TANZU ZA USHAIRI WA KISWAHILI
Ushairi
wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au kumbo mbalimbali. Mulokozi
(1996), ameuainisha ushairi wa kimapokeao katika kumbo kuu tatu za kimtindo.
Kumbo hizo ni: ushairi wa kijadi au kimapokeo; ushairi wa mlegezo; na ushairi
wa maigizo.
1.
Ushairi
wa Kimapokeo
Haya ni mashairi ya kijadi yenye
kufuata kanuni za urari wa mizani na mpangilio wa vina vya mwisho na/au vya
kati. Mfano wa shairi la kimapokeo ni huu hapa:
Namshukuru
Namshukuru
Illahi, Mwenyezi mkamilifu,
Kwa
kuishi nikawahi, kazini kustaafu,
Bado
ningali sahihi, imara na mkunjufu,
Alihamdulilahi, namshukuru Latifu.
Ulimwengu
wa rakadha, umejaa hitilafu,
Sikuweza
mambo kadha: karibu mambo elfu;
Kanipa
hii karadha, Bwana Mungu namsifu,
Alihamdulilahi, namshukuru Latifu.
Hii
sikutazamia, kwamba litanisadifu,
Bahati
imenijia, kwa kupenda Mtukufu,
Mfano
kama ruia, Mungu hana upungufu,
Alihamdulilahi, namshukuru Latifu.
(Shaaban Robert, 2003:
102 – 104)
2.
Ushairi
wa Mlegezo
Haya ni mashairi yenye
kufuata baadhi ya kanuni za arudhi za kimapokeo ambayo wengine huyaita sukui au
“guni” nay ale yasiyofuata kabisa kanuni hizo (mauve au mashairi huru).
(a)
Mfano
wa shairi guni ni:
Muombwa
Muombwa ni wewe Mungu
Na jamii ya umati,
Miili itie nguvu
Na heri katika nchi,
Astawi kila mtu
Zitakae na nafsi.
(Shaaban Robert, 1968:
18)
(b)
Mashairi
ya Mavue (tungo – mtiririko, mashairi – huru)
Wao Pia Walicheza
Na hao wafuasi wa Mzee
Askari wa Mapinduzi
Waliicheza ile ngoma.
Kama asingekuwa Nagona
Kutokeza hadharani
Wangevunja mifupa yao.
Anayeleta sasa ubishi
Amemsahau kiongozi wake.
(E. Kezilahabi, 1988:
18)
3.
Ushairi
wa maigizo
Ushairi wa maigizo ni
fani ngeni kidogo katika ushairi wa Kiswahili. Tunaposema fani ngeni tuna maana
kwamba si fani ya siku nyingi kama zilivyo fani nyingine za ushairi wa
Kiswahili. Ushairi huu unaweza kuwekwa katika makundi mawili ambayo ni:
ngonjera na ushairi wa kidrama.
(a)
Ngojera
Ngonjera ni neno la
kigogo lenye maa ya twende pamoja au kuambatana. Huu ni ushairi wa majibizano
ambao uliasisiwa na Mathias Mnyampala katika kipindi cha miaka ya sitini ili
kueneza siasa ya Ujamaa. Kabala ya Mnyampala, ushairi wa aina hii ulikuwepo
lakini haukuwa na mtindo huu wa kingonjera, ulikuwa unatambwa tu. Kwa mfano
shairi la majibizano ni kama lifuatalo:
Usawa
wa Binadamu
I
Wasema
watu ni sawa, nambie usawa wao,
Kina
hohehahe hawa, ambao hawana vyao,
Na
watu wenye vipawa, wenye vyeo, wenye vyao,
Nambie
usawa wao, watu mbalimbali hawa.
Mwone
mbilikimo huyu, na Mtusi wa Ruanda,
Huyu
kimo cha kibuyu, na kanzu yake ni gwanda,
Yule
ni kama mbuyu, pandikizi mtu panda,
Kibuyu
na kingaranda, ni kibuyu si mbuyu.
II
Watu
ni sawa nasema, zingatia neno watu,
Siwapimi
kwa vilema, ambavyo ni udhia tu,
Siwafanidi
kwa wema, ambao ni tabia tu,
Lakini
watu ni watu, mawalii na wagema.
Niseme
maji ni maji, pengine utaelewa,
Ya
kunywa, ya mfereji, na yanayoogelewa,
Ya
umande na theluji, ya mvua, mito, maziwa,
Asili
yake ni hewa, hayapitani umaji.
Katika shairi hili kuna sehemu
mbili au tuseme wazungumzaji wawili (pande mbili) lakini hawajibizani kama
ilivyo katika ngonjera. Wazungumzaji hawa wanapeana nafasi, mmoja anazungumza
hadi mwisho, na mwingine naye anaanza kujibu hoja za upande mwingine ili kutetea
hoja hiyo. Tofauti na ngonjera, mwishoni hatuoni watu hawa kukubaliana na
maelezo au majibu ya upande pili.
Katika ngonjera huwa
kuna pande mbili zinazojibizana kuhusu jambo Fulani. Upande mmoja ndio ulio
sahihi kwa mujibu wa mtunzi na upande
pili umepotoka. Lengo la mabishano huwa ni kuushawishi upande uliopotoka
ukubaliane na upande wenye msimamo sahihi baada ya kuelimishwa. Hili
ilinapotokea ngonjera huwa imefikia kilele chake, na ujumbe hudhihirika kwa
hadhira bila matatizo. Kwa maneno hayo twaweza kusema kuwa ngonjera ni aina ya
propaganda inayoigizwa jukwaani. Mfano wa ngonjera ni shairi lifuatalo:
Chama
Chetu cha TANU
MWANANCHI
(Anamuuliza Mwanasiasa)
Si chama cha Mabepari, cha watuta ndarahima?
Cha
Makabaila thori, na Wanyonyaji wa Umma?
Ama
bwanyenye viburi, na wapendao kutuma?
Siasa
ya TANU sema, ni chama cha watu gani?
MWANASIASA (Anamjibu Mwananchi)
Ndicho
chama chenye heri, kisaidiaco Umma
Si
chama cha matajiri, wachumao kwa dhuluma
Na
ni chombo chenye ari, si chombo cha uhasama
Ni
chama cha wakulima na wafanyakazi.
(Mnyampala, 1970)
Mifano
zaidi ya ngonjera inapatikana katika Ngonjera za UKUTA kitabu cha kwanza
na kitabu cha pili.
(b)
Ushairi
wa Kidrama
Huu ni ushairi
unaotumiwa katika baadhi ya tamthiliya. Mifano mizuri ya ushairi wa kidrama ni
tafsiri za michezo ya Shakespeare. Ushairi huo ni sehemu tu ya mchezo wa
kuigiza, ni mtindo mmojawapo wa kuandika mazungumzo ya wahusika katika
tamthiliya, hivyo hauwezi kutenganishwa na fani hiyo ya tamthiliya. Kwa mfano:
METELLUS.
Caius Ligarius hampendi kamwe Caezar
Ambaye alimkaripia kwa kumsifu Pompey:
Nashangaa hapana kati yeni al’yemtaja.
BRUTUS.
Bas, Metellus mwema, nenda kamf’ate kwake:
Yeye anipenda sana na nimempa sababu;
Kamwambie aje hapa, mimi nitamshawishi.
CASSIUS.
Asubuhi imetukuta: tutak’wacha, Brutus: -
Nanyi, rafiki, sambaeni; ila kumbukeni
Mliyoyasema, na kuweni Warumi wa kweli.
BRUTUS.
Waungwana wema, changamkeni na furahini,
Nyuso zenu zisidhihirishe azma yetu;
Lakini tusitiri, kama vile wafanyavyo
Warumi wetu wachezaji, kwa mioyo baridi,
Na hali ya kawaida. Basi, nyote kwa herini.
W.
Shakespeare, Julius Caezar (Mf. J.K. Nyerere, OUP 1963:34)
Katika dondoo
hili ni ushairi wa mizani lakini hakuna vina. Pia kanuni ya kujitosheleza
haijafuatwa au imekiukwa. Wazo la mshororo mmoja linaendelezwa katika mshororo
unaofuata. Hili limefanyika ili kuufanya ushairi huu ukaribiane na lugha ya
mazungumzo.
BAHARI
ZA USHAIRI
Bahari za
ushairi ni aina mahususi ya ushairi yenye yenye sifa Fulani kiumbo (nap engine
hata kimaudhui na kimatumizi) zinazoipambanua na aina nyingine ya ushairi.
Wataalamu wa jadi wa ushairi wameainisha bahari tofauti ambapo wengine wanasema
zipo tatu tu yaani wimbo, shairi na utenzi. Wengine wanasema zipo tano, saba au
hata zaidi. ushairi kama utungo wa
fasihi umeainishwa kwa kuzingatia idadi maalumu ya mishororo katika beti (Noor
1988, Kandoro 1983 na Abedi 1954). Zaidi ya kuzingatia idadi mahususi ya mishororo,
mizani na urari wa vina katika ubeti, ushairi wa Kiswahili uliainishwa katika
tanzu mbalimbali kutokana na:
♣Urari wa vina
katika mistari au mishororo katika beti.
♣Mpangilio wa
maneno katika mistari au mishoro katika beti.
♣Idadi ya
vipande katika mistari au mishororo katika beti
♣Idadi maalumu
ya mizani katika mistari au mishororo katika beti.
Katika muktadha
wa vipengele hivyo vinne, muundo na maumbo ya ushairi huweza pia kuainishwa
zaidi kama ifuatavyo:
♦Tathnitha -
shairi ambalo lina mishororo miwili katika kila beti.
♦Tathlitha -
shairi ambalo lina mishororo mitatu katika kila beti.
♦Tarbia - shairi
ambalo lina mishororo minne katika kila beti.
♦Takhmisa -
shairi ambalo lina mishororo minne katika kila beti.
♦Tashlita -
shairi ambalo lina mishororo sita katika kila beti.
♦Ushairi ambao
una zaidi ya mishororo sita.
Masivina -
shairi ambalo lina mlingano wa mizani katika mishororo lakini si urari wa vina.
♦Ukawafi -
shairi ambalo lina vipande vitatu katika kila mshororo.
♦Msuko - shairi ambalo
lina kibwagizo kifupi.
♦Sakarani -
shairi ambalo linashirikisha bahari mbalimbali.
♦Kikwamba -
shairi ambalo linarudia neno moja katika kila mwanzo wa beti.
Kulingana na
Wafula na Njogu (2007) na Mohamed (1990), ni katika kipindi cha urasimi-mpya katika
fasihi ya Kiswahili ambapo palizuka istilahi maalumu za kuelezea dhana
mbalimbali za ushairi wa Kiswahili. Istilahi hizo zilizotumika zaidi ni kama:
♠Mshororo -
ambao ni mstari katika shairi
♠Mwanzo - mstari
au mshororo wa kwanza katika ubeti
♠Mloto - mstari
au mshororo wa pili katika ueti
♠Mleo - Mstari
au mshororo wa tatu katika ubeti
♠Kipokeo -
Mstari au mshororo wa mwisho katika ubeti
♠Ukwapi - Sehemu
ya kwanza katika mshororo
♠Utao - Sehemu
ya pili kaitka mshororo
♠Mwandamizi -
Sehemu ya tatu katika mshororo
♠Tabdila -
Kifupisho cha sauti kaitka neno linalotumika katika mshororo bila ya
kubadilisha maana ya msingi.
♠Inkisari -
Kunga ya kufupisha maneno katika mshororo
♠Mazida - Kunga
ya kurefusha neno bila ya kupotosha maana ya asili.
Kimsingi,
istilahi hizi zilitumika kimakusudi kwa malengo ya kuutambulisha ushairi wa
Kiswahili. Katika muktadha wa nadharia ya Fomula ya kisimulizi ni kwamba, uwepo
wa bahari na istilahi maalumu zinazotumika katika ushairi ni njia mojawapo ya
kubainisha tanzu za ushairi na fasihi kwa ujumla. Uainishaji huo unazingatia
zaidi ushairi wa Kiswahili unaotungwa katika muktadha wa arudhi za kimapokeo
(King‟ei na Kemoli 2001). Hata hivyo, inabainika kuwa ushairi wa Kiswahili
usiozingatia arudhi hizo katika utunzi na uwasilishaji haushirikishwi katika
uainishaji.
Wataalamu
wengine wakiongozwa na Ahmed Sheikh Nabhany wameainisha bahari kumi na tatu
kama ifuatavyo:
1. Shairi: Ni utungo wenye mishororo minne kila beti na vipande viwili vya mizani 8+8 kila kipande. Maudhui
yake yanatokana na jambo lolote lile analoliona mtunzi.
Mfano
wa shairi ni
Mtovu
ndumila kuwili, kwa haya hana mwafaka,
Kwake haki
na batili, kwa pamoja hujivika,
Huku
akakujamili, na kule akaitika,
Ndumila
kuwili si mwema, hujidhuru nafsiye.
2.
Wimbo: Ni utungo wenye mishororo mitatu
kila ubeti na kila mshororo una vipande viwili. Nyimbo nyingi huongelea
mapenzi. Ipo mikondo mingi sana ya nyimbo ambayo imebainishwa na wataalamu
mbalimbali. Mwalimu Ridhiwani amebainisha mikondo kumi.
3.
Tenzi: Ni shairi la masimulizi, mawaidha au maelezo marefu. Tenzi
nyingi zina mizani nane kila mstari. Vina vyake hubadilika kila mstari, ila kina
cha mwisho kiitwacho bahari, hakibadiliki. Tenzi hazifanani kikanuni maana kila
mtunzi huwa na maamuzi na namna yake ya kuandika utenzi wake.
Kwa mfano
Leo nataka binti
Ukae juu ya kiti
Ili uandike hati
Ndogo ya wasia.
Mimi kwako ni baba
Hati hii ya huba
Andika iwe akiba
Asaa itakufaa
(Shaaban
Robert, 2003)
Mfano mwingine
wa utenzi ni
Niliuliza
mwanzoni,
Sera
hii ni ya nani?
Serikali
kuwa tatu,
Hapa Tanzania
kwetu?
Ni ya serikali
yetu,
Au ya Wabunge wetu,
Au ni ya SISIEMU?
Tungependa
tufahamu.
(Julius K.
Nyerere, 1993:1)
4.
Inkshafi/Duramandhuma: Imepata jina lake kutokana na Utenzi wa Al-Inkshafi. Tenzi hizi zina maadili ya kidini japokuwa maudhui yake yanaweza kutumika katika maadili ya
kidunia. Kila ubeti una mishororo minne na kila mshororo una mizani 11 ya
6+5. Kwa mfano:
Makusudi yangu ya kudhamiri
Nda kutunga koja kilidawiri
Mivazi ya duri ikinawiri
Mikinda ya lulu nyuma nitiye.
Inkishafi, ubeti wa saba (Mulokozi, 1996:127)
5.
Ukawafi: Hili ni shairi lenye mishororo
mitatu au zaidi katika kila ubeti na vipande vitatu katika kila mshororo.
Mizani inaweza ikatofautiana au ikawa sawa.
Mfano:
Sifa uta wangu wa kitanzu cha mti roo
Upakwe mafuta unawiri kama kioo
Zipo
pia kawafi za mkondo wa 6+5+6. Maudhui ya kawafi nyingi huhusu dini, japo zipo
chache zenye kuzungumzia masuala ya kidunia.
6.
Wajiwaji/Takhimisa: Bahari hii huwa na mishororo mitano
kila ubeti na mizanai 15 kila mshororo na vipande vitatu katika kila mshororo
vina muundo wa mizani 6+ 4+ 5. Inaelezwa kwamba hapo zamani wajiwaji ilitungwa
na watu wawili tofauti. Maudhui yake yalihusu mambo mazito; huweza kuwa ya
kidini au ya kimaisha tu. Mfano wa wajiwaji ni ule uliotungwa na Sayyid Abdalla
bin Ali bin Nasir uliohusu shujaa Liyongo:
Anami shujaa samba ndole mwondoa ari
Mvunda kilaa na husuni kizidabiri
Nayipija kifa kayitia katika shari
Sichi mata yao na mafumo yanganawiri
Mandi mafuamati na magao mauya nyuma
…
7.
Hamziya: Bahari hii ilipata jina lake
kutokana na Utenzi wa Hamziya ambao ni
utenzi wa kiarabu.
Kilubeti una mishororo miwili yenye kina kimoja a Mishororo ya Hamziya ina vipande 3 vya mizani 5+ 4+ 6
Kilubeti una mishororo miwili yenye kina kimoja a Mishororo ya Hamziya ina vipande 3 vya mizani 5+ 4+ 6
8.
Tiyani-Fatiha: Bahari hii ni ya ushairi wa kidini wa kuomba toba. Huwa una
mishororo 9 kila
ubeti ambayo huweza kutofautiana kwa urefu/mizani kama inavyoonekana hapa chini.
ubeti ambayo huweza kutofautiana kwa urefu/mizani kama inavyoonekana hapa chini.
i.
Mishororo ya 1-2: mizani 6+6
ii.
Mishororo ya 3-4: mizani 3+8
iii.
Mishororo ya 5-7: mizani 4+4
iv.
Mishororo ya 8-9: mizani 6+6
Mfano:
Tiyani Fatiha tuombe Rabana
Huinadi twaha na Mursalina
Kwa nyute jamiina
Ya Ilaha Sayidina
Mshabaha Wewe huna
Kwa swahiha huniona
Moyo raha wangu sina
Taka mswamaha tubu alayna
Rabi
inaLlaha maa swabirina
Bi. Rukiya binti
Fadhil (1892 – 1968) katika Sharif, 1988:57 (katika Mulokozi, 1996:129).
9.
Utumbuizo: Bahari hii haina idadi kamili ya mishororo na mizani, urefu
wa mstari au mshororo hutegemea pumzi aliyonayo mwimbaji na lengo lake.
Utumbuizo huwa na vina vya mwisho, mara chache huwa na vina vya kati, lakini
bila mpangilio maalum. Wimbo ufuatao ni mfano mzuri wa utumbuizo ambao ni wimbo
wa malalamiko ya mwanamke baada ya kupata habari kuwa mumewe kaoa mke mwingine.
Bwana
Wende Yungwa
Bwana
wende Yungwa, koleya mashungwa, mimi humngoja kuwa mbiya kongo.
Hungoja
toka nisimeme hata k’anguka k’enda kwa magongo.
K’amngoja
nili na furaha, hata moyo k’afanya kisongo.
K’angoja,
kingiya kumwambiya k’ongo.
K’ampokeya
mvungu na ucha k’auweka kula penye change.
K’apokeya
kitoka na yembe k’azitiya t’ini ya mlango.
K’amvuwa
shungurere lake k’aliweka mbee za mlango
Umedondolewa
na Sharif, 1988:53 (katika Mulokozi, 1996:130).
1 0.
Wawe: Ni ushairi au wimbo wa kilimo,
huimbwa wakati wa kufyeka misitu, kuchoma magugu, kulima au kupanda hadi
kuvuna. Wawe haina idadi maalum ya mizani au vipande, ila nyingi zina vina vya
mwisho.
1 1.
Kimai: Inahusu shughuli za majini, ni bahari ya wavuvi na
mabaharia. Idadi ya mishororo na vina si lazima.
1 2.
Zivindo: Ni ushairi unaofafanua maana za
maneno, na kazi yake ni kujifunza lugha na kuhifadhi lugha.
Mfano:
Kata ni kata ya nyoka, au kata ya nyeleni
Kata ya tweka, ibandikwayo kitwani
Na kata ni ya kuteka, maji mema balasini
Kata kitu kwa makini, tena kuna kata gani?
(Ahmad Nassir “Nawau za Kimvita” (1971:55)
1 3.
Sama: Neno ‘sama’ ni mahadhi au sauti,
hivyo bahari hii hukusanya washairi wote wenye kufuata mahadhi ya kigeni.
kazi nzuri
JibuFutajaribuni kujitangaza zaidi kazi yenu sio ndogo katika mchango wa kiswahili
JibuFutaKama mshairi mchanga, nayatazama maelezo haya kwa upeo wa thamani ya juu kwani elimu iliyojificha ndanimwe ni urithi wa kudumu.
JibuFutaNashukuru sana nimeendelea kupata maarifa zaidi kuhusu uainishaji wa ushairi hasa ule wa kiswahili!
JibuFutaIko pOa sana endeleeni nakazi nzuri yakuelimisha jamii
JibuFutaIko pOa sana endeleeni nakazi nzuri yakuelimisha jamii
JibuFutaKazi nzuri
JibuFutaIko vizuri sana
JibuFutaIko vizuri sana
JibuFutaVitawe
JibuFutaAina ya majina ya vitawe
JibuFutaKuna aina ya mashairi hayatolewa mifano kama kimai
JibuFuta