Jumamosi, 19 Machi 2016

MCHANGO WA SHAABAN ROBERT KATIKA TAALUMA YA TAFSIRI



Ikisiri
Kazi hii inahusu mchango wa Shaabani Robert katika taaluma ya tafsiri. Katika uga wa fasihi jina la Shaaban Robert limekuwa na mwangwi katika masikio ya wanataaluma wengi hususani taaluma ya fasihi. Katika makala hii tutajadili mchango wake katika taaluma ya tafsiri. Makala hii imegawika katika sehemu kuu tatu, nazo ni utangulizi, kiini na kifungio. Katika utangulizi; tutaangazia historia ya Shaaban Robert kwa ufupi tukidondoa kuzaliwa kwake, ndoa, kazi alizowahi kufanya na mazao ya kazi zake za kibunilizi. Vilevile tutatupia jicho tu dhana yenyewe ya tafsiri kwa kuangalia maana na chimbuko lake. Kiini cha makala hii tutajadili mchango wake katika taaluma ya tafsiri. Na sehemu ya mwisho ni hitimisho. Data za makala hii zimetokana na rejea mbalimbali zikiwemo tafiti, vitabu na makala mbalimbali kuhusu mada tajwa. Aidha tumeona kuwa, Shaabani Robert achilia mbali kuwa ni maarufu katika taaluma ya fasihi, bali pia anamchango mkubwa katika taaluma ya tafsiri.

1.0 Utangulizi
Taaluma ya tafsiri ni taaluma kongwe ukilinganisha na taaluma zingine, kuwapo kwa taaluma hii ndio imepelekea taaluma zingine kueleweka kwa urahisi zaidi. Tumekuwa tukishuhudia maendeleo mbalimbali ya elimu yakipiga hatua kwasababu ya tafsiri. Taaluma kama za sayansi zimeweza kupiga hatua kwa sababu ya tafsiri. Shaabani Robert aliona umuhimu wa taaluma ya tafsiri hivyo alijitosa katika taaluma hii ya tafsiri kinadharia na kivitendo katika fasihi ya Kiswahili. Katika sehemu hii tutaangalia historia ya Shaabani Robert kwa ufupi na dhana ya tafsiri kwa ujumla wake.

1.1 Historia Fupi ya Shaabani Robert
Hapa tutaangalia mambo mbalimbali yamuhusuyo  Shaabani Robert ikijumuishwa  na kuzaliwa kwake, ubini na mbari yake, elimu yake, kazi alizowahi kufanya, tuzo alizowahi kupata, kazi zake za kiuandishi  hali yake ya kindoa na kifo chake.

1.1.1 Kuzaliwa
Shaaban Robert alizaliwa tarehe 1/9/1909, Mtaa wa Vibambani, kijijini Machui, mkoani Tanga na kufariki tarehe 20 Juni 1962 Katika hospitali ya Bombo mjini Tanga, na kuzikwa tarehe 22 Juni 1962 katika makaburi ya familia huko Vibambani, Machui mkoani Tanga. Ni mwana wa nne kwa Bi Mwanamwema kati ya wana 14 na alikuwa mwana wa kwanza kwa baba yake Bwana Suleimani Ufukwe Robert.

1.1.2 Asili ya Majina ya Baba wa Shaaban
Ufukwe, Suleiman, Robert yote ni majina ya baba yake Shaaban, hivyo Shaaban alikuwa anaitwa Shaaban bin Robert, Shaaban bin Suleiman pia Shaban bin Ufukwe.

1.1.2.1 Asili ya Jina la Shaaban Ufukwe
Aliitwa Shaban Ufukwe kwa sababu bibi wa Shaaban alipatwa na uchungu wa uzazi wa baba yake Shaaban akiwa ufukweni akitanda uduvi, hivyo ni jina la kihistoria ya kuzaliwa kwake alilopewa na watani wakimaanisha historia ya kuzaliwa kwake na hivyo kuitwa Ufukwe.

1.1.2.2 Asili ya Jina la Shaaban Robert
Aliitwa Shaabani Robert kwa sababu, babu wa Shabani Robert alikuwa anafanya kazi katika mashamba ya minazi ya wakoloni, hivyo bosi wa babu yake yaani baba wa Ufukwe alifurahi kusikia mfanya kazi wake kapata mtoto wa kiume na aliona aitwe Roberto kwa kuwa yeye jina lake lilikuwa Roberto. Hivyo baba wa Shaabani aliitwa Roberto yaani jina la bosi wa babu yake Shaabani. Lakini kutokana na usomaji wake jina hilo lilipokea mabadiliko yakimatamshi kwa kuwa alisoma shule za waingereza walilibadilisha jina la Roberto kuwa jina la Robert.

1.1.2.3 Asili ya Jina la Shaaban Suleimani
Jina la Suleimani, ni jina la kiimani. Babu wa Shaaban alikuwa ni muislamu kwa hiyo alimpa jina hilo kutokana na imani yake ya kidini. Mwanamwema bint Mwindau ndie mzaa chema ni mama wa Shaabani Robert, alikuwa ni mmwamwande lakini alijiita mswahili. Alitokea katika ukoo wa Mwalimu Kihere.

1.1.3 Elimu yake
Mara baada ya kufikisha miaka 9 mama wa Shaabani Robert alimpeleka madrasa na kupata elimu ya dini ya kiislamu. Baada ya kifo cha Mzee Ufukwe 14/09/1918 Shaban Robert alipelekwa Dar es salaam kwa babu yake aliyeitwa mzee Juma bin Kanduru aliyetokea katika ukoo wa Chemataka huko Tunduru. Babu yake alimpeleka shule iliyoitwa Kichwele ambayo kwa sasa inaitwa Uhuru Mchanganyiko hapo alisoma kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la nne kuanzia mwaka 1922 hadi 1926.

1.1.4 Kazi za Kiserikali (Utawala) Alizofanya
  •        Forodha TRA- Dar es Salaam, Arusha na Tanga,
  •         Idara ya Wanyama pori- Tanga (1944-1946)
  •         Idara ya Kupima Ardhi (Afisa wa kupima Ardhi) na kustaafu 1960

1.1.5 Tunzo Alizotunukiwa
  •                   Tuzo ya uandishi bora ya Margaret Wrong Prize
  •                  Tuzo ya mjumbe wa himaya ya uingereza
  •    .            Tuzo ya mwandishi bora wa wizara inayosimamia utamaduni nchini Tanzania

1.1.6 Kuhusu Ndoa
Alibahatika kuwa na wake wa tatu katika vipindi tofautitofauti, Amina, Sharifa binti Husein na Mwanambazi bint Alii. Amina (1930-1931) alitokea ukoo wa mwalimu Kihere), walizaa watoto wengi waliobahatika kuishi ni wawili, yaani Mwanjaa na Suleimani. Amina Alifariki 1942. Sharifa binti Husein alimuoa 1945 aliyetokea Chumbageni Tanga alizaa nae watoto wanne Akili, Hussein, Mwema na Ikibari. Mke huyu alifariki 1955. Mwanambazi binti Alii, alitokea Tongoni Tanga, hakuzaa na ndiye aliyemkalia eda Shaabani na alifariki baada ya mwaka mmoja kufariki Shaaban 1964 (Kielelezo cha Fasili, 1962: i-xii).

1.1.7 Kazi Zake za Kiuandishi (Taaluma)
Kazi yake ya kwanza aliitoa mwaka 1932 katika gazeti la mamboleo uk 34. Ilikua barua kwa mhariri. Kazi hii aliipa jina la Hirizi ya Shilingi Mia. Ilihusu kupinga ushirikina inapatikana katika kitabu cha barua za Shabani Robert ukurasa 191 waraka wa 11.3. Baada ya kazi hii Shaban Robert alifanikiwa kutunga vitabu vya ushairi na nathari. Hata hivyo kumekuwa na msigano wa kidondozi kuhusu kazi hizi kutokana na baadhi ya wataalamu kutofautiana katika kuidadisha na kudondoa kazi zake. Kwa mfano, Sengo (1975), Kezilahabi (1976) pamoja na Gibbe (1980) wanasema kuwa jumla ya kazi zilizotungwa na Shaaban Robert na zilizochapishwa ni 22, ambazo 14 ni ushairi na 8 ni za nathari. Vilevile kuna kundi la waandishi wa hivi karibuni kama vile Mulokozi (2002), Chuachua (2008) na Ponera (2010) wanaidadisha maandiko yake kuwa ni 24 ikiwa 14 ni ushairi na 10 ni nathari (Ndumbaro, 2014). Zifuatazo ni kazi za Shaaban Robert kama zinavyoainishwa na Ponera (2010).

1.1.7.1 Ushairi
Aliwahi kuandika vitabu vya ushairi takribani 14, vitabu hivyo ni;
  • ·         Almasi za Afrika (1971), Nelson, Nairobi
  • ·         Koja la lugha(1969), Nelson, Nairobi
  • ·         Insha na mashairi,(1967), Nelson, Nairobi
  • ·         Kielelezo cha Fasili, (1962), Nelson, Nairobi
  • ·         Pambo la Lugha, (1968), Oxford, Nairobi
  • ·         Ashiki Kitabu Hiki, (1968), Nelson, Nairobi
  • ·         Mashairi ya Shaban Robert, (1971), Nelson, Nairobi
  • ·         Sanaa ya Ushairi, (1972), Nelson, Nairobi
  • ·         Mwafrika Aimba, (1969), Nelson, Nairobi
  • ·         Masomo Yenye Adili, (1959), Art & Literature, Nairobi
  • ·         Mapenzi Bora, (1969), Nelson, Nairobi
  • ·         Tenzi za Marudi Mema na Omar Khayyam(1973), TPH, Dar es Salaam
  • ·         Utenzi wa Vita vya Uhuru(1961), Oxford, Nairobi
  • ·         Almas za Afrika na Tafsiri ya Kingereza (1960), Art & Literature, Nairobi

1.1.7.2 Nathari
Kwa upande wa nathari hakuwahi kuandika tamthiliya bali  aliwahi kuandika riwaya zipatazo 9 nazo ni;  
  •   Maisha yangu na baada ya miaka hamsini, (1949), Nelson, Nairobi 
  •   Adili na Nduguze,(1977) TPH, Dar es Salaam 
  •   Kusadikika (1951),Nelson, Nairobi 
  •    Kufikirika (1968) Nelson, Nairobi  
  •   Wasifu wa Siti bint Saad (1967) Art & Literature, Nairobi 
  •  Utu bora mkulima,(1968) Nelson, Nairobi 
  •  Siku ya watenzi wote (1968) Nelson, Nairobi 
  •  Barua za Shabani Robert 1931-1958 (2002), TUKI, Dar es Salaam 
  • Kielelzo cha Insha (1954) Witwatersrandd, Nairobi 
  • Mithali na mifano ya Kiswahili, (2007), TUKI, Dar es Salaam

1.2 Ufafanuzi wa Istilahi (Dhana)
1.2.1 Dhana ya Tafsiri
Dhana ya tafsiri imekuwa ikijadiliwa na wataalamu wengi. Mwamsoko (2006) akimnukuu Cartford (1965) anasema kuwa tafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka katika lugha nyingine (lugha lengwa). Pia Newmark (1982) anajadili dhana ya tafsiri kama mchakato wa uhawilishaji wa maneno kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa.  Nida na Taber (1969) wanaeleza kuwa tafsiri hujumuisha kuzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe vya asili vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi kimaana na kimtindo. Wao wanatilia mkazo uzalishaji upya wa ujumbe kwa kutumia visawe asili vinavyokaribiana na matini chanzi kimaana na kimtindo. Kutokana na maana hizi tunaweza kusema kuwa,  tafsiri ni ujumbe uliopo katika maandishi ambao asili yake si lugha ya matini inayosomwa.

Mwansoko na wenzake (2006), wanaeleza kuwa tafsiri ni zoezi la uhawishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine. Wao wanatilia mkazo katika zoezi la uhawishaji na kinachohawilishwa ni mawazo katika maandishi. Kwahiyo tunaona suala la umaandishi linajitokeza katika fasili ya Mwansoko, Cartford. Lakini tukichunguza fasili ya Nida na Taber wao wanasisitiza zaidi maana na kutobadilisha mtindo uliopo katika lugha chanzi.

Kwa ujumla suala la tafsiri lazima lichangamane na uwepo wa lugha mbili yaani chanzi na lengwa, pia kuwe na mchakato wa ubadilishaji wa lugha ya awali na kuweka katika lugha mpya bila kupoteza maana na tena kuwe na suala la kutokubadilika kwa mtindo na muundo wa kazi ya lugha chanzi.

1.2.2 Chimbuko la Tafsiri
Kihistoria, taaluma ya tafsiri inaanzia nchini Misri ambako ndio chimbuko la elimu za kale na kitovu cha maendeleo yote tuliyonayo sasa. Inasadikiwa kuwa miaka 3000 kabla ya Kristo nchi ya Misri iliendelea kwa taaluma za kisayansi na nyingi za kisasa. Ugunduzi na ustaarabu ulioletwa na wamisri kutokana na tafsiri ya elimu ya kale na kuwekwa elimu hiyo katika lugha ya Kiarabu. Ustaarabu huo uliigwa na Wayunani na kuwa ndio sababu ya maendeleo barani Ulaya. Baada ya kufasiri kazi mbalimbali zilizoporwa huko Misri wakati wa vita vya msalaba kati ya Waislamu na Wakristo katika karne ya 15, bara la Ulaya lilianza kujibabadua katika zama za giza na kuingia katika kipindi cha ufufumko. Katika karne ya 19 kazi nyingi zilitafsiriwa na karne ya 20 ndiyo inasadikiwa kuwa ndio karne ya tafsiri iliyopelekea maendeleo ya haraka ya kisayansi na kiteknolojia.
Nchini Tanzania taaluma ya tafsiri haina historia ndefu ilianzia katika karne ya 19. Tunaweza gawa mapito matatu ya tafsiri nchini Tanzania; kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya uhuru.

1.2.2.1 Kabla ya Ukoloni
Mwansoko (1996) katika Mshindo (2010) anadai kuwa utenzi wa Hamziyya ndiyo utenzi wa kwanza kutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili kutoka katika lugha ya Kiarabu. Utenzi huu ulitungwa huko Misri karne ya 13. Utenzi huu ulijulikana kwa lugha ya Kiarabu kwa jina la Al basiry, Qasida Ummal Qura. Aidarus bin Athmani ndiye aliyekuwa mfasiri wa utenzi wa Hamziyya aliyeishi miaka 1700 hadi 1750 nchini Kenya. Pia Wamisionari walifasiri vitabu vya dini ya kikristo kutoka katika lugha ya Kiingereza na kwenda katika lugha ya Kiswahili na lugha zingine za makabila.

1.2.2.2 Wakati wa Ukoloni
Wakati wa ukoloni, waingereza walitafsiri maandiko mbalimbali ya taaluma ya fasihi ya ulaya kwa lugha ya Kiswahili. Riwaya ya Mzimu wa Watu wa Kale ilitafsiriwa kutoka katika lugha ya Kiingereza iliyoitwa Shrine of The Ancestor na kazi kama vile Hekaya za Abunuwasi, Alufulela Ulela, Hadithi za Ethopo na Safari Za Guliver nazo zilitafsiriwa.

 1.2.2.3 Baada ya Uhuru
Baada ya uhuru kuanzia mwaka 1961 walijitokeza wataalamu mbalimbali waliotafsiri kazi mbalimbali na kutoka katika lugha mbalimbali na kuwa katika lugha ya Kiswahili. Mwalimu Julias Nyerere hatutajitanibu kumtaja katika taaluma ya tafsiri kwani alitafsiri vitabu kadhaa kuwa katika lugha ya Kiswahili. Kazi za Shakespare kama vile The Mechant of Venis na kuwa Mabeperi wa Venisi na Julius Caesar na kuwa Julias Kaizari. Licha ya Nyerere wapo waandishi kama Paul Sozigwa aliyetafsiri Songs of Lawino pia East African Literature Bureau 1967 walitafsiri kazi ya The Freeing of The Slaves in East Africa na kuwa Uhuru wa Watumwa. Baada ya kazi hizo kazi nyingi zilizotafsiriwa ziliongezeka. Baadhi yazo ni kama vile Nitaolewa Nikipenda Kilichotafsiriwa na Clement M. Kabugi mwaka 1982 kutoka katika lugha ya Kiingereza (Mwansoko na Wenzake; Mshindo).
2.0 Mchango wa Shaaban Robert katika Taaluma ya Tafsiri
Pamoja na Shaaban Robert kuwa maarufu sana katika taaluma ya fasihi hadi kufikia kupewa lakabu ya ubaba, pia amejitokeza katika taaluma ya tafsiri. Robert anaonekana katika uga huu wa tafsiri kutokana na maandiko yake binafsi aliyoandika kuhusu tafsiri japo kwa kudokeza, pia kufanya kazi yenyewe ya kutafsiri, halikadhalika kuchopeka dhamira za kitafsiri katika baadhi ya kazi zake za kinathari. Hapa tutagawa mchango wake katika taaluma hii ya tafsiri katika nukta kuu tatu, kwanza maandiko ya kitafsiri au mazao ya kazi za tafsiri, pili nadharia kuhusu tafsiri, na tatu ni usanaji wa dhamira za kitafsiri. Na aya zifuatazo zitachanganua kwa uwazi juu ya nukta hizo.

2.1 Mchango Katika Nadharia za Tafsiri
Katika kipengele hiki tutadondoa mchango wa kinadharia ambao Robert ameweza kuutoa katika kitabu chake cha Kielelezo cha Fasili. Robert ameonekana kutolea ufafanuzi dhana ya tafsiri, umuhimu, mbinu, aina zake na miiko ya kazi ya tafsiri. Anatoa maaana ya tafsiri kuwa ni “fasili ni maelezo ya fikira na maoni katika karaa, aghalabu ya mashairi kwa usemi mwepesi wa mjazo. Ni taaluma katika maandiko ya luha na fahamu ya fikira za mwandishi na msomaji”.
Katika nukuu hii tunaona namna Shaaban Robert anavyozungumzia na kuifafanua maana ya tafsiri. Ijapokuwa upo upungufu kidogo wa kitaajia katika neno ‘fasili’ lakini mawazo aliyoyatoa tunaona yanabeba dhana ya tafsiri. Pia Robert anaona kuwa tafsiri bora ni ile inayozingatia maana au kiini cha matini kuliko fasiri ya neno kwa neno.

Aidha, Robert anaeleza umuhimu wa taaluma ya tafsiri katika ukurasa wa xiii wa kitabu hichohicho. Anaona kuwa tafsiri ina umuhimu kwa kuwa inatuwezesha kujua lugha lakini pia lugha yenyewe kukua kwa kujiongezea msamiati na watumiaji wa lugha kutumia msamiati hiyo katika maisha ya kila siku.

Sambamba na hayo, Robert ameweza kuwekea kanuni za tafsri bora katika ukurasa wa xiv wa kazi hii. Anaona kuwa tafsiri ili iwe nzuri lazima mfasiri achunge miiko na aepukane na baadhi ya mambo katika kufasiri.  Anasema ili tafsiri iwe bora mfasiri lazima azingatie haya yafuatayo: “kuandika neno kwa neno, kuelewa dhana ya jumla ya kila fungu, kuwa makini na maana ya kila neno, kuandika fikra za waziwazi, kutunga mfano wa makala na kuzingatia ukubwa wa makala ya asili. Hata hivyo Robert anaweka miiko mingine ambayo mfasiri anapaswa kujiepusha nayo ili kuepukana na matini tenge. Anaona mfasiri si vema kwake kukiusha maana, kuongeza lisilokuwepo kimtindo na mpango wa kazi kwa ujumla wake. Haya yote yamekuwa yakilalamikiwa na wataalamu mbalimbali katika taaluma ya tafsiri kama vile Mtesigwa kama anavyonukuliwa na Mwansoko (2013:91-94). Mtesigwa nalalamika juu ya tafsiri ya wimbo wa Lawino ulivyopotoshwa kimaana katika baadhi ya vipengele. Lakini si kazi hiyo tu iliyopotoshwa kwani tumekuwa tukishuhudia jinsi kazi mbalimbali zinavyokuwa tenge kwa sababu ya kutozingatia kanuni hizi.

Kwahiyo, kanuni hizi ni mihimiri katika kazi yoyote ya tafsiri kwani kufuatwa kwake ni njia ya kuzalisha kazi nzuri na kuupuzwa kwake ni uzalishaji wa matini tenge. Vilevile Robert ameweza kutoa aina kuu za tafsiri yaani; fasili sisisi na fasili sabilia. Ambazo Mwansoko fasili sabilia ameiita tafsiri ya Kisemantiki.

Kwa jumla tunaweza sema kuwa Shaaban Robert ametoa mchango mkubwa katika utangulizi wa taaluma ya tafsiri, hivyo, amekuwadira kwa waandishi wachanga wanaoandika katika taaluma hii ya tafsiri. Kwani baadhi ya istilahi zake bado zinatumika hadi sasa, kwa mfano, tafsiri ya neno kwa neno na hata tafsiri sisisi ijapokuwa zimepanuliwa zaidi lakini msingi wake tunaona unajengwa na Shaaban Robert.

2.2 Fikra za Kitafsiri
Katika dondoo hii tutaona jinsi Robert alivyopenyeza fikra za tafsiri katika riwaya ya Siku ya Watenzi Wote. Katika kazi hii tunaona jinsi mwandishi alivyoweza kuonesha maudhui yanayoonesha ubora, madhara ya tafsiri tenge na hata umuhimu wa tafsiri. Mwandishi anaonesha haya kuna miongoni mwa sura za riwaya hiyo kuna sura ameipa kwa jina la tafsiri. Kinachozungumziwa   katika sura hiyo ni kuhusu umuhimu wa tafsiri na umuhimu na mfasiri kuwa mahiri katika lugha zote mbili, lugha chanzi na na lugha lengwa. Robert anaona kuwa ikiwa mfasiri si mweledi katika masuala ya lugha bila shaka kazi ya tafsiri itakuwa na ukiushi anaeleza katika ukurasa wa 40-41. Anasema kuwa; 
Alisoma tafsiri hiyo mbiombio, kisha akanena;” Kazi yako si nzuri Bi Nunu na tafsiri yako si sahihi kamwe! Hujui kitu-Kiswahili wala Kingereza. Mara ngapi nimekwambia kuwa unavuruga mambo-lugha ngeni katika Kiswahili. Mshupavu kama jiwe. Huambiliki…” Huu ni upeo wa tafsiri ya makala hii, bwana uliza kwa mtaalamu yeyote wa lugha…    
Hapa tunaona kuwa mwandishi anamsemanga bosi wa Nunu kwa kukurupukia taaluma ya tafsiri kiasi kwamba kutokana na ujinga wake katika masuala ya tafsiri anamuona Bi Nunu amevuruga  kazi ya tafsiri wakati yeye ndiye aliyeharibu.

2.3 Mazao ya Kitafsiri
Pamoja na fikra zote hizo kuhusu tafsiri ambazo zinajidhihirisha katika kazi zake za kifasihi lakini Robert alithubutu pia kuitumbukia taaluma ya tafsiri kwa matendo. Aliweza kutafsiri kazi yake mwenyewe iliyokuwa katika lugha ya Kiswahili na kuiweka katika lugha ya Kiingereza aliyoiita kwa jina la Almasi za Afrika na Tafsiri ya Kingereza. Pamoja na kazi hiyo Shaaban Robert ameweza kutafsiri mashairi ya Omari Khayaam yaliyokuwa katika lugha ya Kiingereza kama yalivyotafsiriwa na Bwana Edward FitzGerald kutoka katika lugha ya Kiajemi katika kitabu alichokiita Tenzi za Marudi Mema na Omary Khayyam.

2.3.1 Almasi za Afrika na Tafsiri ya Kingereza
Katika kitabu cha Almasi za Afrika anaeleza kusudi la yeye kutafsiri kitabu hicho katika lugha ya Kiingereza katika ukurasa ii katika utangulizi, anasema; “Kusudi la tafsiri za lugha ya Kingereza katika kitabu hiki ni kuonesha jinsi Kiswahili kiwezavyo kuchukuana vema na lugha nyingine; na kusaidia baadhi ya wasomaji kuelewa kuwa hii si lugha masikini   
Katika tafsiri hii Robert anatumia mbinu ya kisemantiki kama yeye alivyoiita sabilia, amezingatia maana zaidi kuliko mtindo. Hata hivyo mwandishi anaweka msisitizo kuwa tafsiri yake isieleweke vibaya kwa wasomaji kiasi wakadhani kuwa masharti ya Kiingereza yanakuwa katika hali hiyo isipokuwa waelewe kuwa hiyo ni tafsiri tu ya matini chanzi na mashairi ya Kingereza yana utaratibu maalumu wa utunzi, kama vile huwa na mizani na vina pia huwa na maana zaidi ya moja.

2.3.2 Tenzi za Marudi Mema na Omari Khayyam
Shaaban Robert alitafsiri tenzi hizi kwa kupewa ushauri na aliyekuwa Mudiri wa idara ya elimu Tanganyika Bwana A.A.M Isherwood. Robert alitafsiri tenzi hizi kutoka katika lugha ya Kiingereza yaliyojulikana kwa jina la Rubayyat of Omary Khayyam mwaka 1859. Matini chanzi ya kwanza ya tenzi hizi ilitoka katika lugha ya Kiajemi, tenzi hizi zilijulikana kama Rubayyat (Robert, 1973:103-104).

Tafsiri ya hii pia imetoa dira katika mbinu za kutafsiri, kwani mfasiri anatumia pia mbinu ya kisemantiki ambayo hujikita katika sarufi ya lugha lengwa. Mfasiri anatumia mbinu hii kuanzia mwanzo wa ubeti hadi mwisho. Kwa hiyo, kitendo cha Shaaban kutafsiri kazi hii kutoka katika lugha ya kingereza na kuwa katika Kiswahili  tunaweza hesabu kuwa huu ni mchango mkubwa katika taaluma ya tafsiri. Kupitia kazi hii mwandishi anatuongezea idadi ya kazi zilizo tafsiriwa kwa Kiswahili katika makavazi.

3.0 Hitimisho
Hakika Shaaban Raobert amekuwa gumzo katika lugha ya Kiswahili kwa ujumla hasa katika uwanja huu wa fasihi. Uwepo wake unajionesha waziwazi katika kazi alizozifanya. Kutokana na umaarufu huu wa kitaaluma, Shaaban Robert alipewa jina la lakabu la ‘baba’ wa Fasihi ya Kiswahili. Sio hivyo tu, nguli huyu alithubutu kuvamia uga wa tafsiri kupitia eneo lake hili la fasihi. Baadhi ya kazi tulizozithibitisha hapo juu bila shaka zimethibitisha kweli hii. Hivyo basi tunatoa wito kwa wanataaluma na wahakiki kuzamia kwa kina katika tanzu alizozifanyia tafsiri na kuzihakiki kwa jicho la ndani zaidi. Hii itapelekea kugundua mambo mbalimbali yaliyotumiwa na Shaaban Robert katika kutafsiri, pia kugundua udhaifu na ufaafu wa tafsiri yake na tena kufanya ulinganisho wa kitaaluma kati yake na wafasiri wengine.

 MAREJELEO
FitzGerald, E, (1859), The Rubayyat of Omary Khayyam, The University of Adelaide Library, Adelaide, South Australia.
Mshindo, H.B, (2010), Kufasiri na Tafsiri, Oxford Univerasity Press, Dar es Salaam.
Mwansoko, H.J.M na Wenzake, (2006), Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu, TUKI, Dar es Salaam.
Ndumbaru, E, (2014), “Maandiko ya Shaaban Robert” Bubujiko la Maarifa, [Mtandaoni: Imepitiwa 10 Mei 2015 saa5:16 usiku].
ponera, a.s, (2014), Utanguliazi wa Nadharia ya Fasihi Linganishi, Karljamer Print Technology, dar es salaam.
Ponera, A.S, (2010), “Ufutuhi katika Nathari za Shaaban Robert: Maana yake, Sababu za Kutumiwa na Athari zake kwa Wasomaji” tasnifu ya Masomo ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dodoma, [Haijachapishwa].   
Robert, S., (1960), Almas za Afrika na Tafsiri ya Kingereza, Art & Literature, Nairobi.
Robert, S., (1973) Tenzi za Marudi Mema na Omar Khayyam, TPH, Dar es Salaam.
Robert, S., (1968), Siku ya watenzi wote, Nelson, Nairobi
Robert, S., (2004) Kielelezo cha Fasili, Nelson, Nairobi
Sengo, S.Y, (1992), Shaaban Robert: Uhakiki wa Maisha Yake, KAD Associaties, Dar es Salaam, Tanzania.

-----------------------------------------------------------------------------------------------

Zuhura Said Ismail
Chuo Kikuu cha Dodoma 
0718629339 au 0783629339 
 DODOMA, TANZANIA


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni