Makala



 
HISTORIA FUPI YA USHAIRI WA KISWAHILI
1.0 Utangulizi
Kiswahili ni neno linayowakilisha dhana ya lugha iliyo na asili ya Kibantu, hususan lugha zilizo katika mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa Massamba (2007), Kiswahili ni matokeo ya mkutaniko (convergence) wa jamii zilizokuwa zinatumia lugha zenye asili ya Kibantu zilizojikuta katika upwa wa Afrika ya Mashariki baada ya mtawanyiko (divergence) wa miaka mingi. Kwa hiyo, Kiswahili kikawa ni matokeo ya mkutaniko huo wa jamii zenye asili moja[1]. Licha ya athari za wageni mbalimbali waliofika katika maeneo ya Waswahili katika pwani ya Afrika Mashariki, lugha ya Kiswahili imebakia kuwa na tanzu zake za kifasihi, hususan katika usimulizi. Utanzu mkongwe kuliko zingine ni ushairi. Ushahidi wa kihistoria unaonyesha kuwa ushairi wa Kiswahili ulikuwapo karne nyingi kabla ya kuja kwa wageni katika pwani ya Afrika Mashariki. Ushairi huu ulikuwepo sambamba na Waswahili wenyewe, lakini ulikuwa katika hali ya usimulizi. Tungo za Fumo Liyongo[2] ni miongoni mwa ushairi wa zamani wa Kiswahili katika upwa wa Afrika Mashariki. Kabla ya kuja wageni, hasa Waraabu, Waswahili walikuwa wakijulikana kwa majina ya jamii zao za asili za kibantu kama vile Walamu, Wapate, Wapemba, Wadigo, Wavumba, Waunguja, Wangazija na kadhalika. Ushairi wa jamii hizi uliendelea kuwa katika hali ya usimulizi mpaka wageni kutoka nje ya bara la Afrika walipoanza kuja. Kihistoria, tungo za fasihi ya Kiswahili hususan ushairi zilihifadhiwa katika hati ya Kiarabu[3].


2.0 Historia ya Ushairi
Utanzu wa ushairi ni utanzu ambao una historia ndefu miongoni mwa tanzu zote za kifasihi. Hili ni kutokana na misingi kwamba, binadamu ana masuala mengi ya kisaikolojia na kisosholojia ambayo mara nyingi humsumbua. Binadamu hujiona razini na mwenye kipawa cha ubunifu kuliko wanyama wengine. Ndiposasa kila mara yumo katika pilikapilika za kubuni mikakati mipya ya kukabiliana na mazingira yake yanayobadilika kwa kasi mno.

Ushairi kama utanzu  wa fasihi ya Kiswahili una historia tawili ambayo hadi sasa tarehe kamili ya chanzi chake imegubikwa katika utata. Wallah (1988) ana maoni kwamba licha ya utata huu, watafiti wengi wanakubaliana kwamba ushairi huu ulianza pindi tu mwanadamu alipoanza kutumia nyimbo katika kazi zake kama vile uvuvi, ususi, ukulima na uvunaji. Jamii za Kiswahili na za Kiafrika kwa ujumla zilidumisha ushairi wao kupitia kwa masimulizi ya mdomo na nyimbo. Vipengele vya lugha vilivyotawala ushairi huu wa Kiswahili aidha ni vya jadi kama ulivyo ushairi wenyewe. Mojawapo ya hivi vipengele vya fani ni umbo na sitiari.

3.0 Mihula ya Ushairi wa Kiswahili
Kezilahabi (katika Fasihi III, 1983) amegawa historia ya ushairi wa Kiswahili katika mihula minne ambayo ni; Muhula wa Urasimi, Muhula wa Utasa, Muhula wa Urasimi Mpya na Muhula wa Sasa.

3.1 Mhula wa Urasimi
Ni vigumu kueleza ni lini hasa mashairi ya Kiswahili yalianza kuchukua umbo lake la kimapokeo. Ni vigumu zaidi kusema lini shairi fulani lilianza kuonekana katika hali ya maandishi. Tatizo hili linasababishwa na kuwako kwa mashairi hayo katika hali ya fasihi simulizi karne nyingi kabla ya hati za Kiarabu kufika upwa huu wa Afrika Mashariki. Wakati mwingine matukio yatajwayo huweza kumsaidia mchunguzi kwa baadhi ya maandishi, hasa yale yenye athari kubwa ya Kiarabu, huwa vigumu kusema kama mwandishi aliandika kwa uasili wake mwenyewe au alikuwa akijaribu kukumbuka shairi fulani la huko alikotoka. Hili bado ni jambo la kufanyiwa uchunguzi  kuhusu mashairi ya zamani.

Kimaandishi mashairi ya zamani yajulikanayo sana ni Utenzi wa Tambuka (1728) ulioandikwa na bwana Mwengo, Utenzi wa Hamziya (1949)  au (1690) ulioandikwa na Sayyid Abdarus, Utenzi wa Al-Inkishafi (1810 – 1820) ulioandikwa na Sayyid Abdallah A. Nasir na Utenzi wa Mwanakupona ulioandikwa na Mwanakupona mwenyewe. Tarehe za kuandikwa kwa tenzi ni za kukisia, lakini kwa jumla ziliandikwa katika karne ya kumi na nane na nusu ya kwanza ya karne ya kumi na tisa. Kimaandishi Utenzi wa Al-Inkishafi ni utenzi wa kwanza wenye uzito kujadili matatizo na mazingira yaliyohusu Afrika ya Mashariki na utenzi wa kiwango cha juu kabisa katika falsafa ya dini na wa kiwango cha juu kisanaa. Ni utenzi wenye uasili japo hapa na pale unarejea katika Korani. Utenzi wa Hamziya ndiyo umetumia lugha ya zamani kuliko tenzi zingine. Lugha iliyotumika ni Kingozi lakini ni tafsiri ya utenzi wa Kiarabu ujulikanao kama “Kasidatul Hamziya” ulioandikwa na Muhamed bin Said al-Busiry wa Misri. Hii ndiyo tafsiri ya zamani ya kwanza kufanywa katika lugha ya Kiswahili tuliyonayo. Utenzi wa Mwanakupona (1858) ndio utenzi pekee wa zamani ulioandikwa na mwanamke na ukaacha athari kubwa katika maisha ya ndoa katika pwani ya kaskazini. Utenzi mwingine unaostahili kutajwa hapa ni Utenzi wa Fumo Liyongo (193?). utenzi huu ndio utenzi pekee wa zamani wenye athari chache za nje. Ni utenzi wa Kiafrika zaidi. Ni vigumu kusema kama kweli Fumo Liyongo alikuwa mshairi. Hili bado ni jambo la kufanyia uchunguzi. Anayejulikana ni Fumo Liyongo wa kihistoria aliyenyang’anywa ufalme wa Shagga na Daudi Mringwari. Zipo nyimbo hapa na pale ambazo zimeitwa zake bila kuchunguza kama kweli kimtindo na kimaudhui zinaweza kuwa zimeandikwa na mtu mmoja na katika wakati aliopata kuishi. Nyimbo hizo ziliandikwa na mwandishi wa Utenzi wa Al-Inkishafi.
Tenzi nyingine ni Utenzi wa Ayubu, Utenzi wa Ngamia na Paa, utenzi wa Masahibu, Utenzi wa Kiyama, Utenzi wa Mikidadi na Mayasa, Utenzi wa Ras al-Ghuli na Utenzi wa Shufaka. Hizi ni tenzi za zamani ambazo hazisomwi sana  siku hizi.
Upande wa mashairi, kimaandishi mshairi aliyejulikana sana ni Muyaka bin Haji (1776 – 1940) na Bwana Mataka na Ali Koti. Wapo washairi wengine waliokuwa wakiandika wakati huu lakini mashairi yao bado hayajakusanywa na kuwekwa katika hali ya vitabu. Washairi hawa walifuatiwa na Muhammad Kijumwa na Hemedi Abdallah. Hapa tunaweza kusema kuwa ndio mwisho wa muhula wa Urasimi katika fasihi ya Kiswahili. Ni dhahiri kuwa kuhusu muhula huu uchunguzi mdogo sana umefanywa sehemu ya upwa wa Kusini chini ya Tanga. Hemedi Abdallah ndiye mwandishi pekee anayejitokeza.

3.2 Mhula wa Utasa
Miaka kati ya 1885 – 1945 tunaweza kusema kuwa ulikuwa muhula wa utasa katika fasihi ya Kiswahili. Maandishi machache yaliandikwa wakati huu, mengi yakiwa maandishi ya Hemedi Abdallah. Tunapata pia Utenzi wa Vita vya Maji Maji na Utenzi wa Vita vya Uhuru. Kihistoria sababu zinajulikana. Ulikuwa ni wakati ambao mataifa ya Ulaya yalikuwa yakigawana Afrika, vile vile wakati wa vita vya Dunia. Kimaandishi ulikuwa wakati wa kubadilisha hati za maandishi. Mambo haya yalisimamisha fasihi andishi ya Kiswahili kwa muda. Kwa hiyo kanuni za uandishi wa mashairi zilianza kupotea.

3.3 Mhula wa Urasimi Mpya
Miaka ya 1945 – 1960 tunaweza kuuita muhula wa urasimi mpya. Kazi kubwa ilikuwa ni kufufua kanuni hizi. Huu ndio ulikuwa wakati wa Shaaban Robert, Amri Abedi, Khamis Amani (Nyamaume), Mathias Mnyampala, Ahmed Nassir, Mdanzi Hanasa, Kibwana, Abdi Matunga, M.M. Kihere na wengine  wengi. Kwa hiyo kitabu cha Sheria za Kutunga Mashairi kiliandikwa wakati ambao kilikuwa kinahitajika sana ili kuweka kiungo kizuri na wakati uliopita. Lakini kwa sababu fulani fulani muundo ulioshika sana ni muundo wa mizani 16 na katika mistari minne, muundo uliotumika sana na Muyaka bin Haji katika karne ya kumi na nane. Sababu mojawapo kubwa ni kuwa wanamapokeo waliamini kuwa shairi liliandikwa ili liimbwe, wakati huo mghani Radioni Athumani Khalfani alikuwa amezoea kuimba mtindo huo na katika mahadhi ya aina moja. Sababu nyingine ni kutopatikana kwa maandishi ya amani hadi kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilipoundwa. Shaaban Robert ndiye aliyejaribu kutumia mitindo mbalimbali ya wakati uliopita.

Miaka ya 1960 – 1967 ilikuwa miaka ya kuyumbayumba katika ushairi wa Kiswahili. Hii ilisababishwa na nchi za Afrika Mashariki kutokuwa na malengo maalum baada ya uhuru. Ulikuwa pia ni wakati ambapo washairi wawili mashuhuri walifariki. Hata hivyo ulikuwa wakati ambao washairi wapya walikuwa wakijengeka.
3.4 Mhula wa Sasa
Miaka 1967 hadi leo tunaweza kuuita muhula wa sasa. Kwa Tanzania ndio wakati wa kutafuta uhuru kamili katika lengo la kufikia ujamaa. Washairi wengi walianza kuwa na mtazamo mpya kisanaa, mgogoro juu ya kanuni za usahiri uliongezeka. Hapa lazima tujiulize, kwa nini mgogoro huu unatokea katika muhula huu kwa nguvu zaidi? Swali hili limo katika mkondo ule ule wa uhuru wa kiuchumi, uhuru wa kiutamaduni n.k. Kihistoria, swali la uhuru katika ushairi linafuata mkondo huu wa uyakinifu wa kihistoria. Ni tukio ambalo haliwezi kuepukika. Ni tukio muhimu katika historia ya ushairi wa Kiswahili.

4.0 Maoni Mengine
Tunaweza kukubaliana au kutokubaliana na mawazo ya Kezilahabi juu ya mgawanyo wa mihula kuhusu historia ya ushairi. Kama ilivyoelezwa na wataalamu wengine kuwa ushairi wa Kiswahili hauna tarehe maalum ya lini ulianza. Tunakubaliana na mawazo ya wengi kuwa ushairi wa Kiswahili ulianza pale tu binadamu alipoanza kutumia lugha katika kujikimu kimaisha. Na hivyo, ili kuielewa historia ya ushairi huu sharti tuuhusishe na historia ya mswahili mwenyewe. Suala la kuwepo ama kutokuwepo kwa Waswahili haliwezi kuchukua mjadala kwani lilikwisha kujadiliwa na wengi na kufikiwa mwafaka. Hapa tutachunguza tu safari ya mabadiliko ya waswahili kutoka kwenye hatua za mwanzo za kimaisha hadi kufikia hatua waliyomo sasa.

4.1 Ushairi wa Kiswahili Kabla ya Ujio wa Wageni
Katika hatua za mwanzo kabisa, waswahili kama walivyo watu wengine wa mataifa na makabila mengine, waliishi maisha ya ukusanyaji wa matunda, mizizi na uwindaji wa ndege na wanyama wadogowadogo kwa ajili ya chakula. Baada ya kupiga hatua kidogo katika maisha walianza kulima na hatimaye kufuga baadhi ya wanyama na ndege. Wakati wakiendelea na shughuli zao hizo, fasihi yao hasa ushairi, ilifanya kazi kubwa ya kuwahamasisha katika shughuli zao. Kwa hiyo, ushairi wa wakati huo ulikuwa ni nyimbo za kazi, kubembelezea watoto na nyingine. Kila hatua ya maendeleo waliyopitia waswahili na ushairi wao haukuachwa nyuma. Kadiri walivyozidi kubadirika ndivyo ushairi nao ulivyobadirika na kuchukua dhima mpya. Mwanzo kabisa dhima ya ushairi ilikuwa ni dhima za kiuchumi na kijamii. Baada ya jamii kuingia katika matabaka na ushairi nao ukawa na dhima hizo za kitabaka. Kwa muda mwingi zaidi ushairi wa Kiswahili ulikuwa simulizi kwa sababu waswahili hawakujua kusoma na kuandika.
4.2 Ujio wa Waarabu
Ujio wa Waarabu ulileta athari kadhaa katika ushairi wa Kiswahili. Athari kubwa ya kwanza ni kutambulishwa kwa hati za kiarabu. Waarabu walipokuja katika upwa wa Afrika mashariki walianza kuandika mashairi yao kwa Kiswahili kwa kutumia hati za kiarabu. Hapa ndipo tunanza kupata ushairi andishi wa Kiswahili. Waarabu waliwafunza waswahili kusoma na kuandika kwa kutumia hati za kiarabu. Waswahili nao walianza kuhifadhi mambo yao katika maandishi kwa kutumia hati hii ya kiarabu.

Ushairi wa kale zaidi tunaoukuta katika maandishi ni nyimbo za Fumo Liyongo. Kuja kwa Waarabu kunatambulisha migongano kati ya ustaarabu na ushenzi (ukafiri). Hata hivyo Waarabu walifanya juhudi kubwa ya kuwafundisha Waswahili ustaarabu wao kwa kuwasilimisha na kuwafundisha dini. Hapo pia tunashuudia kukua kwa miji ya Waswahili ambapo migongano inachukua nafasi kubwa zaidi, kati ya ushamba na umji.

4.3 Uvamizi wa Wareno
Kipindi cha miaka ya 1500 hadi 1730 kilikuwa kipindi cha Wareno kuvamia Pwani ya Afrika Mashariki, ambapo waliteka miji ya Mombasa na Kilwa/Malindi. Ushairi wa kipindi hiki ulihusu migongano kati ya wazungu na wenyeji. Ulikuwa ni mgogoro kati ya Ukristo na Uislamu. Tenzi nyingi zilitungwa kipindi hiki lakini zaidi zilikuwa za kidini hasa kupinga Ukristo. Baadhi ya tenzi hizo ni Herekali, Tambuka na Hamziya ambao ulikuwa ni utenzi uliosimulia maisha ya mtume Mohamed, nao una mgogoro wa kupinga Ukristo. Kuna wimbo ulioelekezwa kwa mzungu aliyeitwa Miguel (jina la Kireno) kupinga mauaji aliyoyafanya dhidi ya Waswahili.
Mzungu Migeli u mwongo
Mato yako yana chongo
Kwani kuwata mpango
Kwenda kibanga uwani?
(Mulokozi na Sengo, 1995:76)

4.4 Utawala wa Waoman
Kushindwa kwa Wareno mwaka 1730, kuliwaweka Waswahili chini ya utawala wa Waoman baada ya wareno kuondoka, miji iliyotawaliwa ni Zanzibar na Mombasa. Historia ya Waswahili inajikita katika utawala wa Waoman. Washairi wanaojipambanua hapa ni Muyaka bin Haji na washairi wa Pemba kama vile Kibabina, Ali Koti na wengine. Ushairi wa wakati huu ulihusu mgogoro kati ya Waarabu na Waswahili. Pia kuna mgogoro kati ya mji na mji kama vile Pate na Lamu, mmgogoro kati ya dini na siasa.

Muyaka bin Haji anaposema,
Jifungetoni masombo,
Tuje tuteze nao,
Bebeni tezi na ngao, n.k,
Alikuwa akiwaasa Waswahili kuwa tayari kupambana dhidi ya utawala kandamiza wa Waarabu.

Washairi wengine wanaoibukia katika kipindi hiki ni Sayid Abdallah bin Ali bin Nassoro ambaye anatoa ya dini na mtazamo wa Uislamu, anachora miji iliyoporomoka kutokana na athari za wareno – Wakristo. Mwingine ni Mwanakupona binti Musham. Yeye anaibuka na mseto wa utamaduni. Anafundisha malezi ya mwanamke, lakini bado ni utenzi ulioelemea zaidi kwenye dini.

4.5 Ujio wa Wazungu
Mwishoni mwa karne ya 19, upwa wa Afrika Mashariki ulivamiwa na kutawaliwa na Wazungu ambao walileta athari kubwa katika ushairi wa Kiswahili. Kwanza kutambulishwa kwa hati za kirumi ambapo Waswahili walianza kutumia hati hizo kuandika kazi zao. Ushairi kwa kipindi hiki zaidi umejikita katika kupinga ukoloni. Miongoni mwa washairi wanaojipambanua hapa ni Hemed bin Abdallah (1850 – 1928) aliyekuja na tungo za:
Utenzi wa Seyyidina Hussein bin Ali (EALB, 1972)
Utenzi wa Abdirrahamanni na Sufiyani (EALB, 1961)
Utenzi wa Kadhi Kassim bin Jaafar (TUKI, 1974)
Utenzi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima (EALB, 1960)

Kazi nyingine zinazopatikana katika kipindi hiki ni Utenzi wa Vita vya Majimaji. Kazi nyingi zaidi katika kipindi hiki zilihusu maisha ya Washahili chini ya Ukoloni, watu waliojipendekeza kwa wakoloni, wale waliopinga ukoloni, pia yaliibuka mashairi yaliyohusu maadili.

Baadaya kama miaka ya 1930 – 1960 kilikuwa kipindi cha mzinduko wa kitaifa na kitamaduni. Washairi katika kipindi hiki walianza kutetea Uafrika. Mashairi mengi yaliyoandikwa katika magazeti ya mambo leo yalihusu zaidi utamaduni na utu wa Mwafrika. Washairi kama vile Shaaban Robert wanaibuka na kutetea Kiswahili. Shaaban Robert anawahimiza watu wajiunge na chama cha TAA. Washairi wengine ni Mdanzi bin Hanasa, Swalehe kibwana, Mwalimu Mwalimu Kihere na wengine..

Miaka ya 50 kilikuwa ni kipindi cha mwamko wa kisiasa. Baada ya kutetea maadili wanavuka na kuanza harakati za kumwondoa mkoloni. Kipindi hiki washairi walitumia mafumbo zaidi. Washairi wanaojipambanua katika kipindi hiki ni Shaaban Robert, Amri Abedi, Saadan Kandoro na wengine. Kandoro anamwandikia mjomba wake Amri Abedi aliyekuwa anasoma Pakstani akimweleza harakati zilizokuwa zikiendelea huku nyumbani za kumwondoa mkoloni. Miongoni mwa mashairi hayo ni pamoja na: Siafu wamekazana, ondoka nchini kwetu, kwetu ni kwao kwa nini? Waafrika njooni na mengine mengi yanayopatikana katika Mashairi ya Saadan. Sifa kubwa ya mashairi ya kipindi hiki ni kupinga ukoloni.

4.6 Baada ya Uhuru
Baada ya nchi za Afrika Mashariki kujipatia uhuru wake, Waswahili walikuwa kwenye shere za kushangilia uhuru. Washairi nao hawakubaki nyumba kuimba nyimbo za kushangilia uhuru. Baadhi ya mashairi yanayopatikana katika kipindi hiki ni pamoja na: Kujitawala, Chukua hicho kiti na mengine. Mashairi yaliyotawala kipindi hiki ni ya kutafakari Uhuru, mashairi ya kujenga taifa. Washairi wanaojipambanua zaidi hapa ni Kandoro, (Kujitawala kugumu tujikongoje) na Nyerere (Usawa wa Binadamu na Chombo cha Taifa Letu).

Katika harakati za kujenga taifa, kulianzishwa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, falsafa iliyotokana na kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967. Washairi nao wakasimama kuiimba siasa ya ujamaa na kujitegemea. Mashairi yakaanza kuzungumzia ujamaa, ukombozi wa Afrika na Azimio la Arusha. Baadhi ya kazi za kipindi hicho ni pamoja na:
Matunda ya Azimio
Malenga wa Bara
Miaka kumi ya Azimio na mashairi mengine.
4.7 Mgogoro wa Ushairi
Kipindi cha miaka ya 1960 hadi 1970 jamii ya waswahili iliingia katika mgogoro mkubwa ambao uligawa washairi katika makundi mawili. Ni kipindi ambacho nchi ilikuwa katika mabadiliko ambapo baadhi ya watu walielekea kukata tamaa baada ya ahadi nyingi zisizotekelezeka. Sanaa ya ushairi nayo ilikubwa na wimbi hili la mabadiliko na kuanza kuihakiki jamii. Jambo kubwa lililotawala kipindi hiki katika sanaa ya ushairi ni kuwa mashairi yaweje? Baada ya wananchi kuanza kukata tamaa na wengine kuona ujamaa unasalitiwa, wakaanza kuuhakiki ujamaa. Miongoni mwa washairi wanaojitokeza katika kuuhakiki ujamaa ni pamoja na E. Kezilahabi, Mulokozi na Kahigi.

4.8 kKipindi cha Sasa
Kezilahabi na diwani yake ya Dhifa anatuingiza katika kipindi cha sasa ambapo uhuria umetawala. Watu wanagawana mali ya Umma, watu wako kwenye dhifa wanagawana mali ya nchi wanakula.

5.0 Maendeleo
Katika kipindi cha sasa twaweza kuona kuwa idadi ya washairi imeongezeka, idadi ya mashairi imeongezeka na ubora wa mashairi umeimarika. Ushairi leo unashirikisha watu wengi zaidi hasa baada ya kufundishwa shuleni. Mabadiliko ya 1960 yamezua fani mpya kama vile ngojera na sasa ushairi umekuwa sanaa ya umma. Kumekuwa na:
i.                    Mashairi huru mengi
ii.                  Mashairi ya kidrama
iii.                Ushairi wa vijana (Bongo Flever) unaosaili yaliyopo
iv.                Ushairi unabadilika kuendana na hadhira, wanachanganya ushairi na ngoma.

6.0 Matatizo
Pamoja na mafanikio hayo katika ushairi wa Kiswahili bado pana matatizo mengi ambapo leo:
i.                    Kuna matatizo katika masuala ya uchapishaji
ii.                  Diwani siyo nyingi
iii.                Magazeti si mengi yenye kutoa kurasa za mashairi kama zamani
iv.                TV na Redio hawawapi nafasi za upendeleo washairi.



[1] Rejelea katika Massamba 2007
[2] Fumo Liyongo ni shujaa katika historia ya Kiswahili ambaye tungo zake zinasemekana ni za zamani sana, na   
aliishi katika upwa wa Afrika Mashariki.
[3] Waarabu ndio wageni walioiita pwani ya Afrika Mashariki kwa jina la sahel, na wenyeji wake kuitwa wasuahel. Hili ndilo jina walilopewa wenyeji wa pwani kama Waswahili, yaani wenyeji wa pwani, na huu ndio mwanzo wa matumizi ya neno Waswahili. Aidha lugha yao iliitwa Kiswahili.

+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Kiswahili na TEHAMA


MAENDELEO YA KISWAHILI KATIKA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (TEHAMA)
Aritamba Malagira
Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam

Ikisiri
Teknolojia ya habari na mawasiliano imekuwa ikikua kila siku kutoka simu ya kukoroga hadi simu ya mkononi, matumizi ya wavuti na nyinginezo nyingi, kwa kweli ni hatua kubwa ya maendeleo katika teknolojia. Hivi sasa watu wanawasiliana ndani ya sekunde chache kwa umbali wa kutoka bara hadi bara kupitia wavuti. Katika hali kama hii lugha za ulimwengu nazo zimekuwa zikijitahidi kukabiliana na ukuaji huu wa teknolojia kwa kutafuta istilahi mpya ili kuelezea dhana mpya za kiteknolojia zinazoibuka. Katika harakati hizi, Kiswahili hakiko nyuma, istilahi mpya za Kiswahili zimekuwa zikiundwa ili kukidhi haja ya kuwasiliana kupitia Teknolojia ya habari na mawasiliano. Makala hii inalenga kuangalia hatua iliyofikiwa na Kiswahili katika tasnia ya teknolojia ya habari na mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuchunguza istilahi za ki-TEHAMA zinazotumika.

1.      Utangulizi
Teknolojia ya habari na mawasiliano imekuwa kiungo muhimu sana katika maendeleo ya watu duniani. Watu wamekuwa wakitumia teknolojia hii katika kufanya mawasiliano muhimu, kufanya bishara na mambo mengine mengi yanayowanufaisha watu. Kompyuta/ Talakirishi ni moja ya kifaa kilicholeta mapinduzi katika TEHAMA kama asemavyo Katambi (2011) “Kompyuta amaTarakilishi katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha kabisa mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita. Kutokana na kuwapo kifaa hiki dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile katika historia ya kuwapo kwake. Kifaa hiki kimeleta mabadiliko makubwa Sana katika maisha ya kawaida ya binadamu. Kifaa hiki kimesababisha mambo mengi kufanyika katika hali ambayo hakika isingewezekana au ambayo awali ingeonekana kama ya kufikirika!. Kompyuta imeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi. Kompyuta imeifanya dunia kuwa Kama kijiji kidogo ambacho unaweza kukizunguka katika muda mfupi Sana wa sekunde chache”. Maneno haya ya Katambi yanaonesha ni jinsi gani kompyuta ilivyo muhimi katika TEHAMA, mawasiliano yote ya teknolojia ya habari hufanywa kwa kutumia kompyuta, mfano; matangazo ya redio na televisheni, magazeti  na n.k huandaliwa kwa kutumia kompyuta na kuwa tayari kwa ajili ya kupasha habari.
Makala hii, kwa kuzingatia umuhimu wa TEHAMA katika dunia ya sasa imejikita katika kuchunguza maendeleo ya Kiswahili katika uga wa habari na mawasiliano kwa umahususi zaidi katika mawasiliano yanayohusisha matumizi ya kompyuta hususani wavuti na programu nyingine za kompyuta. Tutaangalia umuhimu wa matumizi ya Kiswahili katika TEHAMA, maendeleo yaliyofikiwa, changamoto na mwisho ni hitimisho.

2.      Usuli
Neno Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ujumla wake hurejelea mifumo yote ya kiteknolojia inayotumika kutengeneza, kuhifahdi, kuchakata na kutumia habari katika mifumo yake tofautitofauti (data, picha, uwasilishaji wa medianuwai na mifumo mingine mingi) na mabayo huwezesha, kurahisha na kutegemeza mawasiliano. Kwa umahususi zaidi, TEHAMA inarejelea kukutana au kuingiliana kwa mikroelektroniki,  talakirishi  na mawasiliano ya kutumia redio, simu au televisheni ambavyo hufanya kuwezekana kwa data, ikiwa ni pamoja na matini, video na ishara za video kuweza kusafirishwa mahali popote duniani ambapo ishara za kidijitali huweza kupokelewa… (Howell na Lundall, wakinukuliwa na Akinyi 2010). Kwa ujumla TEHAMA inahusu mambo mengi sana, matumizi ya kompyuta, wavuti, matangazo ya redio na televisheni, satelaiti, picha na mambo mengine mengi yafananayo na hayo hujumuishwa katika teknolojia ya habari na mawasiliano.
2.1  Umuhimu wa TEHAMA katika maendeleo kwa ujumla
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ujumla imechangia sehemu kubwa kuleta maendeleo hasa katika kipindi hiki cha karne ya 21 ambapo utandawazi umeenea ulimwengu mzima na kuifanya dunia kuwa kama kijiji ambapo watu huwasiliana na kufanya kazi na biashara kwa pamoja kama wapo katika kijiji kimoja, mambo haya yote yanafanikiwa kwa kuwezeshwa na TEHAMA. Kama asemavyo Kamau (2009) kuwa ushirikiano wa kimataifa katika mambo kama vile siasa, biashara, uchumi , michezo n.k  huwezeshwa na kurahisishwa na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ambayo imeuunganisha ulimwengu mzima kimawasiliano. Kwa maelezo haya tunaweza kuona ni jinsi gani TEHAMA ilivyo kuwa muhimu katika ulimwengu wa sasa.
Lugha ni muhimu sana katika suala zima la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hatuwezi kuhamisha maarifa yaliyopo katika teknolojia hii bila kutumia lugha na kwa hiyo ili kuwapo na maendeleo endelevu kupitia TEHAMA ni lazima pia lugha inayotumika kuhamisha maarifa ya teknolojia hii iwe inaleweka kwa watumiaji husika. Hii itakuwa rahisi kwao kuilewa na kuitumia teknolojia hii vilivyo kwa sababu lugha inayotumika ni lugha wanayoifahamu na ni lugha yao.
Kama tujuavyo bara la Afrika halijaendelea sana kwa kiwango cha kuzalisha teknolojia zitakazo kubalika katika masoko ya kimataifa kama yafanyavyo mabara mengine hususani mabara ya Ulaya na Marekani, kwa hiyo kulingana na hali hii Afrika imekuwa ikiingiza teknolojia za kigeni kutoka Mabara mengine hasa Marekani na Ulaya, teknolojia hizi zimekuwa zikiingizwa kwa lugha za kigeni jambo ambalo hufanya watumiaji wengi wa Waafrika kushindwa kumudu matumizi ya teknolojia hizi kwa sababu hawajui lugha iliyotumiwa. Kwa mfano kompyuta zinazoingizwa Afrika programu zake huwa zimeandikwa kwa lugha za kigeni hususani kiingereza, watu mabao wataweza kuzitumia kwa urahisi ni wale ambao wanazijua lugha hizi vilivyo na kuwaacha wale wasiojua wakiwa wameduwaa ambao kimsingi ni wengi kuliko wale wanaojua. Kwa hiyo, ili kuondokana na tatizo hili, upo umuhimu mkubwa wa kuziendeleza lugha za Kiafrika kiteknolojia. Suala hili ni la msingi sana, kwani kwa kufanya hivi hatutakuwa tumeendeleza lugha tu bali pia tutakuwa tumeindeleza jamii yetu kiteknolojia.
2.2 Kwa nini Kiswahili katika TEHAMA
Wataalam wengi wanipigia upatu lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya utandawazi barani Afrika, hii ni kwa sababu lugha ya Kiswahili imeendelea sana kuliko lugha nyingine za Kiafrika na ndiyo lugha pekee iliyoonekana kuwa tayari kupokea kwa haraka mabadiliko ya kiteknolojia yanayoibuka kila siku duniani. Kwa maana kwamba lugha ya Kiswahili ina utajiri mwingi wa msamiati kiasi cha kukabiliana na teknolojia za kigeni zinazoibuka bila matatizo yoyote. Kama asemavyo Kamau (2009) “kwa vile utandawazi huhusika na uunganishaji wa mataifa mbalimbali, basi Afrika yahitaji lugha moja yenye asili ya Kiafrika kama lugha ya kusambaza utandawazi. Kwa sasa mfano mzuri wa lugha kama hii ni lugha ya Kiswahili. Lugha hii ndio lugha kutoka barani Afrika ambayo ina matumizi mapana kuliko lugha nyingine hapa barani na kwingineko”. Nukuu hii inatuonesha ni jinsi gani lugha ya Kiswahili ilivyo muafaka katika suala zima la utandawazi wa Afrika. Kimsingi utandawazi husambazwa kupitia lugha na teknolojia, kwa hiyo tunaweza kuona jinsi lugha ilivyo chombo muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia na kwahiyo Kiswahili kama lugha ya kiafrika ni muhimu iwe imejiendeleza na kujitosheleza kiteknolojia kwaajili ya mahitaji ya watu wake.
Kutokana na umuhimu wa TEHAMA kama ilivyofafanuliwa hapo juu na kutokana na  umuhimu wa lugha katika maendeleo ya kiteknolojia, tunaweza kuona jukumu la lugha ya Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Lugha ya Kiswahili imebeba jukumu kubwa la kuhakikisha wakazi wa Afrika Mashariki wanaipata na kuitumia teknolojia mpya kwa lugha wanayoifahamu ambayo ni Kiswahili. Kwa kufanya hivi matumizi ya teknolojia yataimarika katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Kwa misingi hii naweza kusema ndio sababu pekee iliyonisukuma kuichunguza lugha ya Kiswahili katika uwanja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

3.      Hatua iliyofikiwa na lugha ya Kiswahili katika TEHAMA
Kwa kweli lugha ya Kiswahili imepiga hatuta kubwa sana katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kama tulivyo kwisha kusema huko awali kwamba TEHAMA ina uwanja mpana sana, tunapozungumzia TEHAMA tunazungumzia vitu vingi sana kama vile matangazo ya redio na televisheni kwa namna yanavyofanywa, matumizi ya kopmyuta kwa namna yake n.k. Katika makala hii tutajikita zaidi katika matumizi ya kompyuta kwa namna yake, tutajikita hapa kwani hii ndio inaonekana kuwa teknolojia mpya kabisa katika mazingira ya lugha ya Kiswahili na dhana mpya zinazidi kuibuliwa kila siku katika matumizi ya kompyuta.
Kompyuta kimekuwa kifaa muhimu sana katika shughuli nyingi za kimaendeleo, kwa kutumia kompyuta watu wamekuwa wakifanya mambo chungu nzima na kwa urahisi sana. Bila shaka umekwisha sikia kuwa unaweza kununua bidhaa kwa kutumia kompyuta ukiwa nyumbani kwako bila ya hata kwenda huko sokoni au dukani. Bila shaka umekwisha sikia kuwa mabenki, hospitali, taa za kuongozea magari barabarani, kamera za usalama, ndege za abiria na kivita na hata lift unazopanda kila siku unapoingia na kutoka ofisini katika jengo refu huendeshwa kwa msaada wa kompyuta. Bila shaka umekwisha jionea mwenyewe au kusikia habari kama hizi. Umekwisha sikia kuwa mtu anaweza kumchagua mgombea wa urais au ubunge kwa kutumia kompyuta! Haya na mambo chungu nzima hufanyika kwa msaada wa kompyuta. Katika nchi zilizoendelea matumizi ya kifaa hiki yanaendelea kushika hatamu kiasi kwamba kila kitu sasa kinafanywa Kwa kutumia mashine zinazoongozwa kwa kompyuta.
Kwa hiyo unaweza kuona ni jinsi gani matumizi ya kompyuta yalivyokuwa muhimu sana katika maisha ya kila siku. Serikali za Jumuia ya Afika mashariki zimekuwa zikisisitiza matumizi ya kompyuta kuanzia shule za awali, kwa kuzingatia kwamba matumizi ya kompyuta yameongezeka sana katika ulimwengu wa sasa lakini changamoto zinazoikabili progaramu hii imekuwa ni lugha ya kufundishia. Kwa mfano Tanzania somo la TEHAMA linafundishwa kuanzia shule za msingi; shule za msingi kwa Tanzania hutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia na   kwa kuwa programu za kompyuta zimeandikwa kwa kiingereza, italazimika programu hizo zitafsriwe katika Kiswahili ili ufundishaji uweze kuwa rahisi. Na hapa ndipo tunapata istilahi mpya za Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Licha ya uhitaji wa kufundishwa somo la Kiswahili katika shule za awali lakini pia makampuni makubwa yanayohusika na mawasiliano ya kompyuta yamekuwa yakitafuta nija ya kujiimarisha kibishara katika maeneo mbalilimbali duniani. Mbinu moja wapo amabyo wemekuwa wakiitumia ni kuhakikisha wateja wao wanapata huduma kwa lugha yao. Kwa mfano kampuni ya Microsoft kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ilianzisha mradi wa kutafsiri program zake kwa Kiswahili. Kama asemavyo King’ei (2010) “kampuni ya talakirishi iitwayo microsoft ilitekeleza hatua ya kihistoria  mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi maalumu inayowawezesha watumiaji wa talakirishi kutumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta. Programu hii mpya inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote”.
Msanjila na wenzake (2011) pia wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha ingizwa katika mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na mikrosofti. Wanaendelea kusema, kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu hawa ni wazi kwamba mpaka sasa hivi Kiswahili kinatumika katika baadhi ya mifumo ya kompyuta. Katika kufanikisha hili ujanibishaji wa programu kadhaa za kompyuta ulifanyika. Kahigi (2007) anasema “Mradi wa ujanibishaji wa Office 2003 na Windows XP kwa Kiswahili sanifu ulitekelezwa katika kipindi 2004-2005. Malengo ya maradi yalikuwa: (1) kuandaa istilahi za kompyuta kwa Kiingereza-Kiswahili, na (2) kutafsiri programu nne za kawaida za Office (Outlook, Excel, Word na PowerPoint) na Windows XP”. Hii inamaanisha kwamba programu hizi zinapatikana katika lugha ya Kiswahili. Hebu tuangalie mifano ya istilahi kutoka katika programu hizi za Office 2003 na Windows XP kama zilivyoorodheshwa na Kahigi, ni istilahi zaidi ya 600 lakini hapa tutaangalia chache tu:
1.                   Fikia                          Access
2.                   Kibonye fikishi        Access key
3.                   Viziada                    Accessories
4.                   Amilisha                  Activate
5.                   Kirekebu                 Adapter
6.                   Kihadharishi           Alert box
7.                   Program matumizi  Application
8.                   Makaaba                   Archive
9.                   Vitome mchoro       Bit map
10.               Kiashiri mada        Book mark
11.               Sakura                    Browse
12.               Kisakuzi                  Browser
13.               Kwa kaida              By default
14.               Msabidi                  Configuration
15.               Sabidi                     Configure
16.               Puna                       Crop
17.               Kielekezi                Cursor
18.               Tanafsi                   Custom
19.               Pakua                     Download
20.               Kijachini                Footer
21.               Nakala bayana     Hard copy
22.               Kidakuzi                 Cookie
23.               Sanidi                     Install
24.               Kicharazio             Keyboard
25.               Kiolezo                  Template
26.               Tafutatua               Trouble-shoot
27.               Sanidua                  uninstall
28.               Sasaisha                  Update
29.               Kidhulishi                Highlighter
30.               Kichapishi                Printer
31.               Kingavirusi              Antivirus
Hizi ni baadhi tu ya istilahi kati ya nyingine nyingi zilizoundwa katika mradi wa kujanibisha programu za office 2003 na Windows XP. Jitihada za kampuni ya Microsoft hazikuishia hapo tu, mnao mwezi mei mwaka 2011 kampuni hii ilizindua programu ya Windows 7 kwa Kiswahili, hatua hii imezidi kukiimarisha Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Haya ni maendeleo makubwa katika lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo sasa mtumiaji wa Kiswahili anachaguo la kufanya, ama kuendelea kutumia programu hizi kwa lugha ya Kiingereza au kwa lugha ya Kiswahili.
4.      Changamoto zinazoikabili lugha ya Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Kila jitihada zinazofanywa katika kufikia malengo fulani huwa hakukosi changamoto. Katika jitihada za kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kiteknolojia kumetokea changamoto nyingi, moja wapo iliyo kuu kabisa ni kwamba lugha ya Kiswahili haimilikiwi na taifa lolote tajiri kwa hiyo katika harakatika za kuendeleza inakumbana na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa fedha na hata utayari wa viongozi wa kisiasa kukiendeleza Kiswahili ni mdogo sana, hata hivyo harakati hizi zinapingwa na mataifa ambayo lugha zao zimeendelea sana kiteknolojia kwa kuhofia kwamba zitafunikwa na matumizi ya Kiswahili. Wapo tayari kutoa misaada ili kuendeleza lugha zao kukididimiza Kiswahili kitu ambacho kinafanya harakati za kukiendeleza Kiswahili kuwa ngumu kwani nchi kinamozungumzwa Kiswahili hazina pesa za kupambana na mataifa makubwa yanayopigia upatu lugha zao.
Kutokana na sababu hizo, kasi ya uundaji wa istilahi za kiteknolojia imekuwa ndogo sana, kwani kufanya hivyo pia kunahitaji pesa, na mara nyingi pesa zimekuwa zikitolewa na wahisani au makampuni yanayohusika kitu kinachotokea mara moja baada ya muda mrefu sana.
Pia, viongozi wa serikali hawajatilia mkazo suala hili, hawajaona umuhimu wa kukiendeleza Kiswahili kitenolojia. Nguvu zao nyingi wameziweka katika miradi mingine ya kimaendeleo huku wakisahau kabisa kuwa Kiswahili pia kinahitaji kwenda sambamba na maendeleo hayo. Kwa hiyo hii imekuwa ni changamoto katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Kwa kuwa istilahi hizi zimekuwa zikifanywa na watu tofautitofauti,  ni muhimu kuwapo na jopo maalumu la kusanifisha istilahi hizi kabla hazijasamabazwa. Kwa kufanya hivi hakutakuwa na matumizi tofauti ya istilahi katika dhana moja. Hali hii inajitokeza sana endapo uundaji wa istilahi utakuwa umefanywa katika makundi tofauti.
Utayari wa watumiaji; watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili wamekuwa wakilalamika kuhusu kutumia programu za komyuta kwa lugha za Kiswahili. Madai yao ni kwamba istilahi za Kiswahili ni ngumu sana na hivyo si rahisi kuzitumia, kwa mfano, wengi wamezoea kusema password na kwa hiyo ukiwaambi kwamba password kwa Kiswahili huitwa nywila au mouse inaitwa pukuwatabaki wakikushangaa na watona kama unawapa kazi kubwa sana. Kwa hiyo hii nayo inasabaisha matumizi ya Kiswahili katika vifaa vya kiteknolojia hususani kompyuta kuwa hafifu.
5.      Hitimisho
Katika makala hii tumeona TEHAMA ni kitu gani na umuhimu wake katika maisha ya kila siku ya binadamu, tumeona umuhimu wa lugha za kiafrika kuendelezwa katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa umahususi zaidi tumeona jinsi Kiswahili kilivyo muhimu zaidi katika uwanja wa maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Tumengalia pia maendeleo yaliyofikiwa na lugha ya Kiswahili katika TEHAMA huku tukionesha baadhi ya istilahi za Kiswahili zinazotumika katika matumizi ya kompyuta, pia tumeangalia changamotozinazo ikabili lugha ya Kiswahili katika jitihada za kuiendeleza kiteknolojia. Sasa tuangalie mapendekezo juu ya nini kifanyike ili kuhakikisha lugha ya Kiswahili inashika hatamu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano:
Viongozi wa ukanda wa Afrika Mashariki waungane kuhakikisha wanaunda sera nzuri kuhusiana na maendeleo ya lugha ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na kuandaa mradi maalumu wa kuunda istilahi mbalimbali za kiteknolojia, hii itasaidia lugha ya Kiswahili kuimarika katika matumizi ya teknolojia. Pamoja na hilo pia itenge bajeti maalumu kwa ajili ya kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuunda istilahi za Kiswahili katika teknolojia zinazoibuka ili kuahakikisha wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili hawaachwi nyuma katika matumizi ya teknolojia mpya ziibukazo.
Pia kutokana na changamoto ya kutokuwapo na jopo maalumu la kuunda istilahi za kiteknolojia pindi mradi kama huu unapotokea, hali hii imesababisha kuwapo kwa istilahi ambazo hazijasanifishwa na pengine kuwapo na istilahi zaidi ya moja inayorejelea dhana moja, hii ni kwa sababu miradi kama hii hufanywa na watu tofautitofauti na pengine wataalamu hawa wana ujuzi katika lugha tu lakini katika teknolojia hususani kompyuta hawana maarifa ya kutosha au hawana kabisa. Katika hali kama hii ni vigumu kuunda istilahi zinazofanana au zinazobeba dhana kamili kama ilivyokuwa ikikusudiwa katika lugha chanzi. Kwa hiyo katika uundaji wa istilahi za kiteknolojia ni vema kuwepo na jopo maalumu amablo lina ujuzi wa kutosha katika lugha na masuala ya kiteknolojia, hii itasaidia kutoa istilahi nzuri na zinazoeleweka kwa urahisi kwa watumiaji.
Baada ya kuundwa istilahi hizi inatakiwa zisambazwe kwa watumiaji kwa kiwango kinachoridhisha ili waweze kujifunza na kuzifahamu na hatimaye kuzizoea katika matumizi yao ya kila siku katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Nasema hivi kwa saba usambazaji wa istilahi hizi umekuwa haufanywi kwa kiwango kinachohitajika, na katika usambazaji, vyombo vya habari vipewe kipaumbele, kwani istilahi hizi zikitumiwa na vyombo vya habari itakuwa rahisi sana kwa  watumiaji wengine kuzitumia.
Wazungumzaji wa Kiswahili pia wawe tayari kutumia istilahi hizi au programu za Kiswahili katika matumizi yao ya kopmyuta. Programu kadhaa za kompyuta zimejanibishwa kwa Kiswahili lakini wazungumzaji wengi wa Kiswahili bado wanatumia programu zilizoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, program ya Windows 7 inapatikana kwa Kiswahili lakini nina wasiwasi kama miongoni mwetu kuna mtu hata mmoja anayetumia Windows 7 ya Kiswahili. Kwa hiyo napendekeza kwenu suala hili, kwa kuwa sisi tumejitoa kueneza na kuienzi lugha ya Kiswahili pia ni jukumu letu kuchangamkia fursa kama hizi, tuwe wa kwanza kutumia programu kama hizi kwa Kiswahili pindi zinapotokea, kwa kufanya hivi tutakuwa tunakienzi Kiswahili na kukikuza kwani watu wanaotuzunguka watakapotuona tunatumia Windows ya Kiswahili watashawishika na wao kuitumia, hivyo kwa njia hii tutakuwa tumefanikiwa kukuza na kuienzi lugha ya Kiswahili.
Ninaamini kila mmoja  wetu ana ndoto za kuona lugha ya Kiswahili siku moja inakuwa lugha ya bara zima la Afrika, kwa maana kwamba Kiswahili kinazumgumzwa kila kona ya bara hili, basi kama ndio ndoto zetu sote hatuna budi kupigania maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwa nguvu zetu zote, tukifanya hivi kwa pamoja kwa kijishughulisha na masuala yanayohusika na Kiswahili, kwa kuandika, kufanya utafiti katika Nyanja mbalimbali za lugha ya Kiswahili ndoto zetu zitatimia na kumbukumbu zetu zitakumbukwa katika vizazi vinavyokuja kama anavyokumbukwa leo hii Shaaban Robert. Ninaamini kuwa tunaweza!!
Kiswahili, Hazina ya Afika kwa Maendeleo Endelevu!

Marejeo
Akinyi, J.J. (2010). Kiswahili usage in ICT in NEPAD secondary schools in Kenya. Katika                                        TheJournal of Language, Technology & Entrepreneurship in Africa, Vol. 2. No.1.                            www.ajol.info/index.php/kcl/article/vieFile
Kahigi, K.K (2007). Ujanibishaji wa office na windows xp kwa Kiswahili sanifu. Katika Kioo                           cha Lugha juzuu la 5. Dar es salaam. TUKI.
Kamau, S.N. (2009). Kiswahili, utandawazi na umoja wa Afrika. Katika journal of language, technology& entrepreneurship in Africa vol.1. www.ajol.info/index.php/kcl/article/vieFile
Katambi, S (2011). Teknolojia ya Habari na Mawasilianao (TEHAMA). Dar es salaam: Modecs                             Solutions
King’ei, K (2010). Misingi ya isimujamii. Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Msanjila,Y.P, Kihore,Y.M na D.P.B Massamba (2011). Isimujamii sekondari na vyuo.
Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Osborn, D. Z. (2006). African Languages and Information and Communication Technologies:                          Literacy, Access, and the Future. Katika  Selected Proceedings of the 35th Annual                   Conference on African Linguistics, ed. John Mugane et al., 86-93. Somerville, MA:                    Cascadilla Proceedings Project. www.lingref.com, document #1299.
Osborn, D. Z. (2010). African Languages in a Digital Age. Cape Town: HSRC Press.

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI
IDARA YA LUGHA YA KISWAHILI  NA ISIMU


KI113:MBINU ZA UTAFITI  NA UANDISHI WA TASNIFU  KATIKA LUGHA NA FASIHI



RIPOTI YA UTAFITI KUHUSU  MBINU ZILIZOTUMIKA KATIKA UUNDAJI WA ISTILAHI ZA KISWAHILI ZILIZOINGIZWA KATIKA MIFUMO YA MAWASILIANO YA KOMPYUTA: MIFANO KUTOKA MFUMO WA KOMPYUTA WA LINUX.





JINA: MALAGIRA ARITAMBA.
NAMBA YA USAJILI: 2010-04-02466
MWALIMU WA SOMO: E. MAHENGE NA DKT. G. MRIKARIA


SHUKRANI
Utafiti huu umefanikiwa kwa jitihada kubwa za waalimu wangu wa somo.Napenda nimshukuru kwa dhati mwalimu Elizabeth Mahenge kwa kutumia muda wake mwingi  katika kunielekeza na kurekebisha mada yangu ya utafiti.Namshukuru pia Mwalimu G.Mrikaria kwa kututia moyo katika kufanikisha utafiti huu.
Vilevile nawashukuru wanafunzi wenzangu kwa kunishauri na kunitia moyo katika kuendelea na utafiti huu.Wanafunzi wafuatao wamekuwa mchango mkubwa katika kufanikisha utafiti huu;Ally Laila,Thomas Edson,Ndumbaro Eric, Ndege Busalu pamoja na Ntenga Elias.Nawashukuru pia Boniface Jacob na James Balele kwa utayari wao wa kunisaidia kuchapa utafiti huu.Na mwisho nawashukuru wote walionisaidia kwa namna moja ama nyingine,Mungu awabariki sana!

.


YALIYOMO
Sura ya kwanza:Utangulizi na Nadharia ya uundaji istilahi…………………. 1
1.0  Utangulizi……………………………………………………………………………………1
1.1  Tatizo la utafiti……………………………………………………………………….3
1.2  Malengo ya utafiti…………………………………………………………………....3
1.3  Umuhimu wa utafiti…………………………………………………………………4
1.4  Dhana ya istilahi,linux na nadharia ya uundaji istilahi……………………………4
Sura ya pili:Mapitio ya marejeo na mbinu za ukusanyaji data………………..8
2.1 Mapitio ya marejeo………………………………………………………………………….8
2.2 Mbinuza ukusanyaji data ……………………………………………………………..10
Sura ya tatu:Uchambuzi wa data………………………………………………11
3.1 Utangulizi………………………………………………………………………………….11
3.2 Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika Linux………….11
3.3 Ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katka Linux…16
3.3.1 Ubora wa mbinu zilizotumika ……………………………………………………16
3.3.2 Udhaifu wa mbinu zilizotumika…………………………………………………18
3.3.3 Mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili…………………………19
Sura ya nne:Muhtasari na Hitimisho…………………………………………..20
4.1 Matokeo ya utafiti kwa muhtasari…………………………………………………………20
4.2 Hitimisho…………………………………………………………………………………….22


Marejeo
Viambatisho

SURA YA KWANZA
1.0   Utangulizi
Lugha ni kielelezo cha maisha ya jamii kwani huenda sambamba na mabadiliko au maendeleo katika jamii. Kila sekta ya jamii iwe  siasa,elimu,sayansi,teknolojia,utamaduni,dini,kilimo,uhandisi,sanaa,uchumi ama biashara hubadilika kila mara .Uvumbuzi mpya kila mara huzua dhana mpya ambazo zinahitaji maneno mapya kuzielezea(King’ei 2010)
King’ei(ameshatajwa) anaendelea kusema kuwa  ukuzaji wa msamiati na istilahi ni jambo la kawaida katika kurekebisha lugha ili iweze kuambatana na wakati au iwe ya kisasa. King’ei anaendelea kusema kuwa ukuzaji upya wa istilahi hufanyika kwa sababu mbalimbali.Kwanza kabisa lugha sharti iweze kuelezea dhana mpya zinazoingia katika jamii kutokana na mabadiliko katika jamii.Sababu ya pili ni kwamba maana ya maneno yanayotumika katika lugha hupanuliwa ili kuchukua maana mpya au pana kuliko ile ya awali.Sababu ya tatu ya kuwepo haja ya kustawisha istilahi mpya katika lugha ni ile haja ya kufasiri maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.
Msanjila na wenzake (2011) wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha ingizwa katika mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na mikrosofti.Wanaendelea kusema,kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Pia King’ei(ameshatajwa) anaelezea kuwa,kampuni ya talakirishi iitwayo microsoft ilitekeleza hatua ya kihistoria  mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi maalumu inayo wawezesha watumiaji wa talakirishi kutumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta,anaendelea kusema,programu hii mpya inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote.
Katika mchakato wa kuziweka programu hizi katika Kiswahili, ilihitajika kuunda istilahi za

Kiswahili ili kukamilisha shughuli hii mbinu mbalimbali za uundaji istilahi zilitumika.
Katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kuna mbinu mbalimbali zinazotumika. Kwa mujibu wa
Kiango(2004) amebainisha mbinu za kuunda istilahi za Kiswahili kuwa ni pamoja na:Kubuni,anasema,njia hii inaweza kutumika katika kukabili mazigira ya aina mbili; kubuni msamiati ambao utataja mambo yaliyomo katika jamii ambayo hayajapata msamiati wa Kiswahili. Pili ni kubuni msamiati ambao utataja mambo kutoka nje ya jamii yenye msamiati wa kigeni, mbinu nyigine ni kukopa; kukopa kwa kutohoa msamiati wa kigeni,kukopa kwa kutafsiri msamiati wa kigeni na kukopa kwa kuingiza maneno ya kibantu na lahaja na njia nyingine ni ya kufupisha maneno.
Kahigi (2004) anasema mbinu  za kuunda istilahi ni pamoja na: unyambulishaji; unyambulishaji ni kupachika viambishi undaji ili kuunda neno lenye dhana na muafaka. Mfano, modification→ukumushaji. Mbinu nyigine ni ukopaji; ukopaji ni kuchukua neno kutoka lugha chanzi na kulitohoa ili likubaliane na taratibu za kisarufi za lugha pokezi. Mbinu zingine zilizoainishwa na Kahigi ni: tafsiri mkopo;ni aina ya tafsiri kutoka lugha chanzi ambayo ni ya moja kwa moja, mbinu nyigine ni uundaji wa maneno mapya, mbinu hii huhusisha uundaji wa maneno mapya ambayo yalikuwa hayapo kwenye lugha lengwa, mfano byte  >  baiti, uambatani; ni uwekaji wa maneno mawili au zaidi yanayowakilisha dhana moja, mfano magneticfield >ugasumaku, ufupishaji; hii ni mbinu ya kufinyanza maneno na kupata neno moja, mfano, UWT(Umoja wa Wanawake Tanzania).
Mtafiti mwingine ambaye ameelezea mbinu za uundaji istilahi ni Sewangi(2004) yeye anasema mbinu za uundaji istilahi ni pamoja na: kutohoa,kwa mfano; computer > kompyuta, program>programu, mbinu nyingine ni kubuni, kwa mujibu wa Sewangi anasema, mbinu ya kubuni inaweza kufanywa kidhahania au kwa kutumia vigezo mahususi. Kubuni istilahi   kidhahania  hutetewa kwa hoja kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya istilahi na dhana inayo bebwa, hivyo neno lolote laweza kuundwa na kupewa hadhi ya istilahi ya dhana fulani. Njia mojawapo ya kuunda istilahi kidhahania ni kutumia fomula za kompyuta ambapo maneno mengi yanaweza kuzalishwa na kupachikwa dhana mahususi katika uwanja fulani wa maarifa. Njia ya kuunda istilahi kivigezo huweza kufanywa kwa kutumia vigezo mahususi kama

vile kazi, umbo au mwonekano wa kitu. Kwa mfano kwa kutumia kigezo cha kikazi kisawe cha calculator kimebuniwa kuwa ni kikokotozi (kitu kinachofanya kazi ya kukokotoa), kisawe cha data saver kimekuwa kihifadhi data (kitu kinachohifadhi data). Mbinu nyingine iliyoainishwa na Sewangi ni mbinu ya kupanua maana ya maneno yaliyopo; njia hii huchukua neno lenye maana ya jumla na kuliongezea maana ya kihistilahi katika mazingira ya kitaalamu, kwa mfano neno kifaru ambalo maana yake ya jumla ni mnyama lakini katika mazingira ya utaalamu wa kijeshi ni kisawe cha tank.
Kwa kuzingatia maelezo ya wataalamu hawa kuna mbinu tofautitofauti za kuunda istilahi. Kwa hiyo kutokana na kwaba kuna mbinu tofautitofauti za kuunda istilahi,utafiti huu hulenga kubainisha mbinu zilizotumika katika kuunda istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux.

1.1 Tatizo la utafiti
Kulingana na tafiti za wataalamu hawa,wameelezea kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo ya kompyuta ya linux na Microsoft,kwa mfano, Msanjila na wenzake (2011) na King’ei (2010) wameelezea kuhusu hili. Vilevile wataalamu wengine kama vile Kiango (2004), Sewangi (2004) na Kahig i(2004) wao wameainisha mbinu mbalimbali za kuunda istilahi za Kiswahili. Kwa ujumla wataalamu hawa hawajaonyesha mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mifumo ya mawasiliano ya kompyuta hususani mfumo wa kompyuta wa linux,kwa hiyo utafiti huu hulenga kuziba pengo hili kwa kuchunguza mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux.
1.2 Malengo ya utafiti
Malengo ya utafiti huu yamegawanyika katika sehemu kuu mbili:
1.2.1 Lengo kuu na
1.2.2 Malengo mahususi

1.2.1 Lengo kuu
Lengo kuu la utafiti huu ni kutaka kutalii istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa mawasiliano ya kompyuta wa linux na kuainisha mbinu zilizotumika kuunda istilahi hizo.
1.2.2 Malengo mahususi
Malengo mahususi ya utafiti huu ni mawili, ambayo ni: kupambanua ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili  katika linux na kubainisha mbinu bora zaidi inayoweza kutumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
1.3 Umuhimu wa utafiti
Umuhimu wa utafiti huu ni kwamba utasaidia kubainisha mbinu bora za uundaji wa istilahi za Kiswahili. Vilevile utafiti huu utawasaidia watumiaji wa kompyuta wanaotumia programu hii ya linux kwa Kiswahili kuelewa kwa urahisi istilahi zilizotumika baada ya kubainisha mbinu zilizotumika katika kuunda istilahi hizo.
1.4 Dhana ya istilahi, linux na nadharia ya uundaji istilahi
Istilahi ni dhana iliyofasiliwa na wataalamu mbalimbali na wote wanakubaliana kuwa, istilahi ni msamiati utumikao katika uwanja fulani maalumu wa lugha. Wataalamu wanaokubaliana na fasili hii ni pamoja na King’ei(2010), Samson(1988) na Kiango(2004). Kwa hiyo kulingana na fasili hii si kila msamiati ni istilahi bali msamiati huwa istilahi pale unapotumika katika Nyanja maalumu za kitaaluma. Kila uwanja maalumu wa kitaaluma huwa na msamiati wake ambao hauna maana nje ya taaluma hiyo wala haufahamiki kwa wazungumzaji lugha wasiokuwa wataalamu wa lugha hiyo. Kwa mfano msamiti unaotumika katika isimu,fasihi,teknolojia ya habari na mawasiliano na kadhalika ni maalumu na hutumiwa na kueleweka tu na wataalamu wahusikao na nyaja husika.
Linux kwa mujibu wa Msanjila na wenzake(2011) ni mfumo wa kompyuta huria unao ruhusu watu mbalimbali kuchangia katika marekebisho na maendeleo yake. Kimsingi linux ni mfumo endeshi wa kompyuta. Ni program katika kompyuta iayosaidia programu-tumizi na mtumiaji wa kompyuta kufikia vifaa fulani katika kompyuta ili kufanya kazi iliyokusudiwa, linux ni sawa na

program-tumizi zingine kama vile windows (Linux.com).
Nadharia ya uundaji istilahi hujumuisha mambo kadhaa, kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko(2008) mambo hayo ni pamoja na sababu za uundaji wa istilahi, njia au mbinu za uundaji istilahi,vyombo vya uundaji istilahi na misingi ya uundaji istilahi.
Katika sababu ya uundaji istilahi Tumbo-Masabo na Mwansoko wanasema kuwa, uundji wa istilahi ni muhimu panapotokea haja ya kushughulikia nyanja ambazo zilikuwa hazishughulikiwi kwa kutumia lugha fulani. Uundaji huo aghalabu hufanywa ili kukidhi haja ya mawasiliano katika elimu ya juu, ufundi na utaalamu,na shughuli zinazohusu serikali na teknolojia. Kwa hiyo nadharia ya uundaji istilahi huambatana na sababu au haja fulani ya kufanya hivyo. Kwa mfano uundaji wa istilahi za Kiswahili katika mfumo wa kompyuta wa linux umeambatana na sababu kwamba, kuuweka mfumo huu  wa kompyuta katika Kiswahili ili kusudi watumiaji wa Kiswahili waweze kuutumia mfumo huu kwa lugha wanayo ifahamu.
Vyombo vinavyohusika katika uundaji wa istilahi.
Katika kutekeleza kazi ya kuunda istilahi vimewekwa vyombo maalumu vinavyo tekeleza suala hili, kwa mfano Tanzania chombo kilchopewa jukumu hili na serikali ni Barza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).
Vilevile katika nadharia ya misingi ya uundaji istilahi huzingatia mambo yafuatayo:
·         Uundaji wa istilahi ni budi uanzie kwenye dhana.
·         Dhana hizo zieleweke kwa ukamilifu na uwazi.
·         Uhusiano baina ya dhana ndio uwe msingi wa uundaji wa istilahi, istilahi kopwa zichukuliwe kama zilivyo katika umbo lake la asili kwa kufanya marekebisho machache tu kulingana na sarufi na matamshi ya lugha kopaji.
·         Istilahi inafaa ziwe fupi iwezekanavyo lakini zieleweke.
·         Istilahi ziwe na muundo unaoeleweka yaani zifuate mofolojia ya lugha.
·         Uundaji wa istilahi kwa vifupisho na akronomia uepukwe hasa kama istilahi kamili si ndefu sana.
·         Istilahi zisiwe na sinonimia au homonimia.
·         Istilahi ziundwe kwa njia ambayo itakuwa rahisi kuunda istilahi nyingine kwa

mnyambuliko.
·         Istilahi zitolewe kufuatana na mfumo wa dhana yaani ziainishwe kuliko kuandikwa kwa alfabeti.
·         Muundo wa istilahi udokeze maana yake kwa watumiaji wa lugha husika. Kwa hiyo misingi hii haina budi kufuatwa katika mchakato wa uundaji istilahi.
Nadharia nyingine kama ilivyoainishwa na Tumbo-Masabo na Mwansoko(wameshatajwa) ni njia za uundaji istilahi. Katika uundaji wa istilahi kuna njia kuu mbili ambazo zinatumika zaidi, njia hizo ni pamoja na:
(i)                 Kutafsiri hasa kutoka kwenye lugha zinazojulikana kuwa ni za kimataifa kama vile Kifaransa, Kiingereza, Kihisipania.
(ii)               Kuunda istilahi kutokana na mifumo ya dhana.
Njia ya kutafsiri hutumiwa sana na vyombo vingi vya uundaji istilahi kinyume na misingi ya uundaji ambayo inasisitiza kuwa uundaji huo uanze na dhana, msingi wa njia hii ni istilahi za lugha chasili ambazo aghalabu hupangwa kwa alfabeti. Faida ya njia hii ni kwamba istilahi nyingi zinaweza kushughulikiwa  kwa muda mfupi pia istilahi za lugha lengwa huweza kutafsiriwa katika lugha za kimataifa. Hata hivyo hasara ya njia hii ni kwamba kwa vile kila istilahi hushughulikiwa peke yake, hali hii huweza kusababisha mtiririko wa mfumo wa istilahi usio na ulingano.
Kahigi (2004) anasema kuunda istilahi kutokana na mifumo ya kidhana ni kwamba istilahi huundwa kufuatana na mifumo hiyo. Kwa mfano katika hisabati kuna mifumo ya elimu-maumbo, elimu-namba, vipimo na kadhalika. Mathalani katika kuunda istilahi za dhana ya pembe itabidi dhana zifuatazo zishughulikiwe zote kwa pamoja: pembekali, pembenukta, pembetatu, pembemshabaha, pebemstari na kadhalika. Faida ya mkabala huu ni kwamba mwishowe mifumo yote ya dhana huwa na mtiririko wenye ulingano.
Katika nadharia hii ya njia za uundaji istilahi mbinu mbalimbali hutumika, mbinu hizo ni pamoja na:mwabatano; hii ninjia ya uundaji istilahi kwa kuambatanisha maneno mawili au zaidi yaliyo
huru. Mfano ; mbwa kichaa.
Mnyambuliko;ni uundaji wa neno jipya kwa kuambatisha viambishi kewenye mzizi au shina la neno. Mfano;wekeza  >  uwekezaji.
Muungano; hii mbinu ni sawa na mwambatano isipokuwa katika muungano maneno mawili au zaidi huunganishwa ili kuunda neno moja, mfano;kiini+macho  >  kiinimacho.
Kupanua maana ya maneno; huu ni mchakato ambapo neno lililopo kwenye lugha hupewa maana pana zaidi ya maana yake ya awali. Mfano butu maana yake ya kawaida ni –sio kali,-sio kata. Maana ya kihistilahi ni pembe ambayo ni zaidi ya nyuzi 90 na ndogo kuliko nhyuzi180(hisabati).
Ufupisaji; ni mbinu ambayo inatumika kufinyanza fungu la maneno ili kuunda neno moja,mfano; BAKITA (Baraza la Kiswahili laTaifa).
Ukopaji; ni matumizi ya neno kutoka lahaja ama lugha nyingine, aghalabu neno hilo hubadilishwa ili lishabihi muundo wa lugha lengwa.
Tafsiri-sisisi; ni aina ya tafsiri kutoka lugha chasili ambayo ni ya moja kwa moja. Mfasiri habadili lolote ila anahakikisha tu tafsiri inakuwa sahihi kwa mujibu wa lugha lengwa. Kwa hiyo katika mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili mbinu hizi hutumika.

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++


SURA YA PILI
Mapitio ya marejeo na mbinu za utafiti.
2.1 Mapitio ya Marejeo
Kutokana na mabadiliko yanayotokea katika jamii wataalamu wameonesha umuhimu wa lugha kuyakabili mabadiliko hayo. King’ei(2010) anasema lugha ni kielelezo cha maisha ya jamii siasa, elimu, sayansi, teknolojia, utamaduni, dini, kilimo, uhandisi, sanaa, uchumi ama biashara hubadilika kila mara, uvumbuzi mpya kila mara huzua dhana mpya ambazo zinahitaji maneno mapya ya kuzielezea.
Kulingana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano,lugha ya Kiswahili haina budi kuyakabili mazingira haya. King’ei(ameshatajwa) anaelezea hatua ya kihistoria iliyochukuliwa na kampuni ya Microsoft mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi maalumu inayowawezesha watumiaji wa kompyuta kutumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta. Kwa maana kwamba katika programu hii mpya inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza, kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote kwa Kiswahili.
Mtafiti mwingine ni Msanjila na wenzake(2011) wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha ingizwa kwenye mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na mikrosofti. Wanaendelea kusema kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Kimsingi hatua ya kuingiza Kiswahili katika mifumo hii ya kompyuta ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, katika mchakato wa kuiweka mifumo hii katika lugha ya Kiswahili ilihitajika kuundwa istilahi za Kiswahili ili mifumo hii iwekwe katika Kiswahili. Katika kuunda istilahi za Kiswahili mbinu mbalimbali hutumika, wataamu mbalimbali wamejadili kuhusu mbinu hizo:
Tumbo-Masabo na Mwansoko(2008) wanasema mbinu za uundaji istilahi ni pamoja na: Muungano wa maneno, mfano; mwanaisimu, mwambatano wa maneno, mfano; nusu kipenyo,
8
Unyambulishaji, mfano; ambisha  >  uambishaji, upanuzi wa maana za manenouhulutishji, mfano; kizigeu  >  kiziogeu, ukopaji (kukopa kutoka lugha za kigeni, lugha za kibantu au lahaja) na tafsiri-sisisi (tafsiri mkopo), mfano; measure of time  >  kipimo cha wakati.
King’ei(2010) ameainisha mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa ni pamoja na uunganishaji wa maneno, ukopaji, kutafsiri maneno ya kigeni, mbinu ya ufupishaji mfano;UKIMWI (Upungufu wa Kinga Mwilini) na utohozi.
Kahigi (2004) anasema mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili ni pamoja na:unyambulishi, uambatani, uhulutishi, ufupishaji, utemaji, ukopaji, tafsiri mkopo na uundaji wa maneno mapya kabisa.
Vilevile Kiango (2004) ameanisha mbinu zifuatazo katika undaji wa istilahi za Kiswahili: kubuni nakukopa (kutoka lugha za kigeni, lugha za kibantu na lahaja).
Kwa hiyo kulingana na wataalamu hawa tunaweza kuanisha mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa ni:
·         Unyambulishji
·         Muungano wa maneno
·         Mwambatano wa maneno
·         Ukopaji
·         Tafsiri mkopo(tafsiri sisisi)
·         Uhulutishaji
·         Ufipishaji
·         Utemaji
·         Upanuaji wa maana ya maneno yaliyopo na
·         Kubuni
Tafiti za wataalamu hawa zina umuhimu mkubwa kwani zimesaidia kujua kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo ya kompyuta ya linux na Microsoft na vilevi zimetusaidia kujua mbinu za uundji istilahi za Kiswahili. Kwa hiyo katika utafiti wetu tutabainisha mbinu zilizotumika

kuunda istilahi za Kiswahili katika linux kati ya hizo zilizoainishwa na wataalamu hao
2.2 Mbinu za ukusanyaji data
Katika utafiti huu mbinu iliyotumika ni moja, yaani mbinu ya kusoma marejeo mbalimbali hii ni kwa kuwa utafiti huu ni wa kimakitaba. Mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux, ambapo mbinu  hii imetumika kwa kusoma marejeo kwa njia ya wavuti na kukusanya istilahi za Kiswahili zilizokuwepo katika mfumo wa kompyuta wa linux.
Mbinu hii pia imetumika katika kukusanya data zinazohusu mbinu za uundaji istilahi za Kiswahili. Kwa kusoma marejeo mbalimbali data zinazohusu mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili zilikusanywa.
Vilevile mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu ubora na udhaifu na udhaifu wa mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux. Na pia mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu kubainisha mbinu bora katika kuunda istilahi za Kiswahili.
Data katika utafiti huu zimekusanywa kutoka faharasa ya teknolojia ya habari ya KILinux(KlnX) juzuu ya kwanza. Faharasa hii inajumuisha orodha ya istilahi 700Sampuli ya utafiti huu inajumuishaistilahi 100. Sampuli hii imechukuliwa kinasibu (kiholela) yaani hakuna mpangilo au utaratibu wowote maalumu uliofutwa katika uchukuaji wa sampuli.



+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

SURA YA TATU
Uchambuzi wa data
2.1 Utangulizi
Utafiti huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili, sehemu ya kwanza inahusu  uchambuzi wa data zinazohusu mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux na sehemu ya pili inahusu kupambanua ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linuxna kubainisha mbinu iliyo bora katika kuunda istilahi za Kiswahili. Katika uchambuzi wa data hizi tutatumia nadharia ya uundaji istilahi za Kiswahili ambayo imekwishaongelewa katika kipengele cha 1.4.
2.2  Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika linux.
Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux ni kama zilivyobainishwa hapa chini:
Unyambulishi; katika mbinu hii kitenzi kinaweza kugeuzwa kikawa nomino au kivumishi kinaweza kugeuzwa kikawa kitenzi au au nomino. Mbinu hii imetumika kwa kiasi kikubwa, mifano ifuatayo hudhihirisha matumizi ya mbinu hii.
·         Accessing   >   ufikio ( viambishi u-i-o vimeambatiswa katika shina fika).
·         Accsess     >      fikio (viambishi i-o vimenyambulishwa katika shina  fika )
·         Allocation    >     utengaji (viambishi u-aji vimeambatishwa katika shina tenga)
·         Bookmark link   >   alamisho (viambishi ish-o vimeambatishwa katika shina alama).
·         Bookmark   >   alamisha(t) (viambishi ish-a vimeambatishwa na kuunda kitezi alamisha)
·         Deleting    >   ufutaji (viambishi u-aji vimeambatishwa katika kitenzi futa  )
·         Deletion    >    mfuto (viambishi m-o vimeambishwa katika kitenzi futa nakupata neno                                         mfuto)
·         Input   >    ingizo (kiambishi –o kimeambishwa katika shina ingiza na kuunda istilahi ingizo).

·         Interactive   >   wasilianifu ( kiambishi –ifu kimeambishwa katika shina wasiliana na kuunda neno wasilianifu).
·         Allocation(n)   >    mtengo (viambishi m-o vimeambishwa katika shina tenga na kuunda nomino mtengo ikiwa na dhana ya matokeo).
Mwabatano; hii ni njia inayotumika kwa kuambatanisha maneno mawili au zaidi. Katika linux kuna istilahi zenye mwambatano wa maneno mawili na mwambatano wa maneno matatu. Mifano ifuatayo inadhihirisha matumizi ya mbinu hii:
·         Add-on help   >   msaada nyongeza ( yameambatishwa maneno msaada na nyongeza).
·         Alphabet text character   >   kiwambo alfabeti (kiwambo + alfabeti).
·         Aperture value   >    thamani upenyo (thamani + upenyo)
·         Background colour    >   rangi usuli (rangi + usuli).
·         Block device    >     kitunza data ( (ki)tunza + data).
·         Bullet list   >    orodha tobwe (orodha + tobwe).
·         Composer    >    programu tumizi (programu+ tumizi).
·         Configuration utility   >   programu sanidi (programu + sanidi).
·         Checksum    >    namba thibitishi (namba + thibitishi).
·         Encrypted    >    msimbo fiche (msimbo + fiche).
Vilevile kuna istilahi zilizoundwa kwa kuambatanisha maneno matatu. Mfano:
·         Encrypted text   >   matini-msimbo fiche (matini + msimbo + fiche).
·         Full-screen mode   >   modi-skrini nzima (modi + skrini + nzima).
·         Small caps   >      herufi kubwa ndogo (herufi + kubwa + ndogo)
·         Column spam   >    upana-safu wima (upana + safu + wima).
·         Default search engine   >   injini tafuti-msingi (injini + tafuti + msingi).
·         Com port (communication port) >  mlango wa mawasiliano(mlango+wa+mawasiliano).
Muungano; hii ni mbinu ya kuunganisha maneno mawili au zaidi ili kupata neno moja mbinu hii pia imetumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux. Mifano ifuatayo inabainisha

kutumika kwa mbinu hii:
·         Anonymity   >   ufichojina (uficho + jina).
·         Arccosine   >    kosinitao (kosini + tao).
·         Backslashes   >   mkwajunyuma ( mkwaju + nyuma).
·         Data area    >    eneodata (eneo + data).
·         Data bank   >    kanzidata (kanzi + data).
·         Data base    >    kihifadhidata ( (ki)hifadhi + data).
·         Footnote    >    tiniwayo (tini + wayo).
·         Hypertext   >   matinifora (matini + fora).
·         Keybody    >    baobonye (bao + bonye).
·         Newsgroup   >   kundihabari (kundi + habari).
·         Spreadsheet   >   lahajedwari (laha + jedwari).
Ukopaji; njia hii pia imetumika kuunda isuilahi za Kiswahili katika linux. Mifano ifuatayo inaonyesha kutumika kwa mbinu hii.
·         Account    >    akaunti
·         Adapter    >   adapta
·         Ampersand   > ampasendi
·         Applet   >    apuleti
·         Autoformat   >    fomati otomati
·         Baud   >       baudi
·         Boolean   >    buleani
·         Buffer    >     bafa
·         Cursor    >     kasa
·         Daemon    >   dimoni
·         Dial    >     dayo
·         Digit    >   dijiti
·         Icon    >    ikon
·         Kilobyte    >    kilobaiti

·         Pixels    >     pisel
·         Printer   >  printa
Mbinu hii ya ukopaji imetumika kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizopo katika linux.
Mbinu nyingine iliyotumika kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux nimbinu ya tafsiri mkopo (tafsiri sisisi). Tafsiri mkopo nitafsiri ya moja kwa moja kutoka lugha chanzi. Mifano ifuatayo inathibitisha matumizi ya mbinu hii katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katikalinux.
·         Actions menu   >   menyu vitendo.
·         Address book   >   kitabu cha anwani.
·         Alert me    >     nitahadharishe.
·         Auto complete     > kamilisha kiotomati.
·         Boolean operations     >     matendo buleani.
·         Certificate manager    >    meneja ithibati.
·         Certificate viewer      >     kionyeshi hati.
·         Chat group    >     kundi sogozi.
·         Colour capability    >     uwezo kirangi.
·         Connection failure     >     unganisho shinde.
·         Control panel     >    paneli dhibiti.
·         Country code    >     msimbo nchi.
·         Device manager    >    meneja vifaa.
·         Dialogue box     >     kisanduku cha mawasiliano.
·         Drag and drop   >    kokota na dondosha.
·         Eject     >       fyatua.
·         Flow control     >     udhibiti wa mtiririko.
·         Word processor    >    kichakata matini.
·         Web master    >     mtawala tovuti.

Mbinu nyingine ni mbinu ya kuunda maneno mapya kabisa mbinu hii imetawaliwa na maneno ya mkopo. Mfano:
·         Icon   >     ikoni
·         Italic    >   italiki
·         Label    >   lebo
·         Megabyte(MB)   >    megabaiti(MB)
·         Menu proxies    >    menyu proksi
·         Manager   >    meneja
·         Pixels   >     piseli
·         Program    >   programu
·         Scan    >    skani.
·         Scanner    >  skana
·         Tab    >    tabo
·         Tag    >  tagi
Mbinu ya ufupishaji pia imetumika katika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux; hii ni mbinu inayotumika kufinyanza fungu la maneno na kupata neno moja. Mifano ifuatayo huonyesha matumizi ya mbinu hii:
·         Alt(alternate)    >    Kbdl (kibadala)
·         BSS (Bulletin Board Service)     >     HUM (Huduma za Ubao wa Matngazo)
·         Ctrl (ontrol)     >   Kdbt (kidhibiti)
·         ESC (escape)   >    Epa (epuka)
·         FAQ (frequently asked quetions)   >    MYM (Maswali Yaulizwayo Mara kwa mara)
·         FTP (file transfer protocol)    >      IKF (Itifaki ya Kuhawalisha Faili)
·         FYI (For Your Information)    >    KTY (Kwa Taarifa Yako)
·         Megabyte (MB)       >      megabaiti (MB)
·         Ref:           >       Yah:
·         Re:             >        Jb:
·         TCP (Transfer Control Protocol)      >     IKU (Itifaki ya Kudhibiti Urushaji)

·         URL (Uniform Resource Location)   >   KISARA (Kioneshi Sanifu Rasilimali)
·         WWW (World Wide Web)      >    WWW (Wavu Wa Walimwengu)
Uhulutishi ni mbinu pia liyotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux, mbinu hii hutumika katika uundaji wa istilahi kwa kuunganisha sehemu za maneno na kuunda neno moja. Mbinu hii imetumika kwa kiasi kidogo sana, rejea mifano ifuatayo:
·         Bitmap    >   taswidoti ( (taswi)ra + doti)
·         Multimedia    >   medianuwai ((medi)a + anuwai)
Mbinu nyingine iliyotumika katika uundaji wa istilahi za kiswahili katika linux lakini kwa kiasi kidogo sana ni ile mbinu ya upanuzi wa maana za maneno, upanuzi wa maana za maneno ni kuongezea maana maalumu za kihistilahi katika maneno ya Kiswahili. Mfano:
·         Mouse      >       puku
Puku kwa maana ya kawaida ni panya pori lakini hapa limepewa dhana mahususi katika kompyuta kwa maana ya kifaa kinachotumika katika utumiaji wa kompyuta.
Utemaji (clipping) ni mbinu pia iliyojitokeza kwa kiasi kidogo sana, kwa kutumia mbinu hii istilahi huundwa kwa kukata sehemu ya neno na sehemu ya neno itakayobaki hutumika kama istilahi. Mfano: key (on keyboard)     >    kibonye ( kutoka neno bonyeza na kuongeza kiambishi cha ngeli ya saba ki-).
Kwa hiyo hizi ndizo mbinu zilizobainika kutumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux.
2.3 Ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux.
2.3.1 Ubora wa mbinu zilizotumika.
Kwa kiwango kikubwa mbinu zilizotumika zimezingatia misingi na kanuni za uundaji istilahi. Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008) wanabainisha kuwa misingi mahususi

katika uundaji wa istilahi ni pamoja na: Uangavu wa wa istilahi iliyoundwa yaani istilahi ziakisi sifa bainifu za dhana zinazoziwakilisha. Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux kwa kiasi kikubwa zimezingatia msingi huu. Kwa mfano:
Ufikio     >    accessing,         ingizo    >     input,   alamisha     >     bookmark.
Istilahi hizi zinaonyesha wazi dhana zinazowakilishwa, kwa mfano, alamisha inabeba dhana ya   kitendo cha kuweka alama hivyo kwa msingi huu inadhihirisha mbinu zilzotumika ni bora. Vilevile mbinu zilizotumika zimezingatia msingi wa uundaji istilahi unaosema, istilahi sharti ziwe na uwezo mkubwa wa kunyambuliwa na kuunda istilahi nyingine za kikoa au ukanda unaohusika. Msingi huu umefuatwa katika kuunda istilahi za kwenye linux, kwani istilahi nyingi zilizoundwa zina uwezo wa kunyambulishwa. Mfano:
·         Add   >    ongeza
·         Add-on    >    nyongeza
·         Alert(n)    >    thadhari
·         Alert(v)     >    tahadharisha
Pia uundaji wa istilahi za kwenye linux umezingatia msingi wa uundaji istilahi unaosema,uwakilishi wa istilahi moja kwa dhana moja. Msingi huu umezingatiwa kwa kiasi kikubwa kwani istilahi takribani zote huwakilisha dhana moja isipokuwa zile zilizoundwa kwa kupanua maana ambazo ni chache sana.
Mfano: configuration    >  usanidi
Configuration file   >   faili sanidi
Vilevile mbinu zilizotumika ni bora kwani hazijatumia kwa kiasi kikubwa mbinu za uhulutishi na mbinu ya kupanua maana ya maneno yaliyopo, hii ni kwa sababu misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili husisitiza kuepuka matumizi ya mbinu hizi; hii ni kwa kuwa istilahi zinazo uundwa kwa mbinu ya uhulutishi huwa na uvulivuli wa maana na kufanya kuwa ngumu kukumbukwa na kutumiwa. Pia uundaji wa istilahi kwa kupanua maana ya maneno yaliyopo husababisha watumiaji wa istilahi hizi kushindwa kutofautisha maana zake za kawaida na zile za

kihistilahi.
Mbinu za uundaji istilahi za Kiswahili katika linux, pia zimezingatia msingi wa uundaji wa istilahi za Kiswahili unaosema, istilahi sharti ziwe fupi na zenye kueleweka. Istilahi nyingi zimeundwa kwa kuzingatia msingi huu.

2.3.2 Udhaifu wa mbinu zilizotumika
Katika uundaji wa istilahi za Kiswahili za kwenye linux, kuna baadhi ya mbinu zilizotumika zinazoonyesha kuvunja kanuni na misingi ya uundaji istilahi. Kwa mfano kuna istilahi zilizoundwa kwa kukiuka msingi wa uundaji istilahi unaosema, istilahi sharti ziwe fupi na zenye kueleweka. Kuna baadhi ya istilahi ambazo ni ndefu na hivyo kukiuka huu msingi. Mfano:
·         Allow popup from this site    >    ruhusu udukizi kutoka tovuti hii
·         Com port      >        mlango wa mawasiliano
Istilahi hizi zimeonekana kuwa ndefu kwa sababu mbinu iliyotumika ni ya mwambatano wa maneno, na kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko wanasema, “iwapo istilahi zitaundwa kwa kutumia mbinu za muungano na mwambatano wa maneno basi mambo yafuatayo itabidi yazingatiwe”:
i.             Idadi ya maneno yanayounganishwa au yanayoambatanishwa yafaa yasizidi mawili.
ii.            Vistari visitumike kutenga istilahi ambatani kwani katika Kiswahili istilahi za namna hii hutamkwa kama neno moja lenye mkazo mkuu kwenye silabi moja tu.
iii.            Istilahi za namna hii yafaa zisiwe na silabi zaidi ya nane kwani kwa kawaida maneno ya Kiswahili yanawastani kati ya silabi moja na tano tu. Kwa msingi huu mifano ya itilahi zilizotolewa hapo juu zimeundwa na maneno zaidi ya mawili na silabi zaidi ya nane. Mfano ; mlango wa mawasiliano (silabi 10), ruhusu udukizi kutoka tovuti hii (silabi 15) na hivyo huu ni udhaifu uliojitokeza.
Vilevile matumizi ya mbinu za uhulutishi na upanuzi wa maana ya maneno yaliyopo zimetumika, huu ni udhaifu kwani misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili inasema, mbinu ya

uhulutishaji iepukwe kwani etimolojia yake ina uvulivuli na uundaji wa istilahi kwa kupanua maana ya maneno yaliyopo yafaa uepukwe kwani istilahi za namna hii zinawakanganya wengi hasa zinapotumika nje ya muktadha au kwenye taaluma zenye mahusiano ya karibu.
Mifano ya istilahi zilizoundwa kwa uhulutishaji ni:
·         Taswidoti    >      bitmap
·         Medianuwai     >    multimedia
Na mfano wa istilahi iliyoundwa kwa upanuzi wa maana ya neno ni:
Puku    >    mouse. Puku ni istilahi iliyopanuliwa maana ambapo maana yake ya kawaida ni panya pori lakini maana yake maalumu ni kifaa kinachotumika katika utumiaji wa kompyuta.
Kwa hiyo huu ndio udhaifu wa istilahi zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux.

2.3.3 Mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Kulingana na utafiti huu mbinu zilizoonekana kuwa bora zaidi na ambazo zinatumika sana katika uundaji wa istilahi za Kiswahili ni pamoja na, unyambulishaji, ukopaji, mwambatano, muunganiko pamoja na tafsiri mkopo. Mbinu hizi zimeonekana kuwa bora katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kwa sababu zinaruhusu uundaji istilahi kwa wingi iwezekanavyo na mbinu hizi huzingatia misingi ya uundaji istilahi za Kiswahili. Misingi hiyo ni pamoja na ufaavu wa kiisimu, uwekevu wa kiisimu, unyambulifu , uwakilishi wa istilahi moja kwa dhana moja, udhahiri na utoshelevu pamoja na uangavu. Mbinu hizi huakisi kwa kiasi kikubwa misingi hii na hivyo kupendekezwa na waunda istilahi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.




SURA YA NNE
Muhtasri na Hitimisho
4.1 Matokeo ya utafiti kwa muhtasari
Utafiti huu umeongelea malengo matatu. Kwanza utafiti huu umebainisha mbinu za uundaji istilahi zilizotumika katika linux. Pili utafiti umepambanua ubora na udhaifu wa mbinu za uundaji istilahi za Kiswahili zilizotumika katika linux. Tatu umebainisha mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Utafiti huu umeonyesha kuwa mbinu kumi za uundaji istilahi za Kiswahili zimetumika katika istilahi za linux. Mbinu hizo ni pamoja na:
Unyambulishi; mifano ya istilahi zilizoundwa kwa mbinu hii ni kama vile:
·         Ufikio   >    accessing
·         Utengaji   >   allocation
·         Alamisho   >    bookmark link
·         Ingizo   >    input
Muungano wa maneno; mifano ya istilahi zilizoundwa kwa mbinu hii ni pamoja na:
·         Ufichojina   >   anonymity
·         Mkwajunyuma   >   backslashes
·         Kanzidata     >      databank
Ukopaji; mbinu hii pia imetumika katika kuunda istilahi za kwenye linux. Mfano:
·         Akaunti    >   account
·         Apuleti      >   applet
·         Dayo      >      dial
Tafsiri mkopo (tafsiri sisisi); mifano ya istilahi zilizoundwa kwa kutumia mbinu hii ni:
·         Menyu vitendo    >    actions menu

·         Meneja ithibati    >    certificate manager
·         Paneli dhibiti     >       control panel
Mwambatano;  mbinu hii vilevile imebainishwa kutumika katka uundaji wa istilahi za Kiswahili  katika linux:
Mifano:   Rangi usuli    >     background color
Orodha tobwe    >    bullet list
Thamani upenyo   >    aperture value
Kuunda maneno mapya kabisa; mbinu hii pia imetumika. Mfano.
·         Ikoni    >   icon
·         Italiki    >    italic
·         Menyu proksi   >   menu proxies
Ufupishaji; katika utafiti huu mbinu hii pia imetumika. Mfano:
·         Kbdl (kibadala)   >   Alt (alternative)
·         Kdbt (kidhibiti)   >    Ctrl (control)
·         Epa (epuka)     >     Esc (escape)
·         KISARA (Kioneshi Sanifu Rasilimali )   >    URL (Uniform Resource Location)
Uhulutishi; mbinu hii pia imetumika. Mfano:
·         Taswidoti   >   bitmap
·         Medianuwai   >   multimedia
Upanuzi wa maana; mfano, puku (panya pori)   >   mouse.
Utemaji (clipping); mbinu hii pia imetumika. Mfano, kibonye   >   key (on keybody).
Kwahiyo hizi ndizo jumla ya mbinu zilizo tumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux.

Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha mbinu zilizotumika ni bora kwa kiasi kikubwa hii ni kutokana na sababu kwamba, mbinu zilizotumika zimezingatia misingi na kanuni za uundaji istilahi kwa kiasi kikubwa. Lakini vilevile baadhi ya mbinu za uundaji istilahi zimetumika
ambazo kwa mujibu wa misingi ya uundaji istilahi hazifai kutumiwa katika mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili. Mbinu hizi ni pamoja na uhulutishi na upanuzi wa maana ya maneno yaliyopo.
Pia utafiti huu umebainisha mbinu bora katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa niunyambulishaji, muungano wa maneno, uambatishi, mkopo pamoja na tafsiri mkopo. Hii ni kwa sababu mbinu hizi huzingatia misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili kwa kiwango kikubwa.

3.2 Hitimisho
Katika mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili kuna misingi ambayo hainabudi kufuatwa. Ili kuunda istilahi zilizobora mwanahistilahi hanabudi kuzingatia misingi hii.
Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008) wanasema kuwa ili kuinua ubora wa istilahi za Kiswahili waundaji istilahi wanasisitizwa kuzingatia mambo matatu muhimu. Kwanza wanasisitizwa kwa kadri iwezekanavyo wafuate kwa makini kanuni na taratibu za uundaji istilahi za Kiswahili. Kwa kufanya hivi itawezesha kwa kiwango kikubwa kuundwa istilahi za Kiswahili zenye kulandana vizuri kisarufi.
Pili waundaji istilahi wanahimizwa kuachana na mtindo wa kuunda istilahi moja moja kukidhi mahitaji yao ya istilahi ya papo kwa papo kwani mtindo huu unasababisha uundaji wa istilahi zisizo na mtiririko na  utimilifu wa kuridhisha. Kwa kuwa dhana zinazo wakilishwa na istilahi kwa kawaida huwa hazikai pweke pweke bali hukaa kama seti au mifumo maalumu, basi ni vema uundaji istilahi ufuate vilevile mifumo hiyo ya kidhana. Kulingana na maelezo haya kinachosisitizwa ni uundaji wa istilahi kwa kuzingatia mifumo ya kidhana. Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (wameshatajwa) wakimnukuu Mkude (1989:34) wanasema,

uundaji wa istilahi kwa kuzingatia mfumo wa kidhana unafaida kuu nne:
(i)     Utawasaidia waunda istilahi kuonyesha wazi mantiki ya uhusiano baina ya istilahi za ukanda mmoja.
(ii)   Utawahimiza waunda istilahi kubainisha vizuri zaidi tofauti ndogondogo lakini muhimu baina ya istilahi zinazokaribiana.
(iii) Utawasaidia kutambua haraka mapengo katika nasaba au upungufu katika maelezo.
(iv) Utawasaidia waunda istilahi kuona haraka ni istilahi zipi zitaweza kuathiriwa upesi iwapo  kutatokea mabadiliko katika istilahi moja wapo.
Hivyo utaratibu wa uundaji istilahi kinasaba ukitumiwa utaepusha uundaji wa istilahi zinazogongana na zisizo na mtiririko wenye mantiki.
Jambo la tatu kama ilvyoainishwa na Tumbo-Masabo na Mwansoko ni kwamba uundaji wa istilahi haunabudi kuzingatia tofauti za watumiaji, mathalani viwango vyao vya elimu, mazingira yao na kadhalika. Kwa hali hii ili kuhakikisha istilahi bora za Kiswahili zinaundwa ni muhimu hadhira mahususi za watumiaji istilahi ziainishwe na istilahi ziundwe kufuatana na viwango vya elimu ya watumiaji lengwa. Ni kwa kufanya hivyo dhana kama vile istilahi angavu au istilahi zenye uvulivuli zitakuwa na maana halisi kwani zitahusishwa na vikundi mahususi vya watumiaji istilahi.

Na Aritamba Malagira.
Haki zote zimehifadhiwa.


MAREJEO

Kahigi,K.K (2004).Ujanibishaji wa office na windows xp kwa Kiswahili sanifu katika
http//ajol.info.
Kiango,J.G (2004). Uundaji wa msamiti mpya katika Kiswahili: Zoezi lenye njia mbalimbali
katika Kiango.htm.
King’ei, K (2010). Misingi ya isimujamii. Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Msanjila,Y.P, Kihore,Y.M na D.P.B Massamba (2011). Isimujamii sekondari na vyuo.
Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Samson, H.R (1988). Ufundi wa magari, mfano wa ukuzaji wa istilahi za Kiswahili katika
Mulika na.21. Dar es salaam. Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili.
Sewangi,S.S (2004). Maana katika uundaji wa istilahi katika Sewangi,pdf.
Tumb-Masabo,Z.N.Z na Mwansoko,H.J.M (2008). Kiongozi cha uundaji istilahi za Kiswahili.
Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.



+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++


SHAABAN ROBERT KAMA MWANANATHARI
1.0.HISTORIA FUPI YA MWANDISHI

1.1   UZAWA NA MAISHA YAKE

1.1.1 UPANDE WA BABA YAKE

Asili ya wazazi wa Shaaban Robert ni Tunduru-Ruvuma kwa upande wa baba yake na Tanga kwa upande wa Mama yake.

Babu yake Shaaban Robert kwa upande wa baba aliitwa Kanduru. Alikuwa mzaliwa wa Wilaya ta Tunduru, mkoani Ruvuma. Katika suala la imani ya Kidini, Kanduru alikuwa anaamini Miungu ya Ki-mizimu ambayo wakati huo iliaminika kuwa ndiyo chanzo cha yote yaliyojiri katika maisha ya binadamu. Kanduru alipofika Mzizima kwa mara ya pili ili aje kufanya kazi, alimpata mke kutoka kabila la Wazaramo. Mke huyu alikuwa Muislamu kwa sababu eneo lote la Pwani lilikuwa tayari linakaliwa na wakazi wengi waliokuwa Waislamu. Kutokana na kumhitaji binti huyu, ilimlazimu Kanduru asilimu kwanza ndipo aozwe. Hivyo, Kanduru alisilimishwa na kuwa Mwislamu, akaitwa Jumaa, ndipo akaozwa.

Baada ya muda, walipata mtoto waliyempa jina la Ufukwe, jina alilopewa na watani kwa kuwa alizaliwa ufukweni mwa bahari ya Hindi wakati mama yake alipokwenda huko kutandaza Uduvi. Pia aliitwa Selemani, jina ambalo lilikuwa rasmi kwa muktadha wa dini ya Kiislamu. Tajiri wa Jumaa ambaye alikuwa mzungu, aliamua kumpa mtoto huyu jina la Roberto kutokana na mapenzi na furaha aliyokuwa nayo. Hivyo jina hili halihusiani na dhana ya dini. Baabaye, kutokana na athari za matamshi ya lugha ya Kiingereza, jina hili la Roberto lilibadilishwa na kutamkwa Roberts. Roberto au Roberts, ambaye majina yake ya Ufukwe na Selemani yalififia, alimuoa Mwanamwema binti Mwindau na kuishi naye huko Vibambani, Tanga. Mnamo tare 01 Januari 1909, wakamzaa mtoto waliyemuita Shaaban.( Ponera 2010:26).

  1.1.2 UPANDE WA MAMA YAKE

Bibi Mwanamwema binti Mwidau alikuwa ni wa ukoo wa kina Kihere (yaani Kihere Mwalimu Kihere na Mwalimu Mwalimu Kihere), ambao wanatajwa sana katika barua nyingi za Shaaban Robert (kama zilivyo limbikizwa na kuhaririwa na M. M. Mlokozi). Alikuwa ni wakabila la Kimwamwande, na alizaliwa Msengenyeni, Tanga, mwaka wa kuzaliwa haujulikani. Alifariki mwaka 1967.

Bibi Mwanamwema aliolewa mara tatu na alijaliwa kupata jumla ya watoto 14. Mume wake wa kwanza alikuwa Bwana Kibwana. Huyu alizaa naye watoto 3, wa kiume wawili na mmoja wa kike. Watoto hao ni:

(i)                 Jafari Kibwana
(ii)               Mwanagani Kibwana (mwanamke)
(iii)             Khatib Kibwana
Kipindi cha kabla ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1914-1918). Bwana Kibwana alisafiri kwenda Uganda na hakurudi. Hivyo Bibie Mwanamwema akajikuta hana mume, na ndipo alipoolewa na Bwana Selemani au Ufukwe bin Jumaa, au jina jingine Robert. Huyu alikuwa ni Myao Upande wa baba, na Mzaramo upande wa mama, na alipewa jina la “Robert” kwa heshima ya mkulima wa Kizungu ambaye baba yake, yaani Mzee Jumaa, alikuwa akifanyia kazi.
Mwanamwema alizaa na Bwana Ufukwe mtoto mmoja tu, yaani Shaaban Robert. Baadaye wakaachana. Hata hivyo, Bwana Robert alikuwa na watoto wengine kwa wake wengine, ambao ni:
(i)                 Jumaa bin Robert wa Ngamiani, Tanga
(ii)               Abdallah bin Robert wa Mnyanjani, Tanga
(iii)             Mwansaumu binti Robert wa Mnyanjani
Mume wa tatu wa Bibie Mwanamwema alikuwa ni Bwana Mwinyiulenge Mworogo. Huyu alizaa naye watoto 10-wasichana watano na wavulana watano-wafuatao:
(i)                 Mwishehe Ulenge (Mvulana)
(ii)               Mwanaidi Ulenge (msichana)
(iii)             Mwanang’andu Ulenge (msichana)
(iv)             Yusufu Ulenge (Mvulana)
(v)               Mwanahadia Ulenge (Msichana)
(vi)             Asha Ulenge (msichana)
(vii)           Mwidau Ulenge (msichana)
(viii)         Issa Ulenge (mvulana)
(ix)             Ali Ulenge (mvulana)
(x)               Maimuna Ulenge (msichana) (mulokozi: 2002:3)

1.1.3 SHAABAN ROBERT
Shaaban Robert alizaliwa tarehe 01 Januari 1909, (Wakati wa ujana wake Shaaban aliacha kuliandika jina la Roberts, akaanza kujiita Shaaban Robert), alipelekwa madrasa, shule itoayo mafunzo ya dini ya Uislamu na mama yake akiwa na umri wa miaka tisa. Huko alijifunza mambo mengi yahusuyo dini ya Uislamu kama vile Hadithi za Mtume Mohammad (ambaye ni Kiongozi wa Waislam). Alianza masomo ya elimu ya msingi mwaka 1922 katika shule ya msingi ya Kichwele (sasa inaitwa Uhuru mchanganyiko) iliyopo mjini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 13. Wakati huo, tayari alikuwa amekwishapata elimu ya dini kwa kiwango kikubwa. Aliendelea kusoma elimu hiyo ya dini hata alipokuwa anaendelea na masomo haya ya shule ya msingi. Alihitimu masomo hayo mwaka 1926 na kufaulu vizuri kwa kushika nafasi ya pili kati ya wanafunzi kumi na mmoja. Baada ya hapo, aliajiriwa na serikali ya kikoloni na kufanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali. (Ponera 2010: 27).

1.2   KAZI ALIZOZIFANYA
·         Alianza na kazi ya Ukarani wa serikali Forodhani Pangani mwaka 1926-1944.
·         Idara ya hifadhi ya Wanyamapori (Mpwapwa) mwaka 1944-1946.
·         Alifanya kazi katika Afisi ya Mkuu wa Jimbo Tanga mwaka 1946-1952.
·         Afisa wa kupima nchi Tanga (Idara ya ardhi) mwaka 1952-1960.
·         Pia kabla hajastaafu mwaka 1960, aliwahi pia kuhamishiwa Old Moshi.
Alipokuwa kazini aliheshimika katika sehemu zote alizofanya kazi kutokana na adabu, bidii na uadilifu wake.
1.3   KIFO CHAKE
Shaaban Robert alifariki tarehe 20/06/1962 katika hospitali ya Mkwakwani Tanga, Bombo na kuzikwa tarehe 22/06/1962 katika makaburi ya ukoo wa mama yake yaliyopo hapo hapo Vibambani Tanga. Alifariki akiwa na miaka Hamsini na tatu (53).
Chanzo cha kifo chake kinatajwa kuwa ni kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika. Pia wengine wanataja kuwa ni kwa sababu ya homa ya Kifua Kikuu. Alilazwa katik hospitali hiyo kwa muda mrefu akianzia katika wodi ya Kawaida kisha alihamishiwa katika wodi ya wagonjwa mahututi. (Ponera 2010:29).
1.4   MAISHA YA NDOA
Mke wa kwanza wa Shaaban Robert alikuwa ni Amina. Alimuoa mwaka 1930/1931. Aliishi naye kwa miaka kumi tu ambapo walizaa watoto wengi lakini wengi walifariki wakiwa bado wachanga.
Amina anakadiriwa kufariki mwaka 1942 (Kutokana na shairi la Amina, kutungwa Juni 1942) na kumwachia watoto wawili, ambao ni Selemani na Mwanjaa ambao walipona dhidi ya mauti ya mapema. Kutokana na ubovu wa barabara na hali mbaya ya hewa, alishindwa kusafirisha mwili wa Amina hadi Vibambani hivyo alimzika huko huko Pangani.
Baada ya kufariki Amina shaaban alitunga tenzi za Adili na Hatia kwa ajili ya Wanawe, Mwanjaa na Selemani ili zisimame pahala pa marehemu mama yao kimalezi.
Shaaban Robert alikaa takriban miaka mitatu bila ya mke hadi tarehe 14/09/1945 alipomwoa Bi Sharifa binti Hussein wa Chumbageni Tanga, ambapo pia walizaa watoto wengi ambao pia walifariki wakiwa wachanga ambapo watoto wanne tu walipona ambao ni Akili, Hussein, Mwema na Ikibali.
Baadaye Ugane ulimvaa tena Shaaban Robert, ambapo mke huyu wa pili alifariki mwaka 1955. Baada ya kifo cha mke wake wa pili alioa mke wa tatu ambaye ni Bi. Mwanambazi binti Ali. Huyu hakuzaa naye na ndiye aliyemkalia eda mara tu baada ya kifo chake tarehe 20/06/1962.
1.5   MWONEKANO WAKE WA JUMLA
Shaaban Robert alikuwa ni Mcha Mungu ambapo alikuwa Mwislamu aliyeyazingatia maamrisho na miongozo ya dini hiyo kama vile kusali sala tano na mengineyo.
Pia Shaaban Robert alipenda kufurahi nakushirikiana na watu katika kazi na shughuli mbalimbali za kijamii. Aliutumia muda wake mwingi kufanya kazi alizopanga na baada ya kazi alijikita katika kuandika.
   2.0 KAZI ZA KIFASIHI ZA SHAABAN ROBERT
Shaaban Robert ni miongoni mwa waandishi maarufu na wakongwe wa fasihi ya Kiswahili ambao wamejizolea umaarufu mkubwa kutokana na kuandika kazi mbalimbali za kifasihi zenye kutumia ufundi na unadhifu mkubwa wa lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa waandishi hao ni kama vile Amri Abeid Kaluta, Mathias Mnyampala, Ibrahim Hussein, Mohammed Said Abdulla, Penina Mhando na wengine wengi.
Shaaban Robert amejipatia sifa kubwa ikilinganishwa na waandishi wengine kwani ana sifa za kipekee/ upekee mkubwa unajitokeza katika vigezo vifuatavyo;
i.                    Idadi ya kazi zake za kifasihi ni nyingi ikilinganishwa na waandishi wengine.
ii.                  Udhati, uendelevu na uhalisi wa maudhui ya kazi zake.
iii.                Umaridadi wa ufundi wa uandishi wake.
Shaaban Robert ndiye mwandishi pekee aliyeandika na kuchapisha kazi nyingi zaidi za kifasihi ya Kiswahili kwa lugha ya Kiswahili (kazi zilizokwisha kuchapishwa mpaka sasa ni ishirini na nne 24).
Aliandika kazi zilizo katika makundi mawili ambayo ni Nudhumu na Nathari.
Kazi yake ya mwanzo kabisa kuchapishwa ni makala ya “Hirizi ya shilingi mia” ambayo ilitoka katika gazeti la Mambo Leo mwaka 1932. Baada ya hapo aliendelea kuandika kazi nyingi za ushairi na nathari katika Magazeti.
Kisha alitunga tawasifu yake “Maisha Yangu” (ambayo baadaye aliipanua na kuiita “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”).
Mwaka 1939 ilianza Vita vya Pili vya Dunia na kwisha 1945 wakati wote huo alitunga “Utenzi wa Vita vya Uhuru” wenye beti 3000. Baada ya utenzi huo alianza kutunga nathari kama vile Kufikirika, Kusadikika, Adili na Nduguze na kadhalika.
Hakuwahi kuandika kazi yoyote ya Tamthiliya (Ponera 2010).


1 KAZI ZAKE ZA NUDHUMU NI;
1.      Masomo Yenye Adili, (1959), Art & Lit, Nairobi.
2.      Utenzi wa Vita vya Uhuru (1961), Oxford, Nairobi.
3.      Kielezo cha Fasili, (1962), Nelson, Nairobi.
4.      Pambo la Lugha, (1966), Oxford, Nairobi.
5.      Insha na Mashairi, (1967), Nelson, Nairobi.
6.      Ashiki Kitabu Hiki, (1968), Nelson, Nairobi.
7.      Mapenzi Bora (1969) Nelson, Nairobi.
8.      Mwafrika Aimba, (1969), Nelson, Nairobi.
9.      Koja la Lugha, (1969), Oxford, Nairobi.
10.  Maisha ya Shaaban Robert, (1971), Nelson, Nairobi.
11.  Sanaa ya Ushairi, (1972), Nelson, Nairobi.
12.  Almasi za Afrika, (1972), Nelson, Nairobi.
13.  Tenzi za Maadili Mema na Omar Khayyam (1973), T PH, Dar es Salaam.
13. 14. 2.2 KAZI ZAKE ZA NATHARI
Kazi za nathari za Shaaban Robet zinajumuisha kazi za makundi yafuatayo;
(i)                 Barua.
(ii)               Insha.
(iii)             Hadithi Fupi.
(iv)             Riwaya za Kiwasifu.
(v)               Riwaya za Kitawasifu.
Sifa zilizotumika katika kutofautisha makundi haya (hususani hadithi fupi na Riwaya ni;
(i)                 Urefu (idadi ya maneno).
(ii)               Uchangamano wa vitushi (sahili na tata).
(iii)             Lugha iliyotumika katika nathari husika.
(iv)             Wahusika (idadi).
(v)               Dhamira (idadi na uzito).
(vi)             Mandhari (ukubwa na upana-Jiografia, historia, wakati).
Nathari za Shaaban ni kama hizi zifuatazo;
15. Adili na Nduguze, (1952), Mcmillan, Londoni.
16. Kusadikika, (1951), Nelson, Nairobi.
17. Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, (1949), Nelson, Nairobi.
18. Kielezo cha Insha, (1954), Witwatersand, Nairobi.
19. Methali na Mifano ya Kiswahili, (1997), TUKI, Dar es salaam.
20. Kufikirika, (1968), Oxford, Nairobi.
21. Utubora Mkulima, (1968), Nelson, Nairobi.
22. Siku ya Watenzi Wote, (1967), Nelson, Nairobi.
23. Wasifu wa Siti binti Saad, (1967), Nelson, Nairobi.
24. Barua za Shaaban Robert, (2002), TUKI, Dar es salaam.
2.3 UHALISI NA UBUNILIZI KATIKA KAZI ZA SHAABAN ROBERT.
Uhalisi ni ukweli wa jambo kama lilivyo, kuna ukweli wa aina mbili ambao ni;
(a)    Ukweli katika hali halisi.
(b)   Ukweli wa kisanaa (ambao husawiri mambo yaliyobuniwa na mtunzi).
   Ubunilizi, ni utengenezaji wa ukweli wa jambo kadri afikiriavyo msanii kwa kuzingatia uwezekano na azma yake. Hivyo basi yafaa ubunilizi usipitilize kwani ni rahisi kwenda mbali na jamii halisi.
   Vipengele ambavyo ubunilizi hufanywa ni kama vile;
(a)    Mandhari. Kwa mfano katika kusadikika mandhari iliyotumika ni ya kubuni ambapo tunaona nchi ya kusadikika iko hewani inaelea, inamipaka sita ambayo ni Ardhini, Mbinguni, Mashariki, Magharibi, Kusini na Kaskazini.

(b)   Wahusika. Ambapo wahusika katika kazi za Shaaban Robert wanauwezo na sifa maalumu. Kwa mfano wanasifa za aina moja tu, kama ni mwema tu au waovu tu. Kama ilivyo kwa Waziri Majivuno, Karama na kadhalika katika kusadikika. Pia wahusika hawa huundwa kwa sifa ya kutokukata tama kwa mfano karama katika Kusadikika. Vilevile wahusika wengine siyo binadamu ni majini kama wanavyojitokeza katika Riwaya yake ya Adili na Nduguze, kuna wahusika kama vile Mrefu.
(c)     Lugha. Katika kipengele hiki cha lugha kuna matumizi ya Taswira na tamathali za semi ambapo kwa mwandishi huyu Shaaban Robert ameonesha umahiri wa hali ya juu katika kipengele hiki, kuitumia lugha ya Kiswahili.

(d)   Ushikamani, katika kipengele hiki huweza kufanywa kwa kutumia mbinu kama vile;

(i)                 Ubadala mfano katika Adili na Nduguze hakumtaja sana jina la Mfalme Rai bali alimtambulisha kwa vibadala (majina mengine ya ziada).

(ii)               Urejeshi/ Kisengere nyuma. Ni ile hali ya mwandishi kuelezea hadithi Fulani kwa kuanza mbele na kurejea au kulielezea tukio la nyuma (urejeshi). Kwa mfano msuko wa matukio katika nathari ya kusadikika.

(iii)             Udondoshaji, katika Adili na Nduguze mwandishi ameidondosha habari ya mama yao Hasidi, Mwivu na Adili.

(iv)             Uunganishaji/ ujumuishaji. Mfano katika kusadikika kuna vitushi vya Salii na Sapa, safari za Ndege Mangere na kadhalika (kitushi ndani ya kitushi).
Hivyo basi kazi za Shaaban Robert zina mseto wa uhalisi na ubunilizi ambapo kazi zake za mwanzo zina kiasi kikubwa cha ubunilizi. Mfano Kufikirika, Kusadikika na Adili na Nduguze. Ambapo ubunilizi huo unajidhihirisha katika kipengele cha Lugha, Mandhari, Wahusika na namna ya kushikamanisha vitushi vyake ambapo Shaaban Robert ametumia mbinu mbalimbali kama vile Utomelezi, Taharuki, Ujadi na kadhalika.
Kazi zake za uzeeni zina ukweli kwa kiasi kikubwa sana. Kwa mfano Utubora Mkulima na Siku ya Watenzi Wote.
MBINU ZA KIBUNILIZI KATIKA KAZI ZA SHAABAN ROBERT NI;
(i)                 Ujadi.
(ii)               Ufutuhi.
(iii)             Utomelezi.
(iv)             Taharuki.

(I)                MBINU YA UJADI
Ni utumizi wa kauli za Kiutamaduni, kauli zilizozoeleka sana na jamii katika matumizi yao ya kila siku.
Vipengele vya Ujadi ni kama vile, methali, misemo, tamathali za semi. Vilevile mtunzi huweza kuiga kaida maalumu za uzungumzaji ambazo hutumiwa na wazungumzaji wa jamii yake. Mbinu hii ya ujadi husaidia kumweka mtunzi karibu zaidi na hadhira yake.
(II)             MBINU YA UFUTUHI
Ufutuhi ni hali ijengwayo na maneno, matukio au mazingira yoyote yenye mvuto au yasiyo ya kawaida yenye kuwafanya watu watabasamu au wacheke. (Ponera 2010:6).
Hii ni mbinu ambayo mtunzi hutumia maneno au hali nyingine inayoweza kusababisha hadhira yake kupata kicheko/ Ucheshi.
  Mfano: Ufutuhi wa majazi katika “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”.
                Mume ni mume ingawa gumegume ana sifa ya mtume;
               Na mke ni mke ingawa kikwekwe ana manufaa yake. (uk 101).
Tukio hili linazungumzia umuhimu wa maisha ya ndoa kwa mwanadamu. Majina ya “Gumegume” na “Kikwekwe” yanamaanisha sifa za kutokusikiliza na hali ya kukosa utulivu wa kiakili na kimaadili ya ndoa (Ponera 2010).
(III)          UTOMELEAJI
Ni kitendo cha kuchukua vipande vya kazi za utanzu mwingine na kuuingiza katika hadithi. Kwa mfano nathari ya Shaaban Robert ya “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”, utomeleaji umejitokeza kwa kiwango cha juu katika ukurasa wa 4-5 katika shairi la Amina, ukurasa wa 6-20 katika Utenzi wa HATI, ukurasa wa 21-35 Utenzi wa ADILI. Mbinu hii hutumika ili ku’nogesha kazi yake pia kutia msisitizo juu ya jambo Fulani.
(IV)          TAHARUKI
Ni hali ya kuwa na dukuduku la kutaka kujua nini kitafuata katika usimulijia wa hadithi au riwaya. Mbinu hii mtunzi huitumia ili kuamsha hamu ya msomaji kufatilia kisa kinachosimuliwa katika riwaya au tamthiliya fulani. Mbinu hii Shaaban Robert ameitumia kama kijenzi kimojawapo katika utunzi wake. Imejitokeza kwa kiasi kikubwa katika kazi zake nyingi kama vile “Kufikirika”, ambapo tunaona namna alivyounda matukio yake kwa namna ya kutia hamasa kuendelea kufuatilia kisa kwa ukaribu zaidi. Katika Kufikirika tunaona alivyokijenge kisa cha Mfalme na Malkia kuwa matasa, nathari hii ina muundo ufuatao; Mwanzo, Mfalme, Waganga, Matokeo ya Utabili, Mtoto wa Mfalme, Kafara, Baraza na Gereza.
3. MAWAZO AU MTAZAMO WA SHAABAN ROBERT KATIKA MAISHA
Mtazamo ni jinsi ya kuyatazama au kuyaona mambo na mwelekeo wake. Katika kazi za Shaaban Robert zinaonesha kuwa mwandishi aliandika kwa kugusia karibu kila Nyanja ya maisha ya mwanadamu. Baadhi ya mambo hayo ni ukombozi na maendeleo ya nchi, udugu na familia, mapenzi, dini, umuhimu wa elimu, utu, ujumi wa kiafrika na kadhalika.
3.1. UTU
Maisha ya binadamu pasipo utu, hukosa thamani. Baadhi ya maswali yanayoonekana kumshughulisha Shaaban Robert katika maandiko yake ni kama vile Utu ni nini? Utu hujengwa wakati gani? na utu hupatikanaje? Utu wa mtu hujengwa na matendo yake mwenyewe kila siku. Shaaban Robert alilijua vema suala hili na alilichukulia kwa hadhari kubwa kama asemavyo katika nathari yake;
Hapa Shaaban anasema; “Wakati mmoja nilifikiri kuwa yote yaliyo azizi au bora kwa mtu ni matendo yake aliyotenda zamani; na kwa kuwa mimi sikupata kutenda tendo lo lote la maana nilijiona sawa kabisa na maskini. Wazo hili lilibatilishwa na fikira kuwa pengine ubora wa mtu huwezekana kuwa katika wakati ujao”. (Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini: uk 1)
3.2 SHAABAN NA DINI
Shaaban Robert alikuwa Muislamu hivyo aliakikisha pia wote wanaomzunguka pia wanaelekea katika njia ya kidini, Shaaban aliamini kuwa dini ndio msingi wa amani duniani, mkwa mfano aliwahusia wanawe kushika dini katika Tenzi zake za HATI na ADILI.
Kwa mfano katika Utenzi wa HATI anamwambia Mwanjaa na Walimwengu wote kwamba;
    27 Shikamana na ibada,
          Kutimiza kila muda,
          Na kesho ina faida,
          Ikisha hii dunia.

   28  Dini mali ya roho,
         Mwilini kama joho,
         Unapoteza uroho,
         Na anasa za dunia. (Maisha Yangu na Baada Ya Miaka Hamsini, uk 10).
Pia katika kitabu hichohicho ukurasa wa 22 anamuhusia mtoto wake wa kiume Selamani juu ya umuhimu wa dini katika maisha yake.
Vilevile alisisitiza uhuru wa kuabudu (Siku ya Watenzi Wote, ukurasa 111), Dhima za dini (Siku ya Watenzi Wote, ukurasa 16 na 63), Unafiki katika dini (Siku ya Watenzi Wote, ukurasa 10, 36 na 102). Hivyo basi suala hili kwa Shaaban Robert aliliona ni la msingi na lenye umuhimu mkubwa katika maisha ya Mwanadamu akiwa hai hapa duniani.
Pia alitoa maonyo na maelekezo mengi kwa mdogo wake Yusufu Ulenge juu ya suala hili la dini. Katika barua yake ya tarehe 24/07/1931 aliyomwandikia Yusufu Ulenge anadhihirisha hilo. Barua hii ipo katika Barua za Shaaban Robert 1931-1958, barua namba 5 ukurasa wa 32.
3.3 SIASA NA UKOMBOZI
Dhamira halisi ya Shaaban Robert kupitia maandiko yake haikuupenda ukoloni wala wakoloni wenyewe. Wahakiki wengi wanamtazama Shaaban Robert kuwa na mawazo ya hali mbili, uchanya na uhasi kuhusu Ukoloni. Wapo wanomwona kama mpinga ukoloni. Wengine wanamwona kama alikuwa msaliti/ mwoga juu ya ukoloni.
Katika kazi yake ya “Utenzi wa Vita vya Uhuru”, tunaona Mawazo ya Shaaban Robert juu ya Ukoloni. Utenzi huu umezungumzia tukio zima la vita hivyo. Yeye alijiegemeza katika upande wa Waingereza kama asemavyo bayana katika “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini” ukurasa wa 64-65. Hapa Shaaban Robert anasema;
 “…. Mimi si raia wa Jerumani, ni raia wa Uingereza…”.
Hili ni mojawapo ya mambo yaliyozua mjadala kwa wahakiki kuhusu Utanganyika wake, wanadai Shaaban Robert aliwatukuza wakoloni. Maudhui ya utenzi huu huenda yaliathiriwa na lengo lake la kumtabarukia Mudir wa Elimu wa kikoloni kipindi hicho Bwana S. N. Eliufoo.
Mbali na utenzi wa Vita vya Uhuru, Shaaban Robert amezungumzia ukoloni na siasa katika kazi zake za “Kusadikika” na “Kufikirika”. Shaaban amefafanua mengi kuhusu adha za Ukoloni na Wakoloni, kwa mfano katika Tawasifu yake ya “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini” ukurasa wa 50-51, anaeleza naman alivyobaguliwa yeye na watoto wake pale aliposhushwa kutoka katika Lori la Abiria cheo cha pili ili kuwapisha Wahindi waliokuwapo ambao walikosa sehemu ya kukaa kutokana na nafasi katika Lori hilo kujaa.
SHAABAN ROBERT NA SUALA LA JINSI NA JINSIA
JINSI, ni tofauti ya kimaumbile inayojidhihirisha katika via vya uzazi na hivyo kuwatofautisha watu katika makundi ya wanawake na wanamume.
JINSIA, ni dhana ya Kisosholojia. Hii inahusu mgawanyiko wa Majukumu baina ya Mwanamke na Mwanamume.
·         Shaaban Robert amelizungumzia sana jambo hili katika kazi zake zote. Katika Barua za Shaaban Robert, kuna waraka namba 11.9 katika ukurasa wa 196. Shaaban aliandika Waraka huu kwa Bwana mtengenezaji katika gazeti la Mambo Leo, aliupa jina la“UKIJUA KUOA NA KUACHA UJUE”’.
·         Vilevile suala hili amelijadili sana kwenye kitabu chake cha “Wasifu wa Siti Binti Saad”. Siti ameonekana kuwa mfano mwema wa wake watakiwao Afrika ya Mashariki na Afrika kwa ujumla.
·         Katika nathari yake ya “Kusadikika”, anasema; “…..hapana haja ya kudharau mwanamke. Wanawake ni Malaika, makao yao sawa na yale ya pepo…”
·         Pia katika “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”, tunamuona jinsi alivyomsifu Amina ukurasa wa 3. Vilevile anaendelea kumchora kwa kumtetea mwanamke katika ushairi wake. Kwa mfano katika Utenzi wa HATI katika “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”, pia na katika “Pambo la Lugha” katika shairi lisemalo “Mwanamke si Kiatu” (uk 19). Hivyo basi kwa ujumla maoni na kilio cha Shaaban Robert katika suala hili tunapata katika kuchunguza kazi zake zote ambapo anawatetea na kuwalalamikia wanaume kuwa ni watesi na wanyanyasaji wa wanawake. Pia katika maandiko ya Shaaban Robert hakuna andiko hata moja linalomzungumzia mwanamke vibaya.
3.5 LUGHA
Shaaban Robert katika kipengele cha lugha anabainika kama Mwalimu na mtetezi wa lugha, hii ni kutokana na maudhui yanayopatika kutoka katika kazi zake mbalimbali alizozifanya. Kwa mfano katika kitabu chake cha “Insha na Mashairi”, kuna Insha mojawapo ya “Lugha ya Tifa” (uk 25). Katika “Siku ya Watenzi Wote” (uk 41) anasisitiza umuhimu wa mtagusano wa lugha hususani katika kufanya tafsiri.
Pia katika ‘Diwana ya Almasi za Afrika”, kuna shairi la “Kiswahili 1” na “Kiswahili 2’ (uk 59-60), pia shairi la “Kitakoma Kiswahili” (uk 65). Vilevile katika barua zake anajitokeza mara kadhaa kumkosoa Yusufu kuhusu tahajia ya Kiswahili. Katika kazi hizo Shaaban Robert anajitokeza waziwazi kufundisha, kukemea na kurekebisha unapotokea upotoshaji wa matumizi ya Kiswahili.
3.6 UJUMI NA KITAMBULISHO CHA MWAFRIKA
Ujumi ni hali/ taaluma ya masuala ya kutambua uzuri na au ufahamu wa kitu.
Shaaban Robert alikuwa Mwafrika, aliupenda Uafrika wake na mambo yote yaliyoambatana na hali hiyo. Ithibati za kuuthamini Uafrika wake inajitokeza katika kazi zake mbalimbali kama vile;
“Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini” uk 98-100, kupitia utenzi wa ADILI kajitambulisha kuwa yeye ni Mwafrika. Pia katika uk 50 anasema “…Abiria Waafrika tulikua mimi na watoto wangu…”
Pia katika “Wasifu wa Siti Binti Saad” anabainisha utamaduni na Falsafa ya mwafrika wa Kiafrika.
Majina ya Diwani zake “Almasi za Afrika” na “Mwafrika Aimba”, licha ya majina humo pia kuna mashairi yasemayo juu ya suala hili. Kama vile “Istaklahi ya Tanganyika” na ‘Fahari ya nchi yangu”. Hivyo Shaaban Robert ni Mzalendo wa dhati kwani katika kazi zake anaonesha hilo kwa kutete nchi yake na bara lake, rangi yake, utamaduni wake (Kiswahili alichokipenda ni sehemu ya utamaduni), Mila na Desturi zake, Vyakula vya Kiafrika pamoja na Wanawake wa Kiafrika.
3.7 SHAABAN ROBERT NA MAPENZI
Shaaban Robert amejadili kwa kina mapenzi katika vipengele vya maana halisi ya Mpenzi, aina za mapenzi, wapi kwa kuyapata mapenzi, mtazamo wake kuhuzu watu wanavyo ya chukulia mapenzi, faida na hasara za mapenzi.
Mapenzi anayoyajadili Shaaban Robert ni Pamoja na yale ya Kiumbe kwa Muumba wake, mzazi kwa mtoto au mtoto kwa mzazi, ndugu kwa ndugu, Ya ndoa, Jamii na Wananchi kwa nchi yao, Mapenzi ya dhati na ya chati. Katika diwani yake ya “Mapenzi Bora” suala hili la Mapenzi limejadiliwa kwa undani sana.
Mapenzi ya ndugu kwa ndugu tunayaona katika nathari ya “Adili na Nduguze”, ambapo Adili alikuwa akiwapenda sana ndugu zake Mwivu na Hasidi kiasi cha kuwagawia mali zake nusu kwa nusu pale walipofilisika.
4.0 ITIKADI YA SHAABAN ROBERT
Itikadi ya Shaaban Robert ni Usoshalisti uliopea, ijapokuwa si katika hali ya kuufikia Ukomunisti. Itikadi hiyo inasawiri hatua ya juu ya Usoshalisti unaoelekea kwenye Ukomunisti (Chuachua 2010: 180)
5.0 FALSAFA YA SHAABAN ROBERT.
Shaaban Robert anaamini kuwa wema hushinda dhidi ya ubaya. Hii inajidhihirisha katika kazi zake nyingi ambazo mwisho wake huonesha watendewao ubaya huwashinda waovu na kupata haki. Mfano kama inavyojidhihirisha katika Kusadikika, Kufikirika, Adili na Nduguze na kadhalika.
6. MCHANGO WA SHAABAN ROBERT KATIKA FASIHI YA KISWAHILI.
Shaaban ni kiungo dhabiti baina ya fasihi ya kale na ya sasa. Shaaban Robert ni miongoni mwa waandishi wa mwanzo katika fasihi ya Kiswahili na waliotumia nguvu kubwa katika uandishi ilikuitoa fasihi ya Kiswahili sana sana utanzu wa nathari kutoka katika hali ya kihekaya na kuuingiza utanzu huu ili usawiri maisha halisi ndani ya jamii ya waswahili.
Shaaban Robert ni mmoja kati ya waasisi wa uandishi wa nathari za kitawasifu katika fasihi ya Kiswahili kupitia tawasifu yake ya “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”. Tawasifu hii yenye sehemu kuu mbili yaani “MAISHA YANGU” na ‘BAADA YA MIAKA HAMSINI”, inajumla ya kurasa 124. Katika sehemu ya kwanza ya Tawasifu hii (MAISHA YANGU), imebeba sehemu kumi na tatu (13) ambazo ni Umri, Maisha ya nyumbani, Utenzi wa Hati, Utenzi wa Adili, Mke wa pili, Idara ya forodha, Uhamisho, Mapumziko, Abiria cheo cha pili, Idara ya utunzaji wa Wanyama, Naondoka Mpwapwa, Idara ya Utawala na Nilikuwa mshairi. Sehemu ya pili (BAADA YA MIAKA HAMSINI), inasehemu zifuatazo Bima, Siasa, Mwandishi, Ukinzani, Kustaafu, Msuso, Upigishaji chapa na Matukio.
Shaaban Robert, pia ni mmoja kati ya waandishi waliochangia sana katika maendeleo ya nathari ya   Kiswahili. Baadhi ya nathari bunilizi zake ni; Adili na Nduguze, (1952), Kusadikika, (1951), Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, (1949), Kielezo cha Insha, (1954), Methali na Mifano ya Kiswahili, (1997), Kufikirika, (1968), Utubora Mkulima, (1968), Nelson, Nairobi. Siku ya Watenzi Wote, (1967), Nelson, Nairobi. Wasifu wa Siti binti Saad, (1967).
Alikuwa na mchango mkubwa, katika fasihi ya Kiswahili. “Wasifu wa Siti Binti Saad”. Ni moja kati ya nathari za kwanza kabisa za kiwasifu. Nathari hiyo inaeleza Maisha ya mwanamuziki mashuhuri wa Taarab Afrika ya Mashariki “Siti Binti Saad”.
Ndiye aliyeizindua hadhira ya kazi za fasihi ya Kiswahili kuhusu matumizi ya vionjo vya fasihi simulizi katika fasihi andishi.
Ni miongoni mwa waandishi wa wakati wake walioandika na kuchapisha kazi nyingi zaidi za fasihi ya Kiswahili.
HITIMISHO
Shaaban Robetr ni miongoni mwa wanafasihi waliyoiletea heshima kubwa tasnia ya fasihi ya Kiswahili. Kazi zao zimekuwa Lulu na mwongozo kwa wanafasihi wanaochipukia katika uga wa fasihi ya Kiswahili. Msimamo wake wakuwa mwanamapokeo ulikuwa ni msimamo wa wastani kwani sio wakati wote alizitumia kanuni za kimapokeo, alizitumia kanuni hizi pale ilipobidi na pale alipotaka kuziacha aliziacha.Vilevile Shaaban Robert kupitia kazi zake amewasaidia wanazuoni wengi kufikia malengo ya kielimu, waandishi wakongwe kama E. Kezilahabi ametumia nathari za Shaaban Robert katika tasnifu yake ya Shahada ya Uzamili.






                                       MAREJEO
Robert, S, (1949), Maisha Yangu na Baada ya Miaka HamsiniNelson, Nairobi.

                 (1951), Kusadikika, Nelson, Nairobi.

                 (1952), Adili na Nduguze, Mcmillan, Londoni.

                 (1954),  Kielezo cha Insha, Witwatersand, Nairobi.

                 (1967), Siku ya Watenzi Wote, Nelson, Nairobi.

                  (1967), Wasifu wa Siti binti Saad, Nelson, Nairobi.

                  (1968), Kufikirika, Oxford, Nairobi.

                 (1968), Utubora Mkulima, Nelson, Nairobi.

                 (1997), Methali na Mifano ya Kiswahili, TUKI, Dar es salaam.

                 (2002), Barua za Shaaban Robert, TUKI, Dar es salaam.
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni