Jumamosi, 19 Machi 2016

FAIDA NA HASARA ZA TAFSIRI KATIKA UTAMADUNI



IKISIRI
Tunapojadili umuhimu wa taaluma ya tafsiri pamoja na changamoto zake katika jamii, mara nyingi tunajikita katika masuala ya kielimu na mawasiliano na kuusahau upande wa utamaduni ambao unajumuisha vipengele vingi vya maisha katika jamii. Makala hii ina lengo la kuelezea faida na hasara zilizopatikana na zinazoendelea kupatikana katika utamaduni tangu kuasisiwa kwa taaluma hii ya tafsiri nchini Tanzania na Afrika kwa jumla. Hivyo basi, ili kufikia lengo linalokusudiwa, Makala hii itakuwa na sehemu saba. Sehemu ya kwanza itaelezea kuhusu Dhana ya Tafsiri. Sehemu ya pili itaelezea Historia na Maendeleo ya Tafsiri nchini Tanzania. Sehemu ya tatu itahusu Dhana ya Utamaduni. Sehemu ya nne itahusu Faida za Tafsiri katika Utamaduni. Sehemu ya tano itaelezea Hasara za Tafsiri katika Utamaduni. Sehemu ya sita ni Hitimisho na Mapendekezo. Na sehemu ya saba ni Marejeleo. 

UTANGULIZI
Dhana ya Tafsiri
Dhana ya tafsiri imefafanuliwa na wataalamu mbali mbali, miongoni mwao ni kama hawa wafuatao:-
Mwansoko na wenzake (2006), wanafasili tafsiri kwa kusema kuwa:
“Ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi    nyengine”
As-safi akimnukuu Dubois (1974), anaeleza kuwa:
“Tafsiri ni uelezaji katika lugha nyengine au lugha lengwa wa kile kilichoelezwa katika lugha nyengine (lugha chanzi) ikihifadhi maana na mtindo wa matini chanzi”
Catford (1965:20) anasema tafsiri ni,
“Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana katika lugha nyingine (lugha lengwa)”. 
Kutokana na fasili zote hizo kuhusu tafsiri tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa, tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, ujumbe au taarifa iliyopo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa bila kupoteza maana ya msingi na mtindo uliotumika katika matini chanzi. Na maana katika tafsiri inatakiwa iendane na lengo la mtunzi wa matini chanzi lakini pia kwa kuzingatia utamaduni wa jamii unayoitafsiriya.

Historia na Maendeleo ya Tafsiri nchini Tanzania.
Wanjala (2011) anaeleza kuwa, historia ya tafsiri imeangaliwa kwa kuegemea vipindi muhimu vya maendeleo na mabadiliko ya elimu na utamaduni. Nchini Tanzania, tafsiri haina historia ndefu sana kwani imeanzia mnamo karne ya 19 na inaweza kugaiwa katika vipindi vitatu vikuu navyo ni kabla ya utawala wa kikoloni, wakati wa utawala wa kikoloni na baada ya uhuru.
Mbali na Wanjala (2011), pia historia hii imeelezwa na wataalamu kama vile Mwansoko na wenzake (2006), Mshindo (2010) na Sofer (2006) kama ifuatavyo:-
Tukianza na kabla ya utawala wa kikoloni, Wamishionari walitafsiri vitabu mbali mbali vya kikristo ikiwemo Biblia Takatifu kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili na lugha nyengine za makabila kwa lengo la kueneza dini na ustaarabu wa kikristo kwa waafrika.
Kwa upande wa kipindi cha wakati wa kikoloni, hiki ni kipindi kuanzia miaka ya 1800, katika kipindi hiki, wakoloni hasa waingereza walitafsiri maandiko mbali mbali ya kitaaluma na fasihi ya Ulaya kwa lugha ya Kiswahili. Vile vile kabla ya uhuru zipo baadhi ya kazi za fasihi zilizotafsiriwa na watanzania. Kwa mfano tamthiliya ya “MZIMU WA WATU WA KALE” iliyotafsiriwa na Mohammed Said Abdalla (1960) kutoka lugha ya kiingereza (Shrine of The Ancestors).
Baada ya uhuru ambapo ni kuanzia mwaka 1961. Katika kipindi hiki wapo wataalamu waliofanya juhudi za kutafsiri vitabu mbali mbali kwa lugha ya Kiswahili. Mfano mzuri ni Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alitafsiri vitabu viwili vya mwandishi mashuhuri wa tamthiliya wa huko Uingereza aitwaye William Shakespeare ambavyo ni tamthiliya ya Juliasi Kaizari (Julius Caesar) (1963) na tamthiliya ya Mabepari wa Venis (The Merchant of Venis) (1969).
Kazi nyengine zilizotafsiriwa baada ya uhuru ni wimbo wa Lawino (Song of Lawino) iliyotafsiriwa na Paul Sozigwa (1975), riwaya ya Uhuru wa Watumwa (The Freeing of the Slaves in East Africa) iliyotafsiriwa na East African Literature Bureau (1967), Nitaolewa Nikipenda (I Will Marry When I Want) iliyotafsiriwa na Crement M. Kabugi (1982).
Kwa ujumla maendeleo ya taaluma ya tafsiri nchini Tanzania yamepiga hatua kubwa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia. Taaluma ya tafsiri inafundishwa katika elimu ya sekondari na katika vyuo vikuu mbali mbali. Pia taasisi na asasi zinazojishughulisha na tafsiri zimeongezeka kwa mfano Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI), Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na kadhalika. Pia wapo wafasiri binafsi wanaotafsiri maadishi kwa lugha mbali mbali kama vile Kiingereza, Kiswahili, Kiarabu, Kifaransa nakadhalika.
Dhana ya Utamaduni
Kwa upande wa dhana ya utamaduni, wataalamu mbali mbali wameelezea dhana hii kama ifuatavyo:-
Ponera (2014), yeye anaeleza kuwa:
“Utamaduni ni jumla ya matendo, fikra, mifumo ya maisha na kiashiria kingine chochote ambacho kinaweza kutumika kumwongoza na kumtambulisha mtu wa jamii moja kwa jamii nyenginezo”
Pia katika Wikipedia imeelezwa kuwa:
“Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake”
Pia imeelezwa kuwa, neno “Utamaduni” linatumika kimsingi katika njia tatu zifuatazo:-
·         Maonjo ya hali ya juu katika sanaa, vile vile hujulikana kama utamaduni wa juu.
·         Mkusanyiko wa maarifa ya binadamu, itikadi na tabia ambao hutegemea sana uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kwa njia ya ishara.
·         Jumla ya mitazamo, kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi, shirika au kikundi Fulani.
Ama kuhusu maana ya utamaduni wa mtanzania, mtandao wa Jamii Forum unaeleza kuwa, mtanzania ni mtu mwenye utu. Utu ni sifa na ndio utamaduni wa mtanzania kwa sababu unaingia katika vipengele mbali mbali kama vile kwenye uongozi, familia, kilimo, elimu, mavazi, muziki, vyakula, biashara, siasa, uchumi, mahusiano na nchi za nje, mikataba muhimu ya taifa, kazi, dini, nakadhalika.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa hakuna maana ya moja kwa moja kuhusu utamaduni kwa sababu utamaduni unajumuisha mambo mengi katika maisha ya binadamu kama yalivyotajwa katika fasili zilizopo hapo juu. Lakini jambo la kuzingatia ni kuwa, kazi yoyote itakayoandikwa au kufasiriwa kutoka lugha moja kwenda nyengine haina budi kuchunga   misingi ya utamaduni ya jamii husika.

Faida za Tafsiri katika Utamaduni.
Baada ya ufafanuzi huo mfupi kuhusu dhana ya utamaduni, tafsiri pamoja na historia na maendeleo yake nchini Tanzania, sasa moja kwa moja nakwenda kwenye lengo la makala yangu la kujadili faida na hasara za tafsiri katika utamaduni ambapo zaidi tutajikita katika utamaduni wa Tanzania. Kupitia historia ya tafsiri niliyoieleza hapo juu na kwa kuzingatia hali halisi ya maendeleo ya matumizi ya tafsiri yanavyopiga hatua kila siku katika nchi yetu ya Tanzania, faida za tafsiri katika utamaduni wa Tanzania ni kama zifuatazo:-

  • 1.      Tafsiri imesaidia katika kueneza dini na vipengele vyengine vya utamaduni kutoka mataifa ya nje.  
Tafsiri ni nyenzo ya kuenezea utamaduni kutoka taifa moja kwenda jengine au kutoka jamii moja kwenda jengine. Kwa mfano kutokana na wazungu kutafsiri Biblia na waarabu kutafsiri Kur-An kwa lugha ya Kiswahili, kulisababisha waafrika kwa ujumla kubadilisha dini zao za kijadi na kufuata dini ya Ukristo na Uislamu. Vile vile kwa upande wa burudani, vyakula na mavazi kutoka mataifa ya magharibi vilienea katika jamii za watanzania na waafrika kwa ujumla kutokana na kutafsiriwa kazi mbali mbali kama vile nyimbo, mashairi, hadithi nakadhalika ambazo ndani yake mulisheheni vipengele hivyo vya utamaduni.

  • 2.      Tafsiri imesaidia katika kukuza lugha na fasihi ya Kiswahili.
Lugha ya kiswahili ni miongoni mwa vipengele muhimu sana katika utamaduni wa Tanzania kwa sababu kiswahili ni lugha rasmi, lugha ya taifa na tunu ya taifa. Kabla ya kuwepo taaluma ya tafsiri, lugha ya Kiswahili ilionekana kudumaa hasa katika nyanja ya sayansi na teknolojia. Lakini baada ya kuwepo taaluma hii, wataalamu na taasisi mbali mbali za Kiswahili zimekuwa zikifanya jitihada za kutafsiri vitabu vya lugha mbali mbali kwenda lugha ya kiswahili pamoja na kutafuta istilahi na misamiati ya Kiswahili inayoweza kwenda sambamba na istilahi za kisayansi. Mfano wa istilahi hizo ni kama vile Password – Nywila, Keyboard – Kicharazio, Scanner – Mdaki, Flash Disc – Diski Mweko, Mouse – Kiteuzi, nakadhalika.
Kwa upande wa fasihi, hii ni sanaa. Na sanaa ni katika utamaduni wa juu kabisa. Historia inaeleza kuwa, wakati wa ukoloni fasihi ilidumaa kwa sababu waafrika hawakuwa na mwamko wa kusoma vitabu na kazi nyingi za kifasihi ziliandikwa kwa lugha ya kiingereza kwa lengo la kuwafurahisha mabwana. Lakini baada ya wataalamu wa fasihi kuanza kutafsiri kazi mbali mbali za fasihi ya ulaya kwa lugha ya Kiswahili na lugha nyengine za makabila mwamko wa kusoma vitabu uliongezeka. Mfano wa vitabu vya fasihi vilivyotafsiriwa wakati wa ukoloni ni Mzimu wa Watu wa Kale (Shrine of the Ancestors) iliyotafsiriwa na Mohammed Said Abdalla (1960).
Pia kuna kazi mbali mbali za kifasihi zilizotafsiriwa baada ya uhuru. Miongoni mwao ni Juliasi Kaizari (Julius Caesar) (1963) na Mabepari wa Venis (The Merchant of Venis) (1967), zote hizo zimetafsiriwa na Mwalimu Julius K. Nyerere.
Baada ya hapo, kazi mbali mbali za kifasihi kama vile hadithi fupi, riwaya, tamthilia na mashairi yalitafsiriwa kutoka lugha mbali mbali kwenda Kiswahili. Vile vile kazi za fasihi ya Tanzania zilitungwa na kupelekea kukua na kuenea fasihi ya Kiswahili.



  • 3.      Tafsiri imesaidia katika kukuza elimu nchini Tanzania.
Elimu ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa Tanzania, imepiga hatua kutokana na maendeleo ya mitaala na mbinu mbali mbali za kufundishia. Tafsiri ni miongoni mwa mbinu  inayotumiwa na walimu wengi ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafikia lengo la kujifunza kwa mujibu wa viwango vyao. Juhudi mbali mbali zinachukuliwa katika kukuza elimu ya Tanzania. Miongoni mwa juhudi hizo ni kutafsiriwa kwa vitabu vya masomo mbali mbali ili visaidie katika marejeleo. Vile vile taaluma ya tafsiri imekuwa ni kozi muhimu katika shule za sekondari na vyuoni ili kuwapa wanafunzi uwezo wa kuitumia taaluma hii ili waweze kujiajiri kwa kutafsiri kazi mbali mbali.

  • 4.      Tafsiri imesaidia katika kuibua nadharia mpya ya fasihi linganishi.
Kama nilivyotangulia kusema kuwa fasihi ni sanaa na sanaa ni sehemu ya utamaduni. Kwa mujibu wa kitabu cha “UTANGULIZI WA NADHARIA YA FASIHI LINGANISHI” kilichoandikwa na Athumani S. Ponera (2014) ni kwamba, lengo la nadharia hii ni kuchunguza kufanana na kutofautiana kati ya fasihi ya Tanzania na fasihi ya mataifa   mengine hasa Amerika na Ulaya hususan katika vipengele mbali mbali vya utamaduni pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kupitia kitabu hicho, hoja yangu naiegemeza pale mwandishi alipoelezea ulinganisho uliopo kati ya fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili na hapa namnukuu.
“Dhana hii ya fasihi ya Kiswahili ni muhimu sana kuidodosa ili ituwezeshe kufika katika hatua ya kufanya ulinganisho na fasihi za jamii nyenginezo. Kuna mkanganyiko mkubwa miongoni mwa wanazuoni kuhusu dhana za fasihi ya Kiswahili, fasihi katika Kiswahili, fasihi kwa Kiswahili na fasihi ya waswahili”.
Kwa hiyo kutokana na maelezo hayo, ni wazi kuwa kuwepo kwa kazi nyingi za mataifa ya nje zilizofasiriwa kwa lugha ya Kiswahili na zile ambazo hazijafasiriwa, ni sababu tosha iliyomsukuma mwandishi kuanzisha mjadala huu wa nadharia mpya ya fasihi linganishi kama ilivyo kwa nadharia ya isimu linganishi.

  • 5.Tafsiri imesaidia katika kukuza biashara na kuinua uchumi wa taifa.
Kama tulivyotangulia kusema kuwa, utamaduni ni utu na utu ni muhimu katika maisha ya watu. Biashara ni miongoni mwa sekta inayounganisha watu wa aina tofauti.  Kuwepo kwa utu katika biashara ndio kutasaidia kukuza biashara na uchumi wa nchi yetu. Mchango wa tafsiri katika biashara ni kuwa mikataba mingi ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania  inatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao. Vile vile matangazo mbali mbali ya kibiashara na taarifa nyengine katika vyombo vya habari kama vile magazeti hutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kila mwananchi apate kufaidika na huduma zinazotolewa.
Hasara za Tafsiri katika Utamaduni.
Baada ya kuelezea faida mbali mbali za tafsiri katika utamaduni wa Tanzania na afrika kwa jumla. Sasa nitatumia fursa hii kuelezea hasara chache za tafsiri zilizoathiri utamaduni wetu kama ifuatavyo:-  

  •       Tafsiri imesababisha jamii za waafrika kuiga utamaduni wa mataifa ya nje.
Kwa mujibu wa Kamati ya Taarifa za Tovuti Kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizofanyiwa marekebisho mwaka (2015) zinaeleza kuwa:
“Utamaduni wa Tanzania Ni matokeo ya athari za kiafrika, kiarabu, kizungu na kihindi. Maadili, mila na desturi za kiafrika zinabadilishwa polepole Na maisha ya kisasa, ingawa kwa kasi ndogo sana miongoni mwa jamii ya wamasai”.
Kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwa, jamii nyingi za waafrika zikiwemo za watanzania, zimeanza kuathirika kwa kuiga mila na tamaduni za kimagharibi kupitia tafsiri za kazi mbali mbali za kijamii na mpaka sasa hali hiyo inaendelea kupitia njia nyengine mbali mbali kama vile utalii na maingiliano baina ya waafrika, wazungu, waarabu na wahindi.

  •       Tafsiri imesababisha mivutano na makundi ya kidini kati ya jamii za waafrika.
Ukirudia historia ya tafsiri katika nchi za ulaya, utaona, mnamo karne ya 16 kulikuwa na    muamko mkubwa wa kidini ambapo ulianza Ujerumani na kusambaa katika maeneo mbali mbali ulimwenguni. Mwamko huu ulipinga muundo, mwelekeo, falsafa na mafunzo mengi ya kanisa katoliki ya wakati huo na matumizi ya lugha moja ya kilatini katika misa na mafunzo ya kidini. Hali hii ilisababisha mgawanyiko katika dini ya kikiristo. Watu mbali mbali walitafsiri maandiko matakatifu katika lugha mbali mbali. Kwa mfano Martin Luther King alitafsiri Biblia takatifu kutoka kilatini kwenda lugha ya kiingereza (1611) ikaitwa “The King James Bible”, pia alitafsiri Biblia kutoka Kilatini kwenda lugh ya Kijarumani. Baada ya kuona tafsiri ya Kilatini imeacha baadhi ya vipengele katika maandiko hayo matakatifu, Jarome alitafsiri Biblia ya Kigiriki na Kiebrania kutoka lugha ya Kilatini.
Kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwa, mgawanyiko wa kidini haukuishia katika nchi za ulaya na katika dini ya kikristo peke yake bali ulienea ulimwengu mzima zikiwemo nchi za afrika kwa sababu ya kutafsiriwa maandiko matukufu mbali mbali kama vile biblia, kur-an na vitabu vyengine vya mafunzo ya dini . Sasa hivi ukichunguza katika dini zote hasa za uislamu na ukristo utakuta mivutano kati ya waumini juu ya makundi yao. Kwa mfano katika ukristo utakuta makundi kama vile wakatoliki, wasabato nakadhalika. Ama kwa upande wa dini ya kiislamu kuna makundi kama vile suni, ibadhi, shia nakadhalika. Yote hayo yametokana nakufasiriwa kwa maandiko ya dini na ufahamu wa waumini katika maandiko hayo.

  •       Baadhi ya njia za tafsiri husababisha kwenda kinyume na sarufi ya lugha lengwa au utamaduni wa lugha lengwa.
Hoja hii naiegemeza zaidi katika aina za tafsiri ambazo ni tafsiri ya neno kwa neno, tafsiri sisisi, tafsiri ya kisemantiki na tafsiri ya mawasiliano. Lakini hapa nitajikita zaidi katika tafsiri ya neno kwa neno. Mara nyingi tunapotafsiri sentensi au matini kwa kutumia njia hii, lazima tufuate sarufi ya lugha chanzi hivyo husababisha makosa ya kimuundo na kimaana ya lugha lengwa. Mifano ifuatayo inafafanua zaidi.
·         Kiingereza kwenda Kiswahili:
I / like / banana / s / more / than / orange / s /
Mimi / penda/kama / ndizi / wingi / zaidi / kuliko / chungwa / wingi /

·         Kiswahili kwenda kiingereza
Wa / toto / wa / dogo / wa / na / imba / kwa / furaha /
Plural / child / plural / small / they / present continues tense (singular) / by/for / happiness
Unapochunguza mifano ya hapo juu, utakuta kuwa ufuataji wa sarufi ya lugha chanzi hupelekea kuharibu sarufi ya lugha lengwa na kupoteza maana inayokusudiwa kutoka lugha chanzi.
Vile vile tunapotafsiri methali, misemo, nahau na matini nyengine za kifasihi, kwa kutumia njia yoyote ya tafsiri, mfasiri anaweza kwenda kinyume na utamaduni wa lugha lengwa endapo atakuwa si mzoefu wa utamaduni wa jamii hiyo.

  •      Tafsiri husababisha matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili katika maandishi.
Hapa nakusudia kueleza kuwa, moja ya njia ya uchanganyaji wa lugha katika maandishi ni tafsiri. Watu wengi wanaojishughulisha na kutafsiri matini mbali mbali kwenda lugha ya Kiswahili huathiriwa na kazi hio na kuwasababishia kuchanganya lugha pale wanapoandika kazi nyengine za Kiswahili jambo ambalo ni kinyume na utamaduni wa mtanzania. Jambo hili huweza kujitokeza kwa waandisi wa makala mbali mbali za Kiswahili lakini pia wahariri wa magazeti.   
    Hapa nataka nifahamike kuwa, sipingi utumiaji wa neno au maneno ya lugha nyengine kama kiingereza ambayo yana lengo la kutoa ufafanuzi zaidi juu ya jambo fulani ambapo mara nyingi maneno hayo huwekwa katika mabano. Bali nakusudia uchanganyaji wa lugha kwa ujumla. Mfano katika upekuaji wa makala mbali mbali nimegundua matumizi hayo kama ifuatavyo:-        
“Mimi ninadhani values za jamii ni kioo ambacho maendeleo yoyote that we want  and to find out kwa udi na uvumba lazima ya reflect, kama we have not values za          maana ni vipi tutaendelea”
Kwa hiyo mtu anayetumia lugha kama inavyoonekana katika maelezo yaliopo hapo juu, mimi kwa maoni yangu naona mtu huyo ama ameathiriwa na lugha ya kiingereza au kutokana na kufanya kazi nyingi za tafsiri.

Hitimisho na Mapendekezo:
Kwa ujumla makala hii imeelezea kwa kina kuhusu faida na hasara za tafsiri katika utamaduni ambapo maelezo yake, zaidi yamejikita kutoka katika dhana ya tafsiri, dhana ya utamaduni lakini zaidi kupitia historia na maendeleo ya tafsiri nchini Tanzania.
Licha ya uhaba wa historia ya tafsiri nchini Tanzania, na pamoja na kuwepo baadhi ya changamoto katika vipengele mbali mbali vya maisha ya jamii ya watanzania na Afrika kwa ujumla, bado taaluma hii ni muhimu sana hasa katika mawasiliano kati ya jamii zinazozungumza lugha tofauti, pia ni muhimu katika masuala mbali mbali ya kielimu bila ya kusahau katika soko la ajira.  
Kwa hiyo ili kufikia malengo hayo, ni wajibu wetu kuisoma taaluma hii kwa undani zaidi pamoja na kufuata kikamilifu kanuni, taratibu na sheria za tafsiri ili tuweze kupata kazi nzuri za tafsiri zenye kukidhi mahitaji ya matini chanzi, matini lengwa na utamaduni wa jamii husika.  


 MAREJELEO :  
ü  Mshindo, H. B. (2010). KufasirinaTafsiri. Chuo Kikuu cha Elimu. Chukwani, Zanzibar.

ü  Mwansoko, J. M. (1961). Kitangulizi cha tafsiri, nadharianambinu. TUKI. Dar es salaam.
ü  Mwansoko na Wenzake (2006). Tafsiri na Ukalimani. UDSM.

ü  Ponera, A. S. (2014). Utangulizi wa Nadharia ya Fasihi Linganishi. Karljamer Print Technology. Dar es salaam, Tanzania.

MITANDAO
ü  antagonf.blogspot.com. Tafsiri na ukalimani.

ü  chomboz: blogsport.com/2013. MisingiyaTafsirinaUkalimani.

ü   https://sw.m.wikipedia.org. Utamaduni – wikipedia, kamusi elezo huru.

ü  nenothabiti.blogspot.com. Tafsiri. 

ü  www.jamiiforum.com. Ni nini utamaduni wa mtanzania?
 ================================================
 Mtunzi: Said Ali Shehe. 
Muhitimu, Chuo Kikuu cha Sumait Zanzibar.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni