Kategoria za kisarufi
Kategoria ya kisarufi ni kundi la
maneno lenye sifa za kisarufi zinazofanana.
Kwa mfano, mtoto, embe, kiti, mti
n.k. ni maneno ya kategoria
nomino kwa sababu yana sifa shirika.
Maneno ya kategoria moja ya kisarufi yana sifa za kisemantiki, kimofolojia au
kisintaksia zinazofananana ambazo ziwapo katika tungo hujaza nafasi karibu
ileile.
Nomino – hutaja jina la kitu, huwa mtenda au
mtendwa katika sentensi,
huweza kuwa katika umoja au wingi.
Kwa mfano: mtoto – watoto, kitu – vitu, embe –maembe.
Kitenzi – huonyesha tendo au hali ya
kufanyika kwa kitu. Kwa mfano: cheza, imba, kimbia.
Kivumishi – hueleza sifa ya kitajwa ambacho ni
nomino. Kwa mfano: dogo, zuri
Aina nyingine za maneno ni pamoja na
kielezi, kiunganishi, kihusishi n.k.
Aina za maneno hutumika kubainisha
aina za virai kwani jina la kirai hutokana na kategoria ya kisarufi ya neno
kuu.
Maana ya sintaksia
Sintaksia ni tawi la isimu ambalo
linahusu namna maneno yanavyoungana na kuhusiana katika kirai au sentensi. Sintaksia
inachunguza namna maneno yanavyojipanga katika sentensi kwa kuzingatia kanuni
za sarufi ya lugha husika.
Mikabala tofauti ya Sintaksia
Uchambuzi wa muundo wa lugha
umefanywa na wanasarufi wa nyakati tofauti na kuzua mikabala tofauti kuhusu
muundo wa lugha kama walivyouona kwa wakati wao. Mkabala wa awali uliokuwa
umejikita katika lugha kongwe kama Kilatini ulikuja kujulikana baadaye kama wa
kimapokeo kwani ndio uliorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na kutumika
kuchambua
lugha nyingine za
dunia. Mkabala mwingine ni ule ulioichambua lugha kwa kuzingatia vijenzi
vinavyounda sentensi na ulioasisiwa na Chomsky. Mkabala huu ulijulikana kama mkabala
wa kimuundo ambao hata hivyo baadaye ulifanyiwa marekebisho zaidi na mwenyewe
Chomsky na waliomfuata.
Mkabala wa Kimapokeo
Wanamapokeo walichambua sintaksia ya
lugha kwa kuainisha miundo ya sintaksia iliyo katika lugha. Kwa mujibu wa
wanamapokeo, virai na sentensi zimeundwa na kategoria za kisarufi yaani maneno
ambayo kila moja liliainishwa na uamilifu wake kutajwa. Kwa hivyo mwanaisimu
alichambua sentensi kwa:
a) kutaja kategoria za kisarufi za
maneno yanayounda sentensi
b) kueleza kazi au uamilifu wa kila
neno lililounda sentensi.
Kwa mfano: ‘Mama anapika chakula’.
Sentensi hii ilichambuliwa kwa
kueleza:
Muundo: Sentensi hii inaundwa na maneno
matatu: ‘mama’, ‘anapika’ na ‘chakula’ na kwamba kila neno lina kategoria yake
Kategoria za maneno yanayounda
sentensi: ‘mama’ na
chakula’ ni nomino za umoja, na ‘anapika’ ni kitenzi kilicho katika wakati
uliopo.
Uamilifu wa kila neno: ‘Mama’ ni kiima, ‘anapika chakula’ ni
kiarifu.
Aina ya sentensi: Sentensi hii ni kishazi. Hii ni
sentensi arifu.
Aidha wanamapokeo walichambua
sentensi kwa kubainisha kategoria za maneno yaani aina za maneno kwa mujibu wa
maana zake, vipengele vya kimofolojia na au tendo.
Nomino ilifafanuliwa kuwa ni jina la
kitu, mtu, mnyama, hali. Nomino huweza kuhesabika au kutohesabika na kwamba
huwa na umoja na wingi au umoja tu au wingi tu.
Kitenzi kilifasiliwa kuwa ni neno
lenye kudokeza tendo ambalo huchukua viambishi vya wakati uliopo, uliopita au
ujao, mtenda ambaye huwakilisha kiima katika kitenzi , mtendwa n.k. Katika
sentensi kitenzi hufuata kiima ambacho ni nomino mtenda au kufuatwa na nomino
mtendwa au yambwa. Kwa hivyo sentensi ‘ Mama amelala’ ingechambuliwa hivi:
Sentensi hii ina nomino ‘mama’ ambayo
ina uamilifu wa kiima cha sentensi yaani mtenda na kitenzi ‘amelala’ chenye
uamilifu wa kiarifu cha sentensi. Kitenzi hiki ni sielekezi.
Mkabala wa wanamiundo kama
ulivyoasisiwa na Noam Chomsky
Nadharia ya Sintaksia ambayo mwasisi wake ni Noam
Chomsky imejaribu kueleza vipengele vya kisintaksia vya lugha mbalimbali ili
kuonyesha jinsi lugha mahsusi zinavyopanga maneno yao ili kupata sentensi
Lengo la Chomsky katika
uchanganuzi wake wa lugha ni kuunda nadharia ya sintaksia ya jumla
itakayonyesha vipengele vya kisintaksia vinavyopatikana katika kila lugha na
jinsi vinavyotofautiana. Hii inafahamika kama nadharia ya sarufi ya jumla.
Lengo lingine la Chomsky ni kupinga
mtazamo wa wanaisimu wa miaka 1950 (wanamapokeo) waliodai kuwa tofauti za lugha
hazina ukomo, mtazamo ambao hakuuafiki kwani ulimaanisha kuwa ingebidi kila
lugha iwe na nadharia yake. Alidai kuwa tofauti baina ya lugha ni ndogo na
kwamba nadharia ya sarufi ya lugha ingeweza kujumuisha lugha zote isipokuwa kwa
tofauti ndogondogo tu. Alibainisha kategoria za virai kuwa ni: KN, KT, KV, KE,
KH, KU.
Sarufi miundo virai
Muundo ni mpangilio wa vitu vidogo
vilivyowekwa pamoja na kujenga kitu
kikubwa zaidi.
Sarufi miundo virai ni mkabala wa
kuchambua lugha kwa kuigawa sentensi katika virai vinayoiunda na kisha
kuvichanganua zaidi hadi kufikia neno moja moja lililokiunda kirai.
Tungo huundwa na viambajengo kwa
utaratibu maalumu.Tungo za lugha ni neno, kirai, kishazi na sentensi. Virai,
vishazi na sentensi huundwa na maneno.
Muundo wa kirai na sentensi
Kirai, kishazi na sentensi ni
vipashio vya lugha vinavyoundwa na viambajengo ambavyo ni vidogo kuliko
vyenyewe. Kirai hujengwa na maneno, na kishazi na sentensi hujengwa na virai.
Viambajengo vya tungo ndivyo vinavyofanya muundo wa tungo husika.
Muundo wa Kirai
Kirai ni fungu la maneno
yanayohusiana kimuundo lisilokuwa na muundo wa kiima kiarifu. Maneno katika
kirai humilikiwa na neno moja ambalo ndilo neno kuu. Kirai hubainishwa na
kategoria ya neno kuu. Kwa mfano: KN, KT, KV, KE KH n.k.
Virai huundwa na viambajengo.
Kiambajengo ni kikundi cha maneno au hata neno moja pia inayofanya kazi kama
kitu kimoja. Kirai, kishazi au sentensi ni mkusanyiko wa viambajengo kadha.
Kirai ni mkusanyiko wa viambajengo
vilivyojengwa kuzunguka neno kuu. Kwa mfano, KN huundwa na nomino na vivumishi
vyake, kwa hivyo muundo wa kirai ni maneno yanayokiunda yakiwakilishwa na alama
za kategoria za maneno hayo.
Kwa mfano:
a) ‘Mtoto mdogo’.
Hiki ni Kirai Nomino (KN)
kilichoundwa na N (nomino) na V (kivumishi).
Kwa hivyo KN à N+V
b) ‘analima shamba’.
Hiki ni kirai kitenzi (KT) chenye
kuundwa na kitenzi (T) na kirai nomino (KN). Kwa hivyoK
T à T+KN
Muundo wa Vishazi na Sentensi
Kishazi ni kikundi cha maneno kilicho
ndani ya sentensi chenye muundo wa
kiima na kiarifu. Kishazi kina muundo
sawa na sentensi.
Aina za vishazi na miundo yake
a) Vishazi
ambatani
b) Vishazi
tegemezi
Sentensi na Miundo yake
Sentensi ni kikundi cha maneno chenye
maana iliyo kamili. Sentensi ndicho kipashio lugha cha kimuundo ambacho ni
kikubwa kuliko vipashio vingine. Vipashio vya lugha ni pamoja na: mofimu, neno,
kirai, kishazi na sentensi yenyewe. Sentensi na kishazi huundwa na virai vikuu
viwili: KN na KT. KT yaweza kuundwa na kitenzi na nomino, kitenzi na kielezi
n.k.
Kwa hivyo S-à KN + KT
Sentensi na upatanishi wa kisarufi
Sarufi geuza umbo zalishi
Nadharia geuza umbo zalishi huonyesha
ujuzi alionao mzungumzaji ambao humwezesha kutunga sentensi sahihi na zisizo na
kikomo. Uwezo wa mzungumzaji kutunga sentensi zisizo na ukomo unatokana na
kufahamu kanuni za kutunga sentensi sahihi ambazo mzawa wa lugha anazijua kutokana
na kuwa na umilisi na lugha yake. Kanuni za kutunga sentensi sahihi hubainisha
sentensi sahihi na zisizo sahihi.
Kwa mujibu wa nadharia hii, sentensi
ina umbo la nje ambalo ndilo linalojitokeza katika usemaji na hata
inapoandikwa, na umbo la ndani ambalo huwa limefichika na hujidhihirisha katika
umbo jingine wakati wa kuongea (maana).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni