Historia ya lugha ya Kiswahili imegawanyika katika vipindi tofauti katika ukuaji na kuenea kwake, lakini asili ya lugha hii imeelezewa na wataalamu wengi kupitia hoja mbalimbali.
Ni kwa sababu hii, asili ya lugha hii imebaki kuwa jambo la mjadala mrefu. Wapo wanaokinasibisha Kiswahili na Kiarabu kwa kutumia kigezo cha misamiati ya Kiarabu iliyopo kwenye lugha hii.
Wengine wanashikilia msimamo kuwa Kiswahili ni Kibantu kwa kutumia hoja za kiisimu na kihistoria. Wapo wanaokinasibisha Kiswahili kama lugha chotara.
Hoja ya Kiswahili ni Kiarabu
Wanaomini katika mtazamo huu, wanahoji kwamba katika lugha ya Kiswahili kuna maneno mengi ya Kiarabu. Pia wanaeleza kuwa asili ya Kiswahili ni Pwani na kwa kuwa wenyeji wa Pwani ni Waislamu na kwa kuwa Uislamu uliletwa na Waarabu basi hii lugha ya Pwani nayo itakuwa imeletwa na Waarabu.
Mtazamo huu una udhaifu kwa kuwa maelezo yake hayakujikita katika misingi ya kitaalamu.
Kiswahili ni lugha chotara
Wanaofasili Kiswahili kama lugha chotara wanadai kuwa Kiswahili kimetokana na mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na lugha za Kibantu. Hivyo Waswahili ni watu waliotokana na wanaume wa Kiarabu na wanawake wa Kibantu.
Mtazamo huu umezua ukinzani mkubwa wa mawazo kwani hata baadhi ya wazawa wamejinasibisha na Uarabu na Ushirazi.
Kiswahili ni lugha ya vizalia
Wanaounga mtazamo huu wanadai kuwa Kiswahili kilianza kama pijini ya Kiarabu na baadaye kukomaa na kuwa kreoli yake. Pijini ya Kiarabu ni lugha inayotokana na mchanganyiko wa lugha mbili tofauti yaani Kiarabu na lugha za Kibantu. Kreoli ni lugha inayozungumzwa na watoto waliozaliwa na baba Mwarabu na mama Mbantu.
Kiswahili ni Kikongo
Nadharia hii inafafanua kuwa lugha ya Kiswahili ilianzia huko Kongo na kusambaa katika Pwani ya Afrika Mashariki.
Wabantu walipofika Afrika Mashariki, waliingia kwa makundi na katika nyakati mbalimbali. Makundi hayo yalianza kujigawa na kutawanyika, matokeo ya kugawanyika huko ni kutokea kwa makundi mbalimbali ya Wabantu.
Inasadikika kuwa baadhi ya Wabantu walifanya makazi yao ya kudumu katika mabonde ya Kaskazini mwa Mto Tana.
Kiswahili ni Kibantu
Mtazamo huu unaamini kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu na lugha za Kibantu zilikuwapo hata kabla ya kuja wageni kutoka Uajemi, Arabuni, India, China na kwingineko.
Katika mtazamo huu lugha ya Kiswahili inaingizwa katika kundi la lugha za Kibantu.
Vigezo vilivyotumika kufafanua kuwa Kiswahili ni kibantu ni pamoja na: Msamiati, mofolojia, mfumo wa sauti, mfumo wa ngeli na mpangilio wa maneno.
Wataalamu wa lugha wameandika kuhusu lugha ya Kiswahili kama lugha ya taifa na lugha rasmi inayokadiriwa kutumiwa na watu wapatao zaidi ya milioni 60 duniani kote.
Hutumika katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kama Tanzania, Kenya, Uganda na katika eneo la mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Vilevile katika nchi za Burundi, Rwanda, Msumbiji, Zambia, Comoro na Malawi. Kiswahili kinazungumzwa pia katika nchi za Uarabuni kama Dubai, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Yemen, Dubai, n.k.
Kwa kipindi cha miaka zaidi ya miaka elfu moja, kumekuwa na mawasiliano kwa viwango tofauti katika nchi za Mashariki ya Kati, Uajemi, India, China, Ureno na Uingereza. Nchi hizi zimechangia kwa kiwango kikubwa kwa kukopesha maneno mengi ya lugha zao katika lugha ya Kiswahili. Katika sehemu mbalimbali duniani viko vyuo vinavyofundisha lugha hii. Pia viko vituo vingi vya utangazaji vya redio na runinga vinavyotumia Kiswahili.
Ukichunguza muundo wa maneno na miundo wa sentensi za Kiswahili utagundua kuwa Kiswahili kinafanana sana na lugha za Kibantu kuliko Kiarabu, Kiajemi na Kihindi. Inasemekana kuwa idadi ya maneno ya mikopo kutoka lugha za kigeni katika lugha ya Kiswahili inaweza kulinganishwa na mikopo ya maneno katika lugha kongwe kama Kilatini, Kigiriki na Kifaransa ambazo zimechangia sana katika kuikuza lugha ya Kiingereza. Ni dhahiri kuwa ukopaji wa maneno katika lugha yoyote ile ni dalili ya kukua kwa lugha husika.
Nchini Tanzania na Kenya, lugha ya Kiswahili ni lugha za rasmi za mataifa haya. Kwa upande wa Kenya, Kiswahili ni somo la lazima linalofundishwa katika shule za msingi na sekondari. Nchini Tanzania, Kiswahili ni somo la lazima pia katika shule za sekondari hadi kidato cha nne na pia ni lugha ya kufundishia katika shule za msingi.
Asili ya Kiswahili
Yako maneno mawili ambayo tunayochanganya katika matumizi nayo ni asili ya lugha ya Kiswahili na chimbuko lake. Neno asili lina maana ya jinsi jambo lilivyoanza au lilivyotokea. Ama kwa neno chimbuko, maana yake ni mahali kitu au jambo lilipoanza. Kwa hiyo asili na chimbuko yanatofautiana katika maana.
Zimewahi kutokea nadharia kadhaa kuhusu asili ya Kiswahili ambazo nitazieleza hivi punde. Kwanza ipo nadharia kuwa Kiswahili kimetokana na lugha ya Kiarabu. Pili iko nadharia kuwa Kiswahili ni mchanganyiko wa Kiarabu na lugha za Kibantu zilizotumika katika upwa wa Afrika Mashariki. Tatu, ni kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu iliyoathiriwa sana na Kiarabu hasa kimsamiati. Nne, Kiswahili kilitokana na mchanganyiko wa lugha kadhaa za Kibantu zilizokuwa katika upwa wa Afrika Mashariki.
Nadharia isemayo kuwa Kiswahili kilitokana na Kiarabu inaegemea sana wingi wa maneno yenye asili ya Kiarabu na pia dini ya Kiislamu. Inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianza pwani na kwa kuwa idadi kubwa ya wananchi wa pwani ni Waislamu na kwa kuwa Uislamu uliletwa na Waarabu, basi Kiswahili nacho kinashabihiana na Kiarabu. Madai haya hayana mashiko kwani Kiswahili ni lugha kamili iliyokopa maneno kutoka katika lugha za Kiarabu, Kiajemi, Kireno, Kihindi, Kijerumani na Kiingereza kutokana na mawasiliano ya karne nyingi kati ya wenyeji wa pwani na wafanyabiashara wa kigeni
Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa Kiswahili hasa wanaisimu wamegundua kuwa mabadiliko yalihusu msamiati tu na wala siyo maumbo ya maneno wala miundo ya tungo za Kiswahili. Ikumbukwe pia kwamba uchunguzi ulikwishafanywa kuwa kwa kipindi kirefu Kiswahili kilitumia maneno mengi kutoka katika lugha za Kibantu kwa kuwa wasemaji wengi wa Kiswahili ni Wabantu.
Jambo la msingi ni kuwa lugha kuwa na maneno mengi ya kukopa kutoka katika lugha nyingine haifanyi lugha hiyo ionekane imetokana na hiyo lugha ngeni. Inabidi kuzingatia zaidi msingi wa lugha kwa upande wa fonolojia, mofolojia, semantiki na sintaksia ya lugha husika. Kimsingi, vigezo pekee vinavyoweza kutumika ili kuibainisha lugha ni vya kisimu kama vile fonolojia, mofolojia na sintaksia lakini msamiati siyo msingi pekee wa kuzingatia.
Nadharia ambazo zinazaweza kuwa ni msingi wa uhakika ni mbili. Moja ni ile isemayo kuwa Kiswahili kina asili ya Kibantu. Msingi wa pili ni kuwa Kiswahili ni lugha iliyotokana na lugha kadhaa za Kibantu katika eneo la pwani.
Kiisimu lugha ya Kiswahili ina utaratibu maalumu ambao ni herufi kama konsonanti na irabu ambapo huweza kuunda silabi kama ba, ma, ka, la; au konsonanti, konsonanti na irabu kama kwa, gha, mwa, n.k.; au konsonanti, konsonanti, konsonati na irabu kama, mbwa, ng’we n.k.
Chimbuko la Kiswahili
Ni vigumu kusema kwa uhakika mahali ambapo ni chumbuko la Kiswahili. Pengine tunaweza kusema kuwa Kiswahili kilianzia sehemu maalumu na kuenea hadi mahali fulani. Inadaiwa kuwa chimbuko la Kiswahili liko katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya lakini madai haya hayajawahi kuthibitishwa kwa hoja zenye mashiko.
Ni wazi kuwa wanahistoria waliowahi kuandika kuwa mawasiliano na maelewano kati ya watu wa eneo fulani kwa kiasi fulani kulizuka lugha moja iliyoeleweka kwa watu wote katika eneo hilo. Mawasiliano ya aina hii yalizua lugha ambazo zilitofautiana kuanzia kaskazini hadi kusini mwa pwani ya Afrika Mashariki ambazo zilijulikana kama lahaja za Kiswahili. Kuanzia Kaskazini kuna lahaja ya Ci Miini ambayo huzungumzwa katika eneo la Barawa, pwani ya Somalia.
Kusini zaidi kulikuwa na lahaja za Kitukuu na Kibajuni katika eneo la kusini mwa Somalia na Kaskazini mwa Kenya. Nyingine ni Kisiu sehemu za Pate, Kiamu huko Lamu, Kimvita sehemu za Mombasa, Kivumba na Kimtang’ata katika sehemu za pwani ya kaskazini mwa Tanzania, Kimakunduchi, Kihadimu, Kitumbatu sehemu za Unguja na Kipemba eneo la Pemba. Lahaja hizi zinafanana na lugha nyingine za Kibantu. Lahaja hizi zinatofautiana kidogo na
Kiswahili sanifu kwa sababu Kiswahili sanifu kina maneno mengi ya mkopo. Lahaja zote hizo ni lugha zinazojitegemea.
Kuenea kwa Kiswahili
Kama inavyofahamika, chimbuko la Kiswahili ni upwa wote wa Afrika Mashariki. Hata hivyo lugha hii haikubaki tu katika eneo la pwani bali ilienea katika sehemu kubwa ya Afrika Mashariki. Sababu za kuenea katika sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki kulisababishwa na mambo mengi. Yako mambo yaliyosababisha kuenea kwa Kiswahili kutoka pwani hadi bara. Mambo hayo ni shughuli za biashara, dini, ukoloni na hatimaye harakati za kupata uhuru. Tuangalie mchango wa mambo haya manne katika kukieneza Kiswahili.
Biashara
Katika maelezo yaliyotolewa na wanahistoria ni kwamba wageni walikuja Pwani ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kufanya biashara. Hata hivyo walikuwapo wenyeji wa pwani waliosafiri kwenda bara kwa ajili ya kufanya biashara na wageni walipokuja waliwaonyesha njia walizowahi kuzitumia na hivyo Kiswahili kilienezwa kwa njia hiyo. Kwa maana hiyo yalikuwapo mawasiliano baina ya wenyeji wa bara na pwani kwa kipindi kirefu kabla hata ya kuwasili kwa wageni. Wafanya biashara wa Kiarabu walijikita sana katika biashara ya pembe za ndovu, madini na pia utumwa. Waafrika waliokuwa wapagazi ndiyo waliokieneza Kiswahili kwa kuwasiliana na wenzao huko bara.
Wafanyabiashara hawa walifika maeneo ya mbali hadi Mashariki mwa Kongo na Burundi. Kutokana na umbali kutoka pwani hadi Kongo, ilitokea lahaja ya pekee iliyojulikana kama Kingwana ambayo ilitumika na kuenea katika maeneo Kongo. Kimuundo na kimsamiati lahaja ya Kigwana inafanana sana na lugha nyingine za Kibantu zina zotumika huko.
Kuenezwa kwa dini za kigeni
Kuenea kwa dini za kigeni kama Uislamu na Ukristo kulichukua nafasi kubwa katika maisha ya wenyeji. Waarabu waliotopea katika dini ya Uislamu walitumia Kiswahili. Wahubiri wa Kiislamu walilazimika kujifunza Kiswahili kwani wenyeji hawakujua Kiarabu. Wahubiri hawa walilazimika kujifunza Kiswahili kueleza mafungu ya Korani kwa lugha inayoeleweka kwa wengi. Wahubiri hawa walianza kutumia maandishi ya Kiswahli wakitumia alfabeti za Kiarabu. Kwa kufanya hivyo, walisaidia sana kukieneza Kiswahili.
Kwa upande wa dini ya Kikristo, Wamisionari hawakutaka sana kuitumia lugha ya Kiswahili na waliifananisha na Uislamu. Wao walipendelea kutumia lugha za asili lakini walikosea kwani ilikuwa vigumu kujifunza lugha zote za wenyeji pamoja na kuziandika. Wangefanikiwa zaidi kama wangetumia lugha ya Kiswahili kwani ingetumiwa na waumini wengi. Baadaye walilazimika kutumia Kiswahili kuhubiri na kuandika. Kwa kuanzia walianzisha shule za dini kwa ajili ya mafundisho ya Kikristo. Wamisionari ndiyo walioanza kutumia alfabeti za Kirumi kuandikia mahubiri yao.
Kwa kuanzia wamisionari waliandika vitabu na hata kuchapisha magazeti kwa kutumia Kiswahili. Tunayo magazeti yaliyochapishwa na yalisaidia sana kukieneza Kiswahili, kwa mfano:
Habari za mwezi -1988
Pwani na bara - 1910
Barazani - 1910
Rafiki yangu
Habari za Wakilindi 1903
Gazeti la Msimulizi
Kitabu cha Wakilindi.n.k.
Wakati wa Ukoloni
Viko vipindi vitatu vya ukoloni vilivyokuwa na athari kubwa kwa lugha ya Kiswahili. Kipindi cha kwanza kilikuwa ni ukoloni wa Kiarabu. Kipindi hiki kilihusika moja kwa moja na ueneaji wa Kiswahili. Wakati huo Sultani wa Zanzibar alitawala Visiwa vya Pemba na Unguja pamoja na ukanda wa maili kumi wa eneo la Pwani ya Kenya na Tanganyika. Kiswahli kilitumika katika kuandika na kutafsiri mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Shule za madrasa zilitumia Kiswahili kote bara na visiwani.