KISUMBUA KICHWA Na SALUMU
CHIVALAVALA.
KISA CHA BAO.
Niwakumbushe
kuhusu ya kale, kipindi ambacho paka alipokufa tulimzika njia panda huku tukiacha
fagio pembezoni mwa kaburi lake ili kila apitaye asiache kufagia, kaburi la
paka lilidumu kuwa safi siku zote. Na ni katika kipindi hicho hicho ambapo
tulicheza bao kwa mtindo wa kula, kusafiri na hata kutakata.
Mpumbavu
katika umri wa miaka arobaini ni mpumbavu wa milele, mimi sitaki hata kukaribia
huko kabla ya kuondoa kila chembe ya upumbavu akilini mwangu. Nasema hivyo kwa
sababu kupindua misingi ya kale ya kimaadili si kitu chema hata kidogo.
Wapo
vijana wa rika yangu nilikuwa nao katika mti wa kivuli udondoshao majani ya
aina mbili yaani ya kuwasha na ya kulainisha, tukiwa pale tulisimuliana kuhusu
bao, nilieleza uzuri wa bao na hasa mchezo ukikuendea vema ukamla mwenzako mara
kwa mara. Bao ni mchezo wa mababu na tumeukuta hivyo sie vijana. Ukicheza kwa
ustadi na akili utakula sana kila tundu lenye kete nyingi na mwishowe
utajizalishia kete nyingi katika majumba yako.
Wenzangu
walinidhihaki kwa kusema bao la vijana huliwa mbele na nyuma hivyo niachane na
mitindo ya kale, nikauliza “mbele na nyuma walaje!” nikaambiwa “ Muda huo huo
wa kuchezwa ukifika hatua ya kula basi unakomba tundu la mbele na la nyuma huachi
kitu aisee” nilistaajabu ya Musa ndio maana niliyaona ya firauni.
Kwa
uchezaji huo kwakweli ni uharibifu tupu, kwa sababu mchezo wa bao kwa wachezaji
hutumia vitobo vya nyuma kuhifadhi mitaji ya kete zao na kwa lugha rahisi
tunaweza sema kule nyuma ndiko kunakowekezwa nguvu za mchezo, sasa ikitokea mtu
anakula hadi huko basi ni wazi kuna uharibifu mkubwa wafanyika na haiwezi
kutokea kukazaliwa kete nyingine kwa aliyeanza kuliwa bali mlaji ndio anaweza
kuwa na uwezo wa kuzalisha kete kadiri atakavyo japo vidole vitachoka kwa ugumu
wa kuvipeleka hadi nyuma kutafuta ulaji.
Kwa
kuwa mjumbe hauawi, basi nami nasema jamani bao tucheze kama zamani, tule
matundu ya mbele tupu tena tusiache kutakata kabla ya kula. Tukifanya hivyo
tutajikuta tukifurahi siku zote na wala vidole hutakuta vikichoka mapema na
wala hatutaharibu matundu ya nyuma yakabaki tupu kama fuko la mashine ya kusaga
dona. Tuache mitindo ya nje iso na tija!