Ijumaa, 27 Februari 2015

ALOFONI KATIKA LUGHA YA KISWAHILI

ALOFONI KATIKA LUGHA YA KISWAHILI
Imeandaliwa
Na, Mutashobya A. T
(BAED mwaka wa tatu-UDSM)
1.0       UTANGULIZI
Alofoni katika lugha ya Kiswahili ni dhana ambayo haijashughulikiwa vizuri. Hii ni kutokana na wataalamu mbalimbali kutofautiana juu ya dhana hii. Tofauti hizi za wataalam zinajitokeza juu sauti za lugha wanazozitoa kama mifano ya alofoni za Kiswahili. Wengine huenda mbali na kusema kuwa lugha ya Kiswahili haina Alofoni. Madhumuni ya makala hii ni kujaribu kuchunguza alofoni katika lugha ya Kiswahili. Na kufikia hitimisho iwapo lugha ya Kiswahili ina Alofoni au la. Na iwapo lugha ya Kiswahili ina alofoni basi alofoni hizo ni zipi? Tutachunguza dhana ya alofoni kama inavyofasiliwa na wataalam mbalimbali, mbinu mbalimbali za kuzitambua alofoni na fonimu za lugha na kisha tutaichunguza mifano mbalimbali ya alofoni inayotolewa na wataalam mbalimbali. Mwisho nitatoa msimamo wangu na kuhitimisha kwa kuchokoza mjadala.  
2.0       KIINI
Kabla ya kusema Alofoni ni nini kwanza tutoe maana za istilahi za muhimu katika kuelezea dhana nzima ya Alofoni. Istilahi hizi ni pamoja na Fonolojia na Fonimu.

2.1       Fonolojia ni nini?
Habwe na Karanja (2004) wanasema Fonolojia ni utanzu wa isimu unaochunguza jinsi sauti za lugha zinavyopangwa na kuungana katika lugha mahsusi ili kuunda utungo wenye maana kimawasiliano.
Massamba na wenzake (2013) nao wanaeleza kuwa Fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu. Hii ina maana kwamba fonolojia kama tawi la isimu hujishughulisha hasa na zile sauti ambazo hutumika katika kutofautisha maana za maneno katika lugha mahususi.



Ninakubaliana na fasili hizo mbili kama zilivyotolewa na wataalam hawa, kwa sababu zimekidhi sifa za fonolojia kwamba ni tawi la isimu linalojishughulisha na uchunguzi wa sauti katika lugha mahususi.
2.2     Fonimu ni nini?
Kwa malengo ya makala  haya sitotazama katika mitazamo au mikabala mbalimbali ya kuifasili dhana ya fonimu (yaani ile inayoitazama  fonimu kama tukio la kifonetiki, fonimu kama tukio la kifonolojia n.k).  Nitachukua maana ya jumla tu kwa kuwarejelea; Kamusi Sanifu ya Kiswahili, na Massamba na wenzake katika kitabu chao cha FOKISA. 
Kamusi Sanifu ya Kiswahili (TUKI); fonimu (katika sarufi) inaelezwa kuwa ni tamshi katika neno ambalo likibadilishwa na tamshi jingine maana ya neno hilo hubadilika au hupotoka katika lugha hiyo. Kwa mfano, maneno kama “sabuni” na “zabuni” hapa fonimu zinazotofautisha maana  ni /s/ na/z/.
Wakati huo huo Massamba na wenzake (2013:21) wanaifasili fonimu kama kitamkwa kilicho bainifu katika lugha fulani maalum. Wanaeleza zaidi kuwa  ni muhimu kukumbuka kwamba ubainifu wa vitamkwa hutofautiana kutoka lugha moja hadi lugha nyingine. Kwa mfano, wakati sauti inayowakilishwa na herufi /z/ huweza kuchukua dhima ya kifonimu katika lugha ya Kiswahili (lingalisha /zana/ na /sana/), sauti hiyo hiyo haiwezi kuchukua dhima ya kifonimu katika lugha ya Ciruuri kwa sababu lugha hiyo ya Ciruuri haina sauti kama hiyo katika sauti zake.
Ninakubaliana na fasili hizo zote mbili, kwa sababu zimekidhi sifa za msingi za fonimu. Sifa hizo ni kama;
·         Kila fonimu hushiriki kujenga na kutofautisha maana katika maneno, hii ikiwa na maana kuwa kubadili, kuongeza, au kupangua fonimu moja katika neno basi hupelekea kubadili maana ya neno hilo.
·         Kila lugha ina fonimu zake na fonimu za lugha tofauti hazifanani katika uamilifu wao.

2.3        Alofoni ni nini?
Hapa nitatoa fasili ya alofoni kwa kumrejelea mtaalam mmoja tu (Mgullu 1999) nikiamini kwamba fasili hii inakidhi sifa za alofoni ambazo zimetajwa pia na mtaalam huyo. Mjadala 

wa kuchunguza alofoni za Kiswahili nitauleta baada ya kutazama mbinu mbalimbali za kutusaidia kutambua fonimu na alofoni katika lugha.
Mgullu (1999) akimnukuu Hartman (1972) anasema kuwa alofoni ni sauti mojawapo miongoni mwa sauti kadhaa zinazowakilisha fonimu moja.  Alofoni hutokea katika mazingira mahsusi(mazingira ya kiutoano).
Aidha, Mgullu (keshatajwa) akimnukuu Ladefoged (1962) anasema kuwa alofoni ni matamshi tofauti tofauti ya fonimu moja.  Pia anasema alofoni za fonimu moja huunda kundi moja la sauti ambazo;
1.      Hazibadili maana ya neno,
2.      Hutokea katika mazingira tofauti ya kifonetiki, na
3.      Alofoni zote hufanana sana kifonetiki.
Kutokana na fasili hizo, naweza kusema alofoni ni maumbo tofauti tofauti ya fonimu moja, ingawa maumbo hayo huwa na tofauti ndogo ndogo za kifonetiki lakini hayaleti tofauti yoyote katika maana za maneno.
Tuchukue mifano ya maneno kutoka katika lugha ya Kiingereza;

                                                      tea;    eat;     writer;    
                                                    /thi:/     /i:t/      /raita/         
         
Katika maneno yetu hapo juu sauti [th] inayotokea mwanzoni mwa neno, na sauti [t] inayotokea popote ni alofoni za fonimu /t/. Sauti hizi hazibadili maana ya maneno, zinatokea katika mazingira tofauti na zinafanana sana kifonetiki.
Katamba (1996) anasema alofoni zinaweza kujitokeza pia katika maneno:
                                                      tea;           two;         eighth;
                                                       /ti:/          /twu/          /eitɵ/
[t] katika /ti:/  utamkwa wakati midomo ikiwa imesambaa, [tw] katika /twu/  hutamkwa wakati midomo ikiwa mviringo na [t] katika /eitɵ/ ni sauti ya meno. Hivyo [t], [tw]na [t] ni alofoni za fonimu /t/
 
Katamba (keshatajwa) anasema si kila sauti zenye kubadilishana mazingira basi zaweza kuwa alofoni katika lugha ya Kiingereza. Kwa mfano sauti /h/ na /ŋ/ hubadilishana mazingira ya utokeaji (sauti  /h/ hutokea mwanzoni mwa silabi ikifuatiwa na irabu mfano;  hat, head, n.k wakati sauti /ŋ/ hutokea mwishoni mwa silabi katika konsonanti zilizoungana, mfano; longer, long, bung n.k),   lakini hazifanani kifonetiki hivyo haziwezi kuwa alofoni za sauti moja.
Aghalabu alofoni hutumiwa katika muktadha au mazingira ya kifonetiki yaliyo tofauti, ambapo alofoni moja ikitumika katika mazingira fulani basi nyingine haiwezi kutumika  katika mazingira hayo  hayo.
2.3         Mbinu za kuzitambua fonimu na alofoni.
Kuna mbinu mbalimbali kuzibainisha fonimu na alofoni za lugha fulani. Tutazipitia mbinu hizi kwa muhtasari ili zituongoze katika mjadala wetu juu ya alofoni katika lugha ya Kiswahili. Mbinu au njia hizo ni kama; kufanana kifonetiki, jozi za mlinganuo finyu,mgawanyo wa kiutoano na mpishano huru.
2.4.1     Mbinu ya kufanana  kifonetiki.

Mbinu hii huelezea kwamba sauti ambazo huwa na sifa za kifonetiki zinazofanana basi huchukuliwa kuwa ni sauti za fonimu moja (alofoni). Kama sauti hazina sifa za kifonetiki zinazofanana basi huchukuliwa kama ni fonimu mbili tofauti. Kwa mfano tuchunguze sifa za kifonetiki za sauti /i/ na /u/ katika lugha ya Kiswahili;
           /i/                                              /u/
+irabu                                +irabu
+mbele                                +nyuma
+juu                                    +juu
-mviringo                             +mviringo

Kwa mujibu wa kigezo hiki, sauti /i/ na /u/ ni fonimu mbili tofauti katika lugha ya Kiswahili kwa sababu zina sifa tofauti za kifonetiki


2.4.2      Mbinu ya Jozi za Mlinganuo finyu.

Kama anavyoeleza Fischer (1975), mlinganuo finyu ni tofauti ndogo kabisa ya kifonolojia iliyopo baina ya maneno fulani: aghalabu maneno hayo huwa na;
         I.            Idadi sawa ya fonimu
      II.            Fonimu zinazofanana isipokuwa moja katika mazingira sawa ya kifonetiki
   III.            Mpangilio wa fonimu uliosawa
   IV.            Maana tofauti

Tuchunguze seti ya maneno yafuatayo;
Pia      -       tia
Paka    -     taka
Wali    -      hali

Katika seti ya maneno hapo juu tunaona kwamba maneno /pia/ na /tia/ yapo katika jozi mlinganuo finyu kwa sababu yana idadi sawa ya fonimu, yaani fonimu tatu kila neno, fonimu zinazofanana isipokuwa moja, na mpangilio wa fonimu ulio sawa,na maana zikiwa tofauti. Halikadhalika katika seti ya maneno /paka/ na /taka/  kwa sababu nayo yana idadi sawa ya fonimu yaani, fonimu nne zinazofanana isipokuwa moja na mpangilio wa fonimu ulio sawa. Pia katika seti ya maneno /wali/ na /hali/ tunaona kuwa yapo katika jozi mlinganuo finyu kwa sababu yana idadi sawa ya fonimu yaani fonimu nne zinazofanana isipokuwa moja na mpangilio wa fonimu ulio sawa. Njia hii hutusaidia kuzitambua fonimu za lugha kwa sababu tofauti ya fonimu moja yatosha kubadili maana za maneno hayo.
 

2.4.3       Mbinu ya mgawanyo wa kiutoano.

Hyman (1975) anasema katika fonolojia, utoano ni dhana ambayo hutumika kuelezea uhusiano uliopo baina ya sauti mbili (au zaidi) za fonimu moja ambazo haziwezi kutokea katika mazingira sawa katika neno. Hii ina maana kwamba sauti huwa ina mahali/mazingira yake maalum ambayo hayawezi kukaliwa na sauti nyingine ya kundi moja.
Tuchunguze mifano kutoka katika lugha ya Kiingereza; kuhusu sauti /ph/ yenye mpumuo na sauti /p/ isiyo na mpumuo. Sauti /ph/ yenye mpumuo hutokea mwanzoni mwa maneno tu, kwa mfano katika maneno /phin/, /phen/, /phut/ n.k . Kwa upande mwingine /p/ isiyo na mpumuo hutokea sehemu yoyote ya neno isipokuwa mwanzoni; mfano katika maneno kama /top/, /cup/, /span/, /spare/ n.k
Sauti ambazo ziko katika mgawanyo wa kiutoano huwa hazitofautishi maana za maneno, isipokuwa sauti hizo hugawana tu mahala pa kutokea au kutumika. Hivyo sauti hizo huwa ni alofoni za fonimu moja.
Tuchunguze sifa bainifu za sauti /ph/ yenye mpumuo  na  sauti /p/ isiyo na mpumuo;

/ph/                                        /p/
                                                      +kons                                       +kons
+mpumuo                           -mpumuo
-ghuna                                -ghuna
+midomo                           +midomo
+kipasuo                             +kipasuo

 



[ph] yenye mpumuo  na  sauti [p] isiyo na mpumuo ni alofoni za fonimu /p/. Sifa zote za sauti hizi zinafanana isipokuwa moja tu (sifa ya mpumuo).

2.4.4        Mbinu ya Mpishano Huru.

Huu ni uhusiano wa fonimu mbili tofauti kubadilishana nafasi moja katika maneno maalum bila kubadili maana za maneno hayo. Hapa mpishano unatumika kwa ile maana ya “wewe ondoka, mimi niingie.” Kwa kuwa fonimu moja inatolewa katika neno fulani na fonimu nyingine inakaa mahali pake bila kubadili maana ya neno hilo.
Mpishano huru  huhusisha fonimu mbili kubadilishana nafasi moja katika neno moja.  Fonimu hizo huwa ni tofauti kabisa kifonetiki hivyo hatuwezi kuziita alofoni.
Tuchunguze mifano ifuatayo;
·         /buibui/ na /baibui/ sauti /u/ na /a/ zimepishana nafasi bila kubadili maana ya neno.
·         /Wasia/ na /wosia/ sauti /a/ na /o/ zimepishana bila kubadili maana ya maneno.




Tuchunguze sifa bainifu za kifonetiki za sauti /a/ na /u/ katika maneno /baibui/ na /buibui/
                                      /a/                                 /u/
                                 +irabu                             +irabu
                                 +mbele                           +nyuma
                                 +chini                             +juu
                                -mviringo                       +mviringo


Tuchunguze pia sifa bainifu za kifonetiki za sauti /a/ na /o/ katika maneno /wasia/ na /wosia/
                            
                                  /a/                                    /o/
                               +irabu                              +irabu
                               +mbele                            +nyuma
                               +chini                              +nusujuu
                               -mviringo                        +mviringo

Sauti hizi haziwezi kuwa alofoni kwa sababu zinatofautiana sana kifonetiki.
Njia hizi zitumikapo, aghalabu kwa pamoja, kwa kusaidiana huweza kutusaidia kutambua fonimu na alofoni za lugha inayofanyiwa uchunguzi.

3.0     Alofoni katika lugha ya Kiswahili.
Sasa tuchunguze dhana ya alofoni kama inavyojadiliwa na wataalamu mbalimbali wa Isimu ya Kiswahili. Hapa tutaonesha fasili pamoja na mifano ya alofoni katika lugha ya Kiswahili kwa mujibu wa wataalamu hao.
Massamba na wenzake (2013) wanasema alofoni ni sura au maumbo mbalimbali ya fonimu moja.  Fonimu za lugha huweza kupata sura tofauti tofauti kulingana na mazingira katika neno ambamo hutokea. Hii ina maana kwamba fonimu inaweza kubadilika ikachukua umbo moja kutokana na kutokea kwake katika mazingira fulani na ikaweza pia kubadilika ikachukua umbo jingine kutokana na kutokea kwake katika mazingira mengine tofauti katika neno. Wanatoa mifano ya alofoni kutoka katika lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:

            Mofimu za neno                                          Matamshi yake
(a)               ki+ti   ki+refu                                            [kiti kirɛfu]
(b)              ki+ti   ki+eusi                                             [kiti ʦeusi]
(c)              u+limi m+refu                                            [ulimi mrɛfu]
(d)              n+limi n+refu                                            [ndimi ndɛfu]
(e)                 n+buzi                                                           [mbuzi]
(f)                 n+dama                                                          [ndama]
(g)              n+gombe                                                           [ᵑᵓᵐᵇᵋ]
 
Katika mifano ya Kiswahili hapo juu, tunaona mabadiliko ya kifonimu yakijitokeza.  Katika mfano wa (b) fonimu /k/ inapofuatiwa na irabu  /i/  halafu kukawa na mpaka wa mofimu, kisha  ikafuatiwa na irabu /e/ hubadilika na kuwa /ch/  ki+eusi = [tseusi] na katika  (d)  tunaona  wazi  kuwa  fonimu /l/ inapotanguliwa na nazali /n/ hubadilika na kuwa /d/  [n+limi = ndimi]. Halikadhalika katika mifano ya (e) na (g) tunaona kwamba nazali /n/ inapofuatiwa na kitamkwa  /b/ hubadilika na kuwa /m/, inapofuatiwa na kitamkwa /d/ hubakia /n/, na inapoafuatiwa na  kitamkwa /g/ hubadilika na kuwa //.
Hii  ina  maana  kwamba  katika  mazingira  haya  sauti  [ts]  ni  alofani  ya  fonimu  /k/,  [d]  ni  alofoni  ya  fonimu  /l/  na  [m],  [n]  na  []  ni  alofani  za  fonimu  /N/  (katika  fonolijia  herufi  hii  kubwa  hutumika  kuwakilisha dhana  ya  nazali) na alama /N/ ikiwa kama kiwakilishi cha fonimu kuu
Alofoni hizo hapo juu zimetokana na michakato ya mofofonolojia(taaluma ya isimu inayoshughulikia uchunguzi na uainishaji wa vipengere vya kifonolojia vinavyoathiri maumbo ya mofimu au vipegere vya kisarufi vinavyoathiri maumbo ya fonimu). Pamoja na kwamba mabadiliko haya yameitwa mabadiliko ya kifonimu lakini tukichunguza vizuri tutaona kwamba kwa kiasi kikubwa ni maumbo yaliyobadilika na kwa kiasi Fulani fonimu.
Kwa mfano, mofimu ya ngeli ya tisa {n-} katika majina kama vile nyumba, mbuzi, ng’ombe, n.k (inabadilika katika mazingira tabirifu) kuwa mofimi {m},{ŋ} na wakati mwingine hubaki vilevile {n}. Mchakato huu huitwa mchakato wa au kanuni ya konsonanti kuathiri nazali. Hivi kwamba mofimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {m} pale inapokuwa imeitangulia sauti ya midomo. Halikadhalika mofimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {ŋ} pale inapokuwa imeitangulia sauti ya kakaa laini.
Kwa mantiki hii basi maumbo haya yote yatakuwa yanaiwakilisha mofimu moja yaani ngeli ya tisa {n-}. Kama hivi ndivyo basi maumbo hayo yatakuwa ni alomofu na si alofoni.
Alomofu ni mojawapo ya viwakilishi viwili au zaidi vya mofimu moja ambavyo hujitokeza katika mazingira tofauti ya mtoano. Massamba na wenzake(2012)
Katika data ambayo imetolewa na Massamba na wenzake (wameshatanjwa) kuna baadhi ya sauti ambazo zinatokana na michakato ya kifonolojia au badiliko la kifonolojia ambapo nazali huiathiri konsonanti inayoambatana nayo ili kurahisisha matamshi. Sauti zinazoathirika hapa ni sauti za likwidi (kimadende /r/ na kitambaza /l/).
      (a)     u+limi m+refu                                [ulimi mrɛfu]
     (b)   n+limi n+refu                                  [ndimi ndɛfu]
Sauti /l/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya kutanguliwawa na nazali /n/, vilevile sauti /r/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya kutanguliwa na nazali /n/.
Sauti hizi zinatokea katika mazingira ya kiutoano na zinafanana sana kifonetiki hivyo twaweza kuziita alofoni.
Tuchunguze sifa za kifonetiki za sauti /r/ na /d/, na /l/ na /d/


/r/                 /d/                                            /l/                /d/
+kons            +kons                                      +kons            +kons
+ufizi            +ufizi                                       +ufizi            +ufizi
+kimadende    +kipasuo                                 +ktambaza      +kipasuo

Mdee (1986), anadai kuwa sauti [x] na [h] ni alofani za fonimu /h/ kama inavyodhihirika katika  maneno /kheri/ na /heri/.
Tukichunguza sauti hizi, ni kweli kwamba  hazileti  tofauti za maana katika lugha ya  Kiswahili  isipokuwa  sauti  hizi  ni  tofauti  mno  kifonetiki. Wakati sauti /x/ ni ya kakaa  laini,  sauti /h/ ni ya glota.
Je, sauti moja inaweza kutamkiwa katika sehemu mbili tofauti?
Matinde (2012) anasema alofoni ni maumbo mawili au zaidi ambayo huwakilisha fonimu moja. Anaendelea kwa kusema kuwa alofoni ni matamshi tofauti tofauti ya fonimu moja ambayo hujitokeza kutegemea mazingira ya utokeaji wa sauti hiyo.
Matinde(keshatajwa) yeye anatofautiana na wanaisimu kama Mdee (ameshatajwa) ambao wanasema lugha ya Kiswahili ina alofoni kwa kutumia jozi za maneno/kheri/ na /heri/ wakisema /x/ na /h/ ni alofani za fonimu /h/. Anasema tukizingatia vigezo vya kutambulisha alofoni, hizi ni sauti ambazo ni tofauti kabisa kwa misingi ya sifa bainifu za kifonetiki, hususan jinsi ya kutamkwa na mahali pa kutamkiwa.
Matinde (ameshatajwa) anasema alofoni katika lugha ya Kiswahili sawa na lugha ya Kiingereza, hudhihirika na vipasuo hafifu, hivi kwamba kipasuo hafifu kinapokuwa mwanzoni mwa neno kutamkwa kikiwa na mpumuo, ilhali kipasuo hicho kinapotanguliwa na fonimu tofauti hutamkwa bila mpumuo. Kwa mfano  neno /pale/ kipasuo (p) hutamkwa kikiwa na mpumuo (ph) lakini kipasuo hicho kinapotanguliwa na fonimu tofauti kwa mfano katika neno /alipo/ kipasuo /p/ hutamkwa bila mpumuo. Anaendelea kueleza kuwa hali hii hudhihirishwa pia katika maneno;
Neno                                       Utamkaji
Katika                                     /khatika/
Palipo                                      /phalipo/
Panda                                      /phanda/
Kaa                                          /khaa/
Kwa hivyo, maumbo yote mawili yaani  [p] na [ph] ni alofani za fonimu /p/. Aidha, maumbo [k] na [kh] ni alofani za fonimu /k/.
Sauti alizozionesha Matinde (keshatajwa) ambazo  ni  kama alofoni ni vibadala tu katika lugha ambavyo hutokana na tofauti za kilahaja. Lakini pia mtindo wa uzungumzaji waweza kusababisha vibadala hivi. Ndio maana si hajabu kukutana na binti wa kimjini akitamka kwa madaa “palipo uzia penyeza mapenzi”.
Matamshi yake ni kama;  /phalipho uzia phenyeza maphenzi/
 
Mpumuo sio sifa bainifu ya sauti za Kiswahili sanifu. Sina bainifu za sauti za Kiswahili ni kama vile; sifa ya ukonsonanti, namna ya kutamka, mahali pa kutamkia, mkao wa glota na unazali.
4.0       MAONI YANGU
Kwa maoni yangu, lugha ya Kiswahili inazo alofoni, ila ni vizuri zaidi kuwa makini katika kuzibaini alofoni hizo. Vigezo vinavyotupatia alofoni vitumike kwa uangalifu sana. Kwa mfano, katika kigezo cha kufanana sana kifonetiki sauti huchukuliwa kwamba ni tofauti sana iwapo zitatofautiana mahala pa kutamkia. Pia dhana ya alofoni isichanganywe na alomofu kwa sababu afoloni hurejelea sauti wakati alomofu urejelea umbo.
5.0        HITIMISHO
Tumeona kuanzia mwanzo wa mjadala kwamba ni vigumu kubainisha alofoni katika lugha ya Kiswahili. Ugumu huu unatokana na ukweli kwamba wataalam wametoa mifano ambayo inakinzana labda kutokana na vigezo vya uainishaji kutofautiana. Baadhi ya mifano haikidhi sifa za alofoni.
Nihitimishe kwa kutoa rai kwa wanazuoni na wanazuoni watarajiwa kuendelea kufanya tafiti zaidi zitakazolenga kuchunguza alofoni katika lugha ya Kiswahili. Pia Niseme wazi hapa kuwa alofoni hizo zikidhi sifa au vigezo vya kuitwa alofoni. Ninashukuru sana kwa usikivu wenu.
Mungu ibariki Afrika
Mungu ibariki CHAWAKAMA
Mungu tubariki wanachama wa CHAWAKAMA
“LONGA KISWAHILI TUJIKOMBOE KIFIKRA”
 




6.0      MAREJELEO:
Jones, D. (1950) An Outline of English Phonetics. New Delhi, Kalyani Publishers.
Habwe, J na Peter K.(2004). Msingi ya sarufi ya Kiswahili.Phoenix Publishers. Nairobi.
Katamba, F.(1996). An Introduction to Phonology. New York: Longman
Ladefoged, P.(1962) Element of Acoustic Phonetics. London: University of Chicago Press.
Massamba,D.P.B, Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2013) Fonolojia ya Kiswahili Sanifu. Sekondari naVyuo.   Dar es salaam: TUKI.
Massamba,D.P.B, Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2012) Sarufi Maumbo ya Kiswahili. Sekondari na Vyuo. Dar es salaam: TUKI.
Matinde, S.R.(2012) DAFINA YA LUGHA. Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) Ltd.
Mdee, J.(1986). Kiswahili: Muundo na Matumizi Yake. Nairobi: Intercontinental Publishers Ltd.
Mgullu, R. S.(1999) Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na Fonolojia ya Lugha ya Kiswahili.  Nairobi. Longhorn  Publishers.
TUKI (2013) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford University Press.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni