ALOFONI
KATIKA LUGHA YA KISWAHILI
Imeandaliwa
Na, Mutashobya A. T
(BAED mwaka wa tatu-UDSM)
1.0 UTANGULIZI
Alofoni
katika lugha ya Kiswahili ni dhana ambayo haijashughulikiwa vizuri. Hii ni kutokana
na wataalamu mbalimbali kutofautiana juu ya dhana hii. Tofauti hizi za wataalam
zinajitokeza juu sauti za lugha wanazozitoa kama mifano ya alofoni za Kiswahili.
Wengine huenda mbali na kusema kuwa lugha ya Kiswahili haina Alofoni. Madhumuni
ya makala hii ni kujaribu kuchunguza alofoni katika lugha ya Kiswahili. Na
kufikia hitimisho iwapo lugha ya Kiswahili ina Alofoni au la. Na iwapo lugha ya
Kiswahili ina alofoni basi alofoni hizo ni zipi? Tutachunguza dhana ya alofoni
kama inavyofasiliwa na wataalam mbalimbali, mbinu mbalimbali za kuzitambua
alofoni na fonimu za lugha na kisha tutaichunguza mifano mbalimbali ya alofoni
inayotolewa na wataalam mbalimbali. Mwisho nitatoa msimamo wangu na kuhitimisha
kwa kuchokoza mjadala.
2.0 KIINI
Kabla ya kusema Alofoni ni nini kwanza tutoe
maana za istilahi za muhimu katika kuelezea dhana nzima ya Alofoni. Istilahi
hizi ni pamoja na Fonolojia na Fonimu.
2.1 Fonolojia
ni nini?
Habwe
na Karanja (2004) wanasema Fonolojia
ni utanzu wa isimu unaochunguza jinsi sauti za lugha zinavyopangwa na kuungana
katika lugha mahsusi ili kuunda utungo wenye maana kimawasiliano.
Massamba
na wenzake (2013) nao wanaeleza kuwa Fonolojia
ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji
wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha
za binadamu. Hii ina maana kwamba fonolojia kama tawi la isimu hujishughulisha
hasa na zile sauti ambazo hutumika katika kutofautisha maana za maneno katika
lugha mahususi.
Ninakubaliana
na fasili hizo mbili kama zilivyotolewa na wataalam hawa, kwa sababu zimekidhi
sifa za fonolojia kwamba ni tawi la isimu linalojishughulisha na uchunguzi wa
sauti katika lugha mahususi.
2.2 Fonimu ni nini?
Kwa
malengo ya makala haya sitotazama katika
mitazamo au mikabala mbalimbali ya kuifasili dhana ya fonimu (yaani ile
inayoitazama fonimu kama tukio la
kifonetiki, fonimu kama tukio la kifonolojia n.k). Nitachukua maana ya jumla tu kwa kuwarejelea;
Kamusi Sanifu ya Kiswahili, na Massamba na wenzake katika kitabu chao cha FOKISA.
Kamusi
Sanifu ya Kiswahili (TUKI); fonimu
(katika sarufi) inaelezwa kuwa ni tamshi katika neno ambalo likibadilishwa na
tamshi jingine maana ya neno hilo hubadilika au hupotoka katika lugha hiyo. Kwa
mfano, maneno kama “sabuni” na “zabuni” hapa fonimu zinazotofautisha maana ni /s/ na/z/.
Wakati
huo huo Massamba na wenzake (2013:21) wanaifasili fonimu kama kitamkwa kilicho bainifu katika lugha fulani maalum.
Wanaeleza zaidi kuwa ni muhimu kukumbuka
kwamba ubainifu wa vitamkwa hutofautiana kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.
Kwa mfano, wakati sauti inayowakilishwa na herufi /z/ huweza kuchukua dhima ya
kifonimu katika lugha ya Kiswahili (lingalisha /zana/ na /sana/), sauti hiyo
hiyo haiwezi kuchukua dhima ya kifonimu katika lugha ya Ciruuri kwa sababu
lugha hiyo ya Ciruuri haina sauti kama hiyo katika sauti zake.
Ninakubaliana
na fasili hizo zote mbili, kwa sababu zimekidhi sifa za msingi za fonimu. Sifa
hizo ni kama;
·
Kila fonimu hushiriki kujenga na
kutofautisha maana katika maneno, hii ikiwa na maana kuwa kubadili, kuongeza,
au kupangua fonimu moja katika neno basi hupelekea kubadili maana ya neno hilo.
·
Kila lugha ina fonimu zake na fonimu za
lugha tofauti hazifanani katika uamilifu wao.
2.3 Alofoni ni nini?
Hapa nitatoa fasili
ya alofoni kwa kumrejelea mtaalam mmoja tu (Mgullu 1999) nikiamini kwamba
fasili hii inakidhi sifa za alofoni ambazo zimetajwa pia na mtaalam huyo.
Mjadala
wa
kuchunguza alofoni za Kiswahili nitauleta baada ya kutazama mbinu mbalimbali za
kutusaidia kutambua fonimu na alofoni katika lugha.
Mgullu
(1999) akimnukuu Hartman (1972) anasema kuwa alofoni ni sauti mojawapo miongoni
mwa sauti kadhaa zinazowakilisha fonimu moja. Alofoni hutokea katika mazingira mahsusi(mazingira
ya kiutoano).
Aidha,
Mgullu (keshatajwa) akimnukuu Ladefoged (1962) anasema kuwa alofoni ni matamshi
tofauti tofauti ya fonimu moja. Pia anasema
alofoni za fonimu moja huunda kundi moja la sauti ambazo;
1. Hazibadili
maana ya neno,
2. Hutokea
katika mazingira tofauti ya kifonetiki, na
3. Alofoni
zote hufanana sana kifonetiki.
Kutokana na fasili
hizo, naweza kusema alofoni ni maumbo tofauti tofauti ya fonimu moja, ingawa
maumbo hayo huwa na tofauti ndogo ndogo za kifonetiki lakini hayaleti tofauti
yoyote katika maana za maneno.
Tuchukue
mifano ya maneno kutoka katika lugha ya Kiingereza;
tea; eat; writer;
/thi:/ /i:t/
/raita/
Katika maneno yetu hapo
juu sauti [th] inayotokea mwanzoni mwa neno, na sauti [t] inayotokea
popote ni alofoni za fonimu /t/. Sauti hizi hazibadili maana ya maneno,
zinatokea katika mazingira tofauti na zinafanana sana kifonetiki.
Katamba (1996) anasema
alofoni zinaweza kujitokeza pia katika maneno:
tea; two; eighth;
/ti:/
/twu/ /eitɵ/
[t]
katika /ti:/ utamkwa wakati midomo ikiwa imesambaa, [tw] katika /twu/ hutamkwa wakati midomo ikiwa mviringo na [t]
katika /eitɵ/ ni sauti ya meno. Hivyo [t],
[tw]na [t] ni alofoni za fonimu /t/
Katamba
(keshatajwa) anasema si kila sauti zenye kubadilishana mazingira basi zaweza
kuwa alofoni katika lugha ya Kiingereza. Kwa mfano sauti /h/ na /ŋ/
hubadilishana mazingira ya utokeaji (sauti /h/ hutokea mwanzoni mwa silabi ikifuatiwa na
irabu mfano; hat, head, n.k wakati sauti
/ŋ/
hutokea mwishoni mwa silabi katika konsonanti zilizoungana, mfano; longer,
long, bung n.k), lakini hazifanani kifonetiki hivyo haziwezi
kuwa alofoni za sauti moja.
Aghalabu alofoni
hutumiwa katika muktadha au mazingira ya kifonetiki yaliyo tofauti, ambapo alofoni
moja ikitumika katika mazingira fulani basi nyingine haiwezi kutumika katika mazingira hayo hayo.
2.3 Mbinu
za kuzitambua fonimu na alofoni.
Kuna
mbinu mbalimbali kuzibainisha fonimu na alofoni za lugha fulani. Tutazipitia
mbinu hizi kwa muhtasari ili zituongoze katika mjadala wetu juu ya alofoni
katika lugha ya Kiswahili. Mbinu au njia hizo ni kama; kufanana kifonetiki,
jozi za mlinganuo finyu,mgawanyo wa kiutoano na mpishano huru.
2.4.1
Mbinu ya kufanana kifonetiki.
Mbinu hii huelezea kwamba sauti ambazo
huwa na sifa za kifonetiki zinazofanana basi huchukuliwa kuwa ni sauti za
fonimu moja (alofoni). Kama sauti hazina sifa za kifonetiki zinazofanana basi
huchukuliwa kama ni fonimu mbili tofauti. Kwa mfano tuchunguze sifa za kifonetiki
za sauti /i/ na /u/ katika lugha ya Kiswahili;
/i/ /u/
+irabu +irabu
+mbele +nyuma
+juu +juu
-mviringo +mviringo
Kwa mujibu wa kigezo
hiki, sauti /i/ na /u/ ni fonimu mbili tofauti katika lugha ya Kiswahili kwa
sababu zina sifa tofauti za kifonetiki
2.4.2 Mbinu ya Jozi za Mlinganuo finyu.
Kama
anavyoeleza Fischer (1975), mlinganuo finyu ni tofauti ndogo kabisa ya kifonolojia
iliyopo baina ya maneno fulani: aghalabu maneno hayo huwa na;
I.
Idadi sawa ya fonimu
II.
Fonimu zinazofanana isipokuwa moja
katika mazingira sawa ya kifonetiki
III.
Mpangilio wa fonimu uliosawa
IV.
Maana tofauti
Tuchunguze
seti ya maneno yafuatayo;
Pia -
tia
Paka - taka
Wali -
hali
Katika
seti ya maneno hapo juu tunaona kwamba maneno /pia/ na /tia/ yapo katika jozi
mlinganuo finyu kwa sababu yana idadi sawa ya fonimu, yaani fonimu tatu kila
neno, fonimu zinazofanana isipokuwa moja, na mpangilio wa fonimu ulio sawa,na
maana zikiwa tofauti. Halikadhalika katika seti ya maneno /paka/ na /taka/ kwa sababu nayo yana idadi sawa ya fonimu
yaani, fonimu nne zinazofanana isipokuwa moja na mpangilio wa fonimu ulio sawa.
Pia katika seti ya maneno /wali/ na /hali/ tunaona kuwa yapo katika jozi
mlinganuo finyu kwa sababu yana idadi sawa ya fonimu yaani fonimu nne zinazofanana
isipokuwa moja na mpangilio wa fonimu ulio sawa. Njia hii hutusaidia kuzitambua
fonimu za lugha kwa sababu tofauti ya fonimu moja yatosha kubadili maana za
maneno hayo.
2.4.3 Mbinu ya mgawanyo wa kiutoano.
Hyman
(1975) anasema katika fonolojia, utoano ni dhana ambayo hutumika kuelezea
uhusiano uliopo baina ya sauti mbili (au zaidi) za fonimu moja ambazo haziwezi
kutokea katika mazingira sawa katika neno. Hii ina maana kwamba sauti huwa ina
mahali/mazingira yake maalum ambayo hayawezi kukaliwa na sauti nyingine ya
kundi moja.
Tuchunguze
mifano kutoka katika lugha ya Kiingereza; kuhusu sauti /ph/ yenye
mpumuo na sauti /p/ isiyo na mpumuo. Sauti /ph/ yenye mpumuo hutokea
mwanzoni mwa maneno tu, kwa mfano katika maneno /phin/, /phen/,
/phut/ n.k . Kwa upande mwingine /p/ isiyo na mpumuo hutokea sehemu
yoyote ya neno isipokuwa mwanzoni; mfano katika maneno kama /top/, /cup/, /span/,
/spare/ n.k
Sauti
ambazo ziko katika mgawanyo wa kiutoano huwa hazitofautishi maana za maneno,
isipokuwa sauti hizo hugawana tu mahala pa kutokea au kutumika. Hivyo sauti
hizo huwa ni alofoni za fonimu moja.
Tuchunguze
sifa bainifu za sauti /ph/ yenye mpumuo na sauti
/p/ isiyo na mpumuo;
/ph/ /p/
+kons +kons
+mpumuo -mpumuo
-ghuna -ghuna
+midomo +midomo
+kipasuo +kipasuo
[ph]
yenye mpumuo na sauti [p] isiyo na mpumuo ni alofoni za fonimu
/p/. Sifa zote za sauti hizi zinafanana isipokuwa moja tu (sifa ya mpumuo).
2.4.4 Mbinu ya Mpishano Huru.
Huu
ni uhusiano wa fonimu mbili tofauti kubadilishana nafasi moja katika maneno
maalum bila kubadili maana za maneno hayo. Hapa mpishano unatumika kwa ile
maana ya “wewe ondoka, mimi niingie.” Kwa kuwa fonimu moja inatolewa katika
neno fulani na fonimu nyingine inakaa mahali pake bila kubadili maana ya neno
hilo.
Mpishano
huru huhusisha fonimu mbili kubadilishana
nafasi moja katika neno moja. Fonimu
hizo huwa ni tofauti kabisa kifonetiki hivyo hatuwezi kuziita alofoni.
Tuchunguze
mifano ifuatayo;
·
/buibui/
na /baibui/ sauti /u/ na /a/
zimepishana nafasi bila kubadili maana ya neno.
·
/Wasia/
na /wosia/ sauti /a/ na /o/
zimepishana bila kubadili maana ya maneno.
Tuchunguze
sifa bainifu za kifonetiki za sauti /a/ na /u/ katika maneno /baibui/ na /buibui/
/a/ /u/
+irabu +irabu
+mbele +nyuma
+chini +juu
-mviringo +mviringo
Tuchunguze
pia sifa bainifu za kifonetiki za sauti /a/ na /o/ katika maneno /wasia/ na /wosia/
/a/ /o/
+irabu +irabu
+mbele +nyuma
+chini +nusujuu
-mviringo +mviringo
Sauti
hizi haziwezi kuwa alofoni kwa sababu zinatofautiana sana kifonetiki.
Njia
hizi zitumikapo, aghalabu kwa pamoja, kwa kusaidiana huweza kutusaidia kutambua
fonimu na alofoni za lugha inayofanyiwa uchunguzi.
3.0 Alofoni katika lugha ya Kiswahili.
Sasa
tuchunguze dhana ya alofoni kama inavyojadiliwa na wataalamu mbalimbali wa
Isimu ya Kiswahili. Hapa tutaonesha fasili pamoja na mifano ya alofoni katika
lugha ya Kiswahili kwa mujibu wa wataalamu hao.
Massamba
na wenzake (2013) wanasema alofoni ni sura au maumbo mbalimbali ya fonimu moja.
Fonimu za lugha huweza kupata sura
tofauti tofauti kulingana na mazingira katika neno ambamo hutokea. Hii ina
maana kwamba fonimu inaweza kubadilika ikachukua umbo moja kutokana na kutokea
kwake katika mazingira fulani na ikaweza pia kubadilika ikachukua umbo jingine
kutokana na kutokea kwake katika mazingira mengine tofauti katika neno. Wanatoa
mifano ya alofoni kutoka katika lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:
Mofimu za neno Matamshi yake
(a) ki+ti ki+refu [kiti kirɛfu]
(b) ki+ti ki+eusi [kiti ʦeusi]
(c) u+limi m+refu [ulimi mrɛfu]
(d) n+limi n+refu [ndimi ndɛfu]
(e) n+buzi [mbuzi]
(f) n+dama [ndama]
(g) n+gombe [ᵑᵓᵐᵇᵋ]
Katika mifano ya
Kiswahili hapo juu, tunaona mabadiliko ya kifonimu yakijitokeza. Katika mfano wa (b) fonimu /k/ inapofuatiwa na
irabu /i/ halafu kukawa na mpaka wa mofimu, kisha ikafuatiwa na irabu /e/ hubadilika na kuwa /ch/ ki+eusi = [tseusi] na katika (d) tunaona wazi
kuwa fonimu /l/ inapotanguliwa na
nazali /n/ hubadilika na kuwa /d/ [n+limi
= ndimi]. Halikadhalika katika mifano ya (e) na (g) tunaona kwamba nazali /n/
inapofuatiwa na kitamkwa /b/ hubadilika
na kuwa /m/, inapofuatiwa na kitamkwa /d/ hubakia /n/, na inapoafuatiwa na kitamkwa /g/ hubadilika na kuwa /ᵑ/.
Hii ina
maana kwamba katika
mazingira haya sauti
[ts] ni alofani
ya fonimu /k/,
[d] ni alofoni
ya fonimu /l/
na [m], [n]
na [ᵑ] ni
alofani za fonimu
/N/ (katika fonolijia
herufi hii kubwa
hutumika kuwakilisha dhana ya nazali) na alama /N/ ikiwa kama
kiwakilishi cha fonimu kuu
Alofoni
hizo hapo juu zimetokana na michakato ya mofofonolojia(taaluma ya isimu
inayoshughulikia uchunguzi na uainishaji wa vipengere vya kifonolojia
vinavyoathiri maumbo ya mofimu au vipegere vya kisarufi vinavyoathiri maumbo ya
fonimu). Pamoja na kwamba mabadiliko haya yameitwa mabadiliko ya kifonimu
lakini tukichunguza vizuri tutaona kwamba kwa kiasi kikubwa ni maumbo yaliyobadilika
na kwa kiasi Fulani fonimu.
Kwa
mfano, mofimu ya ngeli ya tisa {n-} katika majina kama vile nyumba, mbuzi,
ng’ombe, n.k (inabadilika katika mazingira tabirifu) kuwa mofimi {m},{ŋ} na wakati mwingine hubaki vilevile
{n}.
Mchakato huu huitwa mchakato wa au kanuni ya konsonanti kuathiri nazali. Hivi
kwamba mofimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {m} pale inapokuwa imeitangulia
sauti ya midomo. Halikadhalika mofimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {ŋ} pale inapokuwa imeitangulia sauti ya
kakaa laini.
Kwa mantiki hii basi maumbo haya yote
yatakuwa yanaiwakilisha mofimu moja yaani ngeli ya tisa {n-}. Kama hivi ndivyo
basi maumbo hayo yatakuwa ni alomofu na si alofoni.
Alomofu ni mojawapo ya viwakilishi
viwili au zaidi vya mofimu moja ambavyo hujitokeza katika mazingira tofauti ya
mtoano. Massamba na wenzake(2012)
Katika data ambayo imetolewa na Massamba
na wenzake (wameshatanjwa) kuna baadhi ya sauti ambazo zinatokana na michakato
ya kifonolojia au badiliko la kifonolojia ambapo nazali huiathiri konsonanti
inayoambatana nayo ili kurahisisha matamshi. Sauti zinazoathirika hapa ni sauti
za likwidi (kimadende /r/ na kitambaza /l/).
(a)
u+limi m+refu [ulimi mrɛfu]
(b)
n+limi n+refu [ndimi
ndɛfu]
Sauti
/l/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya kutanguliwawa na nazali
/n/, vilevile sauti /r/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya
kutanguliwa na nazali /n/.
Sauti
hizi zinatokea katika mazingira ya kiutoano na zinafanana sana kifonetiki hivyo
twaweza kuziita alofoni.
Tuchunguze
sifa za kifonetiki za sauti /r/ na /d/, na /l/ na /d/
/r/ /d/
/l/ /d/
+kons +kons
+kons +kons
+ufizi +ufizi
+ufizi +ufizi
+kimadende +kipasuo +ktambaza +kipasuo
Mdee
(1986), anadai kuwa sauti [x] na [h] ni alofani za fonimu /h/ kama
inavyodhihirika katika maneno /kheri/ na
/heri/.
Tukichunguza
sauti hizi, ni kweli kwamba hazileti tofauti za maana katika lugha ya Kiswahili
isipokuwa sauti hizi
ni tofauti mno
kifonetiki. Wakati sauti /x/ ni ya kakaa
laini, sauti /h/ ni ya glota.
Je,
sauti moja inaweza kutamkiwa katika sehemu mbili tofauti?
Matinde
(2012) anasema alofoni ni maumbo mawili au zaidi ambayo huwakilisha fonimu
moja. Anaendelea kwa kusema kuwa alofoni ni matamshi tofauti tofauti ya fonimu
moja ambayo hujitokeza kutegemea mazingira ya utokeaji wa sauti hiyo.
Matinde(keshatajwa)
yeye anatofautiana na wanaisimu kama Mdee (ameshatajwa) ambao wanasema lugha ya
Kiswahili ina alofoni kwa kutumia jozi za maneno/kheri/ na /heri/ wakisema /x/
na /h/ ni alofani za fonimu /h/. Anasema tukizingatia vigezo vya kutambulisha
alofoni, hizi ni sauti ambazo ni tofauti kabisa kwa misingi ya sifa bainifu za
kifonetiki, hususan jinsi ya kutamkwa na mahali pa kutamkiwa.
Matinde
(ameshatajwa) anasema alofoni katika lugha ya Kiswahili sawa na lugha ya
Kiingereza, hudhihirika na vipasuo hafifu, hivi kwamba kipasuo hafifu
kinapokuwa mwanzoni mwa neno kutamkwa kikiwa na mpumuo, ilhali kipasuo hicho
kinapotanguliwa na fonimu tofauti hutamkwa bila mpumuo. Kwa mfano neno /pale/ kipasuo (p) hutamkwa kikiwa na
mpumuo (ph) lakini kipasuo hicho kinapotanguliwa na fonimu tofauti
kwa mfano katika neno /alipo/ kipasuo /p/ hutamkwa bila mpumuo. Anaendelea kueleza
kuwa hali hii hudhihirishwa pia katika maneno;
Neno
Utamkaji
Katika /khatika/
Palipo /phalipo/
Panda /phanda/
Kaa /khaa/
Kwa
hivyo, maumbo yote mawili yaani [p] na [ph]
ni alofani za fonimu /p/. Aidha, maumbo [k] na [kh] ni alofani za
fonimu /k/.
Sauti
alizozionesha Matinde (keshatajwa) ambazo
ni kama alofoni ni vibadala tu
katika lugha ambavyo hutokana na tofauti za kilahaja. Lakini pia mtindo wa
uzungumzaji waweza kusababisha vibadala hivi. Ndio maana si hajabu kukutana na
binti wa kimjini akitamka kwa madaa “palipo uzia penyeza mapenzi”.
Matamshi
yake ni kama; /phalipho
uzia phenyeza maphenzi/
Mpumuo
sio sifa bainifu ya sauti za Kiswahili sanifu. Sina bainifu za sauti za
Kiswahili ni kama vile; sifa ya ukonsonanti, namna ya kutamka, mahali pa kutamkia,
mkao wa glota na unazali.
4.0 MAONI
YANGU
Kwa
maoni yangu, lugha ya Kiswahili inazo alofoni, ila ni vizuri zaidi kuwa makini
katika kuzibaini alofoni hizo. Vigezo vinavyotupatia alofoni vitumike kwa
uangalifu sana. Kwa mfano, katika kigezo cha kufanana sana kifonetiki sauti
huchukuliwa kwamba ni tofauti sana iwapo zitatofautiana mahala pa kutamkia. Pia
dhana ya alofoni isichanganywe na alomofu kwa sababu afoloni hurejelea sauti
wakati alomofu urejelea umbo.
5.0 HITIMISHO
Tumeona
kuanzia mwanzo wa mjadala kwamba ni vigumu kubainisha alofoni katika lugha ya
Kiswahili. Ugumu huu unatokana na ukweli kwamba wataalam wametoa mifano ambayo
inakinzana labda kutokana na vigezo vya uainishaji kutofautiana. Baadhi ya
mifano haikidhi sifa za alofoni.
Nihitimishe
kwa kutoa rai kwa wanazuoni na wanazuoni watarajiwa kuendelea kufanya tafiti
zaidi zitakazolenga kuchunguza alofoni katika lugha ya Kiswahili. Pia Niseme
wazi hapa kuwa alofoni hizo zikidhi sifa au vigezo vya kuitwa alofoni. Ninashukuru
sana kwa usikivu wenu.
Mungu
ibariki Afrika
Mungu
ibariki CHAWAKAMA
Mungu
tubariki wanachama wa CHAWAKAMA
“LONGA KISWAHILI TUJIKOMBOE
KIFIKRA”
6.0 MAREJELEO:
Jones, D. (1950) An
Outline of English Phonetics. New Delhi, Kalyani Publishers.
Habwe, J na Peter K.(2004). Msingi ya sarufi ya Kiswahili.Phoenix
Publishers. Nairobi.
Katamba, F.(1996). An
Introduction to Phonology. New York: Longman
Ladefoged, P.(1962) Element
of Acoustic Phonetics. London: University of Chicago Press.
Massamba,D.P.B, Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2013) Fonolojia ya Kiswahili Sanifu. Sekondari naVyuo. Dar es salaam: TUKI.
Massamba,D.P.B, Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2013) Fonolojia ya Kiswahili Sanifu. Sekondari naVyuo. Dar es salaam: TUKI.
Massamba,D.P.B,
Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2012) Sarufi Maumbo ya Kiswahili.
Sekondari na Vyuo. Dar es salaam: TUKI.
Matinde, S.R.(2012) DAFINA
YA LUGHA. Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T)
Ltd.
Mdee, J.(1986). Kiswahili:
Muundo na Matumizi Yake. Nairobi: Intercontinental Publishers Ltd.
Mgullu, R. S.(1999) Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na
Fonolojia ya Lugha ya Kiswahili. Nairobi. Longhorn Publishers.
TUKI (2013) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford
University Press.