Ijumaa, 26 Agosti 2016

KISA CHA BAO.

KISUMBUA KICHWA Na SALUMU CHIVALAVALA.
KISA CHA BAO.
Niwakumbushe kuhusu ya kale, kipindi ambacho paka alipokufa tulimzika njia panda huku tukiacha fagio pembezoni mwa kaburi lake ili kila apitaye asiache kufagia, kaburi la paka lilidumu kuwa safi siku zote. Na ni katika kipindi hicho hicho ambapo tulicheza bao kwa mtindo wa kula, kusafiri na hata kutakata.
Mpumbavu katika umri wa miaka arobaini ni mpumbavu wa milele, mimi sitaki hata kukaribia huko kabla ya kuondoa kila chembe ya upumbavu akilini mwangu. Nasema hivyo kwa sababu kupindua misingi ya kale ya kimaadili si kitu chema hata kidogo.
Wapo vijana wa rika yangu nilikuwa nao katika mti wa kivuli udondoshao majani ya aina mbili yaani ya kuwasha na ya kulainisha, tukiwa pale tulisimuliana kuhusu bao, nilieleza uzuri wa bao na hasa mchezo ukikuendea vema ukamla mwenzako mara kwa mara. Bao ni mchezo wa mababu na tumeukuta hivyo sie vijana. Ukicheza kwa ustadi na akili utakula sana kila tundu lenye kete nyingi na mwishowe utajizalishia kete nyingi katika majumba yako.
Wenzangu walinidhihaki kwa kusema bao la vijana huliwa mbele na nyuma hivyo niachane na mitindo ya kale, nikauliza “mbele na nyuma walaje!” nikaambiwa “ Muda huo huo wa kuchezwa ukifika hatua ya kula basi unakomba tundu la mbele na la nyuma huachi kitu aisee” nilistaajabu ya Musa ndio maana niliyaona ya firauni.
Kwa uchezaji huo kwakweli ni uharibifu tupu, kwa sababu mchezo wa bao kwa wachezaji hutumia vitobo vya nyuma kuhifadhi mitaji ya kete zao na kwa lugha rahisi tunaweza sema kule nyuma ndiko kunakowekezwa nguvu za mchezo, sasa ikitokea mtu anakula hadi huko basi ni wazi kuna uharibifu mkubwa wafanyika na haiwezi kutokea kukazaliwa kete nyingine kwa aliyeanza kuliwa bali mlaji ndio anaweza kuwa na uwezo wa kuzalisha kete kadiri atakavyo japo vidole vitachoka kwa ugumu wa kuvipeleka hadi nyuma kutafuta ulaji.

Kwa kuwa mjumbe hauawi, basi nami nasema jamani bao tucheze kama zamani, tule matundu ya mbele tupu tena tusiache kutakata kabla ya kula. Tukifanya hivyo tutajikuta tukifurahi siku zote na wala vidole hutakuta vikichoka mapema na wala hatutaharibu matundu ya nyuma yakabaki tupu kama fuko la mashine ya kusaga dona. Tuache mitindo ya nje iso na tija!

Alhamisi, 28 Julai 2016

DONDOO KUHUSU UHUSIANO BAINA YA LUGHA NA JAMII

DONDOO KUHUSU UHUSIANO BAINA YA LUGHA NA JAMII@
Okoa Simile



       a   .      Lugha ni nini?
Lugha - ni mfumo wa sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano yao ya kilasiku ili kueleza hisia, mawazo, matakwa na mahitaji yao.


      b       .      Jamii ni nini?
Jamii - ni kundi la watu wanaoishi katika eneo Fulani, wanao jitambulisha kama kundi moja, wenye utamaduni mmojana na  lugha moja.

      c     .       Isimu jamii ni nini?
Isimu Jamii - ni tawi la isimu (elimu ya lugha) linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano baina yake. Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti; aina mbali mbali za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia.
King’ei (2010), anaeleza kuwa, kwanza lugha ni zao la jamii, na ni kipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii husika. Pili, lugha hutumiwa na jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake na hasa kama chombo maalumu cha kuwezesha wanajamii kuwasiliana. Hivyo isimu jamii hueleza na kufafanua mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo ndiyo mama wa lugha
.
       d      .      Uhusiano huu baina ya lugha na jamii.
               i.            Lugha ni zao la jamii, ni sehemu ya jamii kwani ni sehemu ya utamaduni wa jamii husika. Lugha ni njia inayotumiwa na wanajamii ili kueleza na kusambaza utamaduni wake.
         ii.            Mwanaisimu Sapir na Whorf, wanaeleza kuwa lugha huathiri sana na kudhibiti jinsi wazungumzaji na watumiaji wa lugha wa jamii fulani wanavyoufasili ulimwengu wao. Kulingana na wanaisimu hawa muundo wa maana katika lugha ndiyo msingi wa mawazo au utaratibu wa fikra. Mwanadamu hawezi kufikiri kamwe bila kutumia lugha. Jambo hili linamaanisha kuwa kwa vile mawazo na fikra za mwanadamu vinaukiliwa na lugha  basi inawezekana kudhibiti fikra za wanajamii kwa kuidhibiti lugha yao. Katika muktadha ya Kitanzania nan chi nyingi za Kiafrika , hili limthibitika kwani, miongoni mwa Watanzania walio wengi wanahusisha maarifa na lugha fulani (mathalani kiingereza). Hii inatokana na imani iliyopandikizwa na wakoloni kwamba lugha ya Kiingereza ni lugha ya utaarabu na lugha ya kitaaluma. Hivyo uwezo wao wa kudhibiti matumizi ya lugha kwa kututoa katika matumizi ya lugha mama yamefanikisha kuelekeza fikra za wanajamii hawa kwenye mawazo kwamba taaluma na usomi ni kujua Kiingereza.
              iii.            Kwa mujibu wa King’ei (2010) lugha hulejelea mazingira ya jamii husika, na ndiyo maana watu wenye lugha sawa na wanaishi katika mazingira tofauti wanaweza kuwa na mtazamo tofauti ya kimaisha na ufasili wao wa ulimwengu 
        iv.            Kwa kutumia nadharia ya ‘ukiliaji wa kiisimu’ (Linguistic Determinism) lugha ndiyo inayoongoza mawazo ya watu na huathiri hata maana ambazo watu wanazitoa kuelezea dhana na mitazamo fulani katika lugha zao.
           v.            Kwa njia ya lugha watu wa jamii Fulani wanapata nafasi ya kujadili masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya jamii.
          vi.            Kama hiyo haitoshi, Austin (1962) anasema kuwa, ni muhimu kuhusisha matumizi ya lugha  na muktadha wake wa kijamii kwani lugha huwa na matumizi tofauti kama kutoa mapendekezo, kuahidi, kukaribisha, kuomba, kuonya, kufahamisha, kuagiza, kukashifukusifu, na kuapiza.
          vii.            Lugha ndicho chombo kinachotumika kuwaleta pamoja na kuwaunganisha wanajamii hukuikisaidia kuimarisha uhusiano miongoni mwa wanajamii. Katika muktadha wa Kiafrika, kwa mfano, heshima ya mtu inatambulishwa na jamii ya watu ndiyo maana waswahili wana msemo unaosema “mtu ni watu”. Kauli hii kwa ujumla inatuonesha kuwa katika harakati za maisha za wanajamii heshima na kukubalika kwa mtu pamoja na kueleweka kwake kunatokana na namna mtu anavyohusiana na wanajamii wengine pamoja na mambo mengine ikiwa ni kutumia lugha kwa ufasaha. Haya yote yanawasilishwa kutoka katika jamii moja kwenda katika jamii nyingine kwa kutumia lugha ambacho ndicho chombo muhimu cha mawasiliano.
        viii.            Jamii hutambulika kwa kutumia lugha. Lugha huwa na uwezo wa kuonesha sifa fulani kuhusu mzungumzaji, anayerejelewa na uhusiano uliopo kati ya wanajamii. Utamaduni hutambulishwa katika maeneo mbali mbali ya ulimwengu kwa kutumia lugha pia. Kwa mfano, katika fasihi ya kabila la Wahaya, tunatambua mambo mbali mbali yanayohusu kabila hili hasa katika kipengele cha majigambo kutokana na namna wanajamii hawa wanavyotumia lugha yao kujipambanua kwa jamii nyingine.
                ix.            Lugha pia hutumika katika kurithisha mila na desturi za jamii ikiwa na pamoja na kutolea elimu. Binadamu huweza kufunzwa na kupewa maadili mbali mbali kwa kutumia lugha ili waweze kujitambua kuwa wao ni akina nani na wapo ulimwenguni kwa malengo gani. Kwa mfano, watoto huwezwa kufunzwa masuala yanayohusu uana wao ambao hutokana na jinsia yao.  Kwa kutumia lugha. Pamoja na kuwa wanajamii wanaona matendi yanayotendwa na jamii nyingine au ndani ya jamii hiyo lakini wanahitaji namna ya kuambiwa juu ya uzuri au ubaya wamatendo hayo, kufuata au kuto yafuata. Hapa lugha inachukua nafasi yake.
   Marejeo
   King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimu Jamii. Taasisi ya Taaluma za Kiswahili: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tanzania.

     Austin, J.L. (1962). How to do things with Words. Oxford. Oxford University Press.

Jumamosi, 19 Machi 2016

FAIDA NA HASARA ZA TAFSIRI KATIKA UTAMADUNI



IKISIRI
Tunapojadili umuhimu wa taaluma ya tafsiri pamoja na changamoto zake katika jamii, mara nyingi tunajikita katika masuala ya kielimu na mawasiliano na kuusahau upande wa utamaduni ambao unajumuisha vipengele vingi vya maisha katika jamii. Makala hii ina lengo la kuelezea faida na hasara zilizopatikana na zinazoendelea kupatikana katika utamaduni tangu kuasisiwa kwa taaluma hii ya tafsiri nchini Tanzania na Afrika kwa jumla. Hivyo basi, ili kufikia lengo linalokusudiwa, Makala hii itakuwa na sehemu saba. Sehemu ya kwanza itaelezea kuhusu Dhana ya Tafsiri. Sehemu ya pili itaelezea Historia na Maendeleo ya Tafsiri nchini Tanzania. Sehemu ya tatu itahusu Dhana ya Utamaduni. Sehemu ya nne itahusu Faida za Tafsiri katika Utamaduni. Sehemu ya tano itaelezea Hasara za Tafsiri katika Utamaduni. Sehemu ya sita ni Hitimisho na Mapendekezo. Na sehemu ya saba ni Marejeleo. 

UTANGULIZI
Dhana ya Tafsiri
Dhana ya tafsiri imefafanuliwa na wataalamu mbali mbali, miongoni mwao ni kama hawa wafuatao:-
Mwansoko na wenzake (2006), wanafasili tafsiri kwa kusema kuwa:
“Ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi    nyengine”
As-safi akimnukuu Dubois (1974), anaeleza kuwa:
“Tafsiri ni uelezaji katika lugha nyengine au lugha lengwa wa kile kilichoelezwa katika lugha nyengine (lugha chanzi) ikihifadhi maana na mtindo wa matini chanzi”
Catford (1965:20) anasema tafsiri ni,
“Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana katika lugha nyingine (lugha lengwa)”. 
Kutokana na fasili zote hizo kuhusu tafsiri tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa, tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, ujumbe au taarifa iliyopo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa bila kupoteza maana ya msingi na mtindo uliotumika katika matini chanzi. Na maana katika tafsiri inatakiwa iendane na lengo la mtunzi wa matini chanzi lakini pia kwa kuzingatia utamaduni wa jamii unayoitafsiriya.

Historia na Maendeleo ya Tafsiri nchini Tanzania.
Wanjala (2011) anaeleza kuwa, historia ya tafsiri imeangaliwa kwa kuegemea vipindi muhimu vya maendeleo na mabadiliko ya elimu na utamaduni. Nchini Tanzania, tafsiri haina historia ndefu sana kwani imeanzia mnamo karne ya 19 na inaweza kugaiwa katika vipindi vitatu vikuu navyo ni kabla ya utawala wa kikoloni, wakati wa utawala wa kikoloni na baada ya uhuru.
Mbali na Wanjala (2011), pia historia hii imeelezwa na wataalamu kama vile Mwansoko na wenzake (2006), Mshindo (2010) na Sofer (2006) kama ifuatavyo:-
Tukianza na kabla ya utawala wa kikoloni, Wamishionari walitafsiri vitabu mbali mbali vya kikristo ikiwemo Biblia Takatifu kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili na lugha nyengine za makabila kwa lengo la kueneza dini na ustaarabu wa kikristo kwa waafrika.
Kwa upande wa kipindi cha wakati wa kikoloni, hiki ni kipindi kuanzia miaka ya 1800, katika kipindi hiki, wakoloni hasa waingereza walitafsiri maandiko mbali mbali ya kitaaluma na fasihi ya Ulaya kwa lugha ya Kiswahili. Vile vile kabla ya uhuru zipo baadhi ya kazi za fasihi zilizotafsiriwa na watanzania. Kwa mfano tamthiliya ya “MZIMU WA WATU WA KALE” iliyotafsiriwa na Mohammed Said Abdalla (1960) kutoka lugha ya kiingereza (Shrine of The Ancestors).
Baada ya uhuru ambapo ni kuanzia mwaka 1961. Katika kipindi hiki wapo wataalamu waliofanya juhudi za kutafsiri vitabu mbali mbali kwa lugha ya Kiswahili. Mfano mzuri ni Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alitafsiri vitabu viwili vya mwandishi mashuhuri wa tamthiliya wa huko Uingereza aitwaye William Shakespeare ambavyo ni tamthiliya ya Juliasi Kaizari (Julius Caesar) (1963) na tamthiliya ya Mabepari wa Venis (The Merchant of Venis) (1969).
Kazi nyengine zilizotafsiriwa baada ya uhuru ni wimbo wa Lawino (Song of Lawino) iliyotafsiriwa na Paul Sozigwa (1975), riwaya ya Uhuru wa Watumwa (The Freeing of the Slaves in East Africa) iliyotafsiriwa na East African Literature Bureau (1967), Nitaolewa Nikipenda (I Will Marry When I Want) iliyotafsiriwa na Crement M. Kabugi (1982).
Kwa ujumla maendeleo ya taaluma ya tafsiri nchini Tanzania yamepiga hatua kubwa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia. Taaluma ya tafsiri inafundishwa katika elimu ya sekondari na katika vyuo vikuu mbali mbali. Pia taasisi na asasi zinazojishughulisha na tafsiri zimeongezeka kwa mfano Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI), Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na kadhalika. Pia wapo wafasiri binafsi wanaotafsiri maadishi kwa lugha mbali mbali kama vile Kiingereza, Kiswahili, Kiarabu, Kifaransa nakadhalika.
Dhana ya Utamaduni
Kwa upande wa dhana ya utamaduni, wataalamu mbali mbali wameelezea dhana hii kama ifuatavyo:-
Ponera (2014), yeye anaeleza kuwa:
“Utamaduni ni jumla ya matendo, fikra, mifumo ya maisha na kiashiria kingine chochote ambacho kinaweza kutumika kumwongoza na kumtambulisha mtu wa jamii moja kwa jamii nyenginezo”
Pia katika Wikipedia imeelezwa kuwa:
“Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake”
Pia imeelezwa kuwa, neno “Utamaduni” linatumika kimsingi katika njia tatu zifuatazo:-
·         Maonjo ya hali ya juu katika sanaa, vile vile hujulikana kama utamaduni wa juu.
·         Mkusanyiko wa maarifa ya binadamu, itikadi na tabia ambao hutegemea sana uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kwa njia ya ishara.
·         Jumla ya mitazamo, kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi, shirika au kikundi Fulani.
Ama kuhusu maana ya utamaduni wa mtanzania, mtandao wa Jamii Forum unaeleza kuwa, mtanzania ni mtu mwenye utu. Utu ni sifa na ndio utamaduni wa mtanzania kwa sababu unaingia katika vipengele mbali mbali kama vile kwenye uongozi, familia, kilimo, elimu, mavazi, muziki, vyakula, biashara, siasa, uchumi, mahusiano na nchi za nje, mikataba muhimu ya taifa, kazi, dini, nakadhalika.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa hakuna maana ya moja kwa moja kuhusu utamaduni kwa sababu utamaduni unajumuisha mambo mengi katika maisha ya binadamu kama yalivyotajwa katika fasili zilizopo hapo juu. Lakini jambo la kuzingatia ni kuwa, kazi yoyote itakayoandikwa au kufasiriwa kutoka lugha moja kwenda nyengine haina budi kuchunga   misingi ya utamaduni ya jamii husika.

Faida za Tafsiri katika Utamaduni.
Baada ya ufafanuzi huo mfupi kuhusu dhana ya utamaduni, tafsiri pamoja na historia na maendeleo yake nchini Tanzania, sasa moja kwa moja nakwenda kwenye lengo la makala yangu la kujadili faida na hasara za tafsiri katika utamaduni ambapo zaidi tutajikita katika utamaduni wa Tanzania. Kupitia historia ya tafsiri niliyoieleza hapo juu na kwa kuzingatia hali halisi ya maendeleo ya matumizi ya tafsiri yanavyopiga hatua kila siku katika nchi yetu ya Tanzania, faida za tafsiri katika utamaduni wa Tanzania ni kama zifuatazo:-

  • 1.      Tafsiri imesaidia katika kueneza dini na vipengele vyengine vya utamaduni kutoka mataifa ya nje.  
Tafsiri ni nyenzo ya kuenezea utamaduni kutoka taifa moja kwenda jengine au kutoka jamii moja kwenda jengine. Kwa mfano kutokana na wazungu kutafsiri Biblia na waarabu kutafsiri Kur-An kwa lugha ya Kiswahili, kulisababisha waafrika kwa ujumla kubadilisha dini zao za kijadi na kufuata dini ya Ukristo na Uislamu. Vile vile kwa upande wa burudani, vyakula na mavazi kutoka mataifa ya magharibi vilienea katika jamii za watanzania na waafrika kwa ujumla kutokana na kutafsiriwa kazi mbali mbali kama vile nyimbo, mashairi, hadithi nakadhalika ambazo ndani yake mulisheheni vipengele hivyo vya utamaduni.

  • 2.      Tafsiri imesaidia katika kukuza lugha na fasihi ya Kiswahili.
Lugha ya kiswahili ni miongoni mwa vipengele muhimu sana katika utamaduni wa Tanzania kwa sababu kiswahili ni lugha rasmi, lugha ya taifa na tunu ya taifa. Kabla ya kuwepo taaluma ya tafsiri, lugha ya Kiswahili ilionekana kudumaa hasa katika nyanja ya sayansi na teknolojia. Lakini baada ya kuwepo taaluma hii, wataalamu na taasisi mbali mbali za Kiswahili zimekuwa zikifanya jitihada za kutafsiri vitabu vya lugha mbali mbali kwenda lugha ya kiswahili pamoja na kutafuta istilahi na misamiati ya Kiswahili inayoweza kwenda sambamba na istilahi za kisayansi. Mfano wa istilahi hizo ni kama vile Password – Nywila, Keyboard – Kicharazio, Scanner – Mdaki, Flash Disc – Diski Mweko, Mouse – Kiteuzi, nakadhalika.
Kwa upande wa fasihi, hii ni sanaa. Na sanaa ni katika utamaduni wa juu kabisa. Historia inaeleza kuwa, wakati wa ukoloni fasihi ilidumaa kwa sababu waafrika hawakuwa na mwamko wa kusoma vitabu na kazi nyingi za kifasihi ziliandikwa kwa lugha ya kiingereza kwa lengo la kuwafurahisha mabwana. Lakini baada ya wataalamu wa fasihi kuanza kutafsiri kazi mbali mbali za fasihi ya ulaya kwa lugha ya Kiswahili na lugha nyengine za makabila mwamko wa kusoma vitabu uliongezeka. Mfano wa vitabu vya fasihi vilivyotafsiriwa wakati wa ukoloni ni Mzimu wa Watu wa Kale (Shrine of the Ancestors) iliyotafsiriwa na Mohammed Said Abdalla (1960).
Pia kuna kazi mbali mbali za kifasihi zilizotafsiriwa baada ya uhuru. Miongoni mwao ni Juliasi Kaizari (Julius Caesar) (1963) na Mabepari wa Venis (The Merchant of Venis) (1967), zote hizo zimetafsiriwa na Mwalimu Julius K. Nyerere.
Baada ya hapo, kazi mbali mbali za kifasihi kama vile hadithi fupi, riwaya, tamthilia na mashairi yalitafsiriwa kutoka lugha mbali mbali kwenda Kiswahili. Vile vile kazi za fasihi ya Tanzania zilitungwa na kupelekea kukua na kuenea fasihi ya Kiswahili.



  • 3.      Tafsiri imesaidia katika kukuza elimu nchini Tanzania.
Elimu ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa Tanzania, imepiga hatua kutokana na maendeleo ya mitaala na mbinu mbali mbali za kufundishia. Tafsiri ni miongoni mwa mbinu  inayotumiwa na walimu wengi ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafikia lengo la kujifunza kwa mujibu wa viwango vyao. Juhudi mbali mbali zinachukuliwa katika kukuza elimu ya Tanzania. Miongoni mwa juhudi hizo ni kutafsiriwa kwa vitabu vya masomo mbali mbali ili visaidie katika marejeleo. Vile vile taaluma ya tafsiri imekuwa ni kozi muhimu katika shule za sekondari na vyuoni ili kuwapa wanafunzi uwezo wa kuitumia taaluma hii ili waweze kujiajiri kwa kutafsiri kazi mbali mbali.

  • 4.      Tafsiri imesaidia katika kuibua nadharia mpya ya fasihi linganishi.
Kama nilivyotangulia kusema kuwa fasihi ni sanaa na sanaa ni sehemu ya utamaduni. Kwa mujibu wa kitabu cha “UTANGULIZI WA NADHARIA YA FASIHI LINGANISHI” kilichoandikwa na Athumani S. Ponera (2014) ni kwamba, lengo la nadharia hii ni kuchunguza kufanana na kutofautiana kati ya fasihi ya Tanzania na fasihi ya mataifa   mengine hasa Amerika na Ulaya hususan katika vipengele mbali mbali vya utamaduni pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kupitia kitabu hicho, hoja yangu naiegemeza pale mwandishi alipoelezea ulinganisho uliopo kati ya fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili na hapa namnukuu.
“Dhana hii ya fasihi ya Kiswahili ni muhimu sana kuidodosa ili ituwezeshe kufika katika hatua ya kufanya ulinganisho na fasihi za jamii nyenginezo. Kuna mkanganyiko mkubwa miongoni mwa wanazuoni kuhusu dhana za fasihi ya Kiswahili, fasihi katika Kiswahili, fasihi kwa Kiswahili na fasihi ya waswahili”.
Kwa hiyo kutokana na maelezo hayo, ni wazi kuwa kuwepo kwa kazi nyingi za mataifa ya nje zilizofasiriwa kwa lugha ya Kiswahili na zile ambazo hazijafasiriwa, ni sababu tosha iliyomsukuma mwandishi kuanzisha mjadala huu wa nadharia mpya ya fasihi linganishi kama ilivyo kwa nadharia ya isimu linganishi.

  • 5.Tafsiri imesaidia katika kukuza biashara na kuinua uchumi wa taifa.
Kama tulivyotangulia kusema kuwa, utamaduni ni utu na utu ni muhimu katika maisha ya watu. Biashara ni miongoni mwa sekta inayounganisha watu wa aina tofauti.  Kuwepo kwa utu katika biashara ndio kutasaidia kukuza biashara na uchumi wa nchi yetu. Mchango wa tafsiri katika biashara ni kuwa mikataba mingi ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania  inatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao. Vile vile matangazo mbali mbali ya kibiashara na taarifa nyengine katika vyombo vya habari kama vile magazeti hutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kila mwananchi apate kufaidika na huduma zinazotolewa.
Hasara za Tafsiri katika Utamaduni.
Baada ya kuelezea faida mbali mbali za tafsiri katika utamaduni wa Tanzania na afrika kwa jumla. Sasa nitatumia fursa hii kuelezea hasara chache za tafsiri zilizoathiri utamaduni wetu kama ifuatavyo:-  

  •       Tafsiri imesababisha jamii za waafrika kuiga utamaduni wa mataifa ya nje.
Kwa mujibu wa Kamati ya Taarifa za Tovuti Kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizofanyiwa marekebisho mwaka (2015) zinaeleza kuwa:
“Utamaduni wa Tanzania Ni matokeo ya athari za kiafrika, kiarabu, kizungu na kihindi. Maadili, mila na desturi za kiafrika zinabadilishwa polepole Na maisha ya kisasa, ingawa kwa kasi ndogo sana miongoni mwa jamii ya wamasai”.
Kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwa, jamii nyingi za waafrika zikiwemo za watanzania, zimeanza kuathirika kwa kuiga mila na tamaduni za kimagharibi kupitia tafsiri za kazi mbali mbali za kijamii na mpaka sasa hali hiyo inaendelea kupitia njia nyengine mbali mbali kama vile utalii na maingiliano baina ya waafrika, wazungu, waarabu na wahindi.

  •       Tafsiri imesababisha mivutano na makundi ya kidini kati ya jamii za waafrika.
Ukirudia historia ya tafsiri katika nchi za ulaya, utaona, mnamo karne ya 16 kulikuwa na    muamko mkubwa wa kidini ambapo ulianza Ujerumani na kusambaa katika maeneo mbali mbali ulimwenguni. Mwamko huu ulipinga muundo, mwelekeo, falsafa na mafunzo mengi ya kanisa katoliki ya wakati huo na matumizi ya lugha moja ya kilatini katika misa na mafunzo ya kidini. Hali hii ilisababisha mgawanyiko katika dini ya kikiristo. Watu mbali mbali walitafsiri maandiko matakatifu katika lugha mbali mbali. Kwa mfano Martin Luther King alitafsiri Biblia takatifu kutoka kilatini kwenda lugha ya kiingereza (1611) ikaitwa “The King James Bible”, pia alitafsiri Biblia kutoka Kilatini kwenda lugh ya Kijarumani. Baada ya kuona tafsiri ya Kilatini imeacha baadhi ya vipengele katika maandiko hayo matakatifu, Jarome alitafsiri Biblia ya Kigiriki na Kiebrania kutoka lugha ya Kilatini.
Kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwa, mgawanyiko wa kidini haukuishia katika nchi za ulaya na katika dini ya kikristo peke yake bali ulienea ulimwengu mzima zikiwemo nchi za afrika kwa sababu ya kutafsiriwa maandiko matukufu mbali mbali kama vile biblia, kur-an na vitabu vyengine vya mafunzo ya dini . Sasa hivi ukichunguza katika dini zote hasa za uislamu na ukristo utakuta mivutano kati ya waumini juu ya makundi yao. Kwa mfano katika ukristo utakuta makundi kama vile wakatoliki, wasabato nakadhalika. Ama kwa upande wa dini ya kiislamu kuna makundi kama vile suni, ibadhi, shia nakadhalika. Yote hayo yametokana nakufasiriwa kwa maandiko ya dini na ufahamu wa waumini katika maandiko hayo.

  •       Baadhi ya njia za tafsiri husababisha kwenda kinyume na sarufi ya lugha lengwa au utamaduni wa lugha lengwa.
Hoja hii naiegemeza zaidi katika aina za tafsiri ambazo ni tafsiri ya neno kwa neno, tafsiri sisisi, tafsiri ya kisemantiki na tafsiri ya mawasiliano. Lakini hapa nitajikita zaidi katika tafsiri ya neno kwa neno. Mara nyingi tunapotafsiri sentensi au matini kwa kutumia njia hii, lazima tufuate sarufi ya lugha chanzi hivyo husababisha makosa ya kimuundo na kimaana ya lugha lengwa. Mifano ifuatayo inafafanua zaidi.
·         Kiingereza kwenda Kiswahili:
I / like / banana / s / more / than / orange / s /
Mimi / penda/kama / ndizi / wingi / zaidi / kuliko / chungwa / wingi /

·         Kiswahili kwenda kiingereza
Wa / toto / wa / dogo / wa / na / imba / kwa / furaha /
Plural / child / plural / small / they / present continues tense (singular) / by/for / happiness
Unapochunguza mifano ya hapo juu, utakuta kuwa ufuataji wa sarufi ya lugha chanzi hupelekea kuharibu sarufi ya lugha lengwa na kupoteza maana inayokusudiwa kutoka lugha chanzi.
Vile vile tunapotafsiri methali, misemo, nahau na matini nyengine za kifasihi, kwa kutumia njia yoyote ya tafsiri, mfasiri anaweza kwenda kinyume na utamaduni wa lugha lengwa endapo atakuwa si mzoefu wa utamaduni wa jamii hiyo.

  •      Tafsiri husababisha matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili katika maandishi.
Hapa nakusudia kueleza kuwa, moja ya njia ya uchanganyaji wa lugha katika maandishi ni tafsiri. Watu wengi wanaojishughulisha na kutafsiri matini mbali mbali kwenda lugha ya Kiswahili huathiriwa na kazi hio na kuwasababishia kuchanganya lugha pale wanapoandika kazi nyengine za Kiswahili jambo ambalo ni kinyume na utamaduni wa mtanzania. Jambo hili huweza kujitokeza kwa waandisi wa makala mbali mbali za Kiswahili lakini pia wahariri wa magazeti.   
    Hapa nataka nifahamike kuwa, sipingi utumiaji wa neno au maneno ya lugha nyengine kama kiingereza ambayo yana lengo la kutoa ufafanuzi zaidi juu ya jambo fulani ambapo mara nyingi maneno hayo huwekwa katika mabano. Bali nakusudia uchanganyaji wa lugha kwa ujumla. Mfano katika upekuaji wa makala mbali mbali nimegundua matumizi hayo kama ifuatavyo:-        
“Mimi ninadhani values za jamii ni kioo ambacho maendeleo yoyote that we want  and to find out kwa udi na uvumba lazima ya reflect, kama we have not values za          maana ni vipi tutaendelea”
Kwa hiyo mtu anayetumia lugha kama inavyoonekana katika maelezo yaliopo hapo juu, mimi kwa maoni yangu naona mtu huyo ama ameathiriwa na lugha ya kiingereza au kutokana na kufanya kazi nyingi za tafsiri.

Hitimisho na Mapendekezo:
Kwa ujumla makala hii imeelezea kwa kina kuhusu faida na hasara za tafsiri katika utamaduni ambapo maelezo yake, zaidi yamejikita kutoka katika dhana ya tafsiri, dhana ya utamaduni lakini zaidi kupitia historia na maendeleo ya tafsiri nchini Tanzania.
Licha ya uhaba wa historia ya tafsiri nchini Tanzania, na pamoja na kuwepo baadhi ya changamoto katika vipengele mbali mbali vya maisha ya jamii ya watanzania na Afrika kwa ujumla, bado taaluma hii ni muhimu sana hasa katika mawasiliano kati ya jamii zinazozungumza lugha tofauti, pia ni muhimu katika masuala mbali mbali ya kielimu bila ya kusahau katika soko la ajira.  
Kwa hiyo ili kufikia malengo hayo, ni wajibu wetu kuisoma taaluma hii kwa undani zaidi pamoja na kufuata kikamilifu kanuni, taratibu na sheria za tafsiri ili tuweze kupata kazi nzuri za tafsiri zenye kukidhi mahitaji ya matini chanzi, matini lengwa na utamaduni wa jamii husika.  


 MAREJELEO :  
ü  Mshindo, H. B. (2010). KufasirinaTafsiri. Chuo Kikuu cha Elimu. Chukwani, Zanzibar.

ü  Mwansoko, J. M. (1961). Kitangulizi cha tafsiri, nadharianambinu. TUKI. Dar es salaam.
ü  Mwansoko na Wenzake (2006). Tafsiri na Ukalimani. UDSM.

ü  Ponera, A. S. (2014). Utangulizi wa Nadharia ya Fasihi Linganishi. Karljamer Print Technology. Dar es salaam, Tanzania.

MITANDAO
ü  antagonf.blogspot.com. Tafsiri na ukalimani.

ü  chomboz: blogsport.com/2013. MisingiyaTafsirinaUkalimani.

ü   https://sw.m.wikipedia.org. Utamaduni – wikipedia, kamusi elezo huru.

ü  nenothabiti.blogspot.com. Tafsiri. 

ü  www.jamiiforum.com. Ni nini utamaduni wa mtanzania?
 ================================================
 Mtunzi: Said Ali Shehe. 
Muhitimu, Chuo Kikuu cha Sumait Zanzibar.



MCHANGO WA SHAABAN ROBERT KATIKA TAALUMA YA TAFSIRI



Ikisiri
Kazi hii inahusu mchango wa Shaabani Robert katika taaluma ya tafsiri. Katika uga wa fasihi jina la Shaaban Robert limekuwa na mwangwi katika masikio ya wanataaluma wengi hususani taaluma ya fasihi. Katika makala hii tutajadili mchango wake katika taaluma ya tafsiri. Makala hii imegawika katika sehemu kuu tatu, nazo ni utangulizi, kiini na kifungio. Katika utangulizi; tutaangazia historia ya Shaaban Robert kwa ufupi tukidondoa kuzaliwa kwake, ndoa, kazi alizowahi kufanya na mazao ya kazi zake za kibunilizi. Vilevile tutatupia jicho tu dhana yenyewe ya tafsiri kwa kuangalia maana na chimbuko lake. Kiini cha makala hii tutajadili mchango wake katika taaluma ya tafsiri. Na sehemu ya mwisho ni hitimisho. Data za makala hii zimetokana na rejea mbalimbali zikiwemo tafiti, vitabu na makala mbalimbali kuhusu mada tajwa. Aidha tumeona kuwa, Shaabani Robert achilia mbali kuwa ni maarufu katika taaluma ya fasihi, bali pia anamchango mkubwa katika taaluma ya tafsiri.

1.0 Utangulizi
Taaluma ya tafsiri ni taaluma kongwe ukilinganisha na taaluma zingine, kuwapo kwa taaluma hii ndio imepelekea taaluma zingine kueleweka kwa urahisi zaidi. Tumekuwa tukishuhudia maendeleo mbalimbali ya elimu yakipiga hatua kwasababu ya tafsiri. Taaluma kama za sayansi zimeweza kupiga hatua kwa sababu ya tafsiri. Shaabani Robert aliona umuhimu wa taaluma ya tafsiri hivyo alijitosa katika taaluma hii ya tafsiri kinadharia na kivitendo katika fasihi ya Kiswahili. Katika sehemu hii tutaangalia historia ya Shaabani Robert kwa ufupi na dhana ya tafsiri kwa ujumla wake.

1.1 Historia Fupi ya Shaabani Robert
Hapa tutaangalia mambo mbalimbali yamuhusuyo  Shaabani Robert ikijumuishwa  na kuzaliwa kwake, ubini na mbari yake, elimu yake, kazi alizowahi kufanya, tuzo alizowahi kupata, kazi zake za kiuandishi  hali yake ya kindoa na kifo chake.

1.1.1 Kuzaliwa
Shaaban Robert alizaliwa tarehe 1/9/1909, Mtaa wa Vibambani, kijijini Machui, mkoani Tanga na kufariki tarehe 20 Juni 1962 Katika hospitali ya Bombo mjini Tanga, na kuzikwa tarehe 22 Juni 1962 katika makaburi ya familia huko Vibambani, Machui mkoani Tanga. Ni mwana wa nne kwa Bi Mwanamwema kati ya wana 14 na alikuwa mwana wa kwanza kwa baba yake Bwana Suleimani Ufukwe Robert.

1.1.2 Asili ya Majina ya Baba wa Shaaban
Ufukwe, Suleiman, Robert yote ni majina ya baba yake Shaaban, hivyo Shaaban alikuwa anaitwa Shaaban bin Robert, Shaaban bin Suleiman pia Shaban bin Ufukwe.

1.1.2.1 Asili ya Jina la Shaaban Ufukwe
Aliitwa Shaban Ufukwe kwa sababu bibi wa Shaaban alipatwa na uchungu wa uzazi wa baba yake Shaaban akiwa ufukweni akitanda uduvi, hivyo ni jina la kihistoria ya kuzaliwa kwake alilopewa na watani wakimaanisha historia ya kuzaliwa kwake na hivyo kuitwa Ufukwe.

1.1.2.2 Asili ya Jina la Shaaban Robert
Aliitwa Shaabani Robert kwa sababu, babu wa Shabani Robert alikuwa anafanya kazi katika mashamba ya minazi ya wakoloni, hivyo bosi wa babu yake yaani baba wa Ufukwe alifurahi kusikia mfanya kazi wake kapata mtoto wa kiume na aliona aitwe Roberto kwa kuwa yeye jina lake lilikuwa Roberto. Hivyo baba wa Shaabani aliitwa Roberto yaani jina la bosi wa babu yake Shaabani. Lakini kutokana na usomaji wake jina hilo lilipokea mabadiliko yakimatamshi kwa kuwa alisoma shule za waingereza walilibadilisha jina la Roberto kuwa jina la Robert.

1.1.2.3 Asili ya Jina la Shaaban Suleimani
Jina la Suleimani, ni jina la kiimani. Babu wa Shaaban alikuwa ni muislamu kwa hiyo alimpa jina hilo kutokana na imani yake ya kidini. Mwanamwema bint Mwindau ndie mzaa chema ni mama wa Shaabani Robert, alikuwa ni mmwamwande lakini alijiita mswahili. Alitokea katika ukoo wa Mwalimu Kihere.

1.1.3 Elimu yake
Mara baada ya kufikisha miaka 9 mama wa Shaabani Robert alimpeleka madrasa na kupata elimu ya dini ya kiislamu. Baada ya kifo cha Mzee Ufukwe 14/09/1918 Shaban Robert alipelekwa Dar es salaam kwa babu yake aliyeitwa mzee Juma bin Kanduru aliyetokea katika ukoo wa Chemataka huko Tunduru. Babu yake alimpeleka shule iliyoitwa Kichwele ambayo kwa sasa inaitwa Uhuru Mchanganyiko hapo alisoma kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la nne kuanzia mwaka 1922 hadi 1926.

1.1.4 Kazi za Kiserikali (Utawala) Alizofanya
  •        Forodha TRA- Dar es Salaam, Arusha na Tanga,
  •         Idara ya Wanyama pori- Tanga (1944-1946)
  •         Idara ya Kupima Ardhi (Afisa wa kupima Ardhi) na kustaafu 1960

1.1.5 Tunzo Alizotunukiwa
  •                   Tuzo ya uandishi bora ya Margaret Wrong Prize
  •                  Tuzo ya mjumbe wa himaya ya uingereza
  •    .            Tuzo ya mwandishi bora wa wizara inayosimamia utamaduni nchini Tanzania

1.1.6 Kuhusu Ndoa
Alibahatika kuwa na wake wa tatu katika vipindi tofautitofauti, Amina, Sharifa binti Husein na Mwanambazi bint Alii. Amina (1930-1931) alitokea ukoo wa mwalimu Kihere), walizaa watoto wengi waliobahatika kuishi ni wawili, yaani Mwanjaa na Suleimani. Amina Alifariki 1942. Sharifa binti Husein alimuoa 1945 aliyetokea Chumbageni Tanga alizaa nae watoto wanne Akili, Hussein, Mwema na Ikibari. Mke huyu alifariki 1955. Mwanambazi binti Alii, alitokea Tongoni Tanga, hakuzaa na ndiye aliyemkalia eda Shaabani na alifariki baada ya mwaka mmoja kufariki Shaaban 1964 (Kielelezo cha Fasili, 1962: i-xii).

1.1.7 Kazi Zake za Kiuandishi (Taaluma)
Kazi yake ya kwanza aliitoa mwaka 1932 katika gazeti la mamboleo uk 34. Ilikua barua kwa mhariri. Kazi hii aliipa jina la Hirizi ya Shilingi Mia. Ilihusu kupinga ushirikina inapatikana katika kitabu cha barua za Shabani Robert ukurasa 191 waraka wa 11.3. Baada ya kazi hii Shaban Robert alifanikiwa kutunga vitabu vya ushairi na nathari. Hata hivyo kumekuwa na msigano wa kidondozi kuhusu kazi hizi kutokana na baadhi ya wataalamu kutofautiana katika kuidadisha na kudondoa kazi zake. Kwa mfano, Sengo (1975), Kezilahabi (1976) pamoja na Gibbe (1980) wanasema kuwa jumla ya kazi zilizotungwa na Shaaban Robert na zilizochapishwa ni 22, ambazo 14 ni ushairi na 8 ni za nathari. Vilevile kuna kundi la waandishi wa hivi karibuni kama vile Mulokozi (2002), Chuachua (2008) na Ponera (2010) wanaidadisha maandiko yake kuwa ni 24 ikiwa 14 ni ushairi na 10 ni nathari (Ndumbaro, 2014). Zifuatazo ni kazi za Shaaban Robert kama zinavyoainishwa na Ponera (2010).

1.1.7.1 Ushairi
Aliwahi kuandika vitabu vya ushairi takribani 14, vitabu hivyo ni;
  • ·         Almasi za Afrika (1971), Nelson, Nairobi
  • ·         Koja la lugha(1969), Nelson, Nairobi
  • ·         Insha na mashairi,(1967), Nelson, Nairobi
  • ·         Kielelezo cha Fasili, (1962), Nelson, Nairobi
  • ·         Pambo la Lugha, (1968), Oxford, Nairobi
  • ·         Ashiki Kitabu Hiki, (1968), Nelson, Nairobi
  • ·         Mashairi ya Shaban Robert, (1971), Nelson, Nairobi
  • ·         Sanaa ya Ushairi, (1972), Nelson, Nairobi
  • ·         Mwafrika Aimba, (1969), Nelson, Nairobi
  • ·         Masomo Yenye Adili, (1959), Art & Literature, Nairobi
  • ·         Mapenzi Bora, (1969), Nelson, Nairobi
  • ·         Tenzi za Marudi Mema na Omar Khayyam(1973), TPH, Dar es Salaam
  • ·         Utenzi wa Vita vya Uhuru(1961), Oxford, Nairobi
  • ·         Almas za Afrika na Tafsiri ya Kingereza (1960), Art & Literature, Nairobi

1.1.7.2 Nathari
Kwa upande wa nathari hakuwahi kuandika tamthiliya bali  aliwahi kuandika riwaya zipatazo 9 nazo ni;  
  •   Maisha yangu na baada ya miaka hamsini, (1949), Nelson, Nairobi 
  •   Adili na Nduguze,(1977) TPH, Dar es Salaam 
  •   Kusadikika (1951),Nelson, Nairobi 
  •    Kufikirika (1968) Nelson, Nairobi  
  •   Wasifu wa Siti bint Saad (1967) Art & Literature, Nairobi 
  •  Utu bora mkulima,(1968) Nelson, Nairobi 
  •  Siku ya watenzi wote (1968) Nelson, Nairobi 
  •  Barua za Shabani Robert 1931-1958 (2002), TUKI, Dar es Salaam 
  • Kielelzo cha Insha (1954) Witwatersrandd, Nairobi 
  • Mithali na mifano ya Kiswahili, (2007), TUKI, Dar es Salaam

1.2 Ufafanuzi wa Istilahi (Dhana)
1.2.1 Dhana ya Tafsiri
Dhana ya tafsiri imekuwa ikijadiliwa na wataalamu wengi. Mwamsoko (2006) akimnukuu Cartford (1965) anasema kuwa tafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka katika lugha nyingine (lugha lengwa). Pia Newmark (1982) anajadili dhana ya tafsiri kama mchakato wa uhawilishaji wa maneno kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa.  Nida na Taber (1969) wanaeleza kuwa tafsiri hujumuisha kuzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe vya asili vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi kimaana na kimtindo. Wao wanatilia mkazo uzalishaji upya wa ujumbe kwa kutumia visawe asili vinavyokaribiana na matini chanzi kimaana na kimtindo. Kutokana na maana hizi tunaweza kusema kuwa,  tafsiri ni ujumbe uliopo katika maandishi ambao asili yake si lugha ya matini inayosomwa.

Mwansoko na wenzake (2006), wanaeleza kuwa tafsiri ni zoezi la uhawishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine. Wao wanatilia mkazo katika zoezi la uhawishaji na kinachohawilishwa ni mawazo katika maandishi. Kwahiyo tunaona suala la umaandishi linajitokeza katika fasili ya Mwansoko, Cartford. Lakini tukichunguza fasili ya Nida na Taber wao wanasisitiza zaidi maana na kutobadilisha mtindo uliopo katika lugha chanzi.

Kwa ujumla suala la tafsiri lazima lichangamane na uwepo wa lugha mbili yaani chanzi na lengwa, pia kuwe na mchakato wa ubadilishaji wa lugha ya awali na kuweka katika lugha mpya bila kupoteza maana na tena kuwe na suala la kutokubadilika kwa mtindo na muundo wa kazi ya lugha chanzi.

1.2.2 Chimbuko la Tafsiri
Kihistoria, taaluma ya tafsiri inaanzia nchini Misri ambako ndio chimbuko la elimu za kale na kitovu cha maendeleo yote tuliyonayo sasa. Inasadikiwa kuwa miaka 3000 kabla ya Kristo nchi ya Misri iliendelea kwa taaluma za kisayansi na nyingi za kisasa. Ugunduzi na ustaarabu ulioletwa na wamisri kutokana na tafsiri ya elimu ya kale na kuwekwa elimu hiyo katika lugha ya Kiarabu. Ustaarabu huo uliigwa na Wayunani na kuwa ndio sababu ya maendeleo barani Ulaya. Baada ya kufasiri kazi mbalimbali zilizoporwa huko Misri wakati wa vita vya msalaba kati ya Waislamu na Wakristo katika karne ya 15, bara la Ulaya lilianza kujibabadua katika zama za giza na kuingia katika kipindi cha ufufumko. Katika karne ya 19 kazi nyingi zilitafsiriwa na karne ya 20 ndiyo inasadikiwa kuwa ndio karne ya tafsiri iliyopelekea maendeleo ya haraka ya kisayansi na kiteknolojia.
Nchini Tanzania taaluma ya tafsiri haina historia ndefu ilianzia katika karne ya 19. Tunaweza gawa mapito matatu ya tafsiri nchini Tanzania; kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya uhuru.

1.2.2.1 Kabla ya Ukoloni
Mwansoko (1996) katika Mshindo (2010) anadai kuwa utenzi wa Hamziyya ndiyo utenzi wa kwanza kutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili kutoka katika lugha ya Kiarabu. Utenzi huu ulitungwa huko Misri karne ya 13. Utenzi huu ulijulikana kwa lugha ya Kiarabu kwa jina la Al basiry, Qasida Ummal Qura. Aidarus bin Athmani ndiye aliyekuwa mfasiri wa utenzi wa Hamziyya aliyeishi miaka 1700 hadi 1750 nchini Kenya. Pia Wamisionari walifasiri vitabu vya dini ya kikristo kutoka katika lugha ya Kiingereza na kwenda katika lugha ya Kiswahili na lugha zingine za makabila.

1.2.2.2 Wakati wa Ukoloni
Wakati wa ukoloni, waingereza walitafsiri maandiko mbalimbali ya taaluma ya fasihi ya ulaya kwa lugha ya Kiswahili. Riwaya ya Mzimu wa Watu wa Kale ilitafsiriwa kutoka katika lugha ya Kiingereza iliyoitwa Shrine of The Ancestor na kazi kama vile Hekaya za Abunuwasi, Alufulela Ulela, Hadithi za Ethopo na Safari Za Guliver nazo zilitafsiriwa.

 1.2.2.3 Baada ya Uhuru
Baada ya uhuru kuanzia mwaka 1961 walijitokeza wataalamu mbalimbali waliotafsiri kazi mbalimbali na kutoka katika lugha mbalimbali na kuwa katika lugha ya Kiswahili. Mwalimu Julias Nyerere hatutajitanibu kumtaja katika taaluma ya tafsiri kwani alitafsiri vitabu kadhaa kuwa katika lugha ya Kiswahili. Kazi za Shakespare kama vile The Mechant of Venis na kuwa Mabeperi wa Venisi na Julius Caesar na kuwa Julias Kaizari. Licha ya Nyerere wapo waandishi kama Paul Sozigwa aliyetafsiri Songs of Lawino pia East African Literature Bureau 1967 walitafsiri kazi ya The Freeing of The Slaves in East Africa na kuwa Uhuru wa Watumwa. Baada ya kazi hizo kazi nyingi zilizotafsiriwa ziliongezeka. Baadhi yazo ni kama vile Nitaolewa Nikipenda Kilichotafsiriwa na Clement M. Kabugi mwaka 1982 kutoka katika lugha ya Kiingereza (Mwansoko na Wenzake; Mshindo).
2.0 Mchango wa Shaaban Robert katika Taaluma ya Tafsiri
Pamoja na Shaaban Robert kuwa maarufu sana katika taaluma ya fasihi hadi kufikia kupewa lakabu ya ubaba, pia amejitokeza katika taaluma ya tafsiri. Robert anaonekana katika uga huu wa tafsiri kutokana na maandiko yake binafsi aliyoandika kuhusu tafsiri japo kwa kudokeza, pia kufanya kazi yenyewe ya kutafsiri, halikadhalika kuchopeka dhamira za kitafsiri katika baadhi ya kazi zake za kinathari. Hapa tutagawa mchango wake katika taaluma hii ya tafsiri katika nukta kuu tatu, kwanza maandiko ya kitafsiri au mazao ya kazi za tafsiri, pili nadharia kuhusu tafsiri, na tatu ni usanaji wa dhamira za kitafsiri. Na aya zifuatazo zitachanganua kwa uwazi juu ya nukta hizo.

2.1 Mchango Katika Nadharia za Tafsiri
Katika kipengele hiki tutadondoa mchango wa kinadharia ambao Robert ameweza kuutoa katika kitabu chake cha Kielelezo cha Fasili. Robert ameonekana kutolea ufafanuzi dhana ya tafsiri, umuhimu, mbinu, aina zake na miiko ya kazi ya tafsiri. Anatoa maaana ya tafsiri kuwa ni “fasili ni maelezo ya fikira na maoni katika karaa, aghalabu ya mashairi kwa usemi mwepesi wa mjazo. Ni taaluma katika maandiko ya luha na fahamu ya fikira za mwandishi na msomaji”.
Katika nukuu hii tunaona namna Shaaban Robert anavyozungumzia na kuifafanua maana ya tafsiri. Ijapokuwa upo upungufu kidogo wa kitaajia katika neno ‘fasili’ lakini mawazo aliyoyatoa tunaona yanabeba dhana ya tafsiri. Pia Robert anaona kuwa tafsiri bora ni ile inayozingatia maana au kiini cha matini kuliko fasiri ya neno kwa neno.

Aidha, Robert anaeleza umuhimu wa taaluma ya tafsiri katika ukurasa wa xiii wa kitabu hichohicho. Anaona kuwa tafsiri ina umuhimu kwa kuwa inatuwezesha kujua lugha lakini pia lugha yenyewe kukua kwa kujiongezea msamiati na watumiaji wa lugha kutumia msamiati hiyo katika maisha ya kila siku.

Sambamba na hayo, Robert ameweza kuwekea kanuni za tafsri bora katika ukurasa wa xiv wa kazi hii. Anaona kuwa tafsiri ili iwe nzuri lazima mfasiri achunge miiko na aepukane na baadhi ya mambo katika kufasiri.  Anasema ili tafsiri iwe bora mfasiri lazima azingatie haya yafuatayo: “kuandika neno kwa neno, kuelewa dhana ya jumla ya kila fungu, kuwa makini na maana ya kila neno, kuandika fikra za waziwazi, kutunga mfano wa makala na kuzingatia ukubwa wa makala ya asili. Hata hivyo Robert anaweka miiko mingine ambayo mfasiri anapaswa kujiepusha nayo ili kuepukana na matini tenge. Anaona mfasiri si vema kwake kukiusha maana, kuongeza lisilokuwepo kimtindo na mpango wa kazi kwa ujumla wake. Haya yote yamekuwa yakilalamikiwa na wataalamu mbalimbali katika taaluma ya tafsiri kama vile Mtesigwa kama anavyonukuliwa na Mwansoko (2013:91-94). Mtesigwa nalalamika juu ya tafsiri ya wimbo wa Lawino ulivyopotoshwa kimaana katika baadhi ya vipengele. Lakini si kazi hiyo tu iliyopotoshwa kwani tumekuwa tukishuhudia jinsi kazi mbalimbali zinavyokuwa tenge kwa sababu ya kutozingatia kanuni hizi.

Kwahiyo, kanuni hizi ni mihimiri katika kazi yoyote ya tafsiri kwani kufuatwa kwake ni njia ya kuzalisha kazi nzuri na kuupuzwa kwake ni uzalishaji wa matini tenge. Vilevile Robert ameweza kutoa aina kuu za tafsiri yaani; fasili sisisi na fasili sabilia. Ambazo Mwansoko fasili sabilia ameiita tafsiri ya Kisemantiki.

Kwa jumla tunaweza sema kuwa Shaaban Robert ametoa mchango mkubwa katika utangulizi wa taaluma ya tafsiri, hivyo, amekuwadira kwa waandishi wachanga wanaoandika katika taaluma hii ya tafsiri. Kwani baadhi ya istilahi zake bado zinatumika hadi sasa, kwa mfano, tafsiri ya neno kwa neno na hata tafsiri sisisi ijapokuwa zimepanuliwa zaidi lakini msingi wake tunaona unajengwa na Shaaban Robert.

2.2 Fikra za Kitafsiri
Katika dondoo hii tutaona jinsi Robert alivyopenyeza fikra za tafsiri katika riwaya ya Siku ya Watenzi Wote. Katika kazi hii tunaona jinsi mwandishi alivyoweza kuonesha maudhui yanayoonesha ubora, madhara ya tafsiri tenge na hata umuhimu wa tafsiri. Mwandishi anaonesha haya kuna miongoni mwa sura za riwaya hiyo kuna sura ameipa kwa jina la tafsiri. Kinachozungumziwa   katika sura hiyo ni kuhusu umuhimu wa tafsiri na umuhimu na mfasiri kuwa mahiri katika lugha zote mbili, lugha chanzi na na lugha lengwa. Robert anaona kuwa ikiwa mfasiri si mweledi katika masuala ya lugha bila shaka kazi ya tafsiri itakuwa na ukiushi anaeleza katika ukurasa wa 40-41. Anasema kuwa; 
Alisoma tafsiri hiyo mbiombio, kisha akanena;” Kazi yako si nzuri Bi Nunu na tafsiri yako si sahihi kamwe! Hujui kitu-Kiswahili wala Kingereza. Mara ngapi nimekwambia kuwa unavuruga mambo-lugha ngeni katika Kiswahili. Mshupavu kama jiwe. Huambiliki…” Huu ni upeo wa tafsiri ya makala hii, bwana uliza kwa mtaalamu yeyote wa lugha…    
Hapa tunaona kuwa mwandishi anamsemanga bosi wa Nunu kwa kukurupukia taaluma ya tafsiri kiasi kwamba kutokana na ujinga wake katika masuala ya tafsiri anamuona Bi Nunu amevuruga  kazi ya tafsiri wakati yeye ndiye aliyeharibu.

2.3 Mazao ya Kitafsiri
Pamoja na fikra zote hizo kuhusu tafsiri ambazo zinajidhihirisha katika kazi zake za kifasihi lakini Robert alithubutu pia kuitumbukia taaluma ya tafsiri kwa matendo. Aliweza kutafsiri kazi yake mwenyewe iliyokuwa katika lugha ya Kiswahili na kuiweka katika lugha ya Kiingereza aliyoiita kwa jina la Almasi za Afrika na Tafsiri ya Kingereza. Pamoja na kazi hiyo Shaaban Robert ameweza kutafsiri mashairi ya Omari Khayaam yaliyokuwa katika lugha ya Kiingereza kama yalivyotafsiriwa na Bwana Edward FitzGerald kutoka katika lugha ya Kiajemi katika kitabu alichokiita Tenzi za Marudi Mema na Omary Khayyam.

2.3.1 Almasi za Afrika na Tafsiri ya Kingereza
Katika kitabu cha Almasi za Afrika anaeleza kusudi la yeye kutafsiri kitabu hicho katika lugha ya Kiingereza katika ukurasa ii katika utangulizi, anasema; “Kusudi la tafsiri za lugha ya Kingereza katika kitabu hiki ni kuonesha jinsi Kiswahili kiwezavyo kuchukuana vema na lugha nyingine; na kusaidia baadhi ya wasomaji kuelewa kuwa hii si lugha masikini   
Katika tafsiri hii Robert anatumia mbinu ya kisemantiki kama yeye alivyoiita sabilia, amezingatia maana zaidi kuliko mtindo. Hata hivyo mwandishi anaweka msisitizo kuwa tafsiri yake isieleweke vibaya kwa wasomaji kiasi wakadhani kuwa masharti ya Kiingereza yanakuwa katika hali hiyo isipokuwa waelewe kuwa hiyo ni tafsiri tu ya matini chanzi na mashairi ya Kingereza yana utaratibu maalumu wa utunzi, kama vile huwa na mizani na vina pia huwa na maana zaidi ya moja.

2.3.2 Tenzi za Marudi Mema na Omari Khayyam
Shaaban Robert alitafsiri tenzi hizi kwa kupewa ushauri na aliyekuwa Mudiri wa idara ya elimu Tanganyika Bwana A.A.M Isherwood. Robert alitafsiri tenzi hizi kutoka katika lugha ya Kiingereza yaliyojulikana kwa jina la Rubayyat of Omary Khayyam mwaka 1859. Matini chanzi ya kwanza ya tenzi hizi ilitoka katika lugha ya Kiajemi, tenzi hizi zilijulikana kama Rubayyat (Robert, 1973:103-104).

Tafsiri ya hii pia imetoa dira katika mbinu za kutafsiri, kwani mfasiri anatumia pia mbinu ya kisemantiki ambayo hujikita katika sarufi ya lugha lengwa. Mfasiri anatumia mbinu hii kuanzia mwanzo wa ubeti hadi mwisho. Kwa hiyo, kitendo cha Shaaban kutafsiri kazi hii kutoka katika lugha ya kingereza na kuwa katika Kiswahili  tunaweza hesabu kuwa huu ni mchango mkubwa katika taaluma ya tafsiri. Kupitia kazi hii mwandishi anatuongezea idadi ya kazi zilizo tafsiriwa kwa Kiswahili katika makavazi.

3.0 Hitimisho
Hakika Shaaban Raobert amekuwa gumzo katika lugha ya Kiswahili kwa ujumla hasa katika uwanja huu wa fasihi. Uwepo wake unajionesha waziwazi katika kazi alizozifanya. Kutokana na umaarufu huu wa kitaaluma, Shaaban Robert alipewa jina la lakabu la ‘baba’ wa Fasihi ya Kiswahili. Sio hivyo tu, nguli huyu alithubutu kuvamia uga wa tafsiri kupitia eneo lake hili la fasihi. Baadhi ya kazi tulizozithibitisha hapo juu bila shaka zimethibitisha kweli hii. Hivyo basi tunatoa wito kwa wanataaluma na wahakiki kuzamia kwa kina katika tanzu alizozifanyia tafsiri na kuzihakiki kwa jicho la ndani zaidi. Hii itapelekea kugundua mambo mbalimbali yaliyotumiwa na Shaaban Robert katika kutafsiri, pia kugundua udhaifu na ufaafu wa tafsiri yake na tena kufanya ulinganisho wa kitaaluma kati yake na wafasiri wengine.

 MAREJELEO
FitzGerald, E, (1859), The Rubayyat of Omary Khayyam, The University of Adelaide Library, Adelaide, South Australia.
Mshindo, H.B, (2010), Kufasiri na Tafsiri, Oxford Univerasity Press, Dar es Salaam.
Mwansoko, H.J.M na Wenzake, (2006), Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu, TUKI, Dar es Salaam.
Ndumbaru, E, (2014), “Maandiko ya Shaaban Robert” Bubujiko la Maarifa, [Mtandaoni: Imepitiwa 10 Mei 2015 saa5:16 usiku].
ponera, a.s, (2014), Utanguliazi wa Nadharia ya Fasihi Linganishi, Karljamer Print Technology, dar es salaam.
Ponera, A.S, (2010), “Ufutuhi katika Nathari za Shaaban Robert: Maana yake, Sababu za Kutumiwa na Athari zake kwa Wasomaji” tasnifu ya Masomo ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dodoma, [Haijachapishwa].   
Robert, S., (1960), Almas za Afrika na Tafsiri ya Kingereza, Art & Literature, Nairobi.
Robert, S., (1973) Tenzi za Marudi Mema na Omar Khayyam, TPH, Dar es Salaam.
Robert, S., (1968), Siku ya watenzi wote, Nelson, Nairobi
Robert, S., (2004) Kielelezo cha Fasili, Nelson, Nairobi
Sengo, S.Y, (1992), Shaaban Robert: Uhakiki wa Maisha Yake, KAD Associaties, Dar es Salaam, Tanzania.

-----------------------------------------------------------------------------------------------

Zuhura Said Ismail
Chuo Kikuu cha Dodoma 
0718629339 au 0783629339 
 DODOMA, TANZANIA