizo ambao ni wimbo wa malalamiko ya mwanamke baada ya kupata habari kuwa mumewe                kaoa mke mwingine.

        Bwana Wende Yungwa
        Bwana wende Yungwa, koleya mashungwa, mimi humngoja kuwa mbiya kongo.
        Hungoja toka nisimeme hata k’anguka k’enda kwa magongo.
        K’amngoja nili na furaha, hata moyo k’afanya kisongo.
        K’angoja, kingiya kumwambiya k’ongo.
        K’ampokeya mvungu na ucha k’auweka kula penye change.
        K’apokeya kitoka na yembe k’azitiya t’ini ya mlango.
        K’amvuwa shungurere lake k’aliweka mbee za mlango
        Umedondolewa na Sharif, 1988:53 (katika Mulokozi, 1996:130).

       1    0.  Wawe: Ni ushairi au wimbo wa kilimo, huimbwa wakati wa kufyeka misitu, kuchoma magugu,              kulima au kupanda hadi kuvuna. Wawe haina idadi maalum ya mizani au vipande, ila nyingi zina vina              vya mwisho.

      1    1.   Kimai: Inahusu shughuli za majini, ni bahari ya wavuvi na mabaharia. Idadi ya mishororo na vina          si lazima.

       1    2.  Zivindo: Ni ushairi unaofafanua maana za maneno, na kazi yake ni kujifunza lugha na kuhifadhi            lugha.
       Mfano:
      Kata ni kata ya nyoka, au kata ya nyeleni
      Kata ya tweka, ibandikwayo kitwani
      Na kata ni ya kuteka, maji mema balasini
      Kata kitu kwa makini, tena kuna kata gani?
      (Ahmad Nassir “Nawau za Kimvita” (1971:55)

     1    3.  Sama: Neno ‘sama’ ni mahadhi au sauti, hivyo bahari hii hukusanya washairi wote wenye kufuata        mahadhi ya kigeni.

Maoni 12 :

  1. jaribuni kujitangaza zaidi kazi yenu sio ndogo katika mchango wa kiswahili

    JibuFuta
  2. Kama mshairi mchanga, nayatazama maelezo haya kwa upeo wa thamani ya juu kwani elimu iliyojificha ndanimwe ni urithi wa kudumu.

    JibuFuta
  3. Nashukuru sana nimeendelea kupata maarifa zaidi kuhusu uainishaji wa ushairi hasa ule wa kiswahili!

    JibuFuta
  4. Iko pOa sana endeleeni nakazi nzuri yakuelimisha jamii

    JibuFuta
  5. Iko pOa sana endeleeni nakazi nzuri yakuelimisha jamii

    JibuFuta
  6. Kuna aina ya mashairi hayatolewa mifano kama kimai

    JibuFuta