IKISIRI
Tunapojadili umuhimu wa taaluma ya tafsiri pamoja na
changamoto zake katika jamii, mara nyingi tunajikita katika masuala ya kielimu
na mawasiliano na kuusahau upande wa utamaduni ambao unajumuisha vipengele
vingi vya maisha katika jamii. Makala hii ina lengo la kuelezea faida na hasara
zilizopatikana na zinazoendelea kupatikana katika utamaduni tangu kuasisiwa kwa
taaluma hii ya tafsiri nchini Tanzania na Afrika kwa jumla. Hivyo basi, ili
kufikia lengo linalokusudiwa, Makala hii itakuwa na sehemu saba. Sehemu ya
kwanza itaelezea kuhusu Dhana ya Tafsiri. Sehemu ya pili itaelezea Historia na
Maendeleo ya Tafsiri nchini Tanzania. Sehemu ya tatu itahusu Dhana ya
Utamaduni. Sehemu ya nne itahusu Faida za Tafsiri katika Utamaduni. Sehemu ya
tano itaelezea Hasara za Tafsiri katika Utamaduni. Sehemu ya sita ni Hitimisho na
Mapendekezo. Na sehemu ya saba ni Marejeleo.
UTANGULIZI
Dhana ya Tafsiri
Dhana ya tafsiri imefafanuliwa na wataalamu
mbali mbali, miongoni mwao ni kama hawa wafuatao:-
Mwansoko na wenzake (2006), wanafasili
tafsiri kwa kusema kuwa:
“Ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika
maandishi kutoka lugha moja hadi nyengine”
As-safi akimnukuu Dubois (1974), anaeleza
kuwa:
“Tafsiri ni uelezaji katika lugha nyengine
au lugha lengwa wa kile kilichoelezwa katika lugha nyengine (lugha chanzi)
ikihifadhi maana na mtindo wa matini chanzi”
Catford (1965:20) anasema tafsiri ni,
“Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi
kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana
katika lugha nyingine (lugha lengwa)”.
Kutokana na fasili zote hizo kuhusu tafsiri
tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa, tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, ujumbe
au taarifa iliyopo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa
bila kupoteza maana ya msingi na mtindo uliotumika katika matini chanzi. Na
maana katika tafsiri inatakiwa iendane na lengo la mtunzi wa matini chanzi
lakini pia kwa kuzingatia utamaduni wa jamii unayoitafsiriya.
Historia na Maendeleo ya Tafsiri nchini Tanzania.
Wanjala (2011) anaeleza kuwa, historia ya tafsiri
imeangaliwa kwa kuegemea vipindi muhimu vya maendeleo na mabadiliko ya elimu na
utamaduni. Nchini Tanzania, tafsiri haina historia ndefu sana kwani imeanzia
mnamo karne ya 19 na inaweza kugaiwa katika vipindi vitatu vikuu navyo ni kabla
ya utawala wa kikoloni, wakati wa utawala wa kikoloni na baada ya uhuru.
Mbali na Wanjala (2011), pia historia hii imeelezwa na
wataalamu kama vile Mwansoko na wenzake (2006), Mshindo (2010) na Sofer (2006)
kama ifuatavyo:-
Tukianza na kabla ya utawala wa kikoloni, Wamishionari
walitafsiri vitabu mbali mbali vya kikristo ikiwemo Biblia Takatifu kutoka
lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili na lugha nyengine za makabila kwa lengo la
kueneza dini na ustaarabu wa kikristo kwa waafrika.
Kwa upande wa kipindi cha wakati wa kikoloni, hiki ni
kipindi kuanzia miaka ya 1800, katika kipindi hiki, wakoloni hasa waingereza
walitafsiri maandiko mbali mbali ya kitaaluma na fasihi ya Ulaya kwa lugha ya
Kiswahili. Vile vile kabla ya uhuru zipo baadhi ya kazi za fasihi
zilizotafsiriwa na watanzania. Kwa mfano tamthiliya ya “MZIMU WA WATU WA
KALE” iliyotafsiriwa na Mohammed Said Abdalla (1960) kutoka lugha ya
kiingereza (Shrine of The Ancestors).
Baada ya uhuru ambapo ni kuanzia mwaka 1961. Katika
kipindi hiki wapo wataalamu waliofanya juhudi za kutafsiri vitabu mbali mbali
kwa lugha ya Kiswahili. Mfano mzuri ni Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye
alitafsiri vitabu viwili vya mwandishi mashuhuri wa tamthiliya wa huko Uingereza
aitwaye William Shakespeare ambavyo ni tamthiliya ya Juliasi Kaizari (Julius Caesar)
(1963) na tamthiliya ya Mabepari wa Venis (The Merchant of Venis) (1969).
Kazi nyengine zilizotafsiriwa baada ya uhuru ni wimbo
wa Lawino (Song of Lawino) iliyotafsiriwa na Paul Sozigwa (1975), riwaya ya Uhuru
wa Watumwa (The Freeing of the Slaves in East Africa) iliyotafsiriwa na East African
Literature Bureau (1967), Nitaolewa Nikipenda (I Will Marry When I Want)
iliyotafsiriwa na Crement M. Kabugi (1982).
Kwa ujumla maendeleo ya taaluma ya tafsiri nchini
Tanzania yamepiga hatua kubwa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia.
Taaluma ya tafsiri inafundishwa katika elimu ya sekondari na katika vyuo vikuu
mbali mbali. Pia taasisi na asasi zinazojishughulisha na tafsiri zimeongezeka
kwa mfano Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Taasisi ya Kiswahili na Lugha
za Kigeni (TAKILUKI), Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na kadhalika. Pia
wapo wafasiri binafsi wanaotafsiri maadishi kwa lugha mbali mbali kama vile Kiingereza,
Kiswahili, Kiarabu, Kifaransa nakadhalika.
Dhana ya Utamaduni
Kwa upande wa dhana ya utamaduni, wataalamu mbali
mbali wameelezea dhana hii kama ifuatavyo:-
Ponera (2014), yeye anaeleza kuwa:
“Utamaduni ni jumla ya matendo, fikra, mifumo ya
maisha na kiashiria kingine chochote ambacho kinaweza kutumika kumwongoza na
kumtambulisha mtu wa jamii moja kwa jamii nyenginezo”
Pia katika Wikipedia imeelezwa kuwa:
“Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake”
Pia imeelezwa kuwa, neno “Utamaduni”
linatumika kimsingi katika njia tatu zifuatazo:-
·
Maonjo ya hali ya juu katika sanaa, vile vile hujulikana kama utamaduni
wa juu.
·
Mkusanyiko wa maarifa ya binadamu, itikadi na tabia ambao hutegemea sana
uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kwa njia ya ishara.
·
Jumla ya mitazamo, kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi,
shirika au kikundi Fulani.
Ama kuhusu
maana ya utamaduni wa mtanzania, mtandao wa Jamii Forum unaeleza
kuwa, mtanzania ni mtu mwenye utu. Utu ni sifa na ndio utamaduni wa mtanzania
kwa sababu unaingia katika vipengele mbali mbali kama vile kwenye uongozi,
familia, kilimo, elimu, mavazi, muziki, vyakula, biashara, siasa, uchumi,
mahusiano na nchi za nje, mikataba muhimu ya taifa, kazi, dini, nakadhalika.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa hakuna
maana ya moja kwa moja kuhusu utamaduni kwa sababu utamaduni unajumuisha mambo
mengi katika maisha ya binadamu kama yalivyotajwa katika fasili zilizopo hapo
juu. Lakini jambo la kuzingatia ni kuwa, kazi yoyote itakayoandikwa au
kufasiriwa kutoka lugha moja kwenda nyengine haina budi kuchunga misingi
ya utamaduni ya jamii husika.
Faida za Tafsiri katika Utamaduni.
Baada ya ufafanuzi huo mfupi kuhusu dhana ya
utamaduni, tafsiri pamoja na historia na maendeleo yake nchini Tanzania, sasa moja
kwa moja nakwenda kwenye lengo la makala yangu la kujadili faida na hasara za
tafsiri katika utamaduni ambapo zaidi tutajikita katika utamaduni wa Tanzania.
Kupitia historia ya tafsiri niliyoieleza hapo juu na kwa kuzingatia hali halisi
ya maendeleo ya matumizi ya tafsiri yanavyopiga hatua kila siku katika nchi
yetu ya Tanzania, faida za tafsiri katika utamaduni wa Tanzania ni kama
zifuatazo:-
- 1. Tafsiri imesaidia katika kueneza dini na vipengele vyengine vya utamaduni kutoka mataifa ya nje.
Tafsiri ni nyenzo ya kuenezea utamaduni kutoka taifa
moja kwenda jengine au kutoka jamii moja kwenda jengine. Kwa mfano kutokana na
wazungu kutafsiri Biblia na waarabu kutafsiri Kur-An kwa lugha ya Kiswahili,
kulisababisha waafrika kwa ujumla kubadilisha dini zao za kijadi na kufuata
dini ya Ukristo na Uislamu. Vile vile kwa upande wa burudani, vyakula na mavazi
kutoka mataifa ya magharibi vilienea katika jamii za watanzania na waafrika kwa
ujumla kutokana na kutafsiriwa kazi mbali mbali kama vile nyimbo, mashairi,
hadithi nakadhalika ambazo ndani yake mulisheheni vipengele hivyo vya
utamaduni.
- 2. Tafsiri imesaidia katika kukuza lugha na fasihi ya Kiswahili.
Lugha ya kiswahili ni miongoni mwa vipengele muhimu
sana katika utamaduni wa Tanzania kwa sababu kiswahili ni lugha rasmi, lugha ya
taifa na tunu ya taifa. Kabla ya kuwepo taaluma ya tafsiri, lugha ya Kiswahili
ilionekana kudumaa hasa katika nyanja ya sayansi na teknolojia. Lakini baada ya
kuwepo taaluma hii, wataalamu na taasisi mbali mbali za Kiswahili zimekuwa
zikifanya jitihada za kutafsiri vitabu vya lugha mbali mbali kwenda lugha ya
kiswahili pamoja na kutafuta istilahi na misamiati ya Kiswahili inayoweza
kwenda sambamba na istilahi za kisayansi. Mfano wa istilahi hizo ni kama vile Password
– Nywila, Keyboard – Kicharazio, Scanner – Mdaki, Flash Disc
– Diski Mweko, Mouse – Kiteuzi, nakadhalika.
Kwa upande wa fasihi, hii ni sanaa. Na sanaa ni katika
utamaduni wa juu kabisa. Historia inaeleza kuwa, wakati wa ukoloni fasihi
ilidumaa kwa sababu waafrika hawakuwa na mwamko wa kusoma vitabu na kazi nyingi
za kifasihi ziliandikwa kwa lugha ya kiingereza kwa lengo la kuwafurahisha
mabwana. Lakini baada ya wataalamu wa fasihi kuanza kutafsiri kazi mbali mbali
za fasihi ya ulaya kwa lugha ya Kiswahili na lugha nyengine za makabila mwamko
wa kusoma vitabu uliongezeka. Mfano wa vitabu vya fasihi vilivyotafsiriwa
wakati wa ukoloni ni Mzimu wa Watu wa Kale (Shrine of the Ancestors)
iliyotafsiriwa na Mohammed Said Abdalla (1960).
Pia kuna kazi mbali mbali za kifasihi zilizotafsiriwa
baada ya uhuru. Miongoni mwao ni Juliasi Kaizari (Julius Caesar) (1963) na Mabepari
wa Venis (The Merchant of Venis) (1967), zote hizo zimetafsiriwa na Mwalimu
Julius K. Nyerere.
Baada ya hapo, kazi mbali mbali za kifasihi kama vile
hadithi fupi, riwaya, tamthilia na mashairi yalitafsiriwa kutoka lugha mbali
mbali kwenda Kiswahili. Vile vile kazi za fasihi ya Tanzania zilitungwa na
kupelekea kukua na kuenea fasihi ya Kiswahili.
- 3. Tafsiri imesaidia katika kukuza elimu nchini Tanzania.
Elimu ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa Tanzania,
imepiga hatua kutokana na maendeleo ya mitaala na mbinu mbali mbali za kufundishia.
Tafsiri ni miongoni mwa mbinu inayotumiwa
na walimu wengi ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafikia lengo la kujifunza kwa
mujibu wa viwango vyao. Juhudi mbali mbali zinachukuliwa katika kukuza elimu ya
Tanzania. Miongoni mwa juhudi hizo ni kutafsiriwa kwa vitabu vya masomo mbali
mbali ili visaidie katika marejeleo. Vile vile taaluma ya tafsiri imekuwa ni
kozi muhimu katika shule za sekondari na vyuoni ili kuwapa wanafunzi uwezo wa
kuitumia taaluma hii ili waweze kujiajiri kwa kutafsiri kazi mbali mbali.
- 4. Tafsiri imesaidia katika kuibua nadharia mpya ya fasihi linganishi.
Kama nilivyotangulia kusema kuwa fasihi ni sanaa na
sanaa ni sehemu ya utamaduni. Kwa mujibu wa kitabu cha “UTANGULIZI WA NADHARIA
YA FASIHI LINGANISHI” kilichoandikwa na Athumani S. Ponera (2014) ni kwamba,
lengo la nadharia hii ni kuchunguza kufanana na kutofautiana kati ya fasihi ya Tanzania
na fasihi ya mataifa mengine hasa Amerika na Ulaya hususan katika
vipengele mbali mbali vya utamaduni pamoja na maendeleo ya sayansi na
teknolojia.
Kupitia kitabu hicho, hoja yangu naiegemeza pale
mwandishi alipoelezea ulinganisho uliopo kati ya fasihi ya Kiswahili na fasihi
kwa Kiswahili na hapa namnukuu.
“Dhana hii ya fasihi ya Kiswahili ni muhimu sana
kuidodosa ili ituwezeshe kufika katika hatua ya kufanya ulinganisho na fasihi
za jamii nyenginezo. Kuna mkanganyiko mkubwa miongoni mwa wanazuoni kuhusu
dhana za fasihi ya Kiswahili, fasihi katika Kiswahili, fasihi kwa Kiswahili na
fasihi ya waswahili”.
Kwa hiyo kutokana na maelezo hayo, ni wazi
kuwa kuwepo kwa kazi nyingi za mataifa ya nje zilizofasiriwa kwa lugha ya
Kiswahili na zile ambazo hazijafasiriwa, ni sababu tosha iliyomsukuma mwandishi
kuanzisha mjadala huu wa nadharia mpya ya fasihi linganishi kama ilivyo kwa
nadharia ya isimu linganishi.
- 5.Tafsiri imesaidia katika kukuza biashara na kuinua uchumi wa taifa.
Kama tulivyotangulia kusema kuwa, utamaduni ni utu na
utu ni muhimu katika maisha ya watu. Biashara ni miongoni mwa sekta
inayounganisha watu wa aina tofauti. Kuwepo kwa utu katika biashara ndio kutasaidia
kukuza biashara na uchumi wa nchi yetu. Mchango wa tafsiri katika biashara ni
kuwa mikataba mingi ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania inatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili
kuwawezesha wananchi kupata haki zao. Vile vile matangazo mbali mbali ya
kibiashara na taarifa nyengine katika vyombo vya habari kama vile magazeti
hutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kila mwananchi apate kufaidika na huduma
zinazotolewa.
Hasara za Tafsiri katika Utamaduni.
Baada ya kuelezea faida mbali mbali za tafsiri katika
utamaduni wa Tanzania na afrika kwa jumla. Sasa nitatumia fursa hii kuelezea
hasara chache za tafsiri zilizoathiri utamaduni wetu kama ifuatavyo:-
- Tafsiri imesababisha jamii za waafrika kuiga utamaduni wa mataifa ya nje.
Kwa mujibu wa Kamati ya Taarifa za Tovuti Kuu ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizofanyiwa marekebisho mwaka (2015)
zinaeleza kuwa:
“Utamaduni wa Tanzania Ni matokeo ya athari za
kiafrika, kiarabu, kizungu na kihindi. Maadili, mila na desturi za kiafrika
zinabadilishwa polepole Na maisha ya kisasa, ingawa kwa kasi ndogo sana
miongoni mwa jamii ya wamasai”.
Kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwa, jamii nyingi za
waafrika zikiwemo za watanzania, zimeanza kuathirika kwa kuiga mila na tamaduni
za kimagharibi kupitia tafsiri za kazi mbali mbali za kijamii na mpaka sasa
hali hiyo inaendelea kupitia njia nyengine mbali mbali kama vile utalii na
maingiliano baina ya waafrika, wazungu, waarabu na wahindi.
- Tafsiri imesababisha mivutano na makundi ya kidini kati ya jamii za waafrika.
Ukirudia historia ya tafsiri katika nchi za ulaya,
utaona, mnamo karne ya 16 kulikuwa na
muamko mkubwa wa kidini ambapo ulianza Ujerumani na kusambaa katika
maeneo mbali mbali ulimwenguni. Mwamko huu ulipinga muundo, mwelekeo, falsafa
na mafunzo mengi ya kanisa katoliki ya wakati huo na matumizi ya lugha moja ya
kilatini katika misa na mafunzo ya kidini. Hali hii ilisababisha mgawanyiko
katika dini ya kikiristo. Watu mbali mbali walitafsiri maandiko matakatifu
katika lugha mbali mbali. Kwa mfano Martin Luther King alitafsiri Biblia
takatifu kutoka kilatini kwenda lugha ya kiingereza (1611) ikaitwa “The King
James Bible”, pia alitafsiri Biblia kutoka Kilatini kwenda lugh ya Kijarumani.
Baada ya kuona tafsiri ya Kilatini imeacha baadhi ya vipengele katika maandiko
hayo matakatifu, Jarome alitafsiri Biblia ya Kigiriki na Kiebrania kutoka lugha
ya Kilatini.
Kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwa, mgawanyiko wa
kidini haukuishia katika nchi za ulaya na katika dini ya kikristo peke yake
bali ulienea ulimwengu mzima zikiwemo nchi za afrika kwa sababu ya kutafsiriwa
maandiko matukufu mbali mbali kama vile biblia, kur-an na vitabu vyengine vya
mafunzo ya dini . Sasa hivi ukichunguza katika dini zote hasa za uislamu na
ukristo utakuta mivutano kati ya waumini juu ya makundi yao. Kwa mfano katika
ukristo utakuta makundi kama vile wakatoliki, wasabato nakadhalika. Ama kwa
upande wa dini ya kiislamu kuna makundi kama vile suni, ibadhi, shia
nakadhalika. Yote hayo yametokana nakufasiriwa kwa maandiko ya dini na ufahamu
wa waumini katika maandiko hayo.
- Baadhi ya njia za tafsiri husababisha kwenda kinyume na sarufi ya lugha lengwa au utamaduni wa lugha lengwa.
Hoja hii naiegemeza zaidi katika aina za tafsiri ambazo
ni tafsiri ya neno kwa neno, tafsiri sisisi, tafsiri ya kisemantiki na tafsiri
ya mawasiliano. Lakini hapa nitajikita zaidi katika tafsiri ya neno kwa neno. Mara
nyingi tunapotafsiri sentensi au matini kwa kutumia njia hii, lazima tufuate
sarufi ya lugha chanzi hivyo husababisha makosa ya kimuundo na kimaana ya lugha
lengwa. Mifano ifuatayo inafafanua zaidi.
·
Kiingereza kwenda Kiswahili:
I / like / banana / s / more / than / orange / s /
Mimi / penda/kama / ndizi / wingi / zaidi / kuliko /
chungwa / wingi /
·
Kiswahili kwenda kiingereza
Wa / toto / wa / dogo / wa / na / imba / kwa / furaha
/
Plural / child / plural / small / they / present
continues tense (singular) / by/for / happiness
Unapochunguza mifano ya hapo juu, utakuta kuwa
ufuataji wa sarufi ya lugha chanzi hupelekea kuharibu sarufi ya lugha lengwa na
kupoteza maana inayokusudiwa kutoka lugha chanzi.
Vile vile tunapotafsiri methali, misemo, nahau na
matini nyengine za kifasihi, kwa kutumia njia yoyote ya tafsiri, mfasiri
anaweza kwenda kinyume na utamaduni wa lugha lengwa endapo atakuwa si mzoefu wa
utamaduni wa jamii hiyo.
- Tafsiri husababisha matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili katika maandishi.
Hapa nakusudia kueleza kuwa, moja ya njia ya
uchanganyaji wa lugha katika maandishi ni tafsiri. Watu wengi
wanaojishughulisha na kutafsiri matini mbali mbali kwenda lugha ya Kiswahili
huathiriwa na kazi hio na kuwasababishia kuchanganya lugha pale wanapoandika
kazi nyengine za Kiswahili jambo ambalo ni kinyume na utamaduni wa mtanzania.
Jambo hili huweza kujitokeza kwa waandisi wa makala mbali mbali za Kiswahili
lakini pia wahariri wa magazeti.
Hapa nataka nifahamike kuwa, sipingi
utumiaji wa neno au maneno ya lugha nyengine kama kiingereza ambayo yana lengo
la kutoa ufafanuzi zaidi juu ya jambo fulani ambapo mara nyingi maneno hayo
huwekwa katika mabano. Bali nakusudia uchanganyaji wa lugha kwa ujumla. Mfano
katika upekuaji wa makala mbali mbali nimegundua matumizi hayo kama ifuatavyo:-
“Mimi ninadhani values za jamii ni kioo
ambacho maendeleo yoyote that we want
and to find out kwa udi na uvumba lazima ya reflect, kama we have not values za maana ni vipi tutaendelea”
Kwa hiyo mtu anayetumia lugha kama inavyoonekana katika
maelezo yaliopo hapo juu, mimi kwa maoni yangu naona mtu huyo ama ameathiriwa
na lugha ya kiingereza au kutokana na kufanya kazi nyingi za tafsiri.
Hitimisho na Mapendekezo:
Kwa ujumla makala hii imeelezea kwa kina kuhusu faida
na hasara za tafsiri katika utamaduni ambapo maelezo yake, zaidi yamejikita
kutoka katika dhana ya tafsiri, dhana ya utamaduni lakini zaidi kupitia
historia na maendeleo ya tafsiri nchini Tanzania.
Licha ya uhaba wa historia ya tafsiri nchini Tanzania,
na pamoja na kuwepo baadhi ya changamoto katika vipengele mbali mbali vya
maisha ya jamii ya watanzania na Afrika kwa ujumla, bado taaluma hii ni muhimu
sana hasa katika mawasiliano kati ya jamii zinazozungumza lugha tofauti, pia ni
muhimu katika masuala mbali mbali ya kielimu bila ya kusahau katika soko la
ajira.
Kwa hiyo ili kufikia malengo hayo, ni wajibu wetu
kuisoma taaluma hii kwa undani zaidi pamoja na kufuata kikamilifu kanuni,
taratibu na sheria za tafsiri ili tuweze kupata kazi nzuri za tafsiri zenye
kukidhi mahitaji ya matini chanzi, matini lengwa na utamaduni wa jamii husika.
MAREJELEO :
ü Mshindo,
H. B. (2010). KufasirinaTafsiri. Chuo Kikuu cha Elimu. Chukwani,
Zanzibar.
ü
Mwansoko,
J. M. (1961). Kitangulizi
cha tafsiri, nadharianambinu. TUKI. Dar es salaam.
ü Mwansoko
na Wenzake (2006). Tafsiri na Ukalimani. UDSM.
ü Ponera,
A. S. (2014). Utangulizi wa Nadharia ya Fasihi
Linganishi. Karljamer Print Technology. Dar es salaam, Tanzania.
MITANDAO
ü antagonf.blogspot.com. Tafsiri na
ukalimani.
ü
chomboz: blogsport.com/2013. MisingiyaTafsirinaUkalimani.
ü https://sw.m.wikipedia.org. Utamaduni – wikipedia, kamusi elezo huru.
ü nenothabiti.blogspot.com.
Tafsiri.
================================================
Mtunzi: Said Ali Shehe. Muhitimu, Chuo Kikuu cha Sumait Zanzibar.