MIGOGORO KATIKA TAMTHILIYA YA KISWAHILI
Katika kazi hii,
Istilahi ya tamthiliya itaelezwa, kisha
dhana ya tamthiliya itajadiliwa, historia fupi ya tamthiliya kwa jumla itaongelewa, historia fupi ya
tamthiliya ya Kiswahili, mikondo ya tamthiliya kwa jumla, mikondo ya tamthiliya
ya Kiswahili, migogoro katika tamthiliya ya Kiswahili na hatimaye hitimisho.
Tamthiliya ni moja kati ya Tanzu tatu kubwa na muhimu za fasihi. Tanzu nyingine za fasihi ni Ushairi na Riwaya. Tanzu hizi huingiliana. Kwa jumla tofauti kati ya tanzu hizi zimeambatana na malengo na maumbo yake. Mtunzi wa tamthiliya husawiri mawazo kwa maongezi ya wahusika na kwa kujenga migongano na mijadala baina ya wahusika hao. Mshairi hutimia lugha inayonata, lugha inayojirejelea, kwa kufanya hivyo, Mshairi huelezea mapana kwa maneno machache. Mwandishi wa riwaya hujieleza kwa njia ya hadithi hasa akizingatia matukio wanayoyapata wahusika wake.
Dhana hukanganya kwa sababu imeingiliana sana na dhana nyingine kama drama, uigizaji na sanaa ya utendaji. Kama wataalam mbalimbali wanavyofafanua dhana tamthiliya kama ifuatavyo:
Istilahi “tamthiliya” inatokana na neno “mithali” ambalo lina maana ya “mfano” au ishara ya kitu Fulani. Hivyo katika tamthilya kitu kimoja humithilishwa au huwakilishwa na kitu kingine. Mathalani, katikamchezo wa Kinjeketile, mwigizaji wa sehemu ya “Kinjeketile” huwakilisha mhusika aitwaye Kinjeketile katika mchezo. Hivyo mhusika huyo himithilisha, kwa kiasi Fulani, Kinjeketile wa historia. M.M.Mulokozi,(1996).
Dhana tamthiliya
imejadiliwa na wataalam wengi kama ifuatavyo:
Mlama, P(1993:203) anaeleza kuwa tamthiliya ni sanaa ya maonyesho, sanaa ambayo huwasilishwa, ana kwa ana, tukio Fulani kwa hadhira kwa kutumia usanii wa kiutendaji. Kwa mfano, badala ya kuwasilisha wazo kwa hadhira kwa kutumia maneno kama katika ushairi, sanaa za maonyesho hiliweka wazo lile katika hali ya tukio linaloweza kutendeka kwa kutumia usanii wa utendaji kama vile vitendo, uchezaji n.k.
Cuddon,(1979:512) kama alivyonukuliwa na Said A.Mohamed, (1995:59) anaeleza: Tamthiliya ni kazi ya utendaji ambayo hutazamiwa kuonyeshwa jukwaani au redioni au kwenye televisheni, na ambayo matendo yake hufanywa na watendaji wa kike na kiume.
Mulokozi,(1996:188) anafafanua, tamthiliya au drama ni fani ya fasihi iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira Fulani. Hivyo, lugha ya kawaida, tamthiliya huitwa mchezo wa kuigiza. Tamthiliya huwa na masimulizi ambayo huigizwa na wahusika wa pande mbili au zaidi zinazogongana. Mgogoro huo hatimaye huishia katika mgogoro ambao unaposuluhishwa au kutatuliwa, mchezo huwa umemalizika.
TUKI(2004) nao wanafasili tamthiliya: Ni utungo wa kisanaa ambao huweka wazo Fulani katika matendo na mazungumzo.
Mazrui na Syambo, (1992) wanaelezea tamthiliya: Ni utungo wa fasihi ambao umebuniwa kwa kiasi kikubwa. Kutokana na fasili mbalimbali za tamthiliya, tunaweza kusema kwamba tamthiliya ni aina mojawapo ya sanaa za maonyesho ambayo usanii wa utendaji kama vile ngoma ambazo hutegemea zaidi uchezaji ngoma na upigaji mziki. Tamthiliya ni ule utungo unaweza kuwa umeandikwa au haukuandikwa unaoliweka wazo lilowasilishwa katika umbo la tukio au kuliwezesha kutendeka mbele ya hadhira.
Mhando na Balisidya (1976:83) anasisitiza maelezo hapo kwa kusema : “kigezo kikuu cha tamthiliya ni kuweza kuwasilishwa jukwaani na kutazamwa na hadhira. Tamthiliya huwa na sifa za maonyesho”.
CHIMBUKO LA TAMTHILIYA NA MAENDELEO YAKE KWA UJMLA.
Tamthiliya hupatikana, katika sura mbalimbali duniani kote. Chimbuko lake katika nchi na tamaduni mbalimbali hushabihiana kwa kiasi Fulani kwa vile huhushishwa na visakale na matendo ya kidini.
Tamthiliya ya Ulaya, ambayo ndiyo imeathili zaidi tamthiliya ya Kiswahili, yasemekana kuwa ilitokana na Miviga(rituals) na viviga(rite), hasa ya kidini, katika jamii ya kale ya
Wayunani. Miviga hiyo iliambatana na dura za kuzaliwa, kukua, kufa, kuoza na kuzaliwa upya ambazo hasa zilihusishwa na Mungu aliyeitwa Dionizi, aliyeaminiwa kuwa aliuawa, akakatwakatwa vipande vipande na baadaye akafufuka tena. Brockett, (1979:4) kama ilivyonukiliwa na Mulokozi, M.M.(1996:190).
Afrika, kumbukumbu za kwanza za maigizo ya kitamthiliya zinapatikana Misri,ambako michezo ya miviga iliyohusu kufa na kufufuka kwa mungu na Wamisri walioitwa Osiris ili kuwa ikigizwa kila mwaka kwa miaka kama 2000 kuanzia mwaka 2500 k.m. Brockett,(1979:4) kama ilivyonukuliwa na Mulokozi,M.M.(1996:190).
Huko India, inasemekana drama (tamthiliya) ilitokana na tendi za kidini Mahabhorata na Ramayana, pamoja na miviga iliyofungamana na utendaji wa tendi hizo katika mahekalu ya Kihindu(EA 1982:333; Brockett,1979:240) kama ilivyodondolewa na Mulokozi,M.M. 1996:190). Baadaye drama hizo zilijitenga na udini na kujishughulisha zaidi na masuala ya sanaa na burudani.
Pia huko China, drama ilitokana na sherehe za kidini zilizotendwa na makuhani wa Kibudha kwa kutumia nyimbo, dansa na maigizo bubu.Michezo YA Kichina ni kama vile ya Kijapani, iilkuwa ni faraguzi,hapakuwa na muswada wa mchezo mzima, bali palikuwa na muhtasari tu ambao ulijaziwa na waigizaji wenyewe wakati wa maonyesho. Michezo hiyo ilijitenga na uhalisia, walitumia lafudhi, mavazi na ishara zilizotiwa chumvi makusudi ili kuleta ukengeushi.
Nchini India, palikuwa na drama ya Ki-sangkirt tqngu miaka 200 K.M. Drama hiyo, ilishabihi tendi za kidini za kihindi, daima ilkuwa na lengo la kuleta suluhu au mapatano. Hivyo hapakuwa na tanzia, bali tamthiliya hizo ziliishia kwenye furaha.
Maelezo haya
yanatudhihirishia kuwa huenda tamthiliya duniani ilichipuka kutokana na mambo
matatu ambayo ni:
i) Miviga na viviga vya kijamii na kidini, pamoja na tendi.
ii)
Umathilishaji wa maisha ya kawaida kwa
ajili ya burudani, elimu, maonyo au michezo
iii) Sanaa za maonyesho za kijadi, kwa mfano, ngoma na dansa.
Ingawa asili ya
tamthiliya katika nchi na tamaduni mbalimbali yaelekea kufanana,lakini
maendeleo yake yalichukua mikondo tofauti kutegemeana na historia na utamaduni
wa jamii inayohusika. Kwa mfano, huko Uyunani(ugiriki),yaelekea tamthiliya za
mwanzo zilianza kuandikwa kabla ya mwaka 500K.M. Wayunani walizagawa tamthiliya
katika makundi makuu mawili: Tanzia ambao ni drama juu ya mkasa unamsibu mtu
mashuhuri kutokana na matukio ambayo mara nyingi hana uwezo nayo, na ambayo
yanatokana na udhaifu Fulani alionao na huishia katika majonzi, na komedia ni
drama inayokusudiwa kufurahisha, ambayo zaidi iliwahusu watu wa kawaida, na
aghalabu humalizikia katika furaha badala ya majonzi. Kwa mfano tamthiliya
zilizotungwa na Shakespeare ambazo zilitafsiriwa kwa Kiswahili na Hayati Mwalimu
Julius K.Nyerere ni Julias Kaisari (1964), Mabepari wa Venisi (1969).
Kimsingi kuna aina kadhaa za tamthiliya. Kila aina ina sifa zake maalum. Tunaweza kuvitumia vigezo vya muda(duration) na utanzu(genre) kuigawa tamthiliya katika aina mbalimbali.
Kwa mujibu wa kigezo cha muda, kuna tamthiliya ambazo huwa na tendo moja na huchukua muda mfupi. Kwa mfano tamthiliya ya Samuel Beckett iitwayo “Breath” inachukua dakika moja ili hali “maisha ya subira” iliyoandikwa na Omari, S. itachukua muda mrefu kuigiza.
Kigezo cha muda
hutegemea wakati ilihali cha utanzu hutegemea yaliyomo(maudhui) au mada ya
tamthiliya kutokana na kigezo hiki cha pili tunaweza kuainisha vitanzu
vifuatavyo:
a)
Tanzia (tragegy)
b)
Futuhi /komedia (comedy)- “usaliti
mjini” F. Mbugi
c)
Melodrama (melodrama) - “The Begger’s Opera” John Gay, 1728
d)
Kichekesho (Farce)
e)
Tanzia- ramsa/ Tanzia-
futuhi(tragicomedy)
f)
Tamthiliya ya kihistoria(Historical
play) – Kinjeketile- E. Hussein
g)
Tamthiliya Tatizo(problem play) – mfano,
nguzo mama
na lina ubani(Penina .M Mhando; Mashetani- E. Husein.
h)
Tamthiliya ya kibwege (absurd drama)- mfano, Amezidi(said .A. Mohamed,1995), Upotovu- (Njiru Kimunyi,2000)
Maelezo hapo juu
yanaonyesha kuwa zipo aina nyingi za tamthiliya diniani. Tamthiliya ya Ki-
Aristotle ni aina mojawapo kati ya hizo. Hapa tutaijadili kwa kirefu zaidi kwa
kuwa imeathiri watunzi wengi wa tamthiliya ya Kiswahili. Mulokozi
,M.M.(1996:193), Kwa mujibu wa Ki- Aristotle, tamthiliya yoyote kwa kawaida
huwa na vipengele vifuatavyo:- Hadithi(simulio), vitendo, waigizaji wanaomathilisha wahusika wa hadithi, dialogia(mazungumzo). Mazungumzo huweza kuwa ya maneno au ishara.
i)
Hadithi.
Tamthiliya
husimulia hadithi au kisa Fulani. Hadithi hiyo huweza kuwa ya kubuni, au ni tukio la kweli la historia, au ni mchanganyiko wa yote mawili. Hadithi hiyo kwa kawaida huhusu mzozo Fulani unaohusisha pande mbili. Upande wa shujaa(mbabe) au nguli ambaye ni mtendaji mkuu na upande wa mpinzani wa nguli/ mbabe. Hadithi
hiyo husukwa kwa namna inayojenga migogoro wa pande hizo mbili hadi mwisho
wake. Mlokozi,M.M.(1996:193)
Pia
katika jadi ya utunzi wa Ki- Aristotle, mtiririko wa kimatukio kwa kawaida huwa umbo la piramidi lenye hatua zifuatazo:-
C
B
D
A
------------------------------------------------------------ E
Hatua A: Chanzo
Hapa ndiyo mwanzo/utangulizi wa mchezo
katika hatua hii:
-
Hali ya tamthiliya (ya majonzi, ya
miujiza, ya nderemo) hudhihirishwa.
-
Mandhari9yaani wakati na mahali
panapotokea vitendo vya hadithi) hueleza
-
Baadhi ya wahusika hutambulishwa
-
Taarifa nyingine muhimu (kwa mfano
matukio yaliyotangulia kisa hiki) hudokezwa
Hatua B: Tatizo / kukua kwa mgogoro
Mvotano kati ya pande mbili au zaidi
zinazozozana hujitokeza. Tatizo linalosababisha mgogoro huo hudhihirishwa.
Majaribio ya kutanzua mgogoro hufanywa na kushindwa. Kila hatua muhimu katika
ukuaji wa mgogoro huo huitwa kipeo(turning point), vipeo kadhaa vidogo huweza
kufikiwa kukiukwa bila usuluhishi.\
Hatua C: Kilele
Mantiki ya mvutano na matukio
hatimaye hufikisha hadithi kwenye kilele(climax) katika hatua hii mzozo hufikia
kiwango cha juu kabisa pasi na uwezekano wa kurudi nyuma.
Hatua D: Mshuko
Katika hatua hii mvotano huanza
kulegea na hutokea mshuko wa taharuki. Mgogoro huwaelekeza wahusika kwenye pambano
la mwisho la mkataa.
Hatua E: Mkasa/ suluhisho
Katika kipengele hiki, kama tamthiliya niya kitanzia, mbabe/nguli hushindwa ama kupatwa na mauti ama maanguko, na mgogoro hufikia hatima yake. Na kama tamthiliya ni komedia, mvotano baina ya pande zinazozozana husuluhishwa na hali ya utangamano hurejeshwa.
ii) Vitendo
Tamthiliya nyingi za
Ki- Aristotle hugawanyika katika sehemu ziitwazo vitendo(act) kila kitendo
huzingatia tendo moja kuu ndani ya mchezo. Kwa mfano:- katika mpangilio wa
matukio hapo juu, kila kipengele kingeweza kuwa kitendo kimoja. Hivyo
tamthiliya yenye mpangilio huo kijadi iltakiwa kuwa na vitendo vitano.
Onyesho(scene)
Kila kitendo
hugawanyika katika sehemu ndogo ziitwazo maonyesho. Onyesho (scene)moja kwa
kawaida huwasilishwa tukio moja linalotendeka mahali pamoja. Kwa kawaida
onyesho moja hutenganishwa na jingine kwa kuzingatia mantiki ya kile
kinachosimuliwa, tukio moja likimalizika onyesho nalo huwa limemalizika. Wakati
wa maigizo jukwaani mabadiliko ya maonyesho huashiria kwa kufunga pazia au
kuzima taa, au kwa wahusika kuondoka jukwaani.
iii) wahusika na waigizaji
Usawili wa wahusika wa
tamthiliya hufanywa kwa njia ya matendo, kwani fursa ya kutoa maelezo marefu
haipo. Wahusika wa tamthiliya hawana tofauti na wahusika wa hadithi, huweza
kuwa mviringo, bapa, watu wa tabaka la juu, wanyonge, n.k. Pia huwa na wahusika
wakuu na wadogo.
Wahusika wakuu
Nguli /mbabe: Shujaa wa
tamthiliya ambaye matendo mengi yanahusu maisha na majaliwa yake, kwa mfano,
Kinjeketile katika tamthiliya ya Kinjeketile –Hussein,E. (1969), Ndiye nguli
/mbabe (hero) yaani mhusika kiini alikuwa ni mtu wa tabaka la juu ambaye
aliangamia kutokana na ama ila fulani katika tabia au maamuzi yake –( tragic
flow) kwa sababu ya kusukumwa na mazingira yanayomzidi uwezo.
Wahusika wadogo
Hawa anghalabu huwa ni
wengi, baadhi yao huwa na jukumu dogo tu katika tamthiliya na hutokea mara
chache.
Waigizaji
Mara nyingine huitwa
wamathali. Hutokea jukwaani mahali pa wahusika wa mchezo na kuiga vitendo na
tabia za hao wahusika wanaowawakilisha.
iv) Dialogia (mazungumzo ya wahusika)
Tamthiliya husonga
mbele kwa njia ya vitendo na mazungumzo ya wahusika. Baadhi ya tamthiliya huwa
na monolojia, mhusika huzungumza mwenyewe kudhihirisha mawazo aliyonayo moyoni.
Zipo tamthiliya zinazotumia masimulizi, ambapo hutokea msimulizi na kueleza mambo
yaliyotokea, mithili ya mtambaji wa hadithi au utendi. Mbinu hii hutumika
katika drama- tendi. Baadhi ya tamthiliya za Kiswahili zimefuata mbinu hiyo ya
Ki- Aristotle kwa mfano: Mulokozi,M. Mukava wa Uhehe, (1979).
Historia
ya Tamthiliya ya Tanzania.
Kabla ya kuja kwa
Ukoloni tamthiliya haikuwepo nchini. Aina za sanaa za maonyesho zilizokuwepo
zilitofautiana na tamthiliya hii iliyoingizwa na tamaduni ngeni. Chuo kikuu
huria cha Tanzania (1997:39).
Bertoncini,1989, kama
ilivyodondolewa na Wafula,Richard,(1999:3) anafafanua kuwa: Tamthiliya kama
utanzu wa fasihi- andishi katika lugha ya Kiswahili imeanza kushughulikiwa juzu
juzi, mchezo wa kuigiza ulioandikwa ulikuja na wakoloni. Mgeni aliyejihusisha
na uigizaji hapo mwanzomwanzo aliitwa Graham Hyslop mnamo mwaka 1936 alitunga
filamu iliyoitwa, “Akili ni mali”
Tamthiliya ilianza Tanzania wakati wa Ukoloni miaka ya 1920, tamthiliya hizo
zilizo nyingi zilikuwa za kidini.
Tamthiliya zilizoandikwa ili zigezwe jukwaani hazikuwepo kabla ya Ukoloni. Badala yake, zilikuwepo tamthiliya zisizoandikwa, ziligezwa au kufaraguzwa kwa ajili ya kuonyeshwa kwenye shughuli maalum, kwa mfano, kwenye sherehe za jando na unyago, mazishi, kutawazwa kuwa mtemi, arusi na michezo ya watoto. Tamthiliya hizo zilikuwa na sifa kadhaa za kitamthiliya, yaani hadithi, vitendo, wahusika, na waigizajiwao na dialogia. Kadhalika zilkuwepo na sifa saba za sanaa za maonyesho, nazo ni:
i) Dhana inayotendeka v) hadhira
ii) Uwanja
unaotendewa vi) kusudio la
kisanii
iii) Watendaji vii) muktadha wa
kisanaa
iv) Ubunifu (umathilishaji)
Muhando Mlama na Balisidya 1976:4 na Mlokozi, M . M.(1996:189).
Tamthiliya hizo
hazikuwa na ploti ya Ki- Aristotle wala matini yaliyoandikwa. Hivyo zilikuwa ni
tamthiliya – simulizi. Mulokozi, M.M.(1996:203).
Anaendelea kudondoa kwa
kutolea mfano michezo ya watoto katika kuigiza , umama, mtoto wa kike au
wakiume n.k. Mchezo huu ni tamthiliya halisi
yenye kumathilisha maisha.
Tamthiliya
andishi ya Kiswahili
Tamthiliya za Kiswahili
zilizoandikwa kwanza kabla ya kuigizwa jukwaanizilianza kutokea miaka ya
1950. Tamthiliya za mwanzo zilikuwa za
kidini. Kwa mfano, ilichapishwa tamthiliya ya Frank, C.(1951) iliyoitwa “Imekwisha” (Mulokozi,M.M. 1992:205).
Tamthiliya za mwanzo zisizokuwa za kidini zilianza kutungwa kati ya 1952 na 1956. Shughuli za tamthiliya wakati huo zilisimamiwa na Graham Hyslop, Mwingereza aliyekuwa katika utumishi wa serikali ya kikoloni ya Kenya. Pia alianzisha kikundi cha maigizo kwa ajili ya askari mwaka 1944, na miaka ya 1950 alianza kutunga michezo ambayo iliigizwa na kikundi chake. Michezo ya mwanzo katika lugha ya Kiswahili ni “Afadhali Mchawi” (1957), na “Mgeni Karibu” (1957), hata hivyo Hyslop alianza kuzunguka katika shule na vyuo mbalimbali nchini Kenya akifundisha muziki na uigizaji.
Miongoni mwa wanafunzi
wa mwanzo wa Hyslop waliokuwa wakisoma “Alliance high school” ni Henry Kuria,
Kimani Nyake, Gerishon Ngugi na B.M.Kurutu. Tamthiliya ya Kuria, ‘Nakupenda Lakini’ (1954) iliigizwa kwa
mara ya kwanza 1957, ya Nyake , ‘Maisha
ni Nini’ iliigizwa mwaka 1955, ya Gerishon Ngugi, ‘Nimelogwa nisiwe na Mpenzi’(1961) iliigizwa mwaka 1956, na ya Kurutu ‘Anatakiwa
Polisi’ mwaka 1957, kwa mujibu wa Ngugi wa Thiong’o(1981:39) kama
ilivyodondolewa na Mulokozi,M.M. (1996:205).
Kwa ujumla tulipopata uhuru, tamthiliya zote za Kiswahili zilizochapishwa zilikuwa zimeandikwa na Wakenya. Watanzania hawakujitokeza katika uwanja huu hadi baada ya uhuru. Kwa mujibu wa Mulokozi,M.M.(1996:205).
TAMTHILYA
WAKATI WA UHURU
Tamthilya ya kizungu
iliendelea kuigizwa hata baada ya uhuru, mashuleni na katika kumbi maalum za
maonyesho kama ‘Little Theatres’. Hata hivyo, umaarufu wake ulipungua kiasi,
hususan kwa upande wa Tanzania. Mulokozi, M.M.(1996:207)
Anaendelea kufafanua,
licha ya tamthiliya za kizungu, hali kadhalika tamthiliya za kiafrika zilianza
kuandikwa kwa lugha za Kigeni na zingine za kiafrika, zilifasiriwa kwa
Kiswahili, kwa mfano, “I will marry when
I want” (1982) ilifasiriwa kwa Kiswahili, “Nitaolewa nikipenda” (1982) na Ngugi wa Thiong’o na Ngugi wa Mirii.
Watanzania waliathiriwa sana katika masuala ya sanaa za maonyesho za kigeni kiasi kwamba waliweza kujishirikisha kikamilifu katika kutunga tamthiliya na kuzionyosha majukwaani. Tamthilya hizi hazikuwa na maana yenye uzito wowote kwa tamaduni zao. Tamthiliya hizo ziliongelea juu ya jamii ambayo watanzania hawakuifahamu wala kuielewa wao walivutiwa na mavazi ya washiriki, matumizi ya taa za rangi na kadhalika,
Mlama, P.(1987:119) vol.54/2 jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili .
Mlama , P.(1987:119-
120) anasisitiza, kutokana na tamthiliya za kimagharibi kutokidhi mahitaji ya
watanzania ndipo ilipowapelekea wasanii hao kuanzisha vichekesho.
Mlama, P.M.katika
makala ya semina ya kimataifa ya uandishi wa Kiswahili iii,(1983:206- 207),
afafanua kuwa drama ililetwa Tanzania na Waingereza. Drama iliigizwa mashuleni
ambapo wengi wa walimu walikuwa Waingereza. Madhumuni ya kuigiza drama haikuwa
na uzito mkubwa. Hasa Waingereza
walikuwa na kitu cha kupitisha muda, wakati ambapo walikuwa hawna la kufanya.
Waliona kuendesha drama kwao ni jambo borakwani ilihusu utamaduni wa kwao na
kuweza kujikumbusha kwao. Kwa mfano tamthiliya za William Shakespeare, Julius
Ceasar, Macbeth, n.k. hazikuwa na maana muhimu kwa watanzania kwani
walioshiriki walikuwa wanakariri tu maneno bila kuelewa yale waliyoyasema, mara
nyingi tamthiliya hizi zilikuwa na lengo la kuburudisha tu.
Mlama , naendelea wakati drama hii ya kigeni ilpoendelea kushika mizizi chini ya udhamini wa wazungu. Iliibuka aina nyingine ya drama, hii ni ile ijulikanayo kama, “vichekesho”hii ilitokea kwasababu watanzania ambao walivutiwa kutumia vipaji vyao vya kisanaa kuonyesha tamthiliya, lakini hawakuwa na ujuzi wa ndani wala iwezo wa utunzi na uonyeshaji wa tamthiliya kiasi cha kutoa kazi sawa na zile za wataalam wa
Kiingereza. Badala yake walianzisha kitu kinachofanana na tamthiliya lakini ambacho waliweza kutunga na kuonyesha kutokana na uwezo wao wenyewe. Juhudi zao zilitoa aina ya drama iliyojulikana kama “vichekesho”.
Hii haina maana kuwa vichekesho vilikuwa duni kuliko drama ya wageni. Bali vichekesho vilitoa drama iliyokuwa na tabia kisanaa tofauti na drama yenyewe. Kwa mfano, vichekesho havikutegemea tamthiliya ilyoandikwa bali, tungo zake zilitungwa palepale wakati wa kutenda, vichekesho vilihusu maisha ya kawaida ya Tanzania ya wakati ule, wakati ile drama nyingine ilihusu jamii za Ulaya. Mfano wa kichekesho cha wakati huo ni “Mshamba wa Kioo”
Baada ya uhuru vichekesho vilichukua sura tofauti kidogo. Badala ya kuwasuta “washamba” vilianza kuwasuta “wazungu weusi” Waafrika wanaoringia elimu au vyeo vyao na kudharau utamaduni wao. Kwa mfano, G. Uhinga, 1968, pia viliongelea masuala mbalimbali kwa mfano , matatizo ya kifamilia, ukosefu wa kazi, ukimwi, uhalifu na udanganyifu waganga wa jadi n.k.M.M.Mulokozi(1996:206)
Naye Lihamba,(1985:281)
kama alivyodondolewa na M.M. Mlokozi(1996:206) anasisitiza; vipo vichekesho vya
kisiasa vyenye kuzungumzia siasa ujamaa, ubinafsi wa uongozi, matatizo ya
kuanzisha vijiji vipya n.k. Anaendelea kusisitiza,
“Beside
their informality and flexibility, these plays have two major Other
characteristics: they have displayed a strong alignment with the political and
social issues after Arusha and have a strong comedic bias. The tendency to favour comedic elements or
play for laugh has endowed. The plays
with the collective name of vichekesho.
This has been irrespective of the nature of the content and the
performance objectives.”
Tafsiri:
Hata hivyo baadhi ya
vichekesho vya Radio Tanzania, kwa mfano,
“mahoka” kipindi kilichoanza mwaka 1974 na “pwagu na pwaguzi” mwaka 1979
hukejeli na kukemea tabia mbovu za baadhi ya watu, wakiwemo viongozi wa
kisiasa. Tasnifu ya Lihamba(1985) imeonyesha kuwa baada ya Azimio la Arusha
nchini Tanzania vikundi vya ngoma na maigizo kama ishirini na nane(28) mara kwa
mara vilionyesha maigizo yaliyohusu siasa.
Baadhi ya maigizo hayo yalitukuza siasa ya ujamaa na kutangaza kampeni mbalimbali za wanasiasa. Lihamba, (1985:498- 502). Hata hivyo kwa sasa vichekesho hutangazwa katika vituo vya redio na televisheni, na huonyeshwa kwenye kumbi za starehe.
Baadhi ya maigizo hayo yalitukuza siasa ya ujamaa na kutangaza kampeni mbalimbali za wanasiasa. Lihamba, (1985:498- 502). Hata hivyo kwa sasa vichekesho hutangazwa katika vituo vya redio na televisheni, na huonyeshwa kwenye kumbi za starehe.
Baada ya uhuru, utunzi wa tamthiliya ulipamba moto zaidi, hasa upande wa Tanzania. Mashindano ya utunzi na uigizaji yaliendeshwa na Youth Drama Association nchini Tanzania yaliwawezesha watunzi chipukizi kujitokeza, akiwemo Ebrahim Hussein ambaye tamthiliya yake ya kwanza , “wakati ukuta” 1969 ilishinda tuzo katika mashindano hayo. Wakati huo huo ndipo walipojitokeza watunzi waliohitimu chuo kikuu cha Dar es Salaam. Baadhi yao ni Ebrahim Hussein mwenyewe, Penina Mhando(Mlama), N.Ngahyoma na G. Uhinga.
Miaka ya 1970- 1974 ilishuhudia kuchapishwa kwa tamthiliya nyingi za Kiswahili. E.Hussein alichapisha, Kinjeketile(1969), Mashetani(1971), Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi(1976), Arusi(1980) na Ukingo wa Thim(1989).
Penina Mhando,
alichapisha “Hatia”(1972), Tambueni Haki Zetu(1973), Pambo(1975), Nguzo
mama(1982), Lina Ubani(1984); Pia watunzi wengine waliojitokeza kipindi hiki ni
Emmanuel Mbogo, “Giza Limeingia”(1980), Tone la mwisho,(1981), Ngoma ya
Ngwanamalundi(1988), Morani, (1993); watunzi wengine ni M. M. Mlokozi, S.A.
Mohamed, E. Semsaba na E. Kezilahabi.
Orodha hii ya watunzi inatosha kueleza kuwa utunzi wa tamthiliya ya Kiswahili umepiga hatua kubwa tangu mwaka 1970. Kimaudhui tamthiliya hizo zilianza kusawiri mazingira ya waswahili kwani kwa kuchunguza suala la maudhui tunaweza kuzigawa tamthiliya za Kiswahili za miaka ya 1960- 1994 katika migogoro kama ifutavyo:
Kuna migogoro ya
kitamaduni: Dhamira hii inajitokeza katika umbo la mgongano wa utamaduni wa kijadi na kiafrika na utamaduni
wa kizungu au kati ya mjini na shamba, dhamira hii imejadiliwa zaidi katika
baadhi ya kazi za E,Hussein, wakati ukuta na kwenye ukingo wa thim.
Pia matatizo ya kijamii kwa mfano, mapenzi, ndoa, ufukara, urithi, n.k, vimejadiliwa zaidi katika tamthiliya ya, Nakupenda Lakini na Nimelogwa nisiwe na Mpenzi.
Si hizi tu bali wasanii
wa tamthiliya wa kipindi hiki waliangalia jamii jinsi inavyoishi na kuweza
kutunga kazi zao kusawiri mazingira husika. Kwa mfano maudhui katika tamthiliya
yalikuwa pia; ukombozi na utaifa, ujenzi wa jamii mpya, mfano tamthiliya ya E.
Mbogo, Giza Limeingia, na E. Hussein, Mashetani. Mwanamke na matatizo ya
kijinsia mfano Nguzo Mama(Mhando), Machozi ya Mwanamke(Ngozi), na falsafa ya
maisha mfano E.Kezilahabi.
Katika kazi hii si lengo la mwandishi kueleza historia ya tamthiliya pekee bali sasa tulejee katika swali la msingi ambalo ni mgogoro katika tamthiliya ya Kiswahili. Tamthiliya yakiswahili hasa zile zilizoandikwa, baadhi yake zximejaa mbinu za Kimagharibi. Nyingi zina muundo wa Ki- Aristotle, zinatumia dialogia, zina vitendo, maonyesho na migogoro inayosuluhishwa mwishoni; M.M. Mlokozi,(1996:197).
Aristotle ni
mwanafalsafa wa Kiyunani aliyeishi Uyunani(Ugriki ya kale) kati ya mwaka 386 na
322 kabla ya kristo. Baada ya maandishi yake, maandishi ambayo yamekuwa na
athari kubwa katika maendeleo ya taaluma za Ulaya kwa karne nyingi ni kitabu
chake juu ya, “sanaa ya utunzi” alichokiita “Poetics’ambamo anafafanua sheria
au kanuni za utunzi wa tamthiliya,ambazo kwa muda mrefu sana zilichukuliwa na
wanasanaa wengi wa michezo ya kuigiza kama mwongozo karibu kote Ulaya. Ebrahim
Hussein kama alivyodondolewa na makala za semina ya kimataifa ya maandishi ya
Kiswahili,(1983;197).
Anaendelea kusisitiza, Myunani huyu anatambua vipengele sita; sehemu ya nyimbo, matamshi, mtiririko wa vitendo, wahusika, fikra na utumiaji wa jukwaa. Pia anaona umuhimu kuwa mchezo huu ni wa kufurahisha na kuchekesha au ni wa kuhuzunisha na kuleta majonzi.
Vile vile baada ya kutambua vipengele sita hivyo, Aristotle anaugawanya mchezo wa Kiyunani katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni ile ya mwanzo au utangulizi, sehemu ya pili ni kitendo chenyewe. Anapendelea wimbo uimbwe katika sehemu ya mwisho. Lakini waandishi wengi wa michezo ya kuigiza karne na karne hawakufuata mapendekezo haya. Kwa mfano Shakespeare katika mchezo wake wa “Mfalme Lear” anamfanya kichaa aimbe mara nyingi. Pia Ngugi wa Thiong’o katika mchezo wake wa, “Dedan Kimathi” anatumia nyimbo hata mwanzoni mwa mchezo.
Aristitle alipendelea kuwa mwandishi mchezo wa kuigiza ayafahamu mambo haya ni kuandika matamshi katika umbo lenye mizani.Said A.Mohamed (1995;59).
Anaendelea kufafanua,
lakini si waandishi wengi wa tamthiliya wanatumia lugha ya kishairi na yenye
mizani katika michezo yao. Kwa mfano; Soyinka katika mchezo wake wa “wale wanaoishi kwenye mabwawa” yeye hatumii
ushairi; au Penina Muhando katika mchezo wa “Pambo” yeye pia hatumii lugha ya
kishairi na yenye mizani. Na Zola yeye anapinga kabisa utumizi wa lugha ya
kishairi katika mchezo wa kuigiza. Zola anaungwa mkono katika hili na waandishi
wengi kwa mfano Ibsen na wengine. Wao wanaunga mkono utumiaji wa mazungumzo ya
kitamthiliya (yaani- dramatic dialogue).
Ebrahim Hussein katika makala
za semina ya kimataifa ya waandishi wa Kiswahili, 1983:202- 203 anafafanua;
Wasanii wengi hawakubaliani nayo nadharia ya Aristotle inayosisitiza mpangilio
huo wa mtiririko wa vitendo,hasa vile kuwa unasisitiza kilele na unasiositiza
kwamba kitendo kinachopaswa kuigizwa ni kile chenye kutia hofu na huruma
moyoni.
Brecht, anaona kwamba Aristotle amempa mwandishi au mwigizaji wa tamthiliya nafasi nyembamba. Mila nyingi za uigizaji, kwa mfano mila za kiafrika , kijapani na kihindi hazikubaliani na hizo njia nyembamba. Lewis Nkosi anasema, dhahiri uandishi namna hii yaani unaofuata misingi ya Aristotle, haswa huu wa mpangilio wa mtiririko na vitendo unakwenda dhidi ya mila za kishairi katika Afrika.
Hivyo basi, kuandika tamthiliya kwa kufuata misingi ya Ki-Aristotle ni njia moja ya kuandika tamthiliya, lakini hiisi njia pekee. Na kweli mila ya kiafrika haiowani vizuri na usanifu huu. Pengine njia isiyokuwa ya Aristotle ni muafaka zaidi, hata hivyo ikiwa mwandishi atatumia misingi ya Aristotle au baadhi ya misingi hiyo, jambo muhimu ni kuweka akilini kwamba misingi hii si sheria ila ni vipengele vya tamthiliya. Sheria Kama ipo ni moja tu, kujua nini watu wanapenda kuona na kusikia jukwaani kwa kuangalia ujumi wa wakati husika. Ni vizuri mwandishi wa mchezo wa kuigiza kuwanayo sheria hii kichwani wakati anapoandika mchezo wa kuigiza. Maelezo hayo hapo juu yanaungwa mkono na P. Mlama, alivyodondolewa na makala za semina ya kimataifa ya waandishi wa Kiswahili, 1983:216.
Tutazame kwa kifupi ni vipengele gani muhimu katika utunzi wa tamthiliya. Lakini ieleweke wazi kuwa nia si kutoa fomula inayofaa kutumiwa katika utunzi wa tamthiliya, utunzi wa sanaa hauwezi kuwekewa fomula kwasababu msanii anapotoa kazi ya sanaa anunda kitu kipya na kutokana na kipaji chake cha kisanii wakati anaunda kitu hiki anaweza anaweza kuunda mbinu mpya pale ambapo zile zinazojulikana hazimwezeshi kukamilisha kile anachokiunda. Misukumo inayotokana na mabadiliko mbalimbali katika jamii ya wakati wake humlazimisha msanii kutumia mbinu mpya tofauti na zawaliotangulia. Na kwamba msanii anayeridhika na mbinu zilizopo anadhihirisha upungufu wa uwezo wake wa kisanii.
Pia M.M.Mlokozi, (1996:210- 211) anafafanua kuwa watunzi wachache kuanzia miaka ya 1970, hawakuridhika na upokeaji wa mbinu na kanuni za tamthiliya ya ulaya, hasa ya Ki-A ristotle, walihisi kuwa palihitajika tamthiliya ya kiafrika yenye kuchota mbinu zake kutokana na sanaa za jadi za kiafrika. Hivyo watunzi hao walianzisha maigizo ya kimajaribio.
Miongoni wanamajaribio
hao wa mwanzo ni Ebrahim Hussein. Mtunzi huyu alijaribu kutumia mbinu za
utambaji wa ngano katika maigizo yake ya
Ngao ya jadi na Jogoo kijijini.
Penina Mhando pia, katika tamthiliya zake za “Lina Ubani, na Nguzo Mama”pia alijaribu kutumia mbinu ya utambaji wa ngano.
P .O. Mlama, kama
alivyonukuliwa na makala za semina ya kimataifa ya waandishi wa
Kiswahili,(1983:215) ansisitiza; Baadaye utanzania uliweza kuonekana zaidi
katika fani wakati watunzi walipojaribu kutumia vipengele Fulani Fulani vya
fani za sanaa za maonyesho zenye asili ya Tanzania katika kuandika tamthiliya
hizo. Majaribio haya ni kama ya kutumia nyimbo, utambaji hadithi, majigambo
katika utunzi wa tamthiliya kwa mfano katika ‘Tiba’, (Nkwera,1969), Pambo(Mhando,1975),
Harakati za Ukombozi (Lihamba na Balisidya, Matteru,1978), Kinjeketile(Hussein,
1969) n.k. Majaribio hayo yameleta upya katika fani ya tamthiliya ambayo
iltegemea zaidi usanii wa vitendo na usemaji tu.
Kwa kuhitimisha kazi
hii mwandishi anasema majaribio ya kufanya tamthiliya ioane na utamaduni na
mazingira ya kiafrika bado yanaendelea, na ni vigumu kwa wakati huu kubashiri hatima yake
itakuwaje. Yamkini kutokana na majaribio kama haya tutapataaina ya tamthiliya
tunayoweza kuiita ya kiafrika au ya
Kiswahili.
Hakuna maoni:
Maoni mapya hayaruhusiwi.